Je! Mungu Hujibu Sala Zako?
“MIMI sijahisi kamwe msisimuko wa kujibiwa sala zangu,” akasema mwanamke mmoja mwenye kuishi katika Hokkaido, Japani. Si yeye peke yake katika jambo hilo. Watu wengi huhisi kwamba sala zao hazijibiwi kamwe. Kwa kweli, huenda wewe ukawa washangaa kama Mungu hujibu sala zako.
Mamilioni ya watu huelekeza sala zisizohesabika kwa miungu isiyo na idadi. Kwa nini yaonekana kwamba sala nyingi sana hazijibiwi? Ili kugundua, acheni kwanza tuchunguze aina za sala zinazotolewa.
Watu Fulani Huomba Nini?
Wakati wa Mwaka Mpya, theluthi mbili za idadi ya Japani, au yapata watu milioni 80, husali katika sehemu maalumu za ibada ya Kishinto au mahekalu ya Kibuddha. Wao hutoa sarafu zikiwa matoleo na kuomba nasibu njema na usalama wa kifamilia.
Katika Januari na Februari—kabla tu ya mitihani mikali ya mchujo—wanafunzi humiminika kwenye sehemu maalumu za ibada kama ile iliyo katika Tokyo ambayo yajulikana kwa kuwa na mungu wayo wa elimu. Wao huandika tamaa zao juu ya vibao vya sala na kuviangika juu ya fito za mbao katika eneo linalozunguka sehemu hizo maalumu za ibada. Angalau 100,000 kati ya vibao hivi vilipamba mazingira ya sehemu maalumu ya ibada ijulikanayo sana katika Tokyo wakati wa mtihani wa 1990.
Sala nyingi zahusisha afya. Kwenye sehemu moja maalumu ya ibada katika Kawasaki, Japani, watu husali kuomba ulinzi dhidi ya UKIMWI. “Umaana wa kusali dhidi ya UKIMWI,” akaeleza kuhani wa sehemu maalumu hiyo ya ibada, “ni kwamba jambo hilo litafanya watu wawe na akili katika mwenendo wao.” Lakini je, hayo tu ndiyo yahusikayo kwenye sala?
Kwenye hekalu jingine, mwanamke mzee-mzee alisali kuomba “kifo cha ghafula.” Kwa nini? Kwa sababu alitaka kuepuka kuteswa na ugonjwa wa muda mrefu na hakutaka kuwa mzigo kwa familia yake.
Katika nchi moja iitwayo ya Kikristo eti, kapteni wa timu ya mpira alisali kuombea timu yake ushindi na ulinzi ili isipatwe na madhara. Wakatoliki katika Polandi husali kwa ajili ya hali njema yao ya kibinafsi na hupamba Madonna wao kwa vito vya thamani waaminipo kwamba sala zao husikiwa. Watu wengi humiminika kwenye makanisa kama lile maarufu la Guadalupe katika Jiji la Meksiko, na Lourdes, Ufaransa, wakiomba maponyo ya kimwujiza.
Iwe ni Mashariki au Magharibi, watu hutoa sala kwa sababu nyingi mbalimbali za kibinafsi. Kwa wazi, wao hutaka sala zao zisikiwe na kujibiwa. Hata hivyo, je! ni jambo la akili nzuri kutarajia kwamba sala zote zitasikiwa kwa upendelevu? Namna gani sala zako mwenyewe? Je! hizo hujibiwa? Kwa kweli, je! Mungu hujibu sala hata kidogo?