Je! Mlo Huo Waweza Kuwa na Maana Kwako?
MWEZI mpevu wafunika bara kwa nuru nyororo. Katika chumba cha juu cha kao lililomo katika Yerusalemu la zamani za kale, wanaume 12 wamekusanyika kuzunguka meza. Kumi na mmoja wanasikiliza kwa makini sana huku Mwalimu wao anapoanzisha mwadhimisho wenye maana sana na kusema maneno yaliyo na umaana mkubwa. Usimulizi mmoja wasema hivi:
“Yesu [Kristo] alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu. Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu. Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni.”—Mathayo 26:26-30.
Hilo lilitukia baada ya jua kushuka siku ya 14 ya mwezi wa Kiyahudi wa Nisani katika mwaka wa 33 wa Wakati wa Kawaida wetu. Yesu na mitume wake walikuwa wametoka tu kuadhimisha Sikukuu ya Kupitwa katika kukumbuka kukombolewa kwa Israeli kutoka katika utumwa wa Misri katika karne ya 16 K.W.K. Kristo alikuwa amemwondosha Yuda Iskariote, aliyekuwa karibu kumsaliti. Kwa hiyo, ni Yesu na mitume wake waaminifu 11 tu waliokuwapo.
Mlo huo wa jioni haukuwa mfuatio wa Sikukuu ya Kupitwa ya Kiyahudi. Lilikuwa jambo jipya lililokuja kuitwa Mlo wa Jioni wa Bwana. Kuhusu mwadhimisho huo, Yesu aliwaamuru wafuasi wake hivi: “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” (Luka 22:19, 20; 1 Wakorintho 11:24-26) Kwa nini alisema hivyo? Na tukio hilo la karne nyingi zilizopita linawezaje kwa vyovyote kuwa na maana kwako?