Kuwatunza Majeruhi wa Msiba wa Rwanda
RWANDA, iliyo katika moyo wa Afrika, imeitwa “Uswisi wa Afrika.” Ujanijani wenye usitawi uonwao na watu wanaporuka juu ya nchi hiyo umewapa wazo la bustani ya Edeni. Si ajabu kwamba walikuwa wakiifafanua Rwanda kuwa paradiso.
Wakati mmoja, kwa kila mti uliokatwa, miwili ilipandwa. Siku moja kwa mwaka ilitolewa kwa urudishaji-misitu. Mitunda ilipandwa kandokando za barabara. Usafiri kotekote nchini ulikuwa huru na rahisi. Barabara kuu zilizounganisha zile wilaya mbalimbali na mji mkuu, Kigali, zilikuwa za lami. Mji mkuu huo ulikuwa ukivuvumuka. Mfanyakazi wa wastani alichuma fedha za kutosha mahitaji yake mwisho wa mwezi.
Utendaji wa Kikristo wa Mashahidi wa Yehova ulikuwa pia ukisitawi katika Rwanda. Mapema kidogo mwaka huu zaidi ya Mashahidi 2,600 walikuwa wakihusika katika kuipelekea habari njema ya Ufalme wa Mungu kwa idadi ya wananchi karibu milioni nane ambao sehemu kubwa yao ni Wakatoliki. (Mathayo 24:14) Katika Machi Mashahidi walikuwa wakiongoza zaidi ya mafunzo ya Biblia 10,000 katika nyumba za watu. Tena kulikuwa na makutaniko 15 ndani ya Kigali na sehemu zinazoizunguka.
Mwangalizi anayesafiri wa Mashahidi wa Yehova aliandika hivi: “Katika Novemba 1992, nilikuwa nikitumikia makutaniko 18. Lakini kufikia Machi 1994, yalikuwa yameongezeka kuwa 27. Idadi ya mapainia (wahudumu wa wakati wote) pia ilikuwa ikiongezeka kila mwaka.” Jumamosi, Machi 26, 1994, hudhurio kwenye Ukumbusho wa kifo cha Kristo lilikuwa 9,834.
Ndipo, ghafula, hali ikabadilika kimsiba katika Rwanda.a
Mwisho wa Ghafula kwa Utaratibu Uliothibitishwa
Aprili 6, 1994, karibu saa 2:00 usiku, marais wa Rwanda na Burundi, wote wawili wakiwa Wahutu, waliuawa katika anguko la ndege katika Kigali. Usiku huo filimbi za polisi zingeweza kusikiwa kila mahali katika mji mkuu, na barabara zilitiwa vizuizi. Ndipo katika saa za alfajiri, askari na wanaume wenye panga wakaanza kuua watu waliokuwa Watutsi. Ntabana Eugène—mwangalizi wa mji wa Mashahidi wa Yehova katika Kigali—mke wake, mwana wake, na binti yake wakawa miongoni mwa walio wa kwanza kuchinjwa ovyo.
Familia ya Wanaulaya ya Mashahidi wa Yehova ilikuwa imejifunza Biblia na majirani kadhaa waliokuwa Watutsi. Tisa kati ya majirani hawa walikimbilia kao la wale Wanaulaya huku wauaji wenye kichaa wakienda nyumba kwa nyumba. Mnamo dakika chache, waporaji 40 hivi wakawa ndani ya nyumba, wakivunja-vunja vitu na kupindua fanicha. Kwa kuhuzunisha, wale majirani Watutsi waliuawa. Hata hivyo, wale wengine, wajapofanya jitihada za kuokoa rafiki zao, waliruhusiwa kuponyosha uhai wao.
Machinjo hayo yaliendelea kwa majuma. Hatimaye Warwanda wakadiriwao kuwa 500,000 au zaidi waliuawa. Maelfu walikimbilia usalama wa uhai wao, hasa Watutsi. Ofisi ya tawi ya Zaire ya Mashahidi wa Yehova iliwajulisha akina ndugu katika Ufaransa uhitaji wao wa magawio ya kupunguza shida. “Tuliomba kibweta kimoja cha nguo zilizotumika,” laeleza tawi la Zaire. “Akina ndugu katika Ufaransa wametupelekea vibweta vitano ambavyo kwa kadiri kubwa ni vyenye nguo na viatu vipya.” Katika Juni 11, tani 65 hivi za mavazi zilipelekwa. Tawi la Kenya pia lilipelekea wakimbizi hao mavazi na dawa, na pia magazeti ya Mnara wa Mlinzi katika lugha yao ya kienyeji.
Kufikia Julai yale majeshi yenye kumilikiwa na Watutsi, yaitwayo Kikosi cha Uzalendo cha Rwanda, yalikuwa yameyashinda majeshi ya serikali yenye kumilikiwa na Wahutu. Baada ya hilo, Wahutu walianza kuikimbia nchi wakiwa mamia ya maelfu. Mchafuko ulitokea huku Warwanda milioni mbili au zaidi wakitafuta kimbilio katika kambi zilizoanzishwa kukurukakara katika nchi zilizo jirani.
Walijaribu Kusaidiana
Wawili kati ya sita waliofanya kazi katika Ofisi ya Tafsiri ya Mashahidi wa Yehova katika Kigali walikuwa Watutsi—Ananie Mbanda na Mukagisagara Denise. Jitihada za ndugu Wahutu za kuwalinda zilifanikiwa kwa majuma machache. Ingawa hivyo, kuelekea mwisho wa Mei 1994, Mashahidi wawili hawa Watutsi waliuawa.
Mashahidi wa Yehova walijaribu kulinda Wakristo wenzao wa malezi ya kabila tofauti, kwa kuhatarisha, hata kudhabihu, uhai wao wenyewe. (Yohana 13:34, 35; 15:13) Kwa kielelezo, Mukabalisa Chantal ni Mtutsi. Wakati washirika wa Kikosi cha Uzalendo cha Rwanda walipokuwa wakitafuta Wahutu katika uwanja wa michezo alimokuwa akikaa mwanamke huyo, yeye aliingilia kutetea rafiki zake Wahutu. Ingawa waasi hao waliudhiwa na jitihada zake, mmoja wao alisema hivi kwa mshangao: “Nyinyi Mashahidi wa Yehova kweli mna udugu madhubuti. Dini yenu ndiyo bora zaidi iliyopo!”
Kujiepusha na Chuki ya Kikabila
Hiyo si kusema kwamba Mashahidi wa Yehova hawawezi kamwe kuwa na chuki za kikabila ambazo zimekuwako kwa mamia ya miaka katika eneo hili la Afrika. Shahidi mmoja kutoka Ufaransa aliyekuwa akishiriki katika kazi ya kupunguzia watu shida alisema hivi: “Hata ndugu zetu Wakristo ni lazima watie jitihada kubwa kuepuka kuchafuliwa na chuki ile, ambayo imechangia machinjo ya ovyoovyo yasiyoelezeka.
“Tulikuta akina ndugu walioona familia zao zikichinjwa ovyoovyo mbele ya macho yao. Kwa kielelezo, dada Mkristo mmoja alikuwa amefunga ndoa siku mbili tu wakati mume wake alipouawa. Mashahidi fulani waliona watoto na wazazi wao wakiuawa. Dada mmoja, aliye katika Uganda sasa, aliona familia yake nzima ikichinjwa, kutia na mume wake. Hii yakazia wazi mateso, ya kihisia-moyo na ya kimwili pia, ambayo yamegusa kila familia ya Mashahidi wa Yehova.”
Kwa jumla, karibu Mashahidi 400 waliuawa katika ile jeuri ya kikabila. Hata hivyo hakuna yeyote wa hawa aliyeuawa na Mashahidi wenzake. Hata hivyo, washirika wa Watutsi na Wahutu wa makanisa ya Katoliki ya Kiroma na ya Kiprotestanti walichinja maelfu. Kulingana na uthibitisho wa kutosha, Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote hawashiriki sehemu yoyote ile katika vita, mapinduzi, au mapambano mengine kama hayo ya ulimwengu huu.—Yohana 17:14, 16; 18:36; Ufunuo 12:9.
Mateso Yasiyoelezeka
Kiangazi hiki kilichopita, watu kotekote ulimwenguni waliweza kuona taswira za macho juu ya mateso ya kibinadamu karibu yasiyoaminika. Mamia ya maelfu ya wakimbizi Warwanda walionwa wakimiminika kuingia nchi zilizo jirani na kukaa huko chini ya hali chafu fufufu. Mmoja wa Mashahidi wa Yehova kutoka Ufaransa aliye katika tume ya kupunguza shida aliieleza hali ambayo wajumbe wake waliona katika Julai 30 kama ifuatavyo.
“Tulikabiliwa na tamasha za maogofyo ya kupindukia. Kilometa baada ya kilometa, miili ilizagaa kwa mkururo barabarani. Makaburi ya kijumuiya yalijawa na maelfu ya mizoga. Uvundo uliokuwapo tukipita kati ya ule mtungo wa umayamaya wa watu ulikuwa usiovumilika, huku watoto wakicheza kando ya miili mifu. Kulikuwako mizoga ya wazazi ambao watoto wao walikuwa wangali hai wakiwa wamewashikilia migongoni. Tamasha hizo, zilizotokea tena na tena, zimekazika kikiki akilini. Mtu azidiwa na hisia ya kuwa hoi kabisa, asikose kugusika moyo kwa kadiri maogofyo na ukiwa huo ulivyo mkubwa.”
Wakati wakimbizi walipokuwa wakimiminika kwa makumi ya maelfu kuingia Zaire katikati ya Julai, Mashahidi katika Zaire walienda mpakani na kuinua vichapo vyao vya Biblia ili kwamba ndugu zao Wakristo na wenye kupendezwa waweze kuwatambua. Ndipo Mashahidi wakimbizi kutoka Rwanda walipokusanywa pamoja na kupelekwa kwenye Jumba la Ufalme katika Goma lililo karibu, walikoandaliwa utunzaji. Mashahidi wenye maarifa ya kitiba walijibidiisha kuupunguza msononeko wa walio wagonjwa, japo kukosekana kwa dawa za kutosha na vifaa vipasavyo.
Itikio la Haraka kwa Mateso
Ijumaa, Julai 22, Mashahidi wa Yehova katika Ufaransa walipokea wito wenye dharura wa kuokoa uhai uliopigwa faksi kutoka Afrika. Ulieleza shida kuu ya ndugu zao Wakristo wenye kuikimbia Rwanda. Mnamo dakika tano au kumi za kupokea kitaarifa hicho cha maandishi, akina ndugu waliamua kusheheneza ndege ya mizigo magawio ya kupunguzia shida. Hii iliongoza kwenye mwisho-juma wa matayarisho kabambe, hilo likisifika zaidi kwa sababu wao hawakuwa kamwe na maarifa ya kupanga jitihada kubwa hivyo ya kupunguza shida baada ya taarifa fupi hivyo.
Uhitaji wa kutoa fedha za kupunguza shida uliitikiwa kwa kadiri kubwa ajabu. Mashahidi katika Ubelgiji, Ufaransa, na Uswisi pekee walichanga zaidi ya dola 1,600,000. Vifaa vya kupunguzia shida vilinunuliwa, kutia na chakula, dawa, na zana za uokoaji, na kila kitu kikaingizwa katika masanduku na kutiwa vibandiko kwenye majengo ya Mashahidi wa Yehova katika Louviers, Ufaransa, na katika Brussels, Ubelgiji. Mashahidi walifanya kazi mchana na usiku kutayarisha safirisho hilo ili lipelekwe Ostend, Ubelgiji. Kwenye uwanja wa ndege huko, Jumatano, Julai 27, zaidi ya tani 35 zilipakiwa juu ya jeti ya mizigo. Kesho yake safirisho dogo zaidi, la magawio ya kitiba hasa, lilipelekwa. Jumamosi, siku mbili baadaye, safari nyingine ya ndege ilibeba magawio zaidi ya kitiba kwa ajili ya majeruhi.
Mashahidi kutoka Ufaransa, kutia na daktari wa kitiba, walienda Goma kutangulia lile safirisho kubwa. Jumatatu, Julai 25, wakati Dakt. Henri Tallet alipowasili katika Goma, karibu Mashahidi 20 walikuwa tayari wamekufa kutokana na kipindupindu, na wengine walikuwa wakifa kila siku. Kwa sababu ilikuwa lazima safirisho lile lipelekwe kupitia Bujumbura, Burundi, umbali upatao kilometa 250, halikuwasili katika Goma mpaka asubuhi ya Ijumaa, Julai 29.
Kukabiliana na Maradhi
Kwa wakati huo, Mashahidi wapatao 1,600 na rafiki zao walisongamana pamoja katika kisehemu cha ardhi kilichokuwa na lile Jumba la Ufalme dogo katika Goma. Kwa watu wote hawa, kulikuwako choo kimoja, bila maji, na chakula kidogo sana. Dazani za walioambukizwa kipindupindu walifinyana kwa wingi ndani ya Jumba la Ufalme. Idadi ya vifo ilikuwa ikipanda.
Kipindupindu hukausha mtu kabisa. Macho huwa ya kioo-kioo kisha huzunguka kutazama juu. Matibabu ya kurudisha maji mwilini yakianzwa kwa wakati, mtu huinuka tena katika muda wa siku mbili. Kwa hiyo, jitihada zilifanywa mara hiyo kutumia dawa kidogo iliyokuwapo kurudisha maji katika miili ya akina ndugu.
Kwa kuongezea, akina ndugu walijaribu kuwaweka kando wagonjwa na kuzuia wasiambukize wengine viini. Walijaribu kuhamisha wakimbizi hao kutoka hizo hali mbaya sana katika Goma. Mahali pafaapo palipatikana karibu na Ziwa Kivu, mbali na vumbi na mnuko wa mizoga uliokolea hewani.
Vyoo vilichimbwa, na sheria za kufuatilia sana kanuni za afya zikawekwa. Zilitia ndani kunawa mikono katika bakuli lenye blichi na maji baada ya kwenda chooni. Umaana wa hatua hizi ulikaziwa, na hao watu wakayakubali waliyotakwa wayafanye. Muda si muda ule msambao wa maradhi ulipunguzwa sana.
Wakati lile safirisho kubwa la magawio ya kupunguzia shida lilipowasili Ijumaa, Julai 29, hospitali ndogo ilianzishwa kwenye Jumba la Ufalme katika Goma. Vitanda kama 60 vya kupigia kambi vilisimamishwa, vilevile mfumo wa kutia maji dawa. Kwa kuongezea, mahema yalipelekwa kwa Mashahidi walio kwenye fukwe za Ziwa Kivu. Muda si muda, wakawa wamesimamisha mahema 50 katika safu zilizopangwa kwa unadhifu na utaratibu.
Wakati mmoja karibu Mashahidi 150 na rafiki zao walikuwa wagonjwa mahututi. Kufikia juma la kwanza la Agosti, zaidi ya 40 kati yao walikuwa wamekufa katika Goma. Lakini magawio na usaidizi wa kitiba yaliwasili kwa wakati kuokoa uhai wa wengi na kukomesha mateso makubwa.
Watu wa Kiroho Walio na Shukrani
Wakimbizi Mashahidi walionyesha shukrani isiyo na kipimo kwa yote waliyofanyiwa. Waliguswa na upendo ulioonyeshwa na ndugu zao Wakristo katika nchi nyinginezo na ile ithibati ya wazi kwamba kweli wao ni wa udugu wa kimataifa.
Japo magumu yao, wakimbizi hao wamedumisha hali yao ya kiroho. Kwa kweli, mtazamaji mmoja alisema kwamba “wao waonekana wakihangaikia zaidi kupokea chakula cha kiroho kuliko msaada wa vitu vya kimwili, ingawa wana shida kubwa ya kila kitu.” Nakala 5,000 za ule msaada wa kujifunzia Biblia Unaweza Kuishi Milele Katika Paradiso Duniani katika Kinyarwanda zilipelekwa, zilipoombwa, kwenye kambi mbalimbali za wakimbizi.b
Wakimbizi hao walichunguza andiko la Biblia kila siku, wakapanga kitengenezo mikutano ya kutaniko. Mipango ilifanywa pia kuongoza madarasa ya shule kwa ajili ya watoto. Walimu walitumia fursa ya madarasa haya kutoa mafunzo juu ya kanuni za afya, wakikazia kwamba kuokoka kulitegemea kuzishika.
Utunzaji Wenye Kuendelea Wahitajiwa
Mamia ya wakimbizi Mashahidi walikuwa mahali penginepo zaidi ya Goma, kama vile Rutshuru. Msaada wa jinsi ileile uliandaliwa ndugu hawa. Julai 31, wajumbe Mashahidi saba walisafiri kwa ndege kwenda kusini kutoka Goma hadi Bukavu, kulikokuwa na wakimbizi Mashahidi kama 450. Wengi wa hawa walikuwa wa kutoka Burundi pia. Kipindupindu kilikuwa kimezuka huko, na usaidizi uliandaliwa kwa jaribio la kuzuia vifo vyovyote miongoni mwa akina ndugu.
Kesho yake wajumbe hao walisafiri karibu kilometa 150 kwa barabara hadi Uvira, Zaire, kulikokuwa na karibu Mashahidi 1,600 njiani katika mahali saba hivi kutoka Rwanda na Burundi pia. Maagizo yaliandaliwa juu ya jinsi wangeweza kujilinda na maradhi. Ripoti moja iliyotolewa kwa msingi wa maono ya wajumbe hao ilisema: “Yale ambayo yamefanywa kufikia hapo ni mwanzo tu, na wale watu 4,700 wanaopokea usaidizi wetu sasa watahitaji msaada zaidi kwa muda wa miezi mingi.”
Mamia ya Mashahidi waripotiwa kuwa walirudi Rwanda kufikia Agosti. Hata hivyo karibu nyumba na mali zote zilikuwa zimeporwa. Kwa hiyo kuna kazi ngumu ya kujenga upya makao na Majumba ya Ufalme.
Watumishi wa Mungu waendelea kusali kwa juhudi kwa ajili ya wale ambao wameteseka vibaya sana katika Rwanda. Twajua kwamba kadiri mwisho wa mfumo huu wa mambo ukaribiavyo zaidi, jeuri huenda ikaongezeka. Hata hivyo, Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wataendelea kudumisha kutokuwamo kwao kwa Kikristo na kuonyesha huruma yao halisi.
[Maelezo ya Chini]
a Ona ile makala ya Mnara wa Mlinzi la Desemba 15, 1994, “Msiba Katika Rwanda—Ni Nani Anayelaumika?”
b Kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Ramani katika ukurasa wa 12]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
RWANDA
Kigali
UGANDA
ZAIRE
Rutshuru
Goma
Lake Kivu
Bukavu
Uvira
BURUNDI
Bujumbura
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kushoto: Ntabana Eugène na familia yake walichinjwa ovyo. Kulia: Mukagisagara Denise, Mtutsi, aliuawa, japo jitihada za ndugu Wahutu kumwokoa
[Picha katika ukurasa wa 17]
Juu: Kuwatunza wagonjwa kwenye Jumba la Ufalme kule Goma. Kushoto chini: Zaidi ya tani 35 za magawio ya kupunguza shida yaliyotayarishwa na Mashahidi na kupelekwa kwa jeti ya mizigo. Chini: Karibu na Ziwa Kivu, ambako Mashahidi walihamishiwa. Kulia chini: Wakimbizi Warwanda kwenye Jumba la Ufalme katika Zaire