Maswali Kutoka kwa Wasomaji
◼ Je! inamfaa Mkristo kwenda kuwinda au kuvua samaki?
Mara nyingi maitikio mbalimbali juu ya kuwinda huhusisha hisia za kina kirefu. Kwa hiyo ni vizuri kabisa Wakristo wajitahidi kuelewa na kutumia fikira ya Yehova Mungu juu ya jambo hilo kama ipatikanavyo katika Biblia.
Mungu aliipa ainabinadamu utawala juu ya wanyama “wa mwitu” na hata “wa kufugwa.” Hapo kwanza, wanadamu hawakuwa na ruhusa ya Muumba, wala uhitaji wowote wa kimwili, kuua wanyama kwa chakula. (Mwanzo 1:24, 29, 30) Ni baada ya Gharika tu kwamba Mungu aliipa ainabinadamu haki ya kula mnofu wa mnyama uliosafishwa vizuri “nafsi yao—uhai wao.” (Mwanzo 9:3, 4) Hiyo ingeweza kuwa ni nyama kutoka ama kwa wanyama wa kufugwa ama wa mwitu.
Waisraeli walifuga wanyama, kama kondoo na ng’ombe, ambao wangeweza kuchinjwa kwa chakula wakati ambapo walitamani nyama. Pia waliwinda na kuvua samaki ili wapate chakula. (Kumbukumbu 12:20-24; 14:4-20) Jambo hilo lapatana na usemi wa Mungu wa kitamathali kwamba ‘angetuma wavuvi wengi wakavue samaki kwa ajili ya watu wake na wawindaji wengi wakawinde kwa ajili yao.’ (Yeremia 16:16, NW) Baadaye, Yesu alitia wavuvi miongoni mwa mitume wake na alielekeza shughuli za uvuvi halisi wa samaki.—Mathayo 4:18-22; 17:27; Luka 5:2-6; Yohana 21:4-7.
Wakati Isaka mzee wa ukoo alipoomba mlo wa nyama wenye ladha, Yakobo mwana wake alikuwa na nia ya kuua mbuzi wachanga wawili kumfanyia mlo. Ingawa hivyo, Esau aliwinda mnyama-mwitu kumtafutia baba yake nyama-paa. Angalia kwamba ingawa nyama ya wanyama wa kufugwa ilipatikana, Isaka aliomba nyama ya mnyama wa pori. Angalia, pia, kwamba wana wote wawili waliua wanyama ambao wangekuwa chakula, si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili ya mtu mwingine.—Mwanzo 27:1-19.
Wanyama wangeweza kuuawa kwa sababu nyingine zaidi ya kupata nyama yao. Ngozi zao zingeweza kufanywa mavazi. (2 Wafalme 1:8; Marko 1:6; Waebrania 11:37) Vifuniko vya ulinzi na vyombo pia vilifanyizwa kwa ngozi kavu za wanyama, hata za wanyama wasiokuwa safi kwa ulaji na ambao Waisraeli hawakuwala.—Kutoka 39:33, 34; Hesabu 24:7; Waamuzi 4:19; Zaburi 56:8.
Takwa la Mungu kwamba damu ya wanyama waliochinjwa imwagwe lapasa kukumbusha wawindaji kwamba uhai wa wanyama umetoka kwake na kwa hiyo wapasa kutendewa kwa staha, si kwa mchezo-mchezo. (Walawi 17:13) Yaonekana wazi Nimrodi alichinja wanyama na labda akajivunia ustadi wake wa kuwinda, ukubwa au wingi wa mawindo yake, au tunu ambazo zingaliweza kufanyizwa kutokana nao. Alikuwa “mwindaji hodari katika kumpinga Yehova.”—Mwanzo 10:9, NW.
Msisimuko huo wa kuwinda au kuua wanyama, au kuvuta-vuta samaki kwa ndoana, ungeweza kusitawi katika Mkristo. Wawindaji au wavuvi wengi ambao wamechunguza sana moyo wao wamegundua kwamba waliambukizwa ile ‘shangwe ya kuua mawindo.’ Msisimuko wa jinsi hiyo huambatana na dharau ya kutojali sana uhai wa wanyama. Kwa hiyo ingawa si vibaya kuwinda wala kuvua samaki (wakati ambapo windo au vuo litatumiwa na mtu fulani kwa chakula au kusudi jingine linalofaa), haingefaa kufanya hivyo ikiwa Mkristo ana roho inayokumbusha juu ya ile ambayo Nimrodi alikuwa nayo. Lakini zipo hatari zaidi ya kupata msisimuko kwa kufukuzana na windo lenyewe, kuliua, au kulifanya liwe tunu.
Mnara wa Mlinzi wa Desemba 15, 1983 ulizungumza kwa nini Wakristo wa kweli hawabebi wala kuweka bunduki wazitumie dhidi ya wanadamu au wajilinde nao. (Kurasa 16-20) Kutafakari juu ya shauri hilo kumeongoza Mashahidi fulani wakadirie upya thamani ya kuwa na hata bunduki za kuwinda. Wengi wamechagua kuondoa kabisa bunduki zao au kuepuka kuziweka mahali pa kuonekana wazi na penye kufikika kwa urahisi. Hivyo Wakristo hawa hawangefanya kuwe na maoni ya kwamba wao wanajivunia silaha au kuzitumainia. Zaidi ya hilo, hata kutokuwa na bunduki za kuwinda, au kutoziweka mahali penye kufikika kwa urahisi, kwaweza kuepusha tanzia. Hapo silaha za kufisha hazingeweza kuingia mikononi mwa watoto ambao wangeweza kuumiza mtu au kumwua bila kukusudia, wala bunduki hazingekuwa karibu mkononi ikiwa mtu fulani apatwa na woga mwingi mno au ashuka moyo.—Linganisha Mithali 22:3.
Huenda Wakristo fulani wakawa wanapenda ladha ya wanyama au samaki fulani, na njia ifaayo zaidi kupata chakula hicho ni kwa kuwinda au kuvua. Wengine huona shangwe kupunga upepo na kupata mazoezi yanayohusiana na kuwinda mwituni, au huona kwamba kuvua samaki wakati wa saa zenye utulivu huburudisha. Biblia haineni dhidi ya jambo hilo, kwa hiyo hakuna uhitaji wa kuhukumu wengine juu ya kama wao huona au hawaoni shangwe juu ya mambo hayo. Na kielelezo cha Isaka na wana wake huonyesha kwamba hakuna uhitaji wa kufanya ubishi juu ya atakayekula wanyama au samaki hao.—Mathayo 7:1-5; Warumi 14:4.
Ni wazi kwamba mtume Petro alifungamana sana na uvuvi. Huku samaki fulani wakiwa chini hapo karibu, Yesu mfufuliwa alimsaidia kuchanganua hisia zake mwenyewe juu ya samaki au biashara ya uvuvi. Yesu aliuliza hivi: “Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa?”—Yohana 21:1-3, 9-15; ona Mnara wa Mlinzi, Novemba 1, 1988, ukurasa 31.
Vivyo hivyo, Mkristo ambaye kwa dhamiri njema achagua kwenda kuwinda au kuvua samaki apaswa kuratibu mambo yake ya muhimu. Kwa kielelezo, ikiwa msimu wa kuwinda au kuvua samaki ungeanza wakati ambapo mikutano ya kundi imeratibiwa, yeye angefanya nini? Au maongeo yake huonyesha kwamba yeye hujivunia ustadi wake wa kuwinda au kuvua samaki? Ni vizuri kama nini Mkristo mkomavu ambaye, pindi kwa pindi, huchagua kuwinda au kuvua samaki aweze kusema hivi kwa usadikisho: “Ndiyo, Bwana, wewe wajua mimi nina shauku kwako [kuliko kwa mifuatio hii].”—Yohana 21:16, NW.