Maswali Kutoka kwa Wasomaji
◼ Wanasayansi wanashikilia kwamba nyota fulani huungua au hulipuka, kwa hiyo kwa nini Isaya 40:26 inasema kwamba “hapana moja [ya nyota] isiyokuwapo mahali pake”?
Hapa Yehova hazungumzii juu ya kama yeye huruhusu nyota zipotee. Yeye anakazia kiwango cha hekima na uwezo wake.
Nabii Isaya alipeleka onyo la Mungu kwa Mfalme Hezekia kwamba Wababuloni wangewapeleka Wayahudi katika utekwa. (Isaya 39:5-7) Je! Wababuloni wangeweza kuwaweka watu wa Mungu kwa wakati usio dhahiri? Hapana. Si kwamba Yehova alikusudia tu kuwaweka huru baada ya miaka 70 bali angefanya hivyo. Hakuna kitu ambacho kingemzuia Mmoja huyo ambaye anaweza ‘kuyapima maji kwa konzi ya mkono wake, na kuzikadiri mbingu kwa shubiri.’ Yeye hangelazimika kushauriana na yeyote, kwa kuwa kwake “mataifa ni kama tone la maji katika ndoo.” (Isaya 40:2-17) Ili kukazia uwezo huu wenye kushangaza wa kuweka vitu, Yehova alielekeza fikira kwenye uwezo wake unaodhihirika katika uumbaji, ambao Hezekia alikuwa ametangulia kuukiri. (Isaya 37:16,17) Mungu alijulisha wazi hivi:
“Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye? asema yeye aliye Mtakatifu. Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake.”—Isaya 40:25, 26.
Wanasayansi wanakadiria kwamba kuna maelfu ya mamilioni ya nyota katika galaksi yetu ya Njia ya Kimaziwa, na kuna magalaksi kama milioni mia moja elfu. Hata hivyo Mungu ajua kila nyota kwa jina, labda kwa jina la moja moja au kwa mtajo ulio kama jina, pengine katika lugha ya kimungu. Ndiye mwenye amri ya mahali zipasapo kuwa. Kama vile jenerali anayeweza kukutanisha kikosi cha kijeshi, Yehova anaweza kuziita nyota zikusanyike mahali pamoja. Kama angefanya hivyo, hakuna moja ambayo ‘haingekuwapo.’ Akijua hali ya kila nyota, hata ikiwa nyingine zazo zinafikia kikomo cha asili, hilo si jambo la kushangaza Mmoja huyo anayejua yote yanayotendeka.—Linganisha Isaya 34:16.
Wataalamu wa nyota na wanafizikia wanafikiri kwamba nyota huungua au hulipuka. Katika Red Giants and White Dwarfs, (Majitu Mekundu na Mbilikimo Weupe) Robert Jastrow anatoa nadharia jinsi jambo hili linavyoweza kutukia: “Ndani ya ile . . . nyota mlianza vitendeshano vya nyukilia, na elementi nyingine zote za ulimwengu wote mzima zilifanyizwa kutokana na kianzishi kile cha msingi, haidrojeni. Hatimaye vitendeshano hivi vya nyukilia vilififia vikamalizika, na maisha ya nyota ile yakafikia mwisho. Kwa kunyimwa vyanzo vyayo vya nishati za nyukilia, ilianguka kwa kulemewa na uzito wayo yenyewe, na mlipuko ukatokea kutokana na anguko hilo, ukinyunyizia anga vitu vyote vilivyokuwa vimeumbwa ndani ya nyota ile katika muda wa maisha yayo.”
Inadhaniwa kwamba nyota fulani, zenye kumaliza haidrojeni zazo zinabadilika kuwa majitu mekundu kisha zinakuwa mbilikimo weupe, na hatimaye baadhi yazo zinakuwa nyota za niutroni au, kulingana na nadharia, mashimo meusi.
Ingawa maelezo haya yanakubaliwa kwa wingi, huenda neno la uamuzi wa mwisho likawa halijasikiwa bado; huenda mengi zaidi yakapata kujulikana. Fikiria, kwa kielelezo, mambo yaliyosemwa katika The New York Times la Januari 24, 1989: “Wanasayansi wanaamini kwamba wako karibu kufanya ugunduzi mkubwa-mkubwa kuhusu ‘enzi zenye giza’ za ulimwengu wote mzima, kile kipindi cha maana sana kuanzia dakika tatu za kwanza baada ya kulipuka kwa uumbaji mpaka kutokea kwa magalaksi makubwa mno. . . . Kwa kuwa kuna ushuhuda kidogo sana wa moja kwa moja, wanasayansi hawafahamu kabisa muundo ulianza-anzaje. James S. Trefil, mwanafizikia kwenye Chuo Kikuu cha George Mason katika Fairfax, Va., ameandika hivi: ‘Tatizo la kueleza kuwapo kwa magalaksi limethibitika kuwa mojapo matatizo yenye kuhangaisha sana katika elimu ya nyota. Kulingana na kanuni zote za haki, hazipaswi hata kidogo kuwa pale, na hali hapo ndipo zilipo.”’
Makala hiyo ilizungumzia jambo ambalo huenda likawa lilitukia wakati wa “zile dakika tatu za kwanza,” kama inavyoelezwa na Dakt. John Mather, mwanafizikiawa nyota. Hata hivyo, tunasoma hivi: “Dakt. Mather, akihisi mvurugo unaoendelea wa mwenye kuhojiwa, alikatiza masimulizi yake juu ya maelezo ambayo hukubaliwa kwa ujumla kuhusu uumbaji akasema kwamba, ‘Bila shaka, tunabuni haya yote tu,’ ikimaanisha kwamba ni kutia madoido katika nadharia zinazotegemea kujikatia-katia maneno.”
Ndiyo, wanasayansi wa kibinadamu wamewekewa mpaka juu ya yale wanayojua hasa na wanayoweza kujua. Ingawa hivyo, ni tofauti iliyoje na Muumba. Kwa uhakika maarifa na nishati-msukumo alizo nazo zinastahili kutufanya tuonyeshe kicho. Mtunga zaburi alisema hivi kwa kufaa: “Yeye anahesabu namba ya nyota; zote anaziita kwa majina yazo. Bwana wetu ni mkubwa na mwingi katika uwezo; ufahamu wake hauwezi kusimuliwa. . . . Msifuni Yah, enyi watu!” —Zaburi 147:4,5,20, NW.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Picha ya NASA