Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Kwa kuwa Yesu alitoka ukoo wa Yese na Daudi, kwa nini anaitwa “mzizi” (NW) wa wazazi wake wa kale Yese na Daudi waliokufa?
Kwa kawaida mtu hufikiria mzizi wa mti au wa mmea kuwa ndio hutokea kabla ya shina au matawi. Kwa hiyo huenda ikaonekana kwamba Yese (au mwanawe Daudi) wangesemwa kuwa mzizi ambao Yesu angetokea kwao hatimaye. Bado, Isaya 11:10, (NW) ilitabiri kwamba Mesiya aliyekuwa akija angekuwa “mzizi wa Yese,” na Warumi 15:12 ilitumia unabii huo kumhusu Yesu Kristo. Baadaye Ufunuo 5:5 ilimwita “Simba aliye wa kabila la Yuda, Shina la [“mzizi wa,” NW] Daudi.” Kuna sababu za kutumia majina hayo.
Mara nyingi Biblia hutumia mmea, kama vile mti, kwa njia ya ufananisho. Nyakati nyingine hilo hutokana na jambo la kwamba mbegu inapochipuka na kukua, mizizi husitawi kabla ya vitawi, matawi mengine, au matunda kutegemezwa na mizizi. Kwa kielelezo, Isaya 37:31 yasomwa hivi: “Mabaki yaliyookoka, yaliyobakia ya nyumba ya Yuda, yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu.”—Ayubu 14:8, 9; Isaya 14:29.
Mzizi unapopatwa na madhara, baki la mti huathiriwa pia. (Linganisha Mathayo 3:10; 13:6.) Kulingana na hilo, Malaki aliandika hivi: “Siku ile inayokuja itawateketeza, asema BWANA wa majeshi; hata haitawaachia shina [“mzizi,” NW] wala tawi.” (Malaki 4:1) Maana ni wazi—kukatiliwa mbali kabisa. Wazazi (mizizi) wangekatiliwa mbali, pamoja na wazao wao (vitawi).a Hilo lakazia daraka walio nalo wazazi kuelekea watoto wao wadogo; wakati ujao udumuo wa watoto wadogo ungeweza kuamuliwa kwa msimamo wa wazazi wao mbele ya Mungu.—1 Wakorintho 7:14.
Lugha iliyo kwenye Isaya 37:31 na Malaki 4:1 yatokana na jambo la kwamba vitawi (na matunda yaliyo juu ya matawi ya chini) hupata uhai wavyo kutoka kwa mzizi. Huo ndio ufunguo wa kuelewa jinsi Yesu ni “mzizi wa Yese” na “mzizi wa Daudi.” (NW)
Kwa njia ya kimwili, Yese na Daudi walikuwa wazazi wa kale wa Yesu waliokufa; walikuwa mizizi, yeye alikuwa kichipuko au kitawi. Isaya 11:1 ilisema hivi juu ya Mesiya aliyekuwa akija: “Litatoka chipukizi katika shina la [“mzizi wa,” NW] Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.” Vivyo hivyo, kwenye Ufunuo 22:16, Yesu ajiita “Mzao wa Daudi.” Lakini yeye ajiita pia “mzizi wa Daudi.” (NW) Kwa nini?
Njia moja ambayo Yesu ni “mzizi” wa Yese na Daudi ni kwamba kupitia yeye nasaba yao inaendelea ikiwa hai. Hakuna binadamu leo awezaye kuthibitisha kwamba yeye ni wa kabila la Lawi, Dani, au hata Yuda, lakini twaweza kuwa na uhakika kwamba nasaba ya Yese na Daudi inaendelea kwa sababu sasa Yesu yuko hai mbinguni.—Mathayo 1:1-16; Warumi 6:9.
Yesu alipokea pia cheo cha Mfalme wa kimbingu. (Luka 1:32, 33; 19:12, 15; 1 Wakorintho 15:25) Hilo lahusisha uhusiano wake hata na wazazi wake wa kale waliokufa. Kiunabii, Daudi alimwita Yesu Bwana yake.—Zaburi 110:1; Matendo 2:34-36.
Mwishowe, Yesu Kristo amepewa mamlaka ya kuwa Hakimu. Katika Mileani inayokuja, manufaa za fidia ya Yesu zitafikia pia Yese na Daudi. Wakati huo uhai wao duniani utategemea Yesu, atakayetumikia akiwa “Baba [yao] wa milele.”—Isaya 9:6.
Kwa hiyo, ingawa Yesu alitoka katika nasaba ya Yese na Daudi, cheo ambacho amekuja kuwa nacho na yale atakayofanya bado humstahilisha kuitwa “mzizi wa Yese” na “mzizi wa Daudi.” (NW)
[Maelezo ya Chini]
a Mchoro wa kaburini wa Foinike ya kale ulitumia lugha inayofanana na hiyo. Ulisema hivi juu ya wowote waliofungua kaburi hilo: “Na wasiwe wala na mzizi chini wala na matunda juu!”—Vetus Testamentum, Aprili 1961.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.