Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w91 3/1 kur. 8-9
  • Azikwa Ijumaa—Ziara Tupu Jumapili

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Azikwa Ijumaa—Ziara Tupu Jumapili
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Habari Zinazolingana
  • Azikwa Ijumaa—Ziara Tupu Jumapili
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
  • Mwili wa Yesu Watayarishwa na Kuzikwa
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Je, Wakristo Wanapaswa Kushika Sabato?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Siku ya Mwisho ya Maisha ya Yesu ya Kibinadamu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
w91 3/1 kur. 8-9

Maisha na Huduma ya Yesu

Azikwa Ijumaa—Ziara Tupu Jumapili

SASA ni karibu mwisho wa alasiri ya Ijumaa, na Sabato ya Nisani 15 itaanza wakati jua linapotua. Maiti ya Yesu yanyong’onyea juu ya mti, lakini wale wezi wawili kando zake bado wako hai. Alasiri ya Ijumaa yaitwa Maandalio kwa sababu huu ndio wakati watu wanapotayarisha vyakula na kumaliza kazi nyingine yoyote inayopaswa kufanywa ambayo haiwezi kungoja ifanywe baada ya Sabato.

Sabato ambayo karibu itaanza si Sabato ya kawaida tu (siku ya saba ya juma) lakini ni Sabato maradufu, au “kubwa.” Inaitwa hivyo kwa sababu Nisani 15, ambayo ndiyo siku ya kwanza ya ile Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu ya siku saba (na sikuzote hiyo ni sabato bila kujali siku ya juma inapokuja), imekuja siku ile ile ya Sabato ya kawaida.

Kupatana na sheria ya Mungu, miili haipasi iachwe juu ya mti usiku mzima. Kwa hiyo Wayahudi wanaomba Pilato kwamba vifo vya hao wanaouawa viharakishwe kwa kuivunja miguu yao. Kwa hiyo, askari wanavunja miguu ya wale wezi wawili. Lakini kwa kuwa Yesu aonekana kuwa amekufa, miguu yake haivunjwi. Hilo linatimiza andiko hili: “Hapana mfupa wake utakaovunjwa.”

Hata hivyo, ili kuondoa shaka lolote kwamba kwa kweli Yesu amekufa, aska-ri mmoja adukua upande wake kwa mkuki. Mkuki huo unachoma eneo la moyo wake, na hapo kwa hapo damu na maji yanatoka. Mtume Yohana ambaye ni shahidi aliyeyaona, aripoti kwamba hilo latimiza andiko lingine: “Watamtazama yeye waliyemchoma.”

Yusufu kutoka jiji la Arimathea, ambaye ni mshirika wa Sanhedrini mwenye sifa njema, yupo pia penye uuaji huo. Yeye alikataa kupiga kura ya kupendelea kitendo kisicho cha haki dhidi ya Yesu cha mahakama kuu. Yusufu kwa kweli ni mwanafunzi wa Yesu, ingawa ameogopa kujitambulisha kuwa mmoja. Hata hivyo, sasa, yeye aonyesha moyo mkuu na aendea Pilato kumwomba mwili wa Yesu. Pilato amwita ofisa wa jeshi aliyewekewa jambo hilo, na baada ya ofisa huyo kuthibitisha kwamba Yesu amekufa, Pilato akabidhi maiti hiyo.

Yusufu autwaa mwili na kuufunga kwa nguo nzuri ya kitani kuutayarisha kwa ajili ya mazishi. Asaidiwa na Nikodemo, mshirika mwingine wa Sanhedrini. Nikodemo pia ameshindwa kuungama imani yake katika Yesu kwa sababu ahofu kupoteza cheo chake. Lakini sasa yeye aleta kunjo ambalo lina kilo 33 za manemane na uudi wa bei ghali. Mwili wa Yesu unafungwa kwa vitambaa ambavyo vina vikolezo hivyo, kama tu vile Wayahudi wana desturi ya kutayarisha miili kwa ajili ya mazishi.

Halafu mwili unalazwa katika ziara (kaburi) jipya la ukumbusho la Yusufu ambalo limechongwa katika mwamba kwenye bustani iliyo karibu. Mwishowe, jiwe kubwa lavingirishwa mbele ya ziara. Matayarisho ya mwili ni ya upesi ili kutimiza mazishi kabla ya Sabato. Kwa hiyo, Mariamu Magdalene na Mariamu mama wa Yakobo Mdogo, ambao labda wamekuwa wakisaidia na matayarisho, warudi nyumbani haraka ili watayarishe vikolezo na mafuta yenye manukato mengine. Baada ya Sabato, wao wanapanga kuutia mwili wa Yesu dawa zaidi ili kuuhifadhi kwa muda mrefu zaidi.

Siku ifuatayo, ambayo ni Jumamosi (Sabato), wakuu wa makuhani na Mafarisayo wanamwendea Pilato na kusema: “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza.”

“Mna askari,” Pilato ajibu. “Nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo.” Kwa hiyo wanaenda na kufanya kaburi liwe salama kwa kulitia lile jiwe muhuri na kuweka askari Waroma kuwa walinzi.

Mapema asubuhi ya Jumapili Mariamu Magdalene, Mariamu mama yake Yakobo, pamoja na Salome, Yoana, na wanawake wengine, wanaleta vikolezo kwenye kaburi ili wautie dawa mwili wa Yesu. Njiani wanaambiana hivi: “Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi?” Lakini wanapofika, wanakuta kwamba tetemeko la dunia limetokea na malaika wa Yehova amevingirisha mbali lile jiwe. Walinzi wameondoka, na kaburi liko tupu! Mathayo 27:57–28:2; Marko 15:42–16:4; Luka 23:50–24:3, 10; Yohana 19:31-20:1, 19:14; 12:42; Walawi 23:5-7; Kumbukumbu 21:22, 23; Zaburi 34:20; Zekaria 12:10.

◆ Kwa nini Ijumaa inaitwa Maandalio, na Sabato “kubwa” ni nini?

◆ Ni maandiko gani ambayo yanatimizwa kuhusiana na mwili wa Yesu?

◆ Yusufu na Nikodemo wanahusikaje na mazishi ya Yesu, na wana uhusiano gani na Yesu?

◆ Makuhani wanamwomba Pilato nini, naye anaitikiaje?

◆ Nini kinatokea mapema asubuhi ya Jumapili?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki