Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w91 11/15 kur. 19-23
  • “Ni Lazima Mwangalizi Awe . . . Mwenye Kujidhibiti”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Ni Lazima Mwangalizi Awe . . . Mwenye Kujidhibiti”
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kujidhibiti—Takwa kwa Wazee
  • Wanaposhughulika na Wengine
  • Kujidhibiti Katika Mikutano ya Wazee na Vikao vya Hukumu
  • Kujidhibiti na Mtu wa Jinsia Tofauti
  • Kujidhibiti Katika Hali Nyinginezo
  • Kusitawisha Tunda La Kujidhibiti
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Kujidhibiti —Kwa Nini Ni Kwa Maana Sana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Iweni Wenye Kujidhibiti Ili Mshinde Tuzo!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
  • Jazeni Kwenye Ujuzi Wenu Kujidhibiti
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
w91 11/15 kur. 19-23

“Ni Lazima Mwangalizi Awe . . . Mwenye Kujidhibiti”

“Ni lazima mwangalizi awe . . . mwenye kujidhibiti.”—TITO 1:7, 8, NW.

1, 2. William wa Orange aliandaa mfano gani wa kujizuia, na kukawa na matokeo gani yenye faida?

HISTORIA huandaa mfano wenye kufaa sana unaohusu kuzuia hisia za moyoni. Katikati ya karne ya 16, mwana-mfalme kijana Mholanzi William wa Orange alikuwa katika safari ya kuwinda wanyama pamoja na Mfalme Henry 2 wa Ufaransa. Mfalme alimfunulia William mpango ambao yeye na mfalme wa Hispania walikuwa nao wa kuwafutilia mbali Waprotestanti wote katika Ufaransa na katika Uholanzi—kwa kweli, katika Jumuiya ya Wakristo yote. Mfalme Henry alifikiria kwamba kijana William alikuwa ameshikilia Ukatoliki sana kama yeye mwenyewe na kwa hiyo akafumbua siri yote hata mambo yale madogo madogo ya njama hiyo. Lile ambalo William alisikia lilimhofisha sana kwa sababu wengi wa marafiki wake wa karibu walikuwa Waprotestanti, lakini hakuonyesha jinsi alivyohisi; bali, alionyesha upendezi mwingi katika habari yote ambayo mfalme alimpa.

2 Hata hivyo, William upesi kadiri awezavyo alianza mipango ya kuizuia hiyo njama, na hilo hatimaye likaongoza kwenye kufanya Uholanzi iwe huru na utawala wa Katoliki ya Kihispania. Kwa sababu William aliweza kuzoea kujidhibiti aliposikia njama hiyo kwa mara ya kwanza, alikuja kujulikana kuwa “William Mnyamavu.” William wa Orange alifanikiwa sana hivi kwamba tunaambiwa hivi: “Yeye ndiye aliyekuwa mwanzilishi wa kweli wa uhuru na ukuu wa jamhuri ya Uholanzi.”

3. Ni nani wanaofaidika wakati wazee Wakristo wanapozoea kujidhibiti?

3 Kwa sababu ya kujizuia kwake, William yule Mnyamavu alijifaidi mwenyewe na watu wake pia. Kwa njia yenye kulinganika na hiyo, tunda la roho takatifu la kujidhibiti lapasa kudhihirishwa leo na wazee au waangalizi Wakristo. (Wagalatia 5:22, 23) Kwa kuzoea sifa hiyo, wanajifaidi wenyewe na makundi pia. Kwa upande mwingine, kutozoea kwao kujidhibiti kwaweza kudhuru sana.

Kujidhibiti—Takwa kwa Wazee

4. Ni shauri gani la mtume Paulo linalokazia uhitaji wa wazee kuzoea kujidhibiti?

4 Paulo, yeye mwenyewe akiwa mzee, alithamini umaana wa kujidhibiti. Alipokuwa akiwashauri wazee waliokuwa wamekuja kwake kutoka Efeso, aliwaambia hivi: “Toeni uangalifu kwa ninyi wenyewe na kundi lote la kondoo.” Miongoni mwa mambo mengine, kutoa uangalifu kwa wao wenyewe kulitia ndani uhitaji wa kuzoea kujidhibiti, kuangalia mwenendo wao. Katika kumwandikia Timotheo, Paulo alionyesha wazi jambo sawa na hilo, akisema hivi: “Jitunze [toa uangalifu kwa, NW] nafsi yako, na mafundisho yako.” Shauri la jinsi hiyo lilionyesha kufahamu kwa Paulo kuhusu mwelekeo wa kibinadamu uliokuwa katika wengine wa kushugulikia kufundisha kuliko kuzoea yale wanayofundisha. Kwa hiyo, alikazia kwanza uhitaji wa kujiangalia wenyewe.—Matendo 20:28, NW; 1 Timotheo 4:16, UV.

5. Wazee Wakristo wanawekwaje rasmi, na sifa zao zimeandikwa wapi katika Maandiko?

5 Muda wote wa miaka iliyopita, daraka la wazee la Kimaandiko limekuwa wazi zaidi pole kwa pole. Leo, tunaona kwamba uzee ni cheo cha kuwekwa rasmi. Wazee wanawekwa rasmi na Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova au na wawakilishi walo wa moja kwa moja. Baraza hilo nalo, huwakilisha “mtumwa mwaminifu mwenye akili.” (Mathayo 24:45-47) Sifa za kuwa mwangalizi, au mzee Mkristo, zinatolewa hasa na mtume Paulo katika 1 Timotheo 3:1-7 na Tito 1:5-9.

6, 7. Ni sifa gani hasa za wazee zinazotaka kujidhibiti?

6 Paulo ataarifu katika 1 Timotheo 3:2, 3, NW, kwamba ni lazima mwangalizi awe mwenye kiasi katika mazoea. Hilo na uhitaji wa mzee kuwa mwenye utaratibu hutaka kuzoea kujidhibiti. Mwanamume anayestahili kuwa mwangalizi si mpigaji wala si mtaka vita. Sifa hizo pia hutaka kwamba mzee awe mwenye kujidhibiti. Isitoshe, ili mzee asiwe mpiga kelele ya ulevi, mwenye kujitoa mwenyewe kwa divai, ni lazima aonyeshe kujidhibiti.—Ona pia vielezi-chini kuhusu 1 Timotheo 3:2, 3.

7 Katika Tito 1:7, 8, NW, Paulo alitaarifu mahususi kwamba ni lazima mwangalizi awe mwenye kujidhibiti. Hata hivyo, angalia ni mengine mangapi ya matakwa yale mengine ambayo yameorodheshwa katika mistari hiyo yanahusisha kujidhibiti. Kwa mfano, mwangalizi apaswa awe bila shtaka, naam, bila lawama. Kwa hakika, mzee asingeweza kufikia matakwa hayo kama asingezoea kujidhibiti.

Wanaposhughulika na Wengine

8. Ni sifa gani zinazohitajiwa na wazee katika kutoa shauri ambazo zakazia uhitaji wa kujidhibiti?

8 Kisha pia, ni lazima mwangalizi awe mwenye saburi na mstahimilivu katika kushughulika na waamini wenzake, na hilo lataka kujidhibiti. Kwa mfano, katika Wagalatia 6:1, twasoma hivi: “Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho [“ambao mna sifa za kufaa kiroho,” NW, hasa wazee] mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.” Kudhihirisha roho ya upole kunataka kujidhibiti. Kwa hiyo, kujidhibiti kunahusika pia katika kujiangalia mwenyewe. Vilevile, mzee anapoombwa msaada na mtu aliye katika taabu, kujidhibiti ni kwa muhimu sana. Haidhuru lile ambalo mzee huenda akafikiri juu ya mtu huyo, ni lazima awe mwenye fadhili, mwenye saburi, na mwenye kuelewa hali. Badala ya kuwa mwepesi kutoa shauri, ni lazima mzee awe na nia ya kusikiliza na kuchota katika mtu huyo lile hasa lionekanalo kuwa linamsumbua.

9. Wazee wapaswa kukumbuka shauri lipi wanaposhughulika na ndugu walio na ukali wa kuvurugika mawazo?

9 Shauri hili katika Yakobo 1:19 lafaa hasa wakati mzee anaposhughulika na watu wenye ukali wa kuvurugika mawazo: “Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika.” Naam, hasa wakati anapokabili maitikio ya hasira au ya kihisiamoyo ni lazima mzee asiitikie kwa njia hiyo hiyo. Kujidhibiti kunahitajiwa ili kutojibu maneno yaliyowashwa hisiamoyo kwa maneno yaliyowashwa hisiamoyo, kutolipa “ovu kwa ovu.” (Warumi 12:17) Kuitikia kwa njia hiyo hiyo kunafanya mambo yawe mabaya zaidi tu. Kwa hiyo hapa tena Neno la Mungu linawapa wazee shauri zuri, likiwakumbusha kwamba “jawabu la upole hugeuza hasira.”—Mithali 15:1.

Kujidhibiti Katika Mikutano ya Wazee na Vikao vya Hukumu

10, 11. Ni jambo gani limetokea katika mikutano ya wazee, likionyesha uhitaji wa kujidhibiti katika pindi za jinsi hiyo?

10 Eneo jingine ambamo waangalizi Wakristo wanahitaji kuwa waangalifu kuzoea kujidhibiti ni wakati wa mikutano ya wazee. Nyakati nyingine kuongea kwa utulivu kwa ajili ya masilahi ya kweli na ya haki kunahitaji kujidhibiti kwingi nyakati nyingine. Kujidhibiti kunatakiwa pia ili kuepuka kujaribu kuongoza mazungumzo. Mzee akiwa ana asili ya kuzoea kufanya hivyo, ingekuwa fadhili kwa mzee mwingine kumpa mzee huyo shauri.—Linganisha 3 Yohana 9.

11 Tena pia, katika mikutano ya wazee, mzee mwenye kutaka jambo fulani kupita kiasi huenda akavutwa kuwa mwepesi wa kuonyesha hisia zake za moyoni, hata kuinua sauti yake. Vitendo hivyo huonyesha wazi kama nini ukosefu wa kujidhibiti! Kwa kweli vitendo hivyo vinazuia kutimiza kusudi lake kwa njia mbili. Kwa upande mmoja, kwa kadiri mtu akosavyo kujidhibiti, ni kwa kadiri hiyo hiyo atakavyodhoofisha kisa chake kwa kuacha hisia za moyoni zifunike usababu wa kiakili. Kwa upande mwingine, kwa kadiri mtu anavyokuwa mwepesi wa kuonyesha hisia zake za moyoni, ndivyo aelekeavyo kuwaudhi au hata kuleta uhasama kwa wazee wenzake. Isitoshe, wazee wasipokuwa waangalifu, tofauti kubwa za maoni huenda zikasababisha migawanyiko kati yao. Hilo latokeza madhara kwao wenyewe na kwa kundi pia.—Linganisha Matendo 15:36-40.

12. Ni lazima wazee wawe waangalifu kuzoea kujidhibiti katika kushughulika na hali zipi?

12 Kujidhibiti kunahitajiwa sana pia kwa wazee ili waepuke kuwa wenye upendeleo au kutumia vibaya uwezo wao. Ni rahisi sana kujiachilia kwa kishawishi, kuacha maoni ya kibinadamu yasiyo makamilifu yaongoze lile mtu asemalo au afanyalo! Mara nyingi, wazee wamekosa kutenda kwa uamuzi thabiti wakati mmoja wa watoto wao au mtu mwingine wa ukoo amepatikana kuwa na hatia ya mwenendo mbaya. Katika hali hizo kujidhibiti kunatakiwa ili kutoacha vifungo vya familia vizuie kutenda kwa haki.—Kumbukumbu la Torati 10:17.

13. Kwa nini kujidhibiti kunahitajiwa na wazee hasa katika vikao vya hukumu?

13 Hali nyingine ambayo katika hiyo kujidhibiti ni kwa maana sana ni wakati kuna kikao cha hukumu. Ni lazima wazee wazoee kujidhibiti kwingi ili wasivutwe isivyofaa na hisia za moyoni. Machozi yasifanye wayumbeyumbe kwa urahisi mno. Wakati huo huo, ni lazima mzee awe mwangalifu asipoteze utulivu wake wakati yeye anaporushiwa mashtaka na masingizio, kama vile inavyowezekana katika kushughulika na waasi-imani. Maneno ya Paulo yanafaa sana hapa: “Haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote.” Kujidhibiti kunatakiwa ili kuzoea uanana chini ya mbano. Paulo aendelea kuonyesha kwamba “mtumwa wa Bwana” apaswa awe “mvumilivu [mwenye kuendelea kujizuia, NW]; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye.” Kudhihirisha upole na kuendelea kujizuia wakati mtu anaposhughulika na upinzani kunahitaji kujidhibiti kwingi.—2 Timotheo 2:24, 25.

Kujidhibiti na Mtu wa Jinsia Tofauti

14. Wazee wapaswa kutii shauri gani zuri katika kushughulika kwao na wale wa jinsia tofauti?

14 Ni lazima wazee wawe chonjo sana kuzoea kujidhibiti wanaposhughulika na wale wa jinsia tofauti. Si jambo lenye kupendekezwa mzee kufanya ziara ya uchungaji kwa dada akiwa peke yake. Mzee apaswa aandamane na mzee mwingine au na mtumishi wa huduma. Yaelekea kwa kufahamu tatizo hilo, Paulo alimshauri mzee Timotheo hivi: “Watendee . . . wanawake wazee kama mama yako, na wasichana kama dada zako, kwa usafi wote.” (1 Timotheo 5:1, 2, HNWW) Wazee wengine wameonwa wakimwekelea dada mikono yao kana kwamba kuonyesha upendo wa kibaba. Lakini huenda ikawa wanajidanganya wenyewe, kwa kuwa wonyesho huo waweza sana kuwa ukichochewa na msukumo wa kimahaba badala ya shauku safi ya udugu wa Kikristo.—Linganisha 1 Wakorintho 7:1.

15. Tukio fulani linakaziaje suto liwezalo kuletwa juu ya jina la Yehova wakati mzee anapokosa kuzoea kujidhibiti?

15 Kweli imetendewa madhara makubwa kama nini kwa sababu wazee fulani walikosa kuzoea kujidhibiti katika kushughulika kwao na akina dada kundini! Miaka michache iliyopita, mzee mmoja alitengwa na ushirika kwa sababu alikuwa amefanya uzinzi na dada Mkristo ambaye mumewe hakuwa Shahidi. Usiku ule ule wa kutangaza kutengwa na ushirika kwa yule aliyekuwa mzee, mume mwenye kuudhika sana wa dada huyo aliingia kwa mshindo katika Jumba la Ufalme akiwa na bunduki na kuwapiga risasi wale watu wawili wenye hatia. Hakuna yeyote kati yao aliyeuawa, naye alinyang’anywa bunduki mara moja, lakini keshoye gazeti kuu lilionyesha kwenye ukurasa walo wa kwanza habari kuhusu ‘mfyatuo wa risasi kanisani.’ Ukosefu wa kujidhibiti wa mzee huyo uliletea kundi na jina la Yehova suto kama nini!

Kujidhibiti Katika Hali Nyinginezo

16. Kwa nini ni lazima wazee wawe waangalifu kuzoea kujidhibiti wanapotoa hotuba za watu wote?

16 Kujidhibiti kunahitajiwa sana pia wakati mzee anapotoa hotuba ya watu wote. Msemaji wa hotuba za watu wote apaswa kuwa mfano wa kuwa na uhakika na utulivu. Wengine hujaribu kuwachekesha wasikilizaji wao kwa maneno mengi yenye ucheshi yanayosemwa kwa kusudi tu la kupata vicheko. Hilo huenda likaonyesha kujiachilia kwa kishawishi cha kuwapendeza wasikilizaji wao. Bila shaka, kujiachilia kote kwenye kishawishi ni kukosa kujidhibiti. Hata huenda ikasemwa kwamba kupita wakati katika kutoa hotuba huonyesha ukosefu wa kujidhibiti, pamoja na kutojitayarisha vya kutosha.

17, 18. Kujidhibiti kuna sehemu gani katika kusawazisha kwa mzee madaraka yake mbalimbali?

17 Ni lazima kila mzee mwenye kufanya kazi kwa bidii akabili mwito wa ushindani wa kusawazisha madai mbalimbali kwa wakati na nishati zake. Kujidhibiti kunatakiwa ili asipite kiasi kwa jambo lolote. Wazee wengine wamehangaikia sana mahitaji ya kundi hivi kwamba wameacha familia zao. Hivyo, wakati dada mmoja alipomwambia mke wa mzee mmoja kuhusu ziara ya uchungaji nzuri ambayo mume wake alikuwa amemfanyia, mke wa mzee huyo alisema kwa mshangao: “Laiti angenifanyia mimi ziara ya uchungaji wakati fulani!”—1 Timotheo 3:2, 4, 5.

18 Mzee ahitaji kujidhibiti pia ili kusawazisha wakati anaotumia katika funzo la kibinafsi na ule anaotumia katika huduma ya shambani au katika ziara za uchungaji. Kwa sababu ya udanganyifu wa moyo wa kibinadamu, ni rahisi sana kwa mzee kutumia wakati zaidi ya ule apaswao kutumia kwa jambo ambalo humpendeza zaidi. Ikiwa anapenda vitabu, huenda sana ikawa anatumia wakati mwingi katika funzo la kibinafsi kuliko ule apaswao kutumia. Ikiwa anaona huduma ya nyumba kwa nyumba kuwa ngumu kidogo, huenda akapata udhuru mbalimbali wa kuiacha kwa ajili ya masilahi ya kufanya ziara za uchungaji.

19. Wazee wana wajibu gani unaokazia uhitaji wa kujidhibiti?

19 Wajibu wa kudumisha usiri huhitaji pia kwamba mzee awe chonjo kuzoea kujidhibiti kwa uthabiti. Linalofaa hapa ni shauri hili: “Usifunue siri ya mtu mwingine.” (Mithali 25:9) Yaliyoonwa hudokeza kwamba hilo huenda likawa moja la matakwa yenye kuvunjwa mara nyingi sana miongoni mwa wazee. Ikiwa mzee ana mke mwenye hekima na upendo ambaye ana uwasiliano mzuri pamoja naye, huenda kukawa na mwelekeo kwa upande wake wa kuzungumza au kutaja tu mambo ya kisiri. Lakini hilo si jambo la kufaa wala la hekima. Kwanza, linaondoa kutumainiwa. Ndugu na dada za kiroho huwajia wazee na kuwatumainisha siri kwa sababu wana uhakika kwamba jambo hilo litawekwa siri kabisa. Kumtolea mke mambo ya kisiri ni kosa, ni jambo lisilo la hekima, na lisilo la upendo pia kwa sababu linamwekelea mzigo isivyohitajiwa.—Mithali 10:19; 11:13.

20. Kwa nini kuzoea kujidhibiti ni kwa maana sana kwa wazee?

20 Bila shaka, kujidhibiti ni kwa maana kama nini, na hasa kwa wazee! Kwa sababu ya kukabidhiwa kwao pendeleo la kuongoza miongoni mwa watu wa Yehova, wao wana wajibu zaidi. Kwa kuwa wamepewa mengi, mengi yatatakiwa kwao. (Luka 12:48; 16:10; linganisha Yakobo 3:1.) Ni pendeleo na wajibu wa wazee kuwawekea wengine mfano mzuri. Zaidi ya hayo, wazee wenye kuwekwa rasmi wanaweza kufanya mema zaidi au kusababisha madhara zaidi ya wengine, ikitegemea mara nyingi kama wanazoea kujidhibiti au sivyo. Haishangazi kwamba Paulo alisema: “Ni lazima mwangalizi awe . . . mwenye kujidhibiti.”

Je! Unakumbuka?

◻ Ni matakwa gani ya Kimaandiko kwa wazee yanayoonyesha kwamba ni lazima wazoee kujidhibiti?

◻ Kwa nini kujidhibiti kunahitajiwa na wazee wanaposhughulika na waamini wenzao?

◻ Kujidhibiti kwapasa kuzoewaje kwenye mikutano ya wazee?

◻ Ni mwito gani wa ushindani unaotolewa na uhitaji wa wazee kudumisha usiri?

[Picha katika ukurasa wa 20]

Kuonyesha kujidhibiti ni kwa muhimu kwenye mikutano ya wazee

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ni lazima wazee Wakristo wazoee kujidhibiti na kudumisha usiri

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki