Hazina Kutoka kwa Marundo ya Takataka ya Misri
JE! UNGETAZAMIA kupata hati-mikono za Biblia zenye thamani katika marundo ya takataka? Miongoni mwa michanga ya Misri, mwishoni mwa karne iliyopita, hilo ndilo hasa lililotukia. Jinsi gani?
Kuanzia katika 1778 na kuendelea hadi mwisho wa karne 19, maandishiasilia kadhaa ya funjo yalivumbuliwa Misri bila kutazamiwa. Hata hivyo, kulikuwako utafutaji-tafutaji mdogo sana uliopangwa hadi miaka mia moja iliyopita. Kufikia wakati huo mfululizo wa kawaida wa hati za kale ulikuwa ukipatikana na wakulima wa mahali hapo, na Shirika la Hazina ya Misri ya Uvumbuzi Linalodhaminiwa na Uingereza lilitambua uhitaji wa kutuma kikundi cha wavumbuzi kabla haijawa kuchelewa mno. Walichagua wanachuo wawili wa Oxford, Bernard P. Grenfell, na Arthur S. Hunt, waliopokea ruhusa kutafuta-tafuta eneo la kusini la mkoa wa ukulima wilaya ya Faiyūm (iliyoonyeshwa juu).
Mahali paitwapo Behnesa palisikika kuwa pa kutumainiwa kwa Grenfell kwa sababu ya jina lapo la Kigiriki cha kale Oxyrhynchus (Oksirinkus). Pakiwa kitovu cha Ukristo wa Kimisri, Oksirinkus palikuwa mahali pa maana wakati wa karne za nne na tano W.K. Nyumba nyingi za mapema za watawa-waume zilikuwa zimepatikana karibu na hapo, na magofu ya mji huo mdogo yalienea sana. Grenfell alitumaini kupata vijipande vya vichapo vya Kikristo huko, lakini utafutaji-tafutaji makaburini na katika nyumba zilizoharibika haukutokeza chochote. Ni marundo ya takataka ya mji huo ndiyo iliyobaki tu, mengine yakisimama kwa urefu wa meta 9. Kuchimba huko ili kupata mafunjo kulionekana sana kuwa kukubali kushindwa; hata hivyo wavumbuzi hao waliamua kujaribu.
Hazina Iliyozikwa
Katika Januari 1897 handaki ya kujaribia ilichimbwa, na katika saa chache vifaa vya funjo vya kale vikapatikana. Vilitia ndani barua, maafikiano, na hati rasmi. Mchanga uliopeperushwa na upepo ulikuwa umevifunika, na hali ya hewa kavu ilikuwa imevihifadhi kwa miaka karibu 2,000.
Katika miezi inayozidi mitatu kidogo tu, karibu tani mbili za mafunjo zilipatikana kutoka Oksirinkus. Masanduku makubwa 25 yalijazwa na kupelekwa kwa meli hadi Uingereza. Na kila kipupwe kwa karibu miaka kumi, wanachuo hao wawili wenye ujasiri walirudi Misri kuongezea mkusanyo wao.
Katika pindi moja, walipokuwa wakichimba kaburi katika Tebtunis, hawakufukua chochote ila maiti za mamba zilizohifadhiwa. Mfanyakazi mmoja kwa kufadhaishwa alivunja moja vipande vipande. Kwa mshangao wake, alipata kwamba ilikuwa imefungiliwa katika kurasa za funjo. Mamba wengine, ambao watu hao walivumbua, walikuwa wamefungiliwa vivyo hivyo, na wengine walikuwa na makunjo ya funjo yaliyoingizwa kooni mwao. Vijipande vya maandiko bora ya kale yalivumbuliwa, pamoja na amri na maafikiano ya kifalme yaliyochanganyikana na hesabu za biashara na barua za kibinafsi.
Hati hizo zote zilikuwa na thamani gani? Zilithibitika kuwa zenye kupendeza sana, kwani nyingi zazo zilikuwa zimeandikwa na watu wa kawaida katika lugha ya Koine, Kigiriki cha kawaida cha siku hiyo. Kwa kuwa maneno mengi waliyotumia hupatikana katika Maandiko ya Kigiriki ya Biblia, “Agano Jipya,” kwa ghafula ikawa wazi kwamba lugha iliyo katika Maandiko haikuwa Kigiriki cha kipekee cha Biblia, kama wanachuo fulani walivyokuwa wamedokeza, bali ilikuwa lugha ya kawaida ya watu wa kawaida. Kwa hiyo kwa kulinganisha jinsi maneno yalivyotumiwa katika hali za kila siku, uelewevu wa wazi zaidi juu ya maana yao katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo ulitokea.
Hati-Mikono za Biblia
Vijipande vya hati-mikono za Biblia vilivumbuliwa, na hivyo, ambavyo mara nyingi viliandikwa katika maandishi ovyoovyo bila kurembeshwa na kwenye vifaa visivyo vya hali ya juu, viliwakilisha Biblia ya watu wa kawaida. Acheni tuchunguze baadhi ya mavumbuo hayo.
Hunt alivumbua nakala ya sura ya kwanza ya Gospeli ya Mathayo, mistari 1 hadi 9, 12, na 14 hadi 20, iliyoandikwa katika karne ya tatu W.K. kwa herufi kubwa. Ingekuja kuwa P1, kitu cha kwanza katika orodha ya maandishiasilia ya funjo kutoka mahali mbalimbali, zinazofikia sasa hati-mikono au sehemu za hati-mikono za Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo karibu mia moja. Mistari hiyo michache iliyopatikana na Hunt ilikuwa na faida gani? Namna ya kuandika ilionyesha wazi kwamba ilikuwa ya tarehe kutoka karne ya tatu W.K., na uchunguzi wa usomaji wayo ulionyesha kwamba iliafikiana na maandishiasilia ya wakati huo yaliyotokezwa na Westcott na Hort. P1 sasa imo katika Jumba la Ukumbusho la Chuo Kikuu katika Philadelphia, Pennsylvania, U.S.A.
Ukurasa wa funjo kutoka kodeksi moja, au kitabu kimoja, una sehemu za Yohona sura 1 kwenye upande wao wa kushoto na sehemu za Yohana sura 20 kwenye upande wao wa kulia. Kutokeza upya sehemu zilizokosekana hudokeza kwamba mwanzoni kulikuwako kurasa 25 kwa Gospeli hiyo yote, na tangu wakati wa mapema zaidi, ni lazima hizo zilitia ndani sura 21. Ilipewa nambari P5, kutiwa tarehe kutoka karne ya tatu W.K., na sasa imo katika Maktaba ya Uingereza katika London, Uingereza.
Kijipande chenye Warumi 1:1-7 kiliandikwa katika herufi kubwa sana ya ovyoovyo hivi kwamba wanachuo wamefikiri kwamba kilikuwa mazoezi ya mvulana wa shule. Sasa kimepewa nambari P10 na kutiwa tarehe kutoka karne ya nne W.K.
Mapato mengi zaidi yana karibu theluthi moja ya barua kwa Waebrania. Ilinakiliwa nyuma ya kunjo yenye maandiko bora ya mwanahistoria Mroma Livy kwenye upande wa mbele. Kwa nini upande wa mbele uwe na mambo tofauti sana jinsi hiyo na upande wa nyuma? Katika siku hizo uhaba na bei ya vifaa vya kuandikia ulimaanisha kwamba mafunjo ya zamani yasingeweza kutumiwa vibaya. Ikiwa imeorodheshwa sasa kuwa P13, imetiwa tarehe kutoka karne ya tatu au ya nne W.K.
Ukurasa wa funjo wenye sehemu za Warumi sura 8 na 9, wenye kuandikwa katika herufi ndogo, ulitoka kwa kitabu kilicho kuwa na urefu wa karibu sentimeta 11.5 na upana wa sentimeta 5 tu. Basi, ingeonekana kwamba chapa za ukubwa wa kuchukulia mfukoni za Maandiko zilipatikana katika karne ya tatu W.K. Huo ukawa P27 na huafikiana kwa ujumla na kodeksi ya Vatikanasi.
Sehemu za kurasa nne kutoka kodeksi ya Septuagint ya Kigiriki zina sehemu za sura sita za Mwanzo. Kodeksi hiyo ni ya maana sana kwa sababu ya kutiwa kwayo tarehe kutoka karne ya pili au ya tatu W.K. na kwa sababu sura hizo hazipatikani katika Kodeksi ya Vatikanasi na zinahitilafu fulani katika Kodeksi ya Sinaitikasi. Zikiwa zimepewa nambari Kunjo 656, kurasa hizo sasa zimo katika Maktaba ya Bodleian, Oxford, Uingereza.
Vijipande hivyo vyote havionyeshi tofauti zozote kubwa kutokana na hati-mikono zetu za mapema zilizoko, kwa hiyo vinahakikisha kwamba maandishiasilia ya Biblia yalipatikana katika wakati huo wa mapema miongoni mwa watu wa kawaida katika sehemu hiyo ya mbali ya Misri. Vinahakikisha pia imani yetu katika kutegemeka na usahihi wa Neno la Mungu.
[Picha katika ukurasa wa 27]
Mafunjo kutoka Faiyūm yenye sehemu za Yohana, sura 1
[Hisani]
Kwa idhini ya British Library
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.