Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w94 12/15 kur. 26-29
  • Msiba Katika Rwanda—Ni Nani Anayelaumika?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Msiba Katika Rwanda—Ni Nani Anayelaumika?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wahutu na Watutsi
  • Ni Nani Anayelaumika?
  • Fungu la Dini
  • Wakristo wa Kweli Ni Tofauti
  • Je, Dini Inategemeka Kuhusiana na Vita?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
  • Kuwatunza Majeruhi wa Msiba wa Rwanda
    Amkeni!—1994
  • Ni Nini Kimepata Upendo wa Jirani?
    Amkeni!—1998
  • Kushiriki Faraja Ambayo Yehova Huandaa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
w94 12/15 kur. 26-29

Msiba Katika Rwanda—Ni Nani Anayelaumika?

“Muda tu kabla ya kichwa cha fundi mwenye umri wa miaka 23 kupasuliwa,” U.S.News & World Report lilisema, “mmoja wa washambulizi alimwambia Hitiyise: ‘Ni lazima ufe maana wewe ni Mtutsi.’”

KISA kama hicho kilirudiwa mara nyingi jinsi gani katika nchi ndogo ya Rwanda iliyo katika Afrika ya Kati miezi ya Aprili na Mei! Wakati huo kulikuwa na makutaniko 15 ya Mashahidi wa Yehova ndani na viungani vya Kigali, jiji kuu la Rwanda. Mwangalizi wa jiji, Ntabana Eugène, alikuwa Mtutsi. Yeye, mkeye, mwanaye, na bintiye, Shami mwenye umri wa miaka tisa, walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuchinjwa ghasia yenye jeuri ilipolipuka.

Maelfu ya Warwanda waliuawa kila siku—juma baada ya juma. “Katika majuma sita yaliyopita,” gazeti lililonukuliwa pale juu liliripoti katikati ya Mei, “watu wengi kama 250,000 wamekufa katika kampeni ya mauaji ya kukusudia ya kabila fulani na malipizo ya kisasi kama yale ya Khmer Rouge yaliyokuwa ya kikatili yaliyokumba Kambodia katikati ya miaka ya 1970.”

Gazeti la Time lilisema hivi: “Katika kisa kilichofanana na kile cha Ujerumani ya Nazi, watoto walitolewa miongoni mwa kundi la watoto 500 kwa sababu tu walifanana na Watutsi. . . . Meya wa mji wa Butare ulio upande wa kusini, ambaye amemwoa Mtutsi, alipewa uchaguzi [mgumu] na wakulima waliokuwa Wahutu: angemwokoa mkeye na watoto ikiwa angetoa familia ya mkeye—wazazi na dada zake—wauawe. Alikubali.”

Watu sita walifanya kazi katika Ofisi ya Tafsiri ya Mashahidi wa Yehova katika Kigali, wanne wao wakiwa Wahutu na wawili Watutsi. Watutsi walikuwa Ananie Mbanda na Mukagisagara Denise. Wakati vikundi vyenye silaha pamoja na waporaji walipokuja katika nyumba hiyo, walikasirika kupata Wahutu na Watutsi wakikaa pamoja. Walitaka kuwaua Mbanda na Denise.

“Wakaanza kutoa pini kwa grenedi zao,” akasema Emmanuel Ngirente, mmoja wa ndugu Wahutu, “wakitisha kutuua, maana tulikuwa na adui zao miongoni mwetu. . . . Walitaka pesa nyingi sana. Tuliwapa pesa zote tulizokuwa nazo, lakini hawakutosheka. Waliamua kuchukua kutoka kwetu kama malipo kila kitu ambacho wangetumia, kutia kompyuta ndogo inayotumiwa katika kazi yetu ya kutafsiri, mashine ya fotokopi, redio zetu, viatu vyetu, na vinginevyo. Kwa ghafula wakaondoka bila kuua yeyote wetu, lakini walisema wangerudi baadaye.”

Katika siku zilizofuata, waporaji walikuwa wakirudi kila mara, na kila mara Mashahidi Wahutu waliwasihi wasiwaue marafiki zao Watutsi. Mwishowe, ilipokuwa hatari sana kwa Mbanda na Denise kukaa hapo zaidi, mipango ilifanywa ili waende pamoja na wakimbizi wengine Watutsi katika shule iliyokuwa karibu na hapo. Shule hiyo ilipovamiwa, Mbanda na Denise waliweza kutoroka. Walifaulu kuvuka vituo kadhaa vilivyozuiliwa, lakini, hatimaye, katika mojapo vituo hivyo Watutsi wote walichukuliwa kando, na Mbanda na Denise wakauawa.

Wanajeshi waliporudi katika Ofisi ya Tafsiri na kugundua kwamba Mashahidi Watutsi walikuwa wameondoka, wanajeshi hao waliwapiga sana ndugu Wahutu. Halafu kombora likalipuka karibu na hapo, na ndugu wakaweza kuponyoa uhai wao.

Mauaji yalipoendelea nchini kote, hesabu ya waliokufa ilifika nusu milioni. Hatimaye, kati ya milioni mbili na tatu, au zaidi, ya wakazi wa Rwanda milioni nane wakaacha makao yao. Wengi wao wakakimbilia Zaire na Tanzania zilizo karibu. Mashahidi wa Yehova wapatao mamia kadhaa waliuawa, na wengine wengi walikuwa miongoni mwa wale waliokimbilia kambi zilizokuwa nje ya nchi.

Ni nini kilichoanzisha machinjo hayo yasiyo na kifani na mwongoko mkubwa huo? Je, yangaliweza kuzuiwa? Hali ilikuwaje kabla ya jeuri kulipuka?

Wahutu na Watutsi

Rwanda pamoja na nchi jirani ya Burundi zinakaliwa na Wahutu, ambao kwa ujumla ni Bantu walio wafupi na wanene, na Watutsi, ambao kwa kawaida ni watu warefu, wenye rangi ya maji ya kunde ambao pia huitwa Watusi. Katika hizo nchi zote mbili Wahutu ni asilimia ipitayo 85 na Watutsi asilimia 14 ya wakaaji. Magombano kati ya vikundi hivi vya kikabila yamerekodiwa tangu huko nyuma katika karne ya 15. Hata hivyo, kwa muda mrefu wamekaa pamoja kwa amani.

“Tulikuwa tukiishi pamoja kwa amani,” mwanamke mwenye umri wa miaka 29 akasema juu ya Wahutu na Watutsi 3,000 wanaoishi katika kijiji cha Ruganda, kilichoko kilometa chache mashariki mwa Zaire. Hata hivyo, katika Aprili vikundi vya washambulizi vya Wahutu viliwaua karibu Watutsi wote wa kijiji. Likaeleza The New York Times:

“Hadithi ya kijiji hiki ni hadithi ya Rwanda: Wahutu na Watutsi wakiishi pamoja, wakioana wao kwa wao, bila kujali na bila kujua ni nani aliye Mhutu au aliye Mtutsi.

“Halafu kitu fulani kikatendeka. Katika Aprili, umati wenye ghasia wa Wahutu ukaanza mashambulizi nchini kote, ukiwaua Watutsi popote walipopatikana. Mauaji yalipoanza, Watutsi walikimbilia makanisa kwa usalama. Umati ukawafuata, ukibadili mahali pa salama kuwa makaburi yaliyotapakaa damu.”

Ni nini kilichoanzisha mauaji? Ni vifo vya rais wa Rwanda na Burundi, wote wawili wakiwa Wahutu, katika aksidenti ya ndege katika Kigali, Aprili 6. Tukio hili kwa njia fulani lilianzisha mauaji si ya Watutsi tu bali pia ya Mhutu yeyote aliyefikiriwa kuwa anawahurumia.

Wakati uleule, mapigano yalizidi kati ya majeshi ya waasi—R.P.F. (Rwandan Patriotic Front) yenye Watutsi wengi—na majeshi ya Serikali yenye Wahutu wengi. Kufikia Julai R.P.F. ilikuwa imeshinda majeshi ya Serikali nayo yalikuwa yametawala Kigali na sehemu kubwa ya Rwanda. Wakiogopa kulipizwa kisasi, Wahutu walitoroka nchi hiyo kwa mamia ya maelfu, mapema katika Julai.

Ni Nani Anayelaumika?

Alipoulizwa aeleze sababu iliyofanya jeuri itokee kwa ghafula katika Aprili, Mtutsi mmoja mkulima alisema: “Ni kwa sababu ya viongozi wabaya.”

Kwa kweli, katika karne zote, viongozi wa kisiasa wameeneza uongo kuhusu maadui zao. Wakiwa chini ya mwongozo wa “mkuu wa ulimwengu huu,” Shetani Ibilisi, wanasiasa wa kilimwengu wameshawishi watu wao wenyewe wapigane na kuua watu wa rangi, kabila, au taifa jingine. (Yohana 12:31; 2 Wakorintho 4:4; 1 Yohana 5:19) Ndivyo hali zilivyo katika Rwanda. The New York Times lilisema: “Wanasiasa wamejaribu kwa kurudia-rudia kukuza ushikamanifu wa kikabila na woga—kuhusu Wahutu, kuiongoza Serikali; kuhusu Watutsi, kuunga mkono majeshi ya waasi.”

Kwa kuwa watu wa Rwanda wanafanana kwa njia nyingi, hakuna mtu angeweza kutazamia wachukiane na kuuana. “Wahutu na Watutsi husema lugha moja na kwa ujumla desturi zao zinafanana,” akaandika ripota Raymond Bonner. “Baada ya kuoana kati yao kwa vizazi vingi, tofauti zao za sura—Watutsi kuwa warefu na wembamba, na Wahutu kuwa wafupi na wanene kidogo—zimetokomea kiasi cha kwamba Warwanda mara nyingi hawana hakika ni nani aliye Mhutu au Mtutsi.”

Hata hivyo, hivi karibuni propaganda nyingi zimeleta matokeo yasiyoweza kuaminika. Akitoa kielezi cha jambo hilo, Alex de Waal, mkurugenzi wa kundi la Haki za Waafrika, alisema: “Wakulima katika sehemu zilizoongozwa na R.P.F. wanaripotiwa kuwa walishangaa sana kwamba wanajeshi wa Watutsi hawana pembe, mikia na macho yanayong’aa usiku—habari kama hizo ndizo wanazosikiliza katika redio.”

Si viongozi wa kisiasa tu wanaounda fikira za watu bali pia dini. Ni zipi zilizo dini kuu za Rwanda? Je, hizo pia zinalaumika kwa sababu ya msiba huo?

Fungu la Dini

The World Book Encyclopedia (1994) chasema hivi kuhusu Rwanda: “Watu walio wengi ni wa Katoliki ya Kiroma. . . . Katoliki ya Kiroma na makanisa ya Kikristo mengineyo huendesha nyingi za shule za msingi na za sekondari.” National Catholic Reporter, kwa kweli lasema Rwanda ni “taifa la asilimia 70 Katoliki.”

The Observer, la Uingereza, latoa historia ya hali ya dini katika Rwanda, likieleza hivi: “Katika miaka ya 1930, wakati makanisa yalipokuwa yakipigania kuendesha mfumo wa elimu, Wakatoliki waliwapendelea Watutsi waliotawala wakati Waprotestanti walijiunga na Wahutu walio wengi na kuonewa. Katika 1959 Wahutu walinyakua utawala na upesi wakaanza kuungwa mkono na Wakatoliki na Waprotestanti. Utegemezo wa Waprotestanti kwa Wahutu walio wengi bado ni wenye nguvu sana.”

Kwa mfano, je, viongozi wa kanisa Protestanti, wameshutumu mauaji hayo? The Observer lajibu hivi: “Wafuasi wawili [Waanglikana] waliulizwa kama walishutumu wauaji waliojaza miili ya watoto waliokatwa-katwa katika vijia ndani ya makanisa ya Rwanda.

“Walikataa kujibu. Waliepa maswali, wakakasirika, sauti zao zikainuka juu hata zaidi, na chanzo cha ndani sana cha msiba wa Rwanda kikafunuliwa—washiriki wa vyeo vya juu zaidi vya kanisa Anglikana wakitenda kama wavulana wa kutumwa huku na huku na wanasiasa walio mabwana wakubwa ambao wamehubiri mauaji ya kimakusudi na mito kwa damu.”

Kwa kweli, makanisa ya Jumuiya ya Wakristo katika Rwanda hayana tofauti na makanisa kwingineko. Kwa mfano, kuhusu uungaji mkono wao kwa viongozi wa kisiasa katika Vita ya Ulimwengu 1, Jenerali-Brigedia Frank P. Crozier wa Uingereza alisema hivi: “Makanisa ya Kikristo ndiyo yenye kuchochea umwagaji wa damu zaidi ambayo tumetumia tutakavyo.”

Ndiyo, viongozi wa kidini wanalaumika sana kwa yale yaliyotendeka! National Catholic Reporter la Juni 3, 1994, liliripoti hivi: “Mapigano katika taifa hili la Afrika yanahusu ‘mauaji halisi na ya kweli ya kabila moja ambayo kwa kusikitisha, hata Wakatoliki wanahusika,’ akasema papa.”

Kwa wazi, makanisa yameshindwa kufundisha kanuni za kweli za Ukristo, zinazotegemea maandiko kama Isaya 2:4 na Mathayo 26:52. Kulingana na gazeti la Kifaransa Le Monde, padri mmoja aomboleza akisema: “Wanachinjana mmoja na mwenzake, wakisahau kwamba wao ni ndugu.” Padri mwingine Mrwanda alikiri hivi: “Baada ya karne ya kuhubiri upendo na msamaha, Wakristo wameua Wakristo wenzao. [Kuhubiri huko] hakukufaulu.” Le Monde liliuliza hivi: “Mtu aweza kukosaje kufikiri kwamba Watutsi na Wahutu waliokuwa vitani katika Burundi na Rwanda walizoezwa na wamishonari Wakristo walewale na kuhudhuria makanisa yaleyale?”

Wakristo wa Kweli Ni Tofauti

Wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo wanatii amri yake ya ‘kupendana.’ (Yohana 13:34) Je, waweza kuwazia Yesu au mmoja wa mitume wake akichukua upanga na kukatakata mtu mwingine hadi kifo? Mauaji mabaya kama hayo yanatambulisha watu kuwa “watoto wa Ibilisi.”—1 Yohana 3:10-12.

Mashahidi wa Yehova hawashiriki kamwe katika vita, mapinduzi, au magombano yoyote yaletwayo na wanasiasa wa ulimwengu, walio chini ya mwongozo wa Shetani Ibilisi. (Yohana 17:14, 16; 18:36; Ufunuo 12:9) Badala ya hilo, Mashahidi wa Yehova wanaonyeshana upendo wa kweli. Kwa hiyo, wakati wa mauaji hayo, Mashahidi Wahutu kwa hiari yao walitia maisha zao hatarini katika jitihada ya kuwaficha ndugu zao Watutsi.

Hata hivyo, misiba kama hiyo haipaswi kutushangaza. Katika unabii wa Yesu kuhusu “umalizio wa mfumo wa mambo,” yeye alitabiri hivi: “Ndipo watu . . . watawaua nyinyi.” (Mathayo 24:3, 9, NW) Kwa furaha, Yesu aahidi kwamba walio waaminifu watakumbukwa katika ufufuo wa wafu.—Yohana 5:28, 29.

Kwa wakati huu, Mashahidi wa Yehova katika Rwanda na kwingineko kote wameazimia kuendelea kujithibitisha kuwa wafuasi wa Kristo kwa kupendana. (Yohana 13:35) Upendo wao unatoa ushahidi hata kati ya magumu waliyo nayo sasa, kama vile ripoti inayoandama ya “Mashahidi Katika Kambi za Wakimbizi” ionyeshavyo. Sisi sote tunapaswa kukumbuka yale Yesu aliyosema katika unabii wake: “Mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.”—Mathayo 24:13.

[Sanduku katika ukurasa wa 29]

MASHAHIDI KATIKA KAMBI ZA WAKIMBIZI

Kufikia Julai mwaka huu, zaidi ya Mashahidi 4,700 pamoja na waandamani wao walikuwa katika kambi za wakimbizi. Katika Zaire, 2,376 walikuwa katika Goma, 454 katika Bukavu, na 1,592 katika Uvira. Kwa kuongezea, katika Tanzania walikuwamo wapatao 230 katika Benaco.

Kufikia vituo vya wakimbizi tu haikuwa rahisi. Kutaniko moja la Mashahidi 60 lilijaribu kuvuka daraja la Rusumo, njia iliyo kuu kuelekea kambi za wakimbizi katika Tanzania. Walipozuiliwa kupita, walitanga-tanga kando-kando ya mto kwa juma moja. Halafu wakaamua kujaribu kuvuka kwa mitumbwi. Walifaulu, na baada ya siku chache, walifika salama kwenye kambi katika Tanzania.

Mashahidi wa Yehova katika nchi nyinginezo walifanya mpango wa kutuma misaada kwa wingi. Mashahidi katika Ufaransa walichanga zaidi ya tani mia moja za mavazi na tani tisa za viatu, na vifaa hivyo, pamoja na vyakula na dawa, vilipelekwa katika sehemu zilizokuwa na uhitaji. Hata hivyo, kitu cha kwanza ambacho mara nyingi ndugu waliuliza katika kambi za wakimbizi kilikuwa Biblia au gazeti la Mnara wa Mlinzi au Amkeni!

Watazamaji wengi walivutiwa na upendo ambao Mashahidi katika Zaire na Tanzania walionyesha, waliowatembelea na kusaidia ndugu zao walioondoshwa. “Ninyi mmetembelewa na watu wa dini yenu,” wakimbizi wakasema, “lakini sisi hatujatembelewa na padri hata mmoja kutoka dini yetu.”

Mashahidi wakaja kujulikana sana kambini, hasa kwa sababu ya umoja, utaratibu, na hali yao nzuri ya kupendana. (Yohana 13:35) Ni jambo la kupendeza kutaja kwamba katika Benaco, Tanzania, iliwachukua Mashahidi dakika 15 tu kutafuta na kuwapata Mashahidi wenzao walio wakimbizi miongoni mwa watu wapatao 250,000 kambini.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki