Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Wafilisti wanaotajwa katika Biblia walikuwa nani?
Mara kwa mara Biblia hurejezea watu waitwao Wafilisti, walioishi katika Kanaani watu wa kale wa Mungu walipomiliki Bara Lililoahidiwa. Kwa muda mrefu, Wafilisti hawa wa kale walipinga watu wa Mungu, kama inavyoonyeshwa katika usimulizi wa pambano la Daudi na lile jitu hodari la Kifilisti lililoitwa Goliathi.—1 Samweli 17:1-3, 23-53.
Biblia yaonyesha kwamba Wafilisti wa kale walihama kutoka Kaftori hadi pwani ya kusini-magharibi mwa Kanaani. (Yeremia 47:4) Kaftori ilikuwa wapi? The International Standard Bible Encyclopedia (1979) hujulisha hivi: “Ingawaje hakuna uthibitisho wa kutosha ili kutoa jibu hakika, usomi wa kisasa huelekeza kwenye kisiwa cha Krete (au labda Krete pamoja na Visiwa Vidogo vya Aegea, ambavyo vina utamaduni unaofanana) kwa hakika kuwa mahali ilipokuwa.”—Buku 1, ukurasa 610.
Kwa kupatana na hili, New World Translation of the Holy Scriptures husomeka hivi katika Amosi 9:7: “‘Je, kwangu, ninyi si kama wana wa Wakushi, Enyi wana wa Israeli?’ ndio usemi wa Yehova. ‘Je, sikuleta Israeli yenyewe toka nchi ya Misri, na Wafilisti toka Krete, na Siria toka Kiri?’”
Haijulikani wakati wakale hawa wa bahari walipohama kutoka Krete hadi sehemu ya Kanaani iliyokuja kuitwa Filistia, ile pwani ya kusini-magharibi kati ya Jopa na Gaza. Yaonekana tayari walikuwa wamekuwapo katika sehemu hii ya nyanda za kipwani za chini katika siku za Abrahamu na Isaka.—Mwanzo 20:1, 2; 21:32-34; 26:1-18.
Wafilisti waliendelea kuwa wenye nguvu sana katika eneo hilo muda mrefu baada ya Israeli kuingia katika nchi aliyowaahidi Mungu. (Kutoka 13:17; Yoshua 13:2; Waamuzi 1:18, 19; 3:3, 4; 15:9, 10; 1 Samweli 4:1-11; 7:7-14; 13:19-23; 1 Wafalme 16:15) Wafilisti walibaki katika majiji yao Gathi, Yabne, na Ashdodi hadi wakati wa utawala wa mfalme wa Yudea Uzia. (2 Mambo ya Nyakati 26:6) Mengineyo ya majiji yao mashuhuri katika masimulizi ya Kibiblia yalikuwa Ekroni, Ashkeloni, na Gaza.
Aleksanda Mkuu alishinda jiji la Wafilisti la Gaza, na baada ya wakati fulani yaonekana Wafilisti walikoma kuwa watu wa kikundi kizima kilichojitenga. Profesa Lawrence E. Stager aliandika katika Biblical Archaeology Review (Mei/Juni 1991): “Wafilisti pia walipelekwa uhamishoni katika Babiloni. . . . Hata hivyo, hakuna rekodi iliyopo kuhusu kilichotukia kwa Wafilisti waliopelekwa uhamishoni. Wale ambao huenda waliweza kubaki katika Ashkeloni baada ya ushindi wa Nebukadreza labda walipoteza kabila lao. Taifa hilo lilitoweka katika historia.”
Jina la kisasa Palestina latolewa katika maneno ya Kilatini na Kigiriki, ambayo yaongoza nyuma zaidi kwenye neno la Kiebrania kwa “Filistia.” Tafsiri fulani za Biblia katika lugha ya Kiarabu hutumia neno fulani kwa “Wafilisti” ambalo kwa urahisi hueleweka kimakosa na neno kwa Wapalestina wa kisasa. Hata hivyo, Today’s Arabic Version hutumia neno tofauti la Kiarabu, hivyo kutofautisha kati ya Wafilisti wa kale na Wapalestina wa kisasa.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Baadhi ya magofu katika Ashkeloni
[Hisani]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.