Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w93 12/15 kur. 3-7
  • Je! Yesu Alizaliwa Wakati wa Theluji?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je! Yesu Alizaliwa Wakati wa Theluji?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Umaana Gani kwa Wanafunzi wa Biblia?
  • Hesabu Zenye Msingi wa Kibiblia
  • Kutoka Chanzo Kipi?
  • Je! Ni Jambo la Maana?
  • Yesu Alizaliwa Wakati Gani?
    Amkeni!—2008
  • Yesu Alizaliwa Wakati Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Yesu Alizaliwa Lini?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Krismasi—Je, Kweli Ni ya Kikristo?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
w93 12/15 kur. 3-7

Je! Yesu Alizaliwa Wakati wa Theluji?

“THELUJI Nzito Yakomesha Utendaji Yerusalemu” na “Theluji Yenye Kuendelea Yapiga Kaskazini.” Vichwa vikuu hivyo katika gazeti The Jerusalem Post vilikuwa jambo la kawaida kwa wasomaji Waisraeli katika 1992, katika vile vilivyothibitika kuwa mojapo vipupwe vibaya zaidi vya Israel katika karne hii.

Kufikia Januari kilele cha Mlima Hermoni kilifunikwa kwa meta 7 hadi 12 za theluji, na kipupwe kilikuwa kingali chaendelea. Kutoka Miinuko ya Golani na Sehemu ya Juu Zaidi ya Galilaya kuelekea chini kupita Yerusalemu na karibu na Bethlehemu (ionwayo kwenye jalada), hata kusini zaidi kuingia Negebu, mara kwa mara utendaji wa kawaida wa Waisraeli ulikomeshwa na yule mgeni mwenye madaha na mwororo, lakini mwenye nguvu. Makala moja ya Jerusalem Post ilisema hivi: “Kunyesha kwa theluji nzito jana kulitimiza kile ambacho mmiminiko wa roketi za Katyusha zilishindwa kufanya juma lililopita, kufunga makao na kuzuia wakazi wasitoke kabisa nyumbani mwao.”

Kile kipupwe kikali kilileta hasara kwa wengi zaidi ya wakazi wa jijini. Habari zilikuja juu ya mamia ya ng’ombe na ndama, na pia maelfu ya kuku, walioganda hadi kufa wakati halijoto za usiku ziliposhuka kwa ghafula hadi chini ya kiwango mgando. Kana kwamba theluji haikutosha, mvua nzito, yenye baridi ilileta hasara pia. Siku moja, yaonekana wakati wavulana wachanga wawili waliokuwa wachungaji walipokuwa wakijaribu sana kuokoa kondoo wao kadhaa waliokuwa wamechukuliwa katika furiko la ghafula, wao pia walichukuliwa na kuzama katika mvo huo.

Ingawa hicho hakikuwa kipupwe cha kawaida cha Mashariki ya Kati, gazeti la Israel Eretz liliripoti hivi: “Habari za kimeterolojia ambazo zimekusanywa na kurekodiwa katika bara la Israel kwa muda wa miaka 130 iliyopita zafunua kwamba theluji katika Yerusalemu ni tukio la kawaida zaidi ya vile huenda ikatazamiwa . . . Kati ya 1949 na 1980, jiji la Yerusalemu lilikuwa na vipupwe ishirini na vinne vyenye theluji.” Lakini je, habari hiyo ina thamani ya kimeterolojia na ya kuwapendeza wanadamu tu, au ina maana hususa kwa wanafunzi wa Biblia?

Umaana Gani kwa Wanafunzi wa Biblia?

Wanapofikiria kuzaliwa kwa Yesu, watu wengi huwazia ile mandhari ya hori yenye kuvutia kihisiamoyo ambayo huonyeshwa mara nyingi wakati wa Krismasi. Mtoto mchanga Yesu alala, akiwa amefunikwa ili apate joto na kulindwa na mama yake, theluji laini ikifunika mazingira yanayozunguka. Je! maoni hayo ya walio wengi hufaana na simulizi la Biblia juu ya tukio hilo la kihistoria?

Mwandishi wa Biblia Luka aeleza hivi juu ya simulizi la kuzaliwa kwa Yesu lililoandikwa kwa uangalifu: “Katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana [Yehova, New World Translation] akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana [Yehova, NW] ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi [Bethlehemu] amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”—Luka 2:8-14.

Ikiwa ungesoma simulizi hilo kwa Mwisraeli wa kawaida leo na kumuuliza ni wakati gani wa mwaka hilo lingeweza kuwa lilitukia, yaelekea angejibu, “Wakati fulani katikati ya Aprili na Oktoba.” Kwa nini? Jibu ni sahili. Kutoka Novemba hadi Machi ni majira ya baridi, yenye mvua katika Israel, na kwa hakika Desemba 25 ni katika wakati wa kipupwe. Wachungaji wasingekuwa wakiishi nje, wakichunga makundi yao ya mifugo makondeni wakati wa usiku. Ukifikiria zile ripoti mwanzoni mwa makala hii, waweza kuelewa vema ni kwa sababu gani. Bethlehemu, ambako Yesu alizaliwa, liko katika miinuko ya juu zaidi na kilometa chache tu kutoka Yerusalemu. Hata katika miaka ambayo halihewa si mbaya sana, huko ni baridi sana wakati wa usiku katika kipupwe.—Mika 5:2; Luka 2:15.

Historia ya wakati wa kuzaliwa kwa Yesu yaelimisha juu ya jambo la kwamba yeye hakuzaliwa wakati wa theluji ya Desemba. Ingawa mama ya Yesu, Mariamu, alikuwa katika hatua za mwisho za ujauzito, alilazimika kusafiri kutoka nyumbani kwake Nazareti hadi Bethlehemu. Yeye na Yusufu walifanya hivyo ili kutimiza matakwa ya sensa iliyoamriwa na mtawala Mroma Kaisari Augusto. (Luka 2:1-7) Wakazi Wayahudi, wakiwa wanachukia utawala wa Kiroma na ushuru wao wa juu, tayari walikuwa karibu kuasi. Kwa nini taifa la Roma liwaudhi bila sababu kwa kuwataka wengi wasafiri ili wasajiliwe wakati wa halihewa ya kipupwe iliyo ngumu zaidi na hata yenye hatari? Je! isingefaa zaidi kwamba hilo lingaliamriwa kutukia katika majira yafaayo zaidi usafiri, kama vile majira ya masika au vuli?

Hesabu Zenye Msingi wa Kibiblia

Ithibati ya kihistoria na ya hali ya nchi yaonyesha Desemba, au mwezi mwingine wowote wa kipupwe, kuwa haufaani na masimulizi ya kuzaliwa kwa Yesu. Isitoshe, kupitia unabii Biblia hufunua wakati wa mwaka ambao Yesu alizaliwa. Ni wapi ifanyapo hivyo?

Katika kitabu cha Danieli, sura ya 9, twapata mmojawapo unabii wenye kuvutia zaidi kuhusu Mesiya. Huo wasimulia kuja kwake na pia kukatiliwa kwake mbali katika kifo, kulikoandaa dhabihu ya fidia ya kufunika dhambi na kuweka msingi ili ainabinadamu tiifu ipate “haki ya milele.” (Danieli 9:24-27; linganisha Mathayo 20:28.) Kulingana na unabii huo, yote hayo yangetimizwa katika kipindi cha majuma 70 ya miaka, kuanzia mwaka wa 455 K.W.K., amri ilipotolewa kujenga upya Yerusalemu.a (Nehemia 2:1-11) Kutokana na mgawanyo wa wakati katika unabii huu, yaweza kutambuliwa kwamba Mesiya angetokea mwanzoni mwa juma la 70 la miaka. Hilo lilitukia wakati Yesu alipojitoa mwenyewe abatizwe katika 29 W.K., hilo likianzisha rasmi daraka lake la Kimesiya. “Kwa nusu ya juma hiyo,” au baada ya miaka mitatu na nusu, Mesiya angekatiliwa mbali katika kifo, hivyo akikomesha thamani ya dhabihu zote chini ya agano la Sheria la Kimusa.—Waebrania 9:11-15; 10:1-10.

Unabii huo wafunua kwamba urefu wa huduma wa Yesu ulikuwa miaka mitatu na nusu. Yesu alikufa katika Sikukuu ya Kupitwa, Nisani 14 (kulingana na kalenda ya Kiyahudi), katika masika ya 33 W.K. Tarehe ya mwaka huo inayolingana na hiyo ingekuwa Aprili 1. (Mathayo 26:2) Kuhesabu nyuma muda wa miaka mitatu na nusu kwaweka ubatizo wake katika 29 W.K. mwanzoni mwa Oktoba. Luka atuarifu kwamba Yesu alikuwa karibu miaka 30 alipobatizwa. (Luka 3:21-23) Hilo lingemaanisha kwamba kuzaliwa kwa Yesu kulikuwa pia karibu na mwanzo wa Oktoba. Kwa kupatana na simulizi la Luka, wakati huo wa mwaka wachungaji wangekuwa wangali “wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku.”—Luka 2:8.

Kutoka Chanzo Kipi?

Kwa kuwa ithibati yaonyesha wakati wa kuzaliwa kwa Yesu kuwa mapema katika Oktoba, kwa nini kunasherehekewa katika Desemba 25? The New Encyclopædia Britannica yaonyesha kwamba sherehe hiyo ilianzishwa karne nyingi baada ya kuzaliwa kwa Yesu: “Katika karne ya 4 mwadhimisho wa kuzaliwa kwa Kristo katika Desemba 25 ulianzishwa polepole na makanisa mengi ya Mashariki. Katika Yerusalemu, upinzani dhidi ya Krismasi ulidumu muda mrefu zaidi, lakini ilikubaliwa baadaye.”

Kwa nini desturi hiyo ilikubaliwa kwa urahisi hivyo na wale waliojiita Wakristo karne nyingi baada ya Kristo? The New Encyclopædia Britannica yaelimisha zaidi juu ya habari hiyo: “Desturi za kimapokeo zinazohusianishwa na Krismasi zimesitawi kutokana na vyanzo kadhaa likiwa tokeo la sadfa kati ya sherehe ya kuzaliwa kwa Kristo na miadhimisho ya kipagani ya katikati ya kipupwe iliyohusu kilimo na jua. Katika ulimwengu wa Waroma [sikukuu ya] Saturnalia (Desemba 17) ilikuwa wakati wa kusherehekea na kubadilishana zawadi. Desemba 25 ilionwa pia kuwa tarehe ya kuzaliwa kwa mungu-fumbo wa Irani Mithra, Jua la Uadilifu.”

Je! kweli hayo yote yalikuwa “sadfa”? Hasha! Ni jambo la hakika la historia kwamba katika karne ya nne W.K., chini ya Maliki Konstantino, Milki ya Roma ilibadilika sana kutoka kuwa mnyanyasi wa Ukristo hadi kuwa mdhamini wa “Ukristo” ukiwa dini iliyokubaliwa. Watu wengi zaidi kwa ujumla, ambao hawakuwa na habari ya msingi juu ya maana ya kweli ya Ukristo, walipokubali imani mpya hiyo, walianza kusherehekea sikukuu zao za kipagani walizofahamu zikiwa na majina mapya ya “Kikristo.” Ni tarehe gani ambayo ingefaa zaidi ya kusherehekea kuzaliwa kwa Kristo kuliko Desemba 25, ambayo tayari ilijulikana kuwa tarehe ya kuzaliwa kwa “Jua la Uadilifu”?

Je! Ni Jambo la Maana?

Hakuna shaka lolote kwamba wafuasi wa Yesu wa kwanza, waliokuwa na malezi ya Kiyahudi, hawakusherehekea siku yake ya kuzaliwa. Kulingana na Encyclopaedia Judaica, “kuadhimisha siku za kuzaliwa hakukujulikana katika desturi za kimapokeo za Kiyahudi.” Kwa hakika Wakristo wa mapema wasingalikubali kufuata sherehe kama hiyo. Badala ya kusherehekea kuzaliwa kwake, wangestahi amri ya Yesu ya kukumbuka kifo chake, kilichokuwa na tarehe isiyokanika, yaani, Nisani 14.—Luka 22:7, 15, 19, 20; 1 Wakorintho 11:23-26.

Karne nyingi kabla ya Kristo, watu wa Kiyahudi, ambao wakati huo walikuwa taifa-teule la Mungu, walionywa hivi kiunabii juu ya mwisho wa uhamisho wao katika Babuloni uliokuwa ukija: “Nendeni zenu, nendeni zenu, tokeni huko, msiguse kitu kichafu; tokeni kati yake; iweni safi ninyi mnaochukua vyombo vya BWANA [Yehova, NW].” (Isaya 52:11) Walipaswa kurudi kwenye bara la nyumbani kwao ili kuanzisha upya ibada safi ya Yehova. Isingewazika kwao kufuata desturi za kipagani na unamna-namna wa ibada usio safi waliokuwa wameona katika Babuloni.

Bila kushangaza, amri iyo hiyo inarudiwa kwa Wakristo kwenye 2 Wakorintho 6:14-18. Badala ya taifa la Kiyahudi lililomkatalia mbali Kristo, wafuasi wake walikuja kuwa wawakilishi wa ibada safi. Walikuwa na daraka la kuwasaidia wengine watoke katika giza la kiroho na kuingia katika nuru ya kweli. (1 Petro 2:9, 10) Kwa kweli wangeweza kufanyaje hivyo ikiwa wangechanganya mafundisho ya Kristo pamoja na desturi na sikukuu zenye awali ya kipagani?

Ingawa huenda kukavutia upendezi wa walio wengi, kuadhimisha “Krismasi Yenye Theluji” ni sawa na ‘kugusa kitu kilicho kichafu.’ (2 Wakorintho 6:17) Ni lazima mtu ambaye kwa kweli ampenda Mungu na Kristo aepuke hilo.

Mbali na jambo la hakika kwamba asili yazo ni katika sherehe za kipagani, tumeona pia kwamba Krismasi haiwakilishi kweli, kwa kuwa Yesu alizaliwa katika Oktoba. Ndiyo, haidhuru ni mandhari gani ambayo huenda mtu akawazia, Yesu hakuzaliwa wakati wa theluji hata kidogo.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa mazungumzo kamili zaidi juu ya unabii huu, ona broshua Je! Ulimwengu Usio na Vita Utakuwako Wakati Wowote? ukurasa 26, iliyotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 4, 5]

Yerusalemu lililofunikwa kwa theluji, kama lionwavyo kutoka mashariki

[Hisani]

Garo Nalbandian

[Picha katika ukurasa wa 6]

Theluji kando ya kuta za Yerusalemu

[Picha katika ukurasa wa 7]

Ni katika majira yenye joto tu ambayo wachungaji waweza kukaa pamoja na makundi yao ya mifugo usiku kwenye miteremko ya vilima yenye mawe-mawe, kama vile ionwavyo chini

[Hisani]

Garo Nalbandian

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki