Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w89 11/15 uku. 24
  • Johari Kutokana na Gospeli ya Luka

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Johari Kutokana na Gospeli ya Luka
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mambo Fulani Yasiyoonyeshwa Mahali Penginepo
  • Vituko Vyenye Kugusa Moyo
  • Kutoka Kwenye Kalamu ya Tabibu
  • Muono-Ndani Katika Desturi
  • Masomo ya Unyenyekevu
  • Tabibu Luka Afanya Kazi Iliyo Bora Zaidi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1983
  • Kitabu Cha Biblia 42—Luka
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Luka—Mfanyakazi Mwenzi Mpendwa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Gospeli Kwa Kweli Ni Nini?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
w89 11/15 uku. 24

Johari Kutokana na Gospeli ya Luka

MWANA wa Yehova, Yesu Kristo, ajulikana sana kwa kuwa mwenye huruma. Basi, yafaa kama nini kwamba Luka mwandikaji wa Gospeli apaswa kukazia huruma, rehema, na hisia-mwenzi! Kwa Wayahudi na Wasio Wayahudi pia, yeye aliandika usimulizi wenye kuchangamsha moyo kweli kweli kuhusu maisha ya Yesu ya kidunia.

Pande fulani za Gospeli hii zaonyesha kwamba mtu mwenye ujuzi wa uanachuo ndiye aliyeiandika. Kwa kielelezo, hiyo ina utangulizi ulioandikwa kwa usanifu mwingi na ina msamiati mwingi. Mambo hayo yalingana na uhakika wa kwamba Luka alikuwa tabibu mwenye elimu nzuri. (Wakolosai 4:14) Ingawa yeye hakupata kuwa mwamini mpaka baada ya kifo cha Yesu, aliandamana na Paulo kwenda Yerusalemu baada ya safari ya tatu ya kimisionari ya Paulo. Kwa hiyo, baada ya Paulo kukamatwa huko na kutiwa gerezani kule Kaisaria, mtafiti huyu mwenye uangalifu aliweza kukusanya habari kwa kuhoji mashahidi walioona mambo kwa macho yao wenyewe na kwa kuangalia maandishi ya utumizi wa watu wote. (1:1-4; 3:1, 2) Huenda ikawa Gospeli yake iliandikwa kule Kaisaria muda fulani wakati mtume alipokuwa amezuiliwa kwa miaka miwili huko, karibu 56-58 W.K.

Mambo Fulani Yasiyoonyeshwa Mahali Penginepo

Angalau sita ya miujiza ya Yesu haionyeshwi mahali popote pengine isipokuwa katika Gospeli ya Luka. Hayo ni: kuvuliwa kwa samaki kimuujiza (5:1-6); kufufua mwana wa mjane kule Naini (7:11-15); kuponya mwanamke aliyekunjikana maradufu (13:11-13); kuponya mwanamume mwenye kujazana maji mwilini (14:1-4); kutakasa wakoma kumi (17:12-14); na kurudisha sikio la mtumwa wa kuhani mkuu.—22:50, 51.

Pia jambo ambalo halionyeshwi mahali popote pengine isipokuwa katika usimulizi wa Luka ni baadhi ya mifano ya maneno ya Yesu. Hii ni kutia na: wale wadeni wawili (7:41-47); Msamaria mwenye moyo wa kijirani (10:30-35); mtini usiozaa (13:6-9); ule mlo mkuu wa jioni (14:16-24); mwana mpotevu (15:11-32); tajiri na Lazaro (16:19-31); na yule mjane na hakimu asiye mwadilifu.—18:1-8.

Vituko Vyenye Kugusa Moyo

Tabibu Luka alionyesha hangaiko kwa wanawake, watoto, na wazee-wazee. Yeye peke yake ndiye aliyetaja utasa wa Elisabeti, kuchukua kwake mimba, na kuzaliwa kwa Yohana. Gospeli yake tu ndiyo iliyoripoti kisa cha Gabrieli kumtokea Mariamu. Luka alisukumwa na moyo kusema kwamba kitoto cha Elisabeti kiliruka katika tumbo lake la uzazi wakati Mariamu alipokuwa akinena naye. Yeye peke yake ndiye aliyesimulia kuhusu kutahiriwa kwa Yesu na kuletwa kwake awe tokezo hekaluni, ambako Yeye alionwa na Simeoni mzee na Ana. Na kama isingalikuwa ni kwa sababu ya Gospeli ya Luka tusingalikuwa na maarifa kuhusu utoto wa Yesu na wa Yohana Mbatizaji.—1:1–2:52.

Luka alipoandika kuhusu yule mjane wa Naini mwenye kihoro aliyepoteza mwana wake wa pekee katika kifo, alisema kwamba Yesu “alimwonea huruma” halafu akamrudisha kijana huyo mwanamume kwenye uhai. (7:11-15) Chenye kuripotiwa katika Gospeli ya Luka tu, na pia kikiwa ni chenye kuchangamsha moyo, ni kile kituko chenye kuhusu Zakayo, mkuu mmoja wa wakusanya-kodi. Kwa sababu alikuwa na kimo kifupi, yeye alipanda mti ili aone Yesu. Ulikuwa mshangao ulioje Yesu aliposema angekaa nyumbani kwa Zakayo! Luka aonyesha kwamba ziara hiyo ilikuwa baraka kubwa kwa mkaribishaji huyo mwenye furaha.—19:1-10.

Kutoka Kwenye Kalamu ya Tabibu

Gospeli hii ina mitajo au maneno mengi yenye maana za kitiba. Maneno haya hayakutumiwa kamwe katika maana ya kitiba na waandikaji wengine wa Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Lakini tungeweza kutarajia usemi wa kitiba utoke kwenye kalamu ya tabibu.

Kwa kielelezo, ni Luka peke yake aliyesema kwamba mama-mkwe wa Petro alikuwa na “homa kali.” (4:38) Pia aliandika hivi: “Tazama, palikuwa na mtu amejaa ukoma.” (5:12) Kwa waandikaji wale wengine wa Gospeli, ilitosha kutaja ukoma. Lakini sivyo kuhusu tabibu Luka, aliyeonyesha kwamba ugonjwa wa mwanamume yule ulikuwa katika hatua ya kukolea sana.

Muono-Ndani Katika Desturi

Luka alisema kwamba baada ya kuzaliwa kwa Yesu, Mariamu ‘alimfunga kwa vitambaa vya kufungiliwa.’ (2:7, NW) Kulingana na desturi, kitoto kichanga kilichozaliwa karibuni kilioshwa na kupakwa chumvi, labda ili kukausha ngozi na kuiimarisha. Halafu kitoto hicho kilifungiliwa vitambaa vyembamba, kikakaribia kuwa ni kama maiti yenye kuhifadhiwa. Vitambaa hivyo vilifanya mwili ukae ukiwa umenyooka na wenye joto, na kuvipitisha chini ya kidevu na kichwa huenda kukawa kulizoeza mtoto apumue kupitia puani. Ripoti moja ya karne ya 19 kuhusu desturi zilizo kama hiyo ya kufungilia mtoto vitambaa ilinukuu mgeni mmoja mwenye kuzuru Bethlehemu kuwa akisema hivi: “Mimi nilimtia kiumbe huyo mdogo katika mikono yangu. Mwili wake ulikuwa mgumu na usiobonyea, ukiwa umefungwa kabambe kwa kitani nyeupe na ya rangi ya zambarau. Mikono na nyayo zake zilikuwa zimefunikwa sana, na kichwa chake kilifungwa shali ndogo nyororo nyekundu, ambayo ilipita chini ya kidevu chake na kutoka upande mmoja hadi mwingine wa kipaji chake ikiwa imekunjwa mikunjamano midogo-midogo.”

Gospeli ya Luka yatoa pia muono-ndani kuhusu desturi za maziko katika karne ya kwanza. Yesu alikuwa karibu na lango la Naini alipoona “maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye.” (7:11, 12) Kwa kawaida maziko yalifanywa nje ya jiji, na marafiki wa mtu aliyekufa waliandamana na mwili ule kwenye kaburi. Jeneza lilikuwa machela iliyofanyizwa kwa matete yaliyosukwa nalo lilikuwa na miti yenye kutokeza nje kwenye pembe zalo kuruhusu wanaume wanne walihimili juu ya mabega yao wakati andamano lilipotembea kwenda kwenye uwanja wa maziko.

Katika kielezi kingine kilichoandikwa na Luka, Yesu alinena juu ya mtu mmoja aliyepigwa na wanyang’anyi. Msamaria mwenye moyo wa kijirani ‘alimfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai.’ (10:34) Hii ilikuwa njia ya kidesturi ya kutunza majeraha. Mafuta ya mzeituni yangefanya majeraha yawe mororo na kuyatuliza. (Isaya 1:6) Lakini namna gani ile divai? The Journal of the American Medical Association ilisema hivi: “Divai ilikuwa dawa yenye matumizi mengi katika Ugiriki. . . . Hippocrates wa Cos (460-370 KK) . . . alitumia divai kwa mambo mengi, akiieleza kuwa ni dawa ya kutunza jeraha, kitu cha kutuliza majoto makali ya mwili, cha kuondoa uchafu wa mwili, na cha kuongezea kutoka kwa mkojo.” Kielezi cha Yesu kilidokeza kwamba divai ina vitu vya kuzuia vidonda visioze na kuua viini vibaya humo, na pia kikadokeza juu ya matokeo mazuri ya mafuta ya mzeituni katika kusaidia kuponya majeraha. Bila shaka, maana ya mfano huo wa maneno ni kwamba jirani wa kweli hutenda kwa rehema. Hivyo ndivyo yatupasa tushughulike na wengine.—10:36, 37.

Masomo ya Unyenyekevu

Luka pekee ndiye alisimulia kielezi ambacho Yesu alitoa alipoona wageni wakichagua sehemu za umashuhuri kwenye mlo fulani. Wakati wa karamu, wageni waliegemea viti-vitanda vilivyowekwa kandokando ya pande tatu za meza. Wenye kupakua chakula walikuwa na nafasi ya kuendea meza hiyo kutokea upande ule wa nne. Kulingana na desturi, kiti-kitanda kilikaliwa na watu watatu, kila mmoja akikabiliana na meza huku akiwa ameegemea kiko cha mkono wa kushoto na kula kwa mkono wa kulia. Sehemu tatu hizo zilionyesha kwamba mtu alipewa ile nafasi ya juu, ya katikati, au ya chini katika kiti-kitanda. Mwenye nafasi ya chini katika kiti-kitanda cha tatu alikuwa ndiye mwenye mahali pa chini zaidi kwenye mlo. Yesu alisema: ‘Ukialikwa kwenye karamu, chagua mahali palipo pa chini zaidi na mkaribisha-wageni atakuambia wewe, “Enda juu kidogo.” Ndipo wewe utapata heshima mbele ya wageni wenzako.” (14:7-10, NW) Ndiyo, kwa unyenyekevu acheni sisi tutangulize wengine mbele yetu wenyewe. Kwa uhakika, katika kutumia kielezi hicho, Yesu alisema: “Yeyote anayejikweza atashushwa, na anayejishusha atakwezwa.”—14:11, HNWW.

Jambo ambalo pia linakazia unyenyekevu, ambalo tena halionekani mahali pengine popote isipokuwa katika Gospeli ya Luka, ni kile kielezi cha Yesu kuhusu mkusanya-kodi na Farisayo mwenye kusali katika hekalu. Miongoni mwa mambo mengine, Farisayo alisema, “Mimi nafunga mara mbili kwa juma.” (18:9-14) Sheria ilitaka kuwe na mfungo mmoja tu kila mwaka. Lakini Mafarisayo walifunga kupita kiasi. Yule mmoja aliye katika kielezi hicho alifunga siku ya pili ya juma kwa sababu huo ulifikiriwa kuwa ndio wakati ambapo Musa alipanda kuingia Mlima Sinai, ambamo alipokea tableti mbili za Ushuhuda. Asemwa kuwa alishuka kutoka mlima huo siku ya tano ya juma. (Kutoka 31:18; 32:15-20) Farisayo huyo alitaja ufungaji wake wa kila nusu-juma kuwa uthibitisho wa uchaji wake. Lakini kielezi hiki chapasa kitusukume sisi kuwa wanyenyekevu, si wenye kujihesabia uadilifu.

Johari hizi kutokana na Gospeli ya Luka zathibitisha kwamba ina mambo yasiyoonekana mahali pengine popote na ni yenye kufundisha. Vituko vyenye kusimuliwa katika usimulizi huo vyatusaidia tuhuishwe upya kuhusiana na matukio yenye kugusa moyo katika maisha ya kidunia ya Yesu. Pia twanufaika kutokana na habari za msingi zenye kuhusiana na desturi fulani-fulani. Lakini hasa tutabarikiwa tukitumia masomo kama yale ya rehema na unyenyekevu ambayo yafundishwa vizuri sana katika Gospeli hii iliyoandikwa na Luka, yule tabibu mpendwa.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki