Kataa Mapokeo Yasiyo ya Kimungu!
“KWELI itawaweka huru,” Yesu Kristo alisema. (Yohana 8:32) Ndiyo, Ukristo huweka watu huru—huru kutokana na utumwa wa ushirikina, huru kutokana na itikadi katika mafundisho na matumaini bandia, huru kutokana na matendo yenye kupotoka.
Hata hivyo, kama ilivyokuwa katika nyakati za kale, mara nyingi Wakristo leo hukabili mikazo ya kurudia mapokeo ya zamani. (Wagalatia 4:9, 10) Si kwamba desturi zote zinazopendwa zinadhuru. Kwa kweli, Mkristo aweza kuchagua kufuata desturi za kwao zinazofaa na zenye kuleta faida. Lakini desturi inapopinga Neno la Mungu, Wakristo hawaridhiani. Kwa sababu hiyo Mashahidi wa Yehova wanajulikana sana kwa kukataa kushiriki katika sherehe za Krismasi, siku za kuzaliwa, na desturi nyinginezo zinazopingana na Neno la Mungu.
Msimamo huo wenye moyo mkuu mara nyingi umetokeza dhihaka nyingi na upinzani mwingi kutoka kwa watu wanaofahamiana nao, majirani, na watu wa ukoo wasioamini. Ndivyo mambo yamekuwa hasa katika nchi fulani za Afrika, ambako mapokeo mengi mno hufuatwa katika maziko, harusi, na wakati wa kuzaliwa. Mikazo ya kusonga mtu ashiriki inaweza kuwa mikali sana—mara nyingi ikitia ndani matisho na matendo ya jeuri. Wakristo walioko huko wawezaje kusimama imara? Je, yawezekana kuepuka mkabiliano bila kuridhiana? Ili kujibu swali hilo, ebu tuchunguze jinsi Wakristo waaminifu wameshughulikia mapokeo fulani yasiyo ya Kimaandiko.
Desturi za Maziko za Kishirikina
Katika kusini mwa Afrika mna mapokeo mengi mno yanayohusu maziko na mazishi. Kwa kawaida wenye kufiwa hukesha usiku kucha—au usiku kadhaa—katika nyumba ya maombolezo, ambamo mna moto unaofanywa uwake daima. Wenye kufiwa hukatazwa kupika, kunyoa nywele, au hata kuoga mpaka maziko yawe yamefanywa. Baadaye, wanatakiwa kuoga wakitumia mchanganyiko maalumu wa mimea. Je, desturi kama hizo zakubalika kwa Wakristo? La. Hizo zaonyesha itikadi katika kutoweza kufa kwa nafsi na hofu isiyofaa ya wafu.
Mhubiri 9:5 lasema hivi: “Walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote.” Kujua kweli hiyo huweka mtu huru asiwe na hofu ya ‘roho za wafu.’ Lakini Mkristo afanye nini wakati watu wa ukoo wenye nia nzuri wanaposisitiza kwamba ashiriki katika desturi kama hizo?
Fikiria ono la Shahidi mmoja Mwafrika aitwaye Jane, aliyefiwa na babaye. Alipofika tu katika nyumba ya maziko, aliambiwa kwamba yeye na wengine wote wa familia yao wacheze dansi usiku kucha wakizunguka maiti ili watulize roho ya mfu huyo. “Niliwaeleza kwamba nikiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, siwezi kujiingiza katika matendo kama hayo,” asimulia Jane. “Hata hivyo, siku iliyofuata baada ya mazishi, watu wa ukoo walio wazee-wazee walisema kwamba walikuwa wanataka kuwaogesha washiriki wa familia iliyofiwa ili walindwe zaidi na roho ya yule aliyekufa. Tena nilikataa kushiriki. Na wakati uo huo, mama alitengwa kando katika nyumba fulani. Mtu yeyote aliyetaka kumwona alikuwa lazima anywe kwanza kileo fulani kilichotayarishwa kwa ajili ya jambo hilo.
“Nilikataa kujiingiza katika hayo yote. Badala ya hivyo nilienda nyumbani kutayarisha chakula, nilichopeleka katika nyumba ambayo mama alikuwa akikaa. Jambo hilo lilivunja moyo sana familia yetu. Watu wangu wa ukoo walifikiri sikuwa timamu akilini.” Na zaidi ya hayo, walimdhihaki na kumtakia mabaya, wakisema: “Kwa kuwa umekataa mapokeo yetu kwa sababu ya dini yako, utasumbuliwa na roho ya baba yako. Hata huenda usizae watoto.” Bado Jane akakataa kutishika. Matokeo yakawa nini? Yeye asema hivi: “Wakati huo nilikuwa na watoto wawili. Sasa nina sita! Hilo liliaibisha wale waliosema kwamba sitazaa tena.”
“Utakaso” wa Kingono
Desturi nyingine inahusu utakaso wa kidesturi baada ya kifo cha mume au mke. Mke afapo, familia yao itamletea mjane huyo shemeji yake au mwanamke mwingine mwenye ukoo wa karibu na mke wake aliyekufa. Ni lazima afanye ngono na mwanamke huyo. Ndipo anaweza kuoa mtu yeyote anayetaka. Na ndivyo ilivyo mume wa mwanamke anapokufa. Zoea hilo hufikiriwa kuwa linatakasa mume au mke anayebaki kutokana na “roho” ya mume au mke aliyekufa.
Mtu yeyote anayekataa kupitia “utakaso” huo hujihatarisha kupata ghadhabu ya watu wa ukoo. Anaweza kutengwa na kufanyiwa dhihaka na kutakiwa mabaya. Hata hivyo, Wakristo hukataa kufuata desturi hii. Wao wajua kwamba mbali na kutokuwa namna fulani ya “utakaso,” ngono nje ya ndoa ni uchafu machoni pa Mungu. (1 Wakorintho 6:18-20) Isitoshe, Wakristo wanapaswa kuoa “katika Bwana tu.”—1 Wakorintho 7:39.
Mwanamke mmoja Mzambia aitwaye Violet alipoteza mume wake. Baadaye, watu wa ukoo walimletea mtu fulani, wakisisitiza kwamba afanye ngono naye. Violet alikataa, akaadhibiwa kwa kukatazwa kuchota maji katika kisima cha umma. Pia alionywa asitembelee barabara kuu, asije akapata madhara. Lakini, alikataa kutishwa na watu wa ukoo au wanakijiji wenzake.
Baadaye Violet alipewa samansi na mahakama ya kwao. Huko alieleza kwa uthabiti sababu zake za Kimaandiko za kukataa kujihusisha na ngono haramu. Mahakama ikaamua kwa kumpendelea, ikisema kwamba haingemlazimu kushika desturi na mapokeo yaliyopinga itikadi zake. Kwa kupendeza, kukataa kwake katakata kuridhiana kulisaidia kupunguza mikazo juu ya Mashahidi wengine katika kijiji hicho ambao baadaye walikabili suala hilohilo.
Shahidi mwingine Mwafrika aitwaye Monika alivumilia mkazo kama huo baada ya mume wake kufa. Familia ya mtu huyo ilisisitiza impe mume mwingine. Asema Monika: “Nilikataa, nikiazimia kutii amri iliyo katika 1 Wakorintho 7:39.” Hata hivyo, mkazo haukupungua. “Walinitisha,” akumbuka Monika. “Walisema: ‘Ukikataa, hutaolewa tena.’ Wao hata walidai kwamba baadhi ya Wakristo wenzangu walikuwa wametakaswa kisiri kwa njia hiyo.” Hata hivyo, Monika alisimama imara. “Nilikaa nikiwa mseja kwa miaka miwili, baadaye nikaolewa katika njia ya Kikristo,” yeye asema. Sasa Monika anatumikia akiwa painia wa kawaida.
Kuharibika Mimba na Kuzaliwa kwa Watoto Wakiwa Wamekufa
Ni lazima Wakristo walio kusini mwa Afrika wakabili pia desturi zinazohusu hali za kuharibika mimba na za kuzaliwa kwa watoto wakiwa wamekufa. Matukio kama hayo yenye msiba hutukia kwa sababu ya kutokamilika kwa binadamu—si kwa sababu ya adhabu ya kimungu. (Warumi 3:23) Lakini mwanamke akiharibika mimba, mapokeo mengine ya Kiafrika husisitiza kwamba atendwe kama mtengwa wa jamii kwa muda fulani.
Hivyo, mwanamke mmoja ambaye aliharibika mimba majuzi alishangaa kuona Shahidi mmoja akielekea nyumba yake. Alipokaribia, akampaazia sauti: “Usije hapa! Kulingana na desturi yetu, mwanamke ambaye ametoka tu kuharibika mimba hapaswi kutembelewa.” Hata hivyo, Shahidi huyo alimwambia kwamba Mashahidi wa Yehova hupeleka ujumbe wa Biblia kwa watu wa namna zote na kwamba wao hawafuati desturi za kwao zinazohusu kuharibika mimba. Kisha akamsomea Isaya 65:20, 23, akieleza kwamba chini ya Ufalme wa Mungu kuharibika mimba na kuzaliwa kwa watoto wakiwa wamekufa hakutatukia. Basi, mwanamke yule akakubali funzo la Biblia nyumbani.
Desturi za kishirikina huenda pia zikaandamana na mazishi ya watoto waliozaliwa wakiwa wamekufa. Shahidi mmoja aitwaye Joseph alipohudhuria maziko hayo, aliambiwa kwamba wote waliokuwapo walikuwa lazima waoshe mikono yao katika mchanganyiko fulani wa mimea na kupaka dawa hiyo kifuani pao. Kufanya hivyo kulisemwa kuwa kulizuia “roho” ya kitoto hicho isirudi kuwadhuru. Joseph akakataa kwa staha, akijua fundisho la Biblia kwamba wafu hawawezi kudhuru walio hai. Lakini, bado wengine walijaribu kumkaza atumie dawa hiyo. Joseph akakataa tena. Walipoona msimamo usio na hofu wa Mkristo huyo, wengine waliohudhuria vilevile walikataa dawa hizo.
Epuka Mikabiliano, Lakini Simama Imara
Hofu ya wafu na ogofyo la kutengwa na jamii laweza kuwa kani zenye nguvu za kufanya mtu aridhiane. Mithali 29:25 yasema: “Kuwaogopa wanadamu huleta mtego.” Maono yanayotangulia yaonyesha ukweli wa sehemu ya mwisho ya mstari huu: “Bali amtumainiye BWANA atakuwa salama.”
Hata hivyo, mara nyingi mikabiliano yaweza kuepukwa. Kwa kielelezo, Mkristo akialikwa kwa maziko ya mtu wa ukoo, asingoje mpaka ajikute katika hali iwezayo kumlazimisha aridhiane. “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; bali wajinga huendelea mbele wakaumia.”—Mithali 27:12.
Ingekuwa jambo la hekima kuuliza kwa busara ni desturi zipi zitakazofuatwa. Ikiwa ni zile zinazokatazwa, Mkristo aweza kutumia fursa hiyo kueleza sababu inayomfanya asishiriki, akifanya hivyo “kwa upole na kwa hofu.” (1 Petro 3:15) Mkristo aelezapo kwa staha msimamo wake wenye msingi wa Biblia mapema, mara nyingi watu wake wa ukoo huwa na mwelekeo wa kustahi itikadi zake na kutokuwa na mwelekeo wa kumtisha.
Hata watu wa ukoo waitikie vipi, Mkristo hawezi kamwe kuridhiana kwa kufuata mapokeo yasiyomheshimu Mungu—hata atishwe au atendwe vibaya vipi. Tumewekwa huru kutokana na hofu ya kishirikina. Mtume Paulo alihimiza hivi: “Kwa ajili ya uhuru wa namna hiyo Kristo alituweka huru. Kwa hiyo simameni thabiti, na msijiache wenyewe kufungwa tena katika nira ya utumwa.”—Wagalatia 5:1, NW.
[Picha katika ukurasa wa29]
Watu wengi huamini kwamba mtu aliyetoka tu kufa aweza kuwa mjumbe na kupeleka ujumbe kwa watu wa ukoo waliokufa zamani sana