Baada ya Buchenwald Nilipata Kweli
NILILELEWA Grenoble, Ufaransa, katika miaka ya 1930. Mwalimu wangu wa lugha ya Kijerumani, aliyekuwa mwanamume Mfaransa, alikuwa Mnazi mshupavu. Sikuzote angesisitiza shuleni kwamba lugha ya Kijerumani “ingekuwa ya faida” siku moja. Hata hivyo, walio wengi wa walimu wetu, waliokuwa wanajeshi wa Vita ya Ulimwengu 1, walihangaika juu ya ukuzi wa Unazi katika Ujerumani. Mimi pia nilihisi hangaiko kwani ilizidi kuwa wazi kwamba vita ilikuwa ikikaribia.
Katika 1940, wakati wa mwanzo wa Vita ya Ulimwengu 2, mjomba wangu mpendwa alikufa katika mapigano mazito kwenye mto Somme. Nilihisi uchungu mwingi sana lakini nilikuwa mchanga mno kujiandikisha katika Jeshi la Ufaransa. Lakini, miaka mitatu baadaye, wakati Wajerumani walipoanza kuongoza Ufaransa kijeshi, nilipewa nafasi ya kutumia ujuzi wangu wa kuchora ramani kwa ajili ya Shirika la Upinzani la Ufaransa. Nilikuwa bingwa wa kunakili sahihi na pia nilifanya kazi ya kuigiza stampu za ubani za Kijerumani. Nilipata uradhi mwingi kutokana na kupiga vita katika njia hiyo dhidi ya majeshi ya adui yaliyoongoza hivi kwamba mawazo ya Kikomunisti ya washirika wangu hayakuwa na maana sana kwangu wakati huo.
Kukamatwa
Novemba 11, 1943, Upinzani wa kwetu ulitoa mwito wa kufanya mwandamano ili kuadhimisha yale mapatano ya kuacha Vita ya Ulimwengu 1. Lakini askari Wafaransa wenye magari walikuwa wamezuia njia ya kwenda kwenye daraja lenye kuelekea kwenye ziara ya ukumbusho ya vita, nao wakatutia moyo turudi nyumbani. Mwandamano wetu uliamua badala yake kuendelea kutembea hadi nguzo nyingine ya ukumbusho mjini. Lakini tulisahau jambo moja. Nguzo hiyo ya ukumbusho ilikuwa mwendo mfupi tu kutoka kwa maofisi ya Gestapo (shirika la Kijerumani la polisi wa siri).
Kikundi chetu kilizungukwa upesi na askari-jeshi wenye silaha, waliotupangisha mstari kwenye ukuta. Askari-jeshi hao walipotusongesha, walipata bastola nyingi chini. Kwa kuwa hakuna yeyote aliyetaka kuungama kuwa ni zake, askari-jeshi hao waliachilia wanawake na vijana wenye umri wa miaka 16 na chini. Hivyo, nikiwa na umri wa miaka 18, nilifungwa gerezani, pamoja na wafungwa wengine 450. Siku chache baadaye, tulisafirishwa hadi kambi ya muda karibu na Compiègne, kaskazini mwa Ufaransa.
Njiani Kuelekea Ujerumani
Januari 17, 1944, nilikutana kwa mara ya kwanza—na kwa kusikitisha si ya mwisho—na askari-jeshi Wajerumani ambao kofia zao za chuma zilikuwa zimepambwa kwa ishara ya swastika (msalaba) kwa upande wa kushoto na kwa herufi SS (Schutzstaffel) kwa upande wa kulia. Walikusanya mamia ya wafungwa, na tulitakiwa tutembee hadi stesheni ya Compiègne. Tulipigwa mateke kihalisi ili kuingia katika mabehewa ya gari la moshi. Katika behewa langu pekee, kulikuwamo wafungwa 125. Kwa siku tatu na masiku mbili, hatukuwa na chochote cha kula wala kunywa. Katika muda wa saa chache, waliokuwa wadhaifu zaidi walikuwa tayari wamezirai na wakakanyagwa kwa miguu. Siku mbili baadaye tuliwasili Buchenwald, karibu na Weimar, ndani sana mwa Ujerumani.
Baada ya kupakwa dawa ya kuua vijidudu na kunyolewa nywele kichwani, nilipewa nambari ya usajili 41,101 na kuwekwa katika kikundi cha “Mharamia Mkomunisti.” Katika kipindi cha kutengwa, nilikutana na padre wa Kidominikani Michel Rike, ambaye angekuwa mashuhuri baada ya vita kwa ajili ya mahubiri yake katika Kathedro ya Notre Dame, Paris. Pamoja na vijana wengine wa umri wangu, nilimwuliza ni kwa nini Mungu aliruhusu mambo yenye kuhofisha kama hayo. Alijibu hivi: “Ni lazima upitie kuteseka kwingi ili ustahili kwenda mbinguni.”
Maisha ya Kila Siku
Wakazi wa majumba yale yote 61 walipaswa waamke saa kumi na nusu hivi za asubuhi. Tulitoka nje tukiwa tumevuwa nguo hadi viuno na mara nyingi tulilazimika tuvunje barafu iliyokuwako kwa sababu ya baridi, kabla ya kuoga. Kila mtu alipaswa atii, awe mwenye afya njema au mbaya. Halafu kukaja ugawanyaji mkate—gramu 200-300 kila siku ya mkate usio na ladha, wenye kiasi kidogo sana cha majarini na kitu fulani kilichofanana kidogo na jamu. Saa 11:30 za asubuhi, kila mtu alikusanywa ili kuitwa majina. Lilikuwa ono baya kama nini kubeba mgongoni petu wale waliokuwa wamekufa usiku! Ile harufu kali ya moshi wakati maiti hizo zilipokuwa zikichomwa ilitukumbusha juu ya wenzetu. Tulijawa na hisia za machukio, kukata tamaa, na kuudhika, kwani tulijua kwamba tungeweza kwa urahisi kuwa na mwisho uo huo.
Kazi yangu kwenye BAU 2 Kommando (kikundi cha ujenzi) ilitia ndani kuchimba mahandaki bila kusudi lolote. Muda tu baada ya handaki lenye kina cha meta mbili kuchimbwa tulipaswa kulijaza tena kwa uangalifu uo huo. Kazi ilianza saa 12:00 za asubuhi, kukiwa na kipindi cha kupumzika cha nusu saa wakati wa adhuhuri, ambapo baada yacho tuliendelea kufanya kazi hadi saa 1:00 za jioni. Kipindi cha kuitwa majina cha jioni kilionekana kuwa bila mwisho. Wakati ambao Wajerumani wengi waliuawa kwenye uwanja wa vita karibu na Urusi, kipindi hicho kingeweza kuendelea hadi usiku wa manane.
Kikundi Tofauti
Wowote waliojaribu kuponyoka kutoka kwa kambi wangeweza kutambuliwa kwa urahisi kwa sababu sisi sote tulikuwa na mtindo wa nywele usiokuwa laini. Nywele zetu zilikatwa zikiwa na mstari ulionyolewa au kukatwa kifupi sana katikati ya kichwa au kwa pande za kichwa. Lakini wafungwa wengine, walikuwa na nywele zilizokatwa kikawaida tu. Wao walikuwa akina nani? Kiongozi wa jumba letu alitosheleza udadisi wetu. “Wao ni Bibelforscher (Wanafunzi wa Biblia),” akasema. “Lakini Wanafunzi wa Biblia wanafanya nini katika kambi ya mateso?” nikashangaa. “Wamo humu kwa sababu wao humwabudu Yehova,” nikaarifiwa. Yehova! Hiyo ilikuwa ndiyo mara ya kwanza niliyopata kulisikia jina la Mungu.
Hatimaye nilipata kujua kidogo zaidi juu ya Wanafunzi wa Biblia. Wengi wao walikuwa Wajerumani. Baadhi yao walikuwa wamekuwa katika kambi za mateso tangu katikati ya miaka ya 1930 kwa sababu ya kukataa kumtii Hitla. Wangaliweza kwenda huru, lakini walikataa kuridhiana. Askari wa upelelezi wa SS waliwatumia kuwa vinyozi wao wa kibinafsi, nao walipewa kazi za pekee zilizohitaji wafanyakazi wenye kuaminika, kama vile kazi katika vyeo vya usimamizi. Lile lililotuvutia zaidi lilikuwa ule utulivu wao, kukosa kwao chuki yoyote au roho ya kuteta na kutaka kulipa kisasi. Sikuweza kuelewa jambo hilo. Kwa kusikitisha, sikujua Kijerumani cha kutosha kuweza kuzungumza nao wakati huo.
Gari la Moshi la Kifo
Majeshi ya muungano yaliposonga mbele, wafungwa walipelekwa kwenye kambi zilizokuwa katika sehemu za ndani zaidi za nchi, lakini kambi hizo zilianza kuwa na watu wengi mno. Asubuhi ya Aprili 6, 1945, askari wa upelelezi wa SS walitupeleka sisi watu 5,000, na kutupeleka kwa nguvu hadi kwenye barabara kuelekea Weimar ili tutembee kilometa 9. Wale wasioweza kwenda sambamba na mwendo huo walipigwa risasi shingoni kikatili. Tulipofika Stesheni ya Weimar hatimaye, tulipanda mabehewa yaliyokuwa wazi, na gari la moshi likaondoka. Kwa muda wa siku 20 lilisonga mbele kutoka stesheni moja hadi nyingine kutoka upande mmoja na mwingine wa Ujerumani na kisha kuendelea hadi Chekoslovakia.
Asubuhi moja, sehemu moja ya gari la moshi letu lilienda kando kwenye njia ya upande. Askari-jeshi waliweka bombomu (bunduki zinazopiga risasi kwa mfululizo) tayari kuyafyatua, wakafungua milango ya behewa moja, na kuwaua Warusi wote waliokuwa ndani. Kwa sababu gani? Wafungwa 12 walikuwa wamewaua walinzi wao na kuponyoka usiku. Hata leo naweza kuona akilini damu ikitiririka kupitia sakafu ya behewa hilo hadi kwenye njia ya gari la moshi.
Hatimaye, gari la moshi liliwasili Dachau, ambako siku mbili baadaye tuliwekwa huru na Jeshi la Amerika. Muda wote wa safari hiyo ya siku 20, chakula tulichokuwa nacho tu kilikuwa viazi vibichi vichache na maji. Tulikuwa watu 5,000 tulipoanza safari hiyo, lakini ni 800 tu waliookoka. Wengine wengi walikufa siku kadhaa baadaye. Nami, kwa sehemu kubwa ya safari hiyo nilikuwa nimeketia maiti.
Hatua Mpya
Baada ya kuwekwa kwangu huru jambo la kiasili zaidi kufanya lilikuwa ni kuunga mkono kwa bidii Chama cha Kikomunisti cha Ufaransa, kwa kuwa nilikuwa nimeshiriki kwa ukaribu pamoja na washiriki wacho—kutia na wale mashuhuri—katika Buchenwald. Nilikuwa katibu msaidizi wa sehemu ya msingi ya shirika la Kikomunisti katika Grenoble nami nikatiwa moyo nipitie mtaala wa mazoezi ya maafisa wakuu katika Paris.
Hata hivyo, nilikuja kutamauka upesi. Novemba 11, 1945, tulialikwa kushiriki katika mwandamano huko Paris. Camarade (sahibu) aliyekuwa akiongoza kikundi chetu alipokea kiasi fulani cha pesa ili tupate mahali pa kulala lakini hakuonekana kuwa na nia ya kuzitumia kwa ajili yetu. Tulilazimika kumkumbusha juu ya kanuni za unyoofu na urafiki zilizopasa kutuunganisha. Nikapata kutambua pia kwamba wale wanaume wengi mashuhuri niliopata kuwajua hawakuwa na utatuzi wa matatizo ya ulimwengu hata kidogo. Isitoshe, wengi wao walikuwa wasioamini kuwako kwa Mungu, nami nilikuwa na imani katika Mungu.
Baadaye nilihamia Lyons, ambako niliendelea kufanya kazi ya uchoraji ramani. Katika 1954, nilitembelewa na Mashahidi wa Yehova wawili, nami nikaandikisha gazeti Amkeni!. Siku mbili baadaye, mwanamume mmoja akaja kunizuru pamoja na mmoja wa wale wanawake waliokuwa wamebisha mlangoni pangu. Mke wangu na mimi tukatambua kwa ghafula kwamba sote wawili tulipendezwa na mambo ya kiroho.
Katika mazungumzo yaliyofuata, nilikumbuka wale Bibelforscher katika Buchenwald waliokuwa waaminifu sana kwa imani yao. Ni wakati huo tu ndipo nilitambua kwamba hao Bibelforscher na Mashahidi wa Yehova walikuwa watu wale wale. Kwa sababu ya funzo la Biblia, mke wangu na mimi tulichukua msimamo wetu kwa ajili ya Yehova na kubatizwa katika Aprili 1955.
Kumbukumbu langu halijafifia ni kana kwamba hayo yote yalitukia jana tu. Sijuti juu ya yale mambo niliyoteseka. Yameniimarisha na kunisaidia kuona kwamba serikali za ulimwengu huu hazina mengi ya kutoa. Ingawa mambo tunayoona kibinafsi yaweza kusaidia wengine kwa kadiri fulani tu, ningefurahi ikiwa yangu yangeweza tu kusaidia watu wachanga leo waone unafiki wa ulimwengu huu na kwa hiyo watafute thamani njema, za unyofu katika Ukristo wa kweli, kama ulivyofundishwa na Yesu.
Leo, kuteseka na ukosefu wa haki ni sehemu ya maisha ya kila siku. Kama wale Bibelforscher katika kambi za mateso, mimi pia hutazamia ule ulimwengu bora zaidi utakaokuja, ambako upendo wa kidugu na haki zitaenea badala ya jeuri na kutaka ukamili kwa ushupavu. Kwa sasa, ninajaribu kutumikia Mungu na Kristo kwa njia bora niwezavyo nikiwa mzee katika kundi la Kikristo, pamoja na mke, watoto, na wajukuu wangu. (Zaburi 112:7, 8)—Kama ilivyosimuliwa na René Séglat.
[Picha katika ukurasa wa 28]
Juu: Kuitwa majina kambini
Kushoto: Lango la kuingilia Buchenwald. Maandishi yasomwa hivi: “Kila mtu na apate yale anayostahili”
[Picha katika ukurasa wa 29]
Juu: Mahali pa kuchomea maiti huko Buchenwald
Kushoto: Wafungwa kumi na sita kwa kila safu