Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w95 8/1 kur. 20-24
  • Urithi Wetu wa Kiroho Wenye Thamani Kubwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Urithi Wetu wa Kiroho Wenye Thamani Kubwa
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maisha ya Mapema ya Baba
  • Kwenda Afrika Mashariki
  • Kulelewa Kikristo kwa Upendo
  • Mwaminifu Hadi Mwisho
  • Wazazi Wetu Walitufundisha Kumpenda Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Urithi wa Kikristo Usio wa Kawaida
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Tulipewa Mradi Maishani
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Kufuatia Hatua za Wazazi Wangu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
w95 8/1 kur. 20-24

Urithi Wetu wa Kiroho Wenye Thamani Kubwa

KAMA ILIVYOSIMULIWA NA PHILLIP F. SMITH

“Nuru imewashwa ambayo itang’aa katika giza tititi la kiroho la Afrika.” Tulifurahi kama nini kusoma maneno yaliyoko hapo juu kwenye ukurasa 75 wa Kitabu-Mwaka cha Mashahidi wa Yehova 1994! Maneno hayo yaliandikwa na babu yetu, Frank W. Smith katika 1931, kwenye barua aliyomwandikia Ndugu Joseph F. Rutherford, aliyekuwa msimamizi wa Watch Tower Society wakati huo. Babu alikuwa ameandika akitoa ripoti juu ya safari yake ya kuhubiri aliyokuwa amefanya pamoja na ndugu yake.

HICHO Kitabu-Mwaka cha 1994 kilieleza hivi: “Gray Smith na kaka yake Frank, waliokuwa wahudumu mapainia wawili wajasiri kutoka Cape Town [Afrika Kusini], walifunga safari ya kwenda Afrika Mashariki ya Uingereza waone kama ingewezekana kutangaza habari njema. Walichukua gari aina ya De Soto walilokuwa wameligeuza kuwa la kulala pia, wakaliweka melini pamoja na katoni 40 za vitabu, na kuabiri kuelekea Mombasa, bandari ya Kenya.”

Katika barua yake kwa Ndugu Rutherford, babu alifafanua hivi safari ya kutoka Mombasa hadi Nairobi, mji mkuu wa Kenya: “Tulianza safari ya gari ambayo ndiyo safari yenye kuogopesha zaidi niliyopata kufunga. Ilituchukua siku nne, tukienda siku nzima, kumaliza kilometa 580 . . . Ilinibidi kutoka nje nikiwa na koleo na kulainisha miinuko kilometa baada ya nyingine, kujaza mashimo, na pia kukata nyasi na miti ili kujazia mabwawa ili magurudumu yasikwame.”

Baada ya kufika Nairobi, Frank na Gray walifanya kazi mfululizo kwa siku 21 wakigawanya fasihi zao za Biblia. “Kulingana na yale tunayosikia,” babu akaandika, “kazi yetu imeleta mvurugo miongoni mwa watu wa kidini katika Nairobi.” Baadaye, babu alitaka kurudi nyumbani kumwona mwanaye mwenye umri wa miaka miwili, Donovan, na mkeye, Phyllis, aliyekuwa na mimba ya mtoto wao wa pili, baba yetu, Frank. Babu alichukua meli ya kwanza iliyopatikana kutoka Mombasa, lakini akafa kwa malaria kabla ya kufika nyumbani.

Wakati dada yangu, ndugu yangu na mimi tulipokuwa tukitafakari juu ya masimulizi ya Kitabu-Mwaka hicho, tulimkumbuka baba yetu mpendwa. Katika 1991, miezi michache tu kabla ya kupokea hicho Kitabu-Mwaka cha 1992 cha Kiingereza, alikufa kutokana na matatizo ya upasuaji wa moyo. Ingawa hakumwona kamwe baba yake, alishiriki upendo wenye kina kirefu wa baba yake kwa Yehova. Babu angefurahi kama nini kujua kwamba miaka 28 baadaye, katika 1959, mwanaye angefuata hatua zake akiwa mhudumu Mkristo katika Afrika Mashariki!

Maisha ya Mapema ya Baba

Baba yetu alizaliwa Julai 20, 1931, katika Cape Town, miezi miwili baada ya kifo cha baba yake mwenyewe, ambaye alipewa jina lake. Baba alionyesha upendo wake kwa Yehova tangu umri wa mapema. Akiwa na umri wa miaka tisa tu, alikuwa akisimama kwenye stesheni kuu ya gari-moshi ya Cape Town akitoa ushahidi kwa kuvalia mabango huku wanashule wenzake wakimdhihaki. Akiwa na umri wa miaka 11, alifananisha wakfu wake kwa Yehova kwa ubatizo wa maji. Nyakati nyingine baba alikuwa akipewa mgao wa kutoa ushahidi katika barabara nzima akiwa peke yake. Kufikia wakati alipokuwa na umri wa miaka 18, alikuwa akiongoza Funzo la Mnara wa Mlinzi pamoja na kikundi cha dada Wakristo wazee-wazee katika kitongoji kimoja cha Cape Town.

Katika 1954 Watch Tower Society ilitangaza kwamba mikusanyiko ya kimataifa ilikuwa ifanyiwe Ulaya mwaka uliokuwa ukifuata. Baba alitamani sana kwenda, lakini hakuwa na pesa za kutosha kusafiri hadi huko kutoka Cape Town. Hivyo aliafikiana kufanya kazi kwa miezi mitatu akiwa mkemia kwenye migodi ya shaba katika Rhodesia ya Kaskazini (sasa Zambia). Mahali pa kupima mawe ya madini hizo palikuwa katika msitu wa Afrika.

Baba alijua kwamba kulikuwa na idadi kubwa za Mashahidi Waafrika katika Kaskazini mwa Rhodesia, hivyo alipofika aliwatafuta akawapata na kufahamu mahali walipofanyia mikutano yao. Ingawa hangeweza kusema lugha ya mahali hapo, bado yeye alishirikiana nao na kuhudhuria kwa ukawaida mikutano ya Kutaniko la Mine la Mashahidi wa Yehova. Wazungu kwenye migodi walikuwa wabaguzi wa rangi na walionyesha ubaguzi wao kwa kuwatukana Waafrika mara nyingi. Hata hivyo, sikuzote baba alikuwa mwenye fadhili.

Mwishoni mwa miezi hiyo mitatu, mfanyakazi Mwafrika ambaye hakuwa Shahidi alimwendea baba na kumuuliza hivi: “Unajua sisi hukuitaje?” Mtu huyo akatabasamu na kusema: “Sisi hukuita Bwana Watchtower.”

Katika 1955, baba aliweza kuhudhuria makusanyiko ya “Ufalme Wenye Ushindi” katika Ulaya. Huko alikutana na Mary Zahariou, ambaye alikuja kuwa mke wake mwaka uliofuata. Baada ya ndoa yao, walikaa katika Parma, Ohio, Marekani.

Kwenda Afrika Mashariki

Wakati wa mkusanyiko wa wilaya katika Marekani, wahudhuriaji walipewa mwaliko wa kutumikia mahali ambapo uhitaji wa wahudumu ulikuwa mkubwa zaidi. Wazazi wetu wakaamua kwenda Afrika Mashariki. Walifanya sawasawa na vile Watch Tower Society ilivyodokeza. Waliweka pesa za kutosha za kukata tiketi ya kwenda na kurudi ikiwa baba hangefanikiwa kupata kazi, kwa kuwa ni wale tu waliokuwa na kibali cha kazi walioruhusiwa kukaa katika eneo hilo.

Baada ya kupata pasipoti, viza, na chanjo, katika Julai 1959, baba na mama walisafiri kwa meli ya biashara kutoka New York City hadi Mombasa kupitia Cape Town. Safari hiyo iliwachukua majuma manne. Huko Mombasa gatini walipokea ukaribishaji mchangamfu kutoka kwa ndugu Wakristo waliokuwa wamewatangulia kutumikia mahali ambapo uhitaji ulikuwa mkubwa zaidi. Walipofika Nairobi, baba alipata barua ikimngoja. Ilikuwa jibu la ombi lake la kazi ya mkemia katika Idara ya Uchunguzi wa Mawe katika Entebbe, Uganda. Baba na mama wakapanda gari-moshi kwenda Kampala, Uganda, ambapo baba alihojiwa na kuajiriwa. Wakati huo, kulikuwa na Shahidi mwingine mmoja tu katika eneo la Entebbe na Kampala, George Kadu.

Serikali ya kikoloni ilimlipia baba ili ajifunze lugha ya huko, Kiluganda. Alifurahi, kwa kuwa hata hivyo alikuwa amepanga kujifunza lugha hiyo ili awe na matokeo zaidi katika huduma. Baadaye, baba hata alisaidia kutafsiri kijitabu “Habari Njema Hizi za Ufalme” kwa Kiluganda.

Baba hakuwa mwoga kuhubiria wengine. Alisema na Wazungu wote katika idara yake, naye alishiriki kwa ukawaida kuhubiria Waganda. Hata alimtolea ushahidi mkuu wa sheria Mwafrika wa Uganda. Mtu huyo alisikiliza ujumbe wa Ufalme na hata akawakaribisha baba na mama kwa chakula cha jioni.

Dada yangu, Anthe alizaliwa katika 1960, nami nikafuata katika 1965. Familia yetu ikawa na ukaribu sana na ndugu na dada katika kutaniko dogo lakini lenye kukua katika jiji kuu, Kampala. Tukiwa Mashahidi wazungu pekee karibu-karibu Entebbe, tulikuwa na maono yenye kuchekesha. Siku moja rafiki ya baba alikatisha safari yake na kutembelea Entebbe bila kutazamiwa akatafuta kukutana na baba. Hakufanikiwa hadi alipouliza: “Unajua mume na mke wazungu hapa walio Mashahidi wa Yehova?” Aliyeulizwa alimleta kwa gari moja kwa moja kwenye nyumba ya mama na baba.

Pia tulikuwa na maono magumu, kutia ndani kuvumilia mapinduzi mawili yenye kutumia silaha. Vikosi vya serikali wakati mmoja vilikuwa vikifyatulia risasi yeyote wa kikundi fulani cha kikabila. Siku nzima mchana na usiku, kulikuwa na kufyatua risasi kusikokoma. Kwa kuwa kulikuwa na mkatazo wa kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni hadi saa 12 asubuhi, mikutano ilifanywa wakati wa alasiri katika nyumba ya wazazi wangu katika Entebbe.

Baadaye, mkatazo huo ulipoondolewa, baba alitupeleka kwa gari Kampala tukafanye Funzo la Mnara wa Mlinzi. Mwanajeshi alitulenga bunduki, akasimamisha gari letu, na kusisitiza ajue tulikokuwa tukienda. Wakati huo nilikuwa kitoto kichanga tu, na Anthe alikuwa na umri wa miaka mitano. Baba alipoeleza kwa utulivu, huku akimwonyesha mwanajeshi huyo Biblia na fasihi zetu, akatuacha tuende.

Katika 1967, baada ya karibu miaka minane katika Uganda, wazazi wetu wakaamua kurudi Marekani kwa sababu ya matatizo ya afya na madaraka ya familia. Tukawa sehemu ya Kutaniko la Canfield, Ohio, ambapo baba alitumika akiwa mzee. Huko wazazi wangu wakaja kuwapenda sana ndugu kama walivyopenda kutaniko dogo la Kampala.

Kulelewa Kikristo kwa Upendo

Katika 1971 ndugu yangu David alizaliwa. Tulipokuwa tukikua, tulilelewa katika mazingira ya nyumbani yaliyojaa upendo na uchangamfu. Bila shaka hili lilitokana na uhusiano wenye upendo ambao wazazi wetu walionyeshana.

Tulipokuwa wachanga, sikuzote baba angetusomea hadithi ya Biblia wakati wa kulala, asali, na kisha, bila mama kujua, alitupatia chokoleti iliyofungwa kwa karatasi yenye kung’aa. Sikuzote, tulijifunza Mnara wa Mlinzi pamoja tukiwa familia hata iwe tuko wapi. Tukiwa katika likizo ya familia, siku moja tulijifunza Mnara wa Mlinzi kando ya milima na wakati mwingine tukiwa tunakabili bahari. Mara nyingi baba alisema kwamba hizo zilikuwa pindi zenye kumfurahisha zaidi. Alisema kwamba alionea huruma wale waliokosa shangwe kuu ambayo funzo la familia laweza kuleta.

Wakati wa kuonyesha upendo kwa Yehova, baba alifundisha kwa kielelezo. Wakati wowote nakala mpya ya gazeti la Mnara wa Mlinzi au Amkeni! ilipofika au wakati tungepokea kichapo kingine cha Mnara wa Mlinzi, baba alikuwa akikisoma chote kwa hamu nyingi. Tulijifunza kutoka kwake kwamba kweli za Biblia hazipaswi kuchukuliwa vivi hivi bali zapaswa kuheshimiwa kama hazina yenye thamani. Kitu chetu cha thamani sana ni Reference Bible ya baba. Kila ukurasa wayo umejaa maandishi yaliyotokana na kujifunza kwake. Sasa tusomapo kutoka kwa maandishi yake ya kando, ni kama twamsikia akitufundisha na kutushauri.

Mwaminifu Hadi Mwisho

Katika Mei 16, 1991, akiwa kwenye huduma ya shambani, baba alipatwa na maradhi ya ghafula ya moyo. Majuma kadhaa baadaye, alifanyiwa upasuaji wa moyo ambao ulionekana kuwa umefaulu. Hata hivyo, usiku uliofuata upasuaji huo, tulipokea simu kutoka hospitali. Baba alikuwa akitokwa damu, na madaktari walikuwa na wasiwasi sana. Alipelekwa kupasuliwa tena mara mbili usiku huo ili kujaribu kusimamisha damu lakini haikufaulu. Damu ya baba haikuwa ikitungama.

Siku iliyofuata, hali ya baba ilipozidi kuharibika, kwanza madaktari walimpeleka mama yangu kando kisha ndugu yangu mdogo kuwashurutisha wakubali baba atiwe damu mishipani. Hata hivyo, mbeleni baba alikuwa amewaambia madaktari kwamba hangekubali utiaji-damu mishipani chini ya hali zozote. Aliwaeleza sababu zake za Kimaandiko za kukataa damu lakini akasema angekubali vibadala visivyo vya damu.—Mambo ya Walawi 17:13, 14; Matendo 15:28, 29.

Uhasama mwingi wa upande wa washiriki wa wafanyakazi kadhaa wa kitiba ulileta hali yenye mkazo sana katika chumba cha utibabu wa dharura. Jambo hilo, pamoja na hali ya baba kuzidi kuwa mbaya, mara nyingine lilionekana kuwa zaidi ya yale tungeweza kuvumilia. Tulimsihi Yehova atupe msaada na pia kujaribu kutumia madokezo yenye kutumika tuliyokuwa tumepokea. Hivyo tulipotembelea chumba cha utibabu wa dharura, sikuzote tulikuwa tukivalia vizuri na wenye heshima kuelekea wafanyakazi wa tiba. Tulipendezwa sana na hali ya baba kwa kuuliza maswali yenye maana, nasi tulishukuru kila mfanyakazi aliyehusika na utunzaji wa baba.

Jitihada zetu hazikukosa kuonwa na wafanyakazi wa kitiba. Muda wa siku chache, hali yenye mkazo ilibadilika kuwa yenye fadhili. Wauguzi waliokuwa wakimtunza baba waliendelea kuchunguza maendeleo yake hata ingawa hawakuwa wakimtunza tena. Hata daktari mmoja aliyekuwa mbaya sana kwetu alinyenyekea kiasi cha kuuliza mama jinsi alivyokuwa akikabili hali. Kutaniko letu na watu wa ukoo pia walitutegemeza kwa upendo. Walipeleka chakula na kadi nyingi zenye kufariji, wakasali kwa niaba yetu.

Kwa kusikitisha, baba hakupona. Alikufa siku kumi baada ya upasuaji wake wa kwanza. Sisi twamwomboleza baba sana. Nyakati nyingine hisia za kumpoteza ni zenye nguvu kupita kiasi. Kwa furaha, Mungu wetu huahidi kwamba ‘siku kwa siku atatuchukulia mzigo wetu,’ nasi tumejifunza kumtegemea sana kuliko wakati mwingine wowote.—Zaburi 68:19.

Sote tumeazimia kwamba sisi pia tutaendelea kumtumikia Yehova kwa uaminifu ili tuje kupata shangwe ya kumwona baba katika ulimwengu mpya.—Marko 5:41, 42; Yohana 5:28; Matendo 24:15.

[Picha katika ukurasa wa21]

Frank Smith na mama yake, Phyllis, katika Cape Town

[Picha katika ukurasa wa22]

Baba na mama wakati wa harusi yao

[Picha katika ukurasa wa23]

Kwa ajili ya ubatizo wa kwanza katika Entebbe, ndugu walikodi kidimbwi cha chifu mmoja Mwafrika

[Picha katika ukurasa wa23]

Salamu ya kidesturi

[Picha katika ukurasa wa24]

Baba na mama muda mfupi kabla ya kifo cha baba

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki