Kazi-Maisha Iliyo Nzuri Sana
Miaka 57 ya Maisha ya Kimisionari
Kama ilivyosimuliwa na Eric Cooke
KATIKA utusitusi wa mapambazuko, niliegemea ufito mrefu wa mashua ya kuvukia mfereji-bahari na kuzidi kuutazama unyenyezi kwenye upeo wa macho. Ndugu yangu na mimi tulikuwa tumetoka Southampton, Uingereza, jioni iliyotangulia na tulikuwa tukielekea Saint-Malo, Ufaransa. Tulikuwa watalii? La, tulikusudia kupeleka ujumbe wa Ufalme wa Mungu Ufaransa. Tulipowasili Saint-Malo, tulikusanya baiskeli zetu tukaziendesha kusini.
Hivyo ndivyo ndugu yangu mchanga John na mimi tulipoondoka kwenda kufanya kazi ya misionari katika nchi ya kigeni zaidi ya miaka 57 iliyopita. Ni nini kilichokuwa kimetuongoza kuingia utumishi wa wakati wote? Ni nini kilichotushurutisha kuacha maisha ya utulivu katika nyumba yenye starehe ya Kiingereza?
Kilichoongoza Maisha Yetu
Katika 1922 mama yangu alihudhuria hotuba ya watu wote “Wafu Wako Wapi?” Alisisimuliwa nayo na karibuni akawa mtumishi aliyejiweka wakfu wa Yehova. Lakini Baba hakufurahi. Yeye alikuwa mshiriki wa Kanisa la Kianglikana, na kwa miaka mingi alitupeleka kanisani asubuhi ya Jumapili huku Mama akitufundisha mambo ya Biblia alasiri.
Katika 1927 John akawa na miaka 14 na kuanza kuhudhuria mikutano pamoja na Mama na kushiriki katika ushuhuda wa mlango kwa mlango. Lakini mimi nilikuwa na kinaya, kwa maana nilikuwa na kazi nzuri katika Benki ya Barclay. Hata hivyo, kwa kustahi Mama, hatimaye nilianza kujifunza Biblia, pamoja na vichapo vya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi. Baada ya hapo, niliendelea haraka kiroho, na katika 1930 nikabatizwa.
Alipoacha shule katika 1931, John alianza huduma ya wakati wote akiwa painia. Alipodokeza kwamba niandamane naye katika kazi ya painia, mimi niliacha kazi-maisha yangu ya benki nikajiunga naye. Jina letu jipya, Mashahidi wa Yehova, tulilokuwa tumelipokea karibuni tu liliimarisha hali yetu ya kupiga moyo konde. Mgawo wetu wa kwanza ulikuwa mji wa La Rochelle na eneo lenye kuuzunguka katika pwani ya magharibi ya Ufaransa.
Kupainia kwa Baiskeli katika Ufaransa
Tulipokuwa tukiendesha baiskeli kusini kutoka Saint-Malo, tulipata shangwe ya kuona viunga vya matofaa vya Normandy na kunusa-nusa harufu nzuri zilizotoka kwenye mashine za kuminya umajimaji wa matofaa hayo. Hatukung’amua kwamba zile fuo zilizo karibu baharini katika Normandy zingeharibiwa vibaya miaka 13 baadaye, wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, na baadhi ya mapigano yenye kumwaga nyingi zaidi katika historia; wala hatukung’amua kwamba huduma yetu ya wakati wote ingeendelea kwa muda mrefu jinsi hii. Mimi nilimwambia John kwa mzaha hivi: “Nafikiri tutawahi kuwa mapainia miaka mitano. Har-Magedoni haiwezi kuwa mbali mno!”
Baada ya siku tatu za kuendesha baiskeli, tukawasili La Rochelle. Sisi wote wawili tulijua Kifaransa kwa kiasi, kwa hiyo hatukutatizwa kupata chumba cha kadiri chenye fanicha. Kwa kuendesha baiskeli, tulifanya kazi katika vijiji vyote vya umbali wa kilometa 20 kila upande, tukigawanya fasihi za Biblia. Halafu tukahamia jiji jingine na kurudia utaratibu huo. Hamkuwa na Mashahidi wengine katika sehemu hiyo ya Ufaransa.
Katika Julai 1932, John, aliyekuwa amejifunza Kihispania shuleni, alitumwa na Sosaiti akatumikie Hispania. Mimi niliendelea katika Ufaransa ya kusini na kwa miaka miwili nikawa na mfululizo wa wenzi wa kikazi kutoka Uingereza. Kwa sababu hakukuwa na ushirika mwingine pamoja na Mashahidi, sala ya ukawaida na funzo la Biblia vilikuwa muhimu ili kudumisha imara yetu ya kiroho. Pia tulirudi Uingereza mara moja kwa mwaka kwa ajili ya mikusanyiko ya kila mwaka.
Katika 1934 tuliondoshwa Ufaransa. Kanisa Katoliki la Kiroma, likiwa na uvutano mwingi wakati huo, ndilo lilisababisha. Badala ya kurudi Uingereza, nilijiunga na mapainia wengine wawili Waingereza, nasi tukaelekea Hispania—kwa kuendesha baiskeli zetu kama kawaida. Usiku mmoja tulilala chini ya vichaka, usiku mwingine juu ya rundo la majani makavu ya mifugo, na usiku mwingine katika ufuo wa bahari. Mwisho tukawasili Barcelona kaskazini-mashariki mwa Hispania na kujiunga na John, aliyetukaribisha.
Tatizo Tulilokabili Hispania
Hakukuwa na makundi ya Mashahidi wa Yehova katika Hispania wakati huo. Baada ya kufanya kazi katika Barcelona kwa miezi michache, tulisonga mbele Tarragona. Huko ndiko kwa mara ya kwanza tulianza kutumia kinanda chenye kubebeka na sahani zilizorekodiwa hotuba fupi za Biblia katika Kihispania. Zilikuwa na matokeo sana, hasa katika mikahawa na nyumba za vinywaji zilizosongamana watu.
Katika Lerida, upande wa kaskazini-magharibi, Shahidi mkaa-peke-yake, Salvador Sirera, alijiunga nasi. Kwa kutiwa moyo na kukaa kwetu katika eneo hilo, yeye alitumikia kwa muda akiwa painia. Katika Huesca, Nemesio Orus alitukaribisha kwa shauku kwenye nyumba yake ndogo juu ya duka la mtengeneza saa. Alikuwa ndiye mtu wa kwanza tuliyemwongoza funzo la nyumbani la Biblia, tukitumia kimoja cha vijitabu vya mapema vya Sosaiti. Tulifanya funzo hilo muda wa saa kadhaa kila siku, na karibuni akajiunga nasi kuwa painia.
Katika jiji tulilofuatisha kufanya kazi, Zaagoza, tulipata shangwe ya kusaidia Antonio Gargallo na Jose Romanos, hao wakiwa ni vijana wawili matineja. Kila jioni walikuja kwenye chumba chetu kidogo kwa ajili ya funzo la Biblia tuliloongoza katika kitabu Government. Baada ya muda, wote wawili wakajiunga nasi katika kazi ya painia.
Twashtakiwa Kuwa Wafashisti
Kwa sasa, matata yalikuwa yakianza kuwaka. Vita ya Kihispania ya Wenyewe kwa Wenyewe ilikuwa karibu kufoka, hilo likiwa ni pigano ambalo mamia ya maelfu wangekufa hatimaye. Katika kijiji kimoja karibu na Zaragoza, Antonio na mimi tuliingia katika magumu. Mwanamke mmoja aliyekubali vijitabu vyetu alikosea kwa kudhani ni propaganda za Kikatoliki naye akatushtaki kuwa Wafashisti. Tulikamatwa tukapelekwa kituo cha polisi. “Mnafanya nini katika kijiji hiki?” sajini akadai tumweleze. “Watu hapa ni wakomunisti na hawataki propaganda za Kifashisti!”
Tulipokwisha kueleza kazi yetu, akaridhika. Akatufadhili kwa kutupa chakula cha mchana na kutushauri tuondoke kijiji kwa unyamavu wakati ambapo watu wangekuwa katika usingizi kidogo wa mchana. Lakini tulipoondoka, wanaghasia wakawa wakitungoja. Walichukua kwa nguvu fasihi zetu zote. Ilikuwa hali mbaya. Hata hivyo, tulishukuru kwamba sajini yule aliwasili akaongea na wanaghasia hao kwa busara. Aliwaridhisha alipojitolea kutupeleka Zaragoza tukaone wenye mamlaka. Huko akatutetea kwa ofisa wa jiji, nasi tukaachiliwa.
Katika Julai 1936, vita ya wenyewe kwa wenyewe ilipoanza, Antonio alikataa kupigana na majeshi ya Franco naye akauawa. Itakuwa shangwe iliyoje kwa John na mimi kumkaribisha katika ufufuo na kuona tena tabasamu yake yenye uanana!
Twaitwa Wakomunisti Katika Ailandi
Muda mfupi kabla haijatokea vita ya wenyewe kwa wenyewe, John na mimi tulirudi Uingereza kwa likizo yetu iliyo kawaida ya kila mwaka. Ndipo vita ikafanya isiwezekane kurudi Hispania, kwa hiyo tukapainia majuma kadhaa katika Kent, katika Broadstairs karibu na nyumbani kwetu. Ndipo ukaja mgawo wetu uliofuata—Ailandi. Msimamizi wa Sosaiti, Joseph F. Rutherford, alitupangia kwenda huko tukagawe trakti maalumu yenye kichwa You Have Been Warned (Umeonywa). Hakukuwa na makundi katika Ailandi ya kusini, ni Mashahidi wachache tu hapa na hapa.
Wakati huu, kwa uchochezi wa makasisi Wakatoliki, tulishtakiwa kuwa wakomunisti—kinyume hasa cha shtaka lililofanywa dhidi yetu katika Hispania! Wakati mmoja genge la Wakatoliki wenye hasira kali liliingia kwa kishindo katika nyumba tulimokuwa tukikaa, likachukua kartoni zetu za fasihi, na kuzichoma. Tulipatwa na vituko kadhaa vya jinsi hiyo kabla hatujarudi Uingereza katika kiangazi cha 1937.
Vita ya Ulimwengu 2 Hadi Gileadi
Vita ya Ulimwengu 2 ilipotangazwa katika Septemba 1939, John alikuwa akitumikia katika Bordeaux, Ufaransa, nami nilikuwa mwangalizi wa kundi katika Derby, Uingereza. Mapainia fulani, kutia na John, waliokuwa wamejiunga nami upya, walipewa ruhusa ya kutolazimishwa utumishi wa kijeshi, lakini wengine, kama mimi, tukanyimwa ruhusa. Kwa hiyo mimi nilikuwa nikiingia na kutoka gerezani wakati wa vita. Uvumilivu ulihitajiwa ili kuchukuliana na hali zilizokuwa katika magereza ya wakati huo wa vita, lakini tulijua kwamba ndugu zetu Ulaya walikuwa wakiteseka zaidi.
Baada ya vita msimamizi mpya wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, Nathan H. Knorr, alizuru Uingereza akapanga mapainia fulani wahudhurie Shule ya Biblia ya Gileadi ya Mnara wa Mlinzi katika mkoa wa juu wa New York, kwa mazoezi ya kimisionari. Kwa hiyo Mei 1946 ilikuta John na mimi tukivuka Bahari Kuu ya Atlantiki tukiwa katika meli ya Uhuru iliyojengwa wakati wa vita.
Darasa la nane la Gileadi ndilo lililokuwa la kwanza kuwa la kimataifa kweli kweli. Ilichangamsha moyo kama nini kujifunza na kushirikiana na mapainia wa muda mrefu wakati wa mtaala ule wa miezi mitano! Hatimaye, siku ya kuhitimu ikafika, na mwishowe tukajua migawo yetu. Mimi niligawiwa kwenda Rhodesia ya Kusini, inayojulikana kuwa Zimbabwe sasa, na John akatumwa Ureno na Hispania.
Utumishi wa Kimisionari Katika Afrika
Nilikanyaga Cape Town, Afrika Kusini, katika Novemba 1947. Merikebu nyingine ilileta wanadarasa wenzetu Ian Fergusson na Harry Arnott. Ndugu Knorr akazuru baada ya muda mfupi, nasi tukahudhuria mkusanyiko katika Johannesburg. Ndipo tukasonga mbele kaskazini kwenye migawo yetu—Ian akaenda Nyasaland (sasa Malawi), Harry akaenda Rhodesia ya Kaskazini (sasa Zambia), nami nikaenda Rhodesia ya Kusini (Zimbabwe). Baada ya muda Sosaiti ikaanzisha tawi, nami nikawekwa rasmi kuwa mwangalizi wa tawi. Tulikuwa na makundi 117 yakiwa na wahubiri karibu 3,500 nchini.
Baada ya muda mfupi wamisionari wanne wapya wakawasili. Walitarajia mgawo wao uwe wa vijumba vya matope vilivyoezekwa majani, huku simba wakinguruma usiku, nyoka wakiwa chini ya kitanda, na zikiwako hali za kishamba. Badala ya hivyo, waliiita Bulawayo paradiso ya painia kwa sababu ya kuwako miti ya maua kandokando ya barabara kuu, mazingira ya kufurahisha, na watu walio tayari kusikiliza ujumbe wa Ufalme.
Marekebisho Mawili ya Kibinafsi
Nilipobatizwa katika 1930, uelewevu ulikuwa kidogo kuhusu wale ambao wangepata uhai wa milele duniani. Kwa hiyo John na mimi tulishiriki mifano wakati wa Ukumbusho, hali moja na kila mtu wakati huo. Hata katika 1935, wakati “umati mkubwa” wa Ufunuo sura ya 7 ulipotambulishwa kuwa jamii ya kidunia ya “kondoo,” kufikiri kwetu hakukubadilika. (Ufunuo 7:9, NW; Yohana 10:16) Halafu katika 1952, Mnara wa Mlinzi (Kiingereza) ukatangaza kwa chapa katika ukurasa 63 tofauti kati ya tumaini la kidunia na tumaini la kimbingu. Tukaja kung’amua kwamba hatukuwa na tumaini la uhai wa kimbingu, bali tumaini letu lilikuwa la uhai katika dunia-paradiso.—Isaya 11:6-9; Mathayo 5:5; Ufunuo 21:3, 4.
Namna gani lile rekebisho jingine? Mimi nilikuwa nikizidi kumpenda sana Myrtle Taylor, aliyekuwa amekuwa akifanya kazi pamoja nasi kwa miaka mitatu. Kwa maana ilionekana wazi kwamba yeye alihisi hivyo hivyo juu yangu na kwamba sisi wote wawili tulithamini utumishi wa kimisionari kwa kina kirefu, tuliposana na kufunga ndoa katika Julai 1955. Myrtle amethibitika kuwa mke mwenye kuniunga sana mkono.
Huduma Katika Afrika ya Kusini
Katika 1959 Ndugu Knorr alizuru Rhodesia ya Kusini, na Myrtle na mimi tukagawiwa upya kwenda Afrika ya Kusini. Muda si muda tukaanza kusafiri katika mgawo wangu katika kazi ya mzunguko. Hizo zilikuwa siku bora weee. Lakini mimi nilikuwa nikiongezeka umri, na afya ya Myrtle ilikuwa imetuhangaisha kwa kadiri fulani. Baada ya muda hatukuweza kuvumilia mwendo wa kazi ya mzunguko, kwa hiyo tukaanzisha makao ya kimisionari katika Cape Town na kutumikia huko kwa miaka kadhaa. Baadaye, tuligawiwa upya kwenda Durban, katika Natal.
Mgawo wetu huko ukawa Chatsworth, jumuiya kubwa ya Kihindi. Huo ulikuwa mgawo wa kigeni ndani ya mgawo wa kigeni—dai halisi la kukabiliana nalo tukiwa wamisionari wazee-wazee. Tulipowasili katika Februari 1978, kulikuwa na kundi la Mashahidi 96, sana-sana Wahindi. Tukalazimika kuchunguza fikira za kidini za Wahindu na kuelewa desturi zao. Njia ya kufikia watu iliyotumiwa na mtume Paulo katika kutoa ushuhuda katika Athene ikawa kielelezo chenye msaada kwetu.—Matendo 17:16-34.
Baraka za Utumishi wa Kimisionari
Sasa mimi nina miaka 78, nikiwa nimeacha nyuma miaka 57 ya utumishi wa kimisionari. Inatia moyo kama nini kuona maongezeko ya kustaajabisha katika nchi ambazo nimetumikial Ufaransa imefikia wapiga mbiu ya Ufalme 100,000, Hispania zaidi ya 70,000, na Afrika ya Kusini imeongezeka kutoka 15,000 wakati tulipowasili ikawa na zaidi ya 43,000.
Nyinyi vijana, je! hali zenu zinawaruhusu kuingia huduma ya wakati wote? Ikiwa ndivyo, mimi naweza kuwahakikishia kwamba hiyo ndiyo kazi-maisha iliyo bora zaidi. Si kwamba ni ulinzi tu kutoka kwenye matatizo na vishawishi vinavyowazinga vijana leo bali pia inaweza kufinyanga utu wenu upatane na kanuni adilifu za Yehova. Ni faida na pendeleo kama nini kwa vijana na wazee pia kumtumikia Yehova sasa!
[Picha katika ukurasa wa 29]
Mgeni aja kwenye jiko la kambi ya Myrtle Cooke