Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Kwa kuwa mara nyingi Biblia hutaja “mvulana asiye na baba,” (NW) je, hilo laonyesha kutowafikiria wasichana sana?
Sivyo hata kidogo.
New World Translation of the Holy Scriptures hutumia fungu la maneno “mvulana asiye na baba” katika mistari mingi idhihirishayo ufikirio wa Mungu kuelekea watoto wasio na mzazi. Mungu alionyesha ufikirio huo wazi katika sheria alizotoa kwa Israeli.
Kwa kielelezo, Mungu alisema hivi: “Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima [mvulana asiye na baba, NW]. Ukiwatesa watu hao katika neno lo lote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima [wavulana wasio na baba].” (Kutoka 22:22-24) “BWANA [Yehova, NW], Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa. Huwafanyia yatima [mvulana asiye na baba, NW] na mjane hukumu ya haki.”—Kumbukumbu la Torati 10:17, 18; 14:29; 24:17; 27:19.
Fasiri nyingi za Biblia husomwa “mtoto asiye na baba” au “yatima” katika mistari hiyo, hivyo zikitia ndani wavulana na wasichana. Hata hivyo, fasiri hizo hupuuza sifa inayopatikana katika neno la msingi la Kiebrania (ya·thohmʹ), lililo katika hali ya kiume. Badala ya hivyo, New World Translation of the Holy Scriptures hutumia fasiri sahihi “mvulana (wavulana) asiye na baba,” kama vile kwenye Zaburi 68:5, isomwayo hivi: “Baba wa yatima [wavulana wasio na baba, NW] na mwamuzi wa wajane, [ni] Mungu katika kao lake takatifu.” Ikitegemea maana ya neno la msingi la Kiebrania, hali ya kike ya kitenzi katika Zaburi 68:11 hupendekeza isomwe hivi: “Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa.”a
Hata ingawa “mvulana asiye na baba” ni fasiri ya msingi ya ya·thohmʹ, haipaswi ionwe kuwa yadokeza kutokuwa na ufikirio kuelekea wasichana wasio na mzazi. Mafungu ya maneno yaliyonukuliwa na mengine yaonyesha kwamba watu wa Mungu walitiwa moyo watunze wanawake, wajane. (Zaburi 146:9; Isaya 1:17; Yeremia 22:3; Zekaria 7:9, 10; Malaki 3:5) Katika Sheria, Mungu alitia ndani pia simulizi juu ya uamuzi wa kihukumu uliohakikisha urithi kwa ajili ya binti za Selofehadi wasiokuwa na baba. Uamuzi huo ulikuja kuwa sheria ya kushughulikia hali kama hizo, hivyo ikitegemeza haki za wasichana wasio na baba.—Hesabu 27:1-8.
Yesu hakubagua jinsia alipoonyesha fadhili kwa watoto. Badala ya hivyo, twasoma hivi: “[Watu] wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.”—Marko 10:13-16.
Neno la Kigiriki litafsiriwalo hapa kuwa “watoto wadogo” limo katika hali ya kati. Kamusi moja mashuhuri ya Kigiriki yasema kwamba neno hilo “hutumiwa kuhusiana na wavulana na wasichana.” Yesu alikuwa akionyesha upendezi uliofanana na ule wa Yehova kuelekea watoto wote, wavulana na wasichana. (Waebrania 1:3; linganisha Kumbukumbu la Torati 16:14; Marko 5:35, 38-42.) Hivyo yapasa itambuliwe kwamba shauri katika Maandiko ya Kiebrania juu ya kuwatunza “wavulana wasio na baba” ni shauri juu ya jinsi tupaswavyo kuwa na ufikirio kuelekea watoto wote wasio na mzazi au wazazi.
[Maelezo ya Chini]
a Tanakh ya Kiyahudi husomwa hivi: “BWANA atoa amri; wanawake waletao habari ni kikosi kikubwa.”