Wapiga Mbiu ya Ufalme Waripoti
Utafutaji wa Ukweli wa Biblia Wathawabishwa Katika Israeli
WATU zaidi na zaidi katika Israeli kama vile kwingineko wanaona ubatili wa jitihada za mwanadamu za kuleta amani yenye kudumu na kuandaa tumaini kwa wakati ujao. Wale Mashahidi wa Yehova 370 katika bara hilo zuri la kihistoria, wanaleta tumaini lenye kutoa uhai kwa wale wanaotafuta Mungu. (Isaya 55:2, 3) Ripoti zifuatazo kutoka ofisi ya tawi ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi katika Tel Aviv zaonyesha kwamba Mungu huthawabisha wale ambao hutafuta ukweli wa Biblia.
“Zile ghasia za wanaghasia wenye kushikilia dini bila akili zimetulia, na matokeo ya jitihada zao za wakati uliopita za kuingilia mikutano yetu yaendelea kuwarudia wao wenyewe. Kutoa kielelezo, mume na mke Warusi wenye umri mkubwa walikuwa wakishirikiana na kikundi cha Adventisti lakini wakakosa kuridhika na mambo waliyokuwa wakijifunza. Wao hawakuona ushahidi wowote wa minyanyaso ambayo ilitabiriwa kwamba ingetia alama Ukristo wa kweli. Ndipo siku moja wakapata gazeti kuukuu la Kiromania lililotupwa ambalo lilikuwa na ripoti ya mashambulio ambayo wanaghasia wajeuri walifanya huko nyuma katika 1985 juu ya jengo la ofisi ya tawi ya Sosaiti na Jumba la Ufalme katika Tel Aviv. Upendezi wao ukiwa umechochewa, walisafiri kwenda Tel Aviv na wakatembea huku na huku kwa saa nne mpaka wakapata jengo lililoelezwa katika ile makala ya karatasi-habari. Walishangilia kupokea majibu kwa baadhi ya maswali yao na wakabaki kwa ajili ya mkutano wa jioni, ambapo walifurahia kukutana na baadhi ya Mashahidi wasemao Kirusi. Tangu hapo, funzo la Biblia la ukawaida limefanywa pamoja nao, Walivyozidi kujifunza, ndivyo walivyozidi kusadikishwa kwamba wamepata kile kile walichokuwa wakitafuta—ukweli!
“Katika kisa kingine, ndugu mmoja alitolea ushuhuda mwanamume kijana mwenye jamaa ambaye hakuafikiana na baadhi ya mambo aliyojaribu kumwelezea na hivyo hakuendelea kuchunguza ujumbe wa Ufalme. Miaka kadhaa baadaye, binti ya mwanamume uyu huyu akawa mgonjwa, naye akaambiwa na marafiki wenye hofu ya kishirikina kwamba yaelekea tatizo linahusiana na mezuza iliyoshikanishwa na mwimo wa mlango wake. Walipendekeza kwamba amlete rabi aichunguze. Aliamua kufanya hivyo. Wakati ule ule, yeye alisali kwa Mungu kwa bidii apate mwongozo katika kupata ukweli.
“Akiwa njiani kwenda nyumbani kwa rabi, mwanamume yule akaamua ghafula kwenda akachukue dawa alizoandikiwa kwenye kliniki. Alipowasili, apate nani akiketi pale ila Shahidi yule yule aliyekuwa amemhubiri miaka kadhaa huko nyuma? Ndugu yule anataarifu kwamba yeye hakuwa amekuwa na mipango ya kwenda kwenye kliniki jioni hiyo mpaka akakumbuka ghafula kitu fulani alichohitaji. Ndugu yule na mwanamume yule wakakaa na kuongea kwa saa kadhaa jioni hiyo, na funzo la Biblia likapangwa pamoja na kijana huyo. Alianza kuhudhuria mikutano, maendeleo yake yakawa thabiti, naye akajiunga na Shule ya Huduma ya Kitheokrasi. Upesi yeye akawa akienda katika huduma ya shambani, na sasa yeye ni ndugu aliyebatizwa. Yeye hakupata kamwe kufika kwenye nyumba ya rabi!”
Utafutaji wa ukweli wa Biblia wa watu hawa ulithawabishwa kwa njia yenye kutajirisha sana, kwa kuwa wamepata hazina yenye thamani zaidi ya dhahabu nzuri.—Mithali 3:13-18.