Walithawabishwa kwa Kutembea Bila Lawama
YEHOVA hubariki na kuthawabisha watumishi wake waaminifu. Huenda wakahitaji kungojea kwa muda fulani kabla ya kuona makusudi ya Mungu yakitimizwa, lakini inafurahisha kama nini tupatapo baraka zake!
Jambo hilo lilionyeshwa vema miaka elfu mbili iliyopita katika kisa cha kuhani wa Kiyahudi Zekaria pamoja na mke wake, Elisabeti, wote wakiwa wa familia ya Haruni. Mungu aliahidi kubariki Waisraeli kwa kuwapa wazao kama wangalimtumikia kwa uaminifu. Alisema kwamba watoto ni thawabu. (Mambo ya Walawi 26:9; Zaburi 127:3) Hata hivyo, Zekaria na Elisabeti hawakuwa na mtoto nao walikuwa wazee sana.—Luka 1:1-7.
Maandiko yasema kwamba Zekaria na Elisabeti “wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea [“wakitembea,” NW] katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.” (Luka 1:6) Walimpenda Mungu sana hivi kwamba haukuwa mzigo kwao kufuatia mwendo wa uadilifu na kushika amri zake.—1 Yohana 5:3.
Baraka Zisizotarajiwa
Ebu turudi nyuma katika msimu wa mwisho-mwisho wa masika au msimu wa mapema katika kiangazi cha mwaka wa 3 K.W.K. Herode Mkuu anatawala akiwa mfalme katika Yudea. Siku moja, kuhani Zekaria aingia ndani ya Patakatifu pa hekalu katika Yerusalemu. Huku watu wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya sala nje ya patakatifu, yeye avukiza uvumba katika madhabahu ya dhahabu. Labda ukionwa kuwa utumishi mkuu zaidi kati ya utumishi wa kila siku, hiyo hufanywa baada ya dhabihu kutolewa. Huenda kuhani alikuwa akipata pendeleo hilo mara moja maishani mwake mwote.
Zekaria haamini macho yake. Kwani, malaika wa Yehova asimama kwenye upande wa kulia wa madhabahu ya uvumba! Kuhani huyo mzee-mzee apatwa na fadhaiko na hofu. Lakini malaika yule asema: “Usiogope, Zekaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.” Naam, Yehova amesikia sala zenye bidii za Elisabeti na Zekaria.—Luka 1:8-13.
Malaika huyo aongezea: “Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa [“roho takatifu,” NW] hata tangu tumboni mwa mamaye.” Yohana atakuwa Nadhiri aliyejazwa roho takatifu ya Mungu maishani mwake mwote. Malaika huyo aendelea kusema: “Wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa.”—Luka 1:14-17.
Zekaria auliza hivi: “Nitajuaje neno hilo? maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi.” Yule malaika ajibu: “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake.” Zekaria atokapo patakatifu, hawezi kusema, na watu wafikiria kwamba ameona ono lizidilo nguvu za asili. Yeye angeweza kutoa ishara tu, akizitumia kuwasilisha mawazo yake. Utumishi wake wa umma uishapo, yeye arudi nyumbani.—Luka 1:18-23.
Sababu ya Shangwe
Kama ilivyoahidiwa, upesi Elisabeti akawa na sababu ya kushangilia. Ashika mimba, akiondoa suto la kuwa tasa. Mtu wake wa ukoo Mariamu vilevile awa mwenye shangwe, kwa sababu malaika yuleyule, Gabrieli, amwambia hivi: “Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.” Mariamu yuko tayari kutimiza fungu la kuwa “mjakazi wa Bwana.”—Luka 1:24-38.
Mariamu aharakisha kwenda nyumbani kwa Zekaria na Elisabeti katika jiji moja la Yudea katika nchi ya milimani. Kwa kusikia tu sauti ya salamu ya Mariamu, kitoto kichanga katika tumbo la Elisabeti kikaruka. Akiwa chini ya uvutano wa roho takatifu ya Mungu, Elisabeti apaaza sauti akisema: “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.” Mariamu aitikia kwa shangwe kuu. Naye akaa na Elisabeti kwa karibu miezi mitatu.—Luka 1:39-56.
Yohana Azaliwa
Baada ya muda Elisabeti na Zekaria walio wazee-wazee wapata mwana. Katika siku ya nane, mtoto huyo mchanga atahiriwa. Watu wa ukoo wataka mwana huyo aitwe Zekaria, lakini Elisabeti asema: “La, sivyo; bali, ataitwa Yohana.” Je! mume wake ambaye angali ni bubu akubali? Kwenye bamba yeye aandika: “Jina lake ni Yohana.” Papo hapo, ulimi wa Zekaria walegezwa, naye aanza kusema, akimbariki Yehova.—Luka 1:57-66.
Akiwa amejazwa roho takatifu, kuhani huyo mwenye shangwe atoa unabii. Yeye asema kana kwamba yule Mkombozi aliyeahidiwa—‘yule pembe ya wokovu katika nyumba ya Daudi’—tayari ameinuliwa kwa kupatana na agano la Kiabrahamu kuhusu Mbegu ya kubarikia mataifa yote. (Mwanzo 22:15-18) Akiwa mtangulizi wa Mesiya, mwana wa Zekaria aliyezaliwa kimuujiza ‘atatangulia mbele za uso wa Bwana amtengenezee njia zake; awajulishe watu wake wokovu.’ Miaka ilipozidi kupita, Yohana aliendelea kukua na kuwa na nguvu kiroho.—Luka 1:67-80.
Wathawabishwa Sana
Zekaria na Elisabeti walikuwa vielelezo vizuri vya imani na saburi. Waliendelea kumtumikia Yehova kwa uaminifu hata ingawa walilazimika kumngojea Mungu, na baraka zao kubwa zaidi zilikuja tu walipokuwa wazee sana.
Naam, Elisabeti na Zekaria walifurahia baraka iliyoje! Wakiwa chini ya uvutano wa roho ya Mungu, wote wawili walitoa unabii. Walipata pendeleo la kuwa wazazi na wafunzi wa mtangulizi wa Mesiya, Yohana Mbatizaji. Isitoshe, Mungu aliwaona kuwa waadilifu. Vilevile, wale ambao leo wanafuatia mwendo wa kimungu waweza kuwa na msimamo wenye uadilifu mbele ya Mungu na watapokea thawabu zenye baraka kwa kutembea bila lawama katika amri za Yehova.