Twahitaji Ulimwengu Mpya
PIGA hatua nyuma utazame hali zikuzungukazo. Je! wapenda uyaonayo?
Labda wewe binafsi una nyumba nzuri katika eneo lenye upendezi, lidumishwalo vizuri. Huenda pia ukawa una kazi yenye mshahara mzuri uipendayo. Kwa kuongezea, wewe na wapendwa wako huenda mkaonea shangwe kadiri fulani ya afya nzuri. Kwa ujumla, huenda ukahisi una usalama wa kutosha na furaha.
Lakini fikiria maeneo mengine ya ujirani, sehemu nyingine za nchi uishimo, mabara mengine. Tazama ulimwengu mzima. Je! uonayo yana sura nzuri? Je! ni ya kuridhisha, ya amani, na ya ufanisi kikweli?
Kulingana na matabiri fulani mapema katika karne hii, kufikia sasa sayansi ingalipaswa kuwa imefutilia mbali magonjwa yote makubwa, ikaandaa chakula kingi kwa wote, ikaimarisha na kuleta nafuu ya mazingira, na kuingiza enzi ya amani. Lakini kwa kweli kumetukia nini?
Hauhitajiwi uchunguzi mwingi ili kuona kwamba amani imeiepa sayari yetu. “Tangu nyakati za kibiblia, watu wameonywa kwa upole wafue panga zao kuwa majembe ya plau,” aandika Michael Renner katika State of the World 1990. “Ushauri huo haujapata kufaa kama ulivyo sasa. Mfuatio usiokoma wa uweza wa kijeshi umeleta jamii ya kibinadamu kwenye ukingo wa angamizo.”
Kuna ripoti nyingi juu ya magomvi na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo huua fungu kubwa la watu katika nchi nyingi sana kuzunguka tufe lote. Kulingana na chanzo kimoja, vita 22 vilipiganwa katika 1988.a Ni wangapi waliokuwa wamekufa katika vita hivyo? Kufikia na kuhusisha ndani mwaka huo, “jumla ya watu waliouawa katika vita vyote vyenye kupiganwa katika 1988 ilikuwa 4,645,000. Asilimia sabini na sita ya wale waliouawa walikuwa raia,” lasema St. Louis Post-Dispatch.
Je! matukio ya ulimwengu ya hivi karibuni yaonyesha kuna ulimwengu wenye amani kule mbele? “Habari zasema kwamba ile Vita Baridi inapungua na amani imepewa nafasi. Lakini tazama tena,” yasema makala moja katika San Jose Mercury News la Kalifornia, U.S.A. “Katika Ulimwengu wa Tatu, vita yasonga mbele kwa kishindo kukiwa na tumaini kidogo tu la kukomeshwa. Hivi ni vile vita vilivyofichwa vya ulimwengu. Sana-sana huwa ni mapigano ambayo hupambanisha serikali dhidi ya watu wao wenyewe: ming’ang’ano ya kumwaga damu wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya ardhi, dini, tofauti za rangi ya ngozi na za kikabila, mamlaka ya kisiasa, hata dawa za kulevya. . . . Kuanzia Pembe ya Afrika hadi Kusini-mashariki mwa Esia, vita imelazimisha mamilioni wakimbie kutoka kwenye nyumba zao. Mazao huwa hayapandwi, kliniki za afya hushambuliwa, mifugo huharibiwa, wazazi huuawa kinyama mbele ya watoto wao, wavulana wa miaka 10 hufanywa kuwa wapagazi kisha wakafanywa askari, wasichana wachanga hulalwa kinguvu. Katika mabara haya ambayo husahauliwa sana-sana, vita imeacha dalili za mabomoko na fujo ya kijamii ambayo huenda jamii hizi zisipone kabisa kutokana nayo. . . . Utafiti waonyesha miaka ya 1980 imeona vita vingi kuliko mwongo mwingine wowote katika historia.”
Wengi wa wale ambao huweza kukimbilia nchi zilizositawi zaidi hukuta amani waliyotumainia ikivunjwa-vunjwa na tisho la uhalifu wenye jeuri. “Mazingiwa ya uhalifu [United States] yameendelea muda wa miaka ya 1980 japo matabiri ya kwamba yangekoma,” laripoti U.S.News & World Report. “Katika mwaka wa kawaida: Kuna visa milioni 8.1 vya uhalifu mzito kama uuaji, ushambulizi na uvunjaji nyumba. . . . Jambo lenye kusononesha kabisa ni jinsi umwagaji damu umeenea sana na kuwa usiotabirika. Kutumia watu kama wahanga wa kutendwa mabaya ni hali iliyosedeka. Ofisi ya United States ya Takwimu za Haki yakadiria kwamba asilimia 83 ya watoto walio na miaka 12 sasa watakuwa wahanga wa jeuri halisi au ya majaribio ikiwa uhalifu utaendelea kwa kadiri za sasa. . . . Hakuwi na uhakika wa kutoa adhabu kwa watenda makosa wala uharaka wa kuitoa. Taifani pote, katika visa 5 vya uhalifu mkubwa polisi huweza kutatua 1 tu.” Hali kama hizo zipo ulimwenguni pote. Baraza Kuu la UM laripoti “ongezeko la utukio na uzito pia wa uhalifu katika sehemu nyingi za ulimwengu.”
Lakini hata kama vita vyote, silaha zote, na uhalifu ungetoweka duniani kwa mara moja, bado uhai ungetishwa. “Umaskini wenye kulemea kabisa, ugonjwa wa kotekote, na ukosefu mwingi mno wa elimu ni wonyesho wa jinsi zilivyo maisha za mamia ya mamilioni katika nchi zinazositawi,” yasema Taasisi Worldwatch katika ripoti yao State of the World 1990. “Wanadamu wote—matajiri au maskini, walio imara au dhaifu kijeshi—wakabiliana na hofu ya kuharibiwa kwa mazingira kwa kadiri isiyopata kuonekana.”
Ndiyo, mifumo ile ile yenye kuendeleza uhai ambayo wanadamu wote huitegemea inabomolewa. “Dunia kwa ujumla imo katika hali mbaya zaidi [kuliko katika 1970],” aandika mhariri Paul Hoffman katika gazeti Discover. “Takataka zinafurika kutoka kwenye mashimo yetu ardhini. Gesi zenye joto kali mno zinaipasha joto halianga. Ule ukanda wa ozoni ulio kinga ya sayari unakuwa mwembamba. Majangwa yanatanuka, na misitu ya mvua inapungua. Jamii-jamii za mimea na wanyama zinamalizika kwa kadiri ya 17 kwa saa.”
Halafu ongezea zile athari za uchafuaji unaoendelea wa ardhi na maji. Jumlisha lile ongezeko thabiti la idadi ya watu ulimwenguni, lenye matokeo ya kujenga majengo au kuparuza njia katika sehemu zaidi na zaidi za ardhi ya mazao, na hivyo kuongezea kumalizika kwa jamii-jamii za wanyama na mimea. Fikiria ule uhaba unaoongezeka wa ugavi wa maji safi na tatizo la mvua ya asidi. Unganisha hayo na yale matokeo yenye kutisha afya ya hewa iliyochafuzwa sana na matatizo ya takataka zilizo hatari. Yakiwa pamoja, hayo yamaanisha msiba kwa jamii ya kibinadamu. Wowote tuwao na popote tuwapo, twahitaji hewa, chakula, maji, na mali ghafi ili tuendelee kuwako. Twazihitaji zikiwa bila kuchafuzwa na kwa kadiri ya kutosha. Tayari, “kwa walio maskini, miaka ya themanini ilikuwa msiba halisi, wakati wa vyakula haba na hesabu zenye kuongezeka za kifo,” yasema State of the World 1990.
Huku jamii ya kibinadamu ikiwa inatishwa kwa njia nyingi sana, je! mtu yeyote aweza kukanusha kwamba ulimwengu mpya wahitajiwa vibaya sana? Lakini je! huo ni uwezekano halisi? Ulimwengu wa jinsi hiyo ungekuja kutoka chanzo gani? Ni vipingamizi gani ambavyo ni lazima vishindwe kabla sayari yetu haijaweza kikweli kufikiriwa kuwa salama na yenye usitawi? Acheni tuone.
[Maelezo ya Chini]
a “Vita” hufafanuliwa kuwa pambano ambalo huhusisha angalau serikali moja na ambamo watu angalau 1,000 huuawa katika mwaka mmoja.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]
WHO photo by P. Almasy