Je! Kazi Ngumu Huleta Furaha?
“INGAWAJE, hakuna jambo jingine la kumfaa mwanadamu ila kazi, au sivyo?” akauliza Bunpei Otsuki, tajiri mkubwa katika ulimwengu wa kibiashara katika Japani. Yeye alikuwa akieleza ni kwa nini hakutaka kuchukua likizo la kiangazi. Maneno yake yalingana kabisa na yale ya Wajapani waliorekebisha vurugu kubwa iliyokuwa humo nchini baada ya vita. Wajapani wameelezwa kuwa watu wenye bidii sana tangu Amiri Perry wa United States alipoifungua Japani kutoka kipindi chayo kirefu cha upweke wa kutengwa kabisa na nchi nyinginezo. Nao huona fahari kuwa wafanya kazi wenye bidii.
Hata hivyo, sasa Japani inachambuliwa kwa kufanya kazi kwa bidii mno, kwa kuwa miongoni mwa yale yaitwayo mataifa yenye viwanda, hiyo ndiyo hutumia saa nyingi zaidi za kazi kila mwaka. Serikali ya Japani inajaribu kufutilia mbali sifa hiyo ya kuonwa imekolewa na ulevi wa kazi. “Wizara ya Kazi Yasema ‘Acheni Kufanya Kazi kwa Bidii Sana,’ “chasema kichwa kimoja kikuu cha karatasi-habari. Katika wito wake wa kuhimiza sana kuwe na kipindi cha likizo la kiangazi katika 1987, wizara hiyo hata ilifikia hatua ya kusema, “Kuchukua likizo ni uthibitisho wa kwamba wewe ni hodari wa kazi.” Ndiyo kusema, serikali inaliuliza taifa hivi, “Mbona mfanye kazi kwa bidii sana?”
Bila shaka, si watu wote katika Japani walio wafanya kazi wenye kujitoa sana na wenye bidii. Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi na Kitovu cha Ukaguzi wa Mafanikio ya Kazi kuhusu wafanya kazi wapya zaidi ya 7,000 ulifunua kwamba ni asilimia 7 tu kati yao waliotanguliza kazi mbele ya maisha yao ya faragha. Elekeo hili laweza kuonwa katika nchi nyinginezo pia. Katika Ujeremani, shirika Allensbacher Institut fur Demoskopie lilipata kujua kwamba ni asilimia 19 tu ya Wajeremani wa kati ya miaka 18 hadi 29 waliodai kuwa hufanya yote wawezayo kazini bila kujali watapata malipo gani.
Kwa kulinganishwa na vijana wenye kuchukua mambo kirahisi tu, wafanya kazi walio wageni nchini Japani hufanya kazi kwa bidii zaidi. Mwajiri mmoja katika Tokyo hung’aa uso kwa furaha akimsifu mwajiriwa wake Mwaljeria ambaye hufanya kazi ya mikono. Yeye asema hivi: “Wajapani hawatajaza ombi wapewe kazi ya aina hii, na hata kama wakijaza, wangeiacha mara hiyo.” Hata Wajapani wenyewe walio wafanya kazi wenye bidii hawakuzaliwa wakiwa na asili ya bidii-nyendelevu, hapana. Watu wafanyapo kazi kwa bidii, lazima kuwe kuna kichocheo imara.
Sababu za Kufanya Kazi kwa Bidii
“Utajiri, uimara, mali, na kupanda ngazi katika ulimwengu”—mambo haya ndiyo yanayotafutwa na Wajeremani wenye bidii, charipoti kichapo cha Kijeremani Der Spiegel cha kila juma. Ndiyo, wengi hufanya kazi kwa bidii wapate utajiri ili waweze kuwa na shangwe ya kupata kadiri fulani ya uimara maishani. Wengine hufanya kazi kwa bidii wakiwa na lengo la “kupanda ngazi katika ulimwengu” au kuinua cheo chao katika shirika. Jambo la kusikitisha ni kwamba wengi wenye kusukumwa sana na mfumo wa kushindania elimu ili wafuatie miradi hiyo huja kujikuta wakijikokota tu katika kazi ya viwandani isiyowafurahisha—wakinyong’onyea bila kupata walichotazamia.
Hata hivyo, sababu zenye kufanya watu watie bidii kazini si pesa na cheo tu. Watu fulani hufanya kazi ili wafanye kazi tu. Kwa maoni yao, hakuna jambo jingine la kumfaa mtu ila kazi tu. Wengine huona shangwe kuhusu kazi yao. “Mimi nilipendezwa sana na kazi niliyokuwa nikifanya katika maabara yangu,” anakiri Haruo, “hivi kwamba shughuli za kiroho zilisongwa zikafifia.”
Halafu kuna wale ambao wamejitoa sana kufuatia shabaha zenye ustahiki kwa utumishi na kujali masilahi ya wengine. Wao hufanya kazi kwa bidii ili waokoe uhai wa watu. Mathalani, mzima-moto hufanya kazi kwa bidii kila siku ili adumishe vifaa vyake katika utaratibu mzuri.
Lakini je! zote hizi ni sababu zifaazo za kufanya kazi kwa bidii? Je! zitaongoza kwenye furaha? Hasa, ni kazi gani iwezayo kukufurahisha wewe kweli kweli?