Mandhari Kutoka Bara Lililoahidiwa
Gerizimu—‘Tuliabudu Katika Mlima Huu’
MWANAMKE Msamaria kisimani. Je! fungu hilo la maneno lakukumbusha juu ya ule usimulizi wenye kugusa moyo wa Yesu akitoa ushahidi wa vivi hivi kwa mwanamke kwenye “kisima cha Yakobo” katika Sikari, jiji la Samaria? Je! ungependa kuona vizuri zaidi tukio hilo la maana?—Yohana 4:5-7.
Angalia milima hiyo miwili iliyo juu, iliyo kilometa 50 kaskazini mwa Yerusalemu.a Kwa upande wa kushoto (kusini) ni Gerizimu wenye miti mingi; vijito vingi huchangia hali yao yenye rutuba na uzuri wao. Kwenye upande wa kulia (kaskazini) ni Ebali, ulio wa juu zaidi kidogo lakini wenye miamba na ukame.
Bonde lenye rutuba la Shekemu hupitia kati yao. Kumbuka kwamba wakati rafiki ya Mungu Abramu (aliyeitwa Abrahamu baadaye) aliposafiri kuja chini kupitia Bara Lililoahidiwa, alipumzika kidogo Shekemu. Alijenga madhabahu huko kwa ajili ya Yehova, aliyekuwa tu amemtokea na kuahidi bara hilo kwa mbegu yake. (Mwanzo 12:5-7) Hapo palikuwa mahali pafaapo kama nini kufanya ahadi hiyo, katikati ya bara hilo! Kutoka kilele cha ama Gerizimu ama Ebali, mzee huyo wa ukoo angeweza kuona sehemu kubwa za Bara Lililoahidiwa. Jiji la Shekemu (Nablus la ki-siku-hizi) lilikuwa kitovu muhimu, likiwa kwenye barabara ya mlima iliyoelekea kusini na kaskazini ambayo ilikuwa karibu na barabara iliyotokea mashariki kuelekea magharibi kati ya pwani na Bonde la Yordani.
Madhabahu ya Abrahamu ilikuwa tukio moja tu la kidini lenye kutokeza huko. Baadaye, Yakobo alinunua bara katika eneo hilo na akaendeleza ibada ya kweli. Pia alichimba au kulipia uchimbaji wa kisima kirefu, karibu na sehemu ya chini ya Gerizimu. Karne kadhaa baadaye mwanamke Msamaria alimwambia Yesu hivi: “Baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki . . . , akanywa maji yake.” Huenda ikawa chanzo cha maji yacho kilikuwa kijito, jambo liwezalo kueleza kwa nini mtume Yohana alikiita “bubujiko la Yakobo” (NW).
Mtajo wa ibada ya kweli kuhusiana na Gerizimu na Ebali huenda ukakukumbusha kwamba Yoshua alileta Israeli huku, kama vile Musa alivyoelekeza. Yoshua alijenga madhabahu juu ya Ebali. Ebu wazia nusu ya watu wakiwa mbele ya Gerizimu na waliobaki wakiwa mbele ya Ebali huku Yoshua akisoma “torati, baraka na laana.” (Yoshua 8:30-35; Kumbukumbu la Torati 11:29) Miaka kadhaa baadaye, Yoshua alirudi akasema hivi likiwa himizo la mwisho: “Lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA [Yehova, NW].” Watu wakaahidi kufanya vivyo hivyo. (Yoshua 24:1, 15-18, 25) Lakini je, wangefanya hivyo kweli?
Jibu laweza kukusaidia uyaelewe mazungumzo ya Yesu pamoja na mwanamke huyo Msamaria. Ni hivi, ibada ya kweli iliyofuatwa na Abrahamu, Yakobo, na Yoshua haikuendelea huku katika Samaria.
Baada ya makabila kumi ya kaskazini kujitenga, yaligeukia ibada ya ndama. Kwa hiyo Yehova aliwaruhusu Waashuru washinde eneo hilo katika 740 K.W.K. Walichukua idadi kubwa ya wakaaji, wakiweka mahali pao wageni kutoka kwingineko katika Milki ya Ashuru, waabudu wa vijimungu vya kigeni. Yaelekea kwamba baadhi ya wapagani hao walioana na Waisraeli na kujifunza baadhi ya mafundisho ya dini ya kweli, kama vile tohara. Lakini namna ya ibada ya Kisamaria iliyotokea kwa hakika haikumpendeza Mungu kikamili.—2 Wafalme 17:7-33.
Katika ibada yao yenye kuchanganyika, Wasamaria walikubali Maandiko kuwa tu vile vitabu vitano vya kwanza vya Musa, Pentateuki. Yapata karne ya nne K.W.K. walijenga hekalu juu ya Mlima Gerizimu, kwa kushindana na hekalu la Mungu katika Yerusalemu. Baadaye hekalu la Gerizimu liliwekwa wakfu kwa Zeu (au, Sumbula) na kuharibiwa mwishowe. Bado, ibada ya Kisamaria iliendelea kuwa na kitovu chayo katika Gerizimu.
Hadi leo, Wasamaria huwa na mwadhimisho wa Sikukuu ya Kupitwa ya kila mwaka juu ya Gerizimu. Wana-kondoo kadhaa huchinjwa. Mizoga yao hutumbukizwa katika mitungi yenye maji yanayochemka ili sufu iweze kunyonyolewa, kisha nyama hupikwa katika mashimo ya makaa kwa muda wa saa kadhaa. Katika usiku wa manane mamia ya Wasamaria, wengi kutoka Yerusalemu, huwa na mlo wao wa pasaka. Upande wa kushoto, unaweza kuona kuhani mkuu Msamaria, kichwa chake kikiwa kimefunikwa, akisimamia kwenye mwadhimisho wa Sikukuu ya Kupitwa juu ya mlima Gerizimu.
Kumbuka lile ambalo mwanamke Msamaria alimwambia Yesu: “Baba zetu waliabudu katika mlima huu.” Yesu alimtolea yeye na sisi pia elezo hili sahihi: “Saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. . . . Lakini saa inakuja, nayo saa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”—Yohana 4:20-24.
[Maelezo ya Chini]
a Unaweza kuchunguza picha hiyo ikiwa na ukubwa zaidi katika 1993 Calendar of Jehovah’s Witnesses.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Garo Nalbandian
Garo Nalbandiany