Wakathari—Je, Walikuwa Wakristo Wafia-Imani?
“WACHINJENI wote; Mungu atawajua walio Wake.” Katika siku hiyo ya kiangazi ya 1209, wakazi wa Béziers, katika kusini mwa Ufaransa, waliangamizwa katika machinjo makubwa. Mtawa wa kiume Arnold Amalric, aliyewekwa kuwa mjumbe rasmi wa papa akiwa kiongozi wa wakrusedi Wakatoliki, hakuwa na huruma. Watu wake walipouliza jinsi wangeweza kutofautisha kati ya Wakatoliki na wazushi, inaripotiwa kwamba alitoa jibu hilo maarufu lililonukuliwa hapo juu. Wanahistoria Wakatoliki huipuuza na kusema kwamba alijibu: “Msijali. Naamini ni wachache sana watageuzwa imani.” Hata jibu lake liwe lilikuwa nini, matokeo yalikuwa machinjo makubwa ya angalau wanaume, wanawake, na watoto 20,000 yaliyofanywa na wakrusedi wapatao 300,000 wakiongozwa na viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki.
Ni nini iliyotokeza machinjo hayo makubwa? Huo ulikuwa mwanzo tu wa ile Krusedi ya Waalbi ambayo Papa Innocent 3 alikuwa ameanzisha dhidi ya wale walioitwa eti wazushi katika mkoa wa Languedoc, kusini ya kati ya Ufaransa. Kabla ya kwisha miaka ipatayo 20 baadaye, yawezekana watu milioni moja—Wakathari, Wawaldo, na hata Wakatoliki wengi—walikuwa wamepoteza uhai wao.
Ukaidi wa Kidini Katika Ulaya ya Enzi za Kati
Ukuzi wa upesi wa biashara katika karne ya 11 W.K. ulileta mabadiliko makubwa katika mifumo ya kijamii na kiuchumi ya Ulaya ya enzi za kati. Miji ilichipuka ili kuipa makao idadi iliyokuwa ikiongezeka ya mafundi na wenye maduka. Hiyo ilitokeza hali ya kupata mawazo mapya. Ukaidi wa kidini ukakua sana katika Languedoc, iliyokuwa na staarabu yenye kuachilia mambo na yenye maendeleo kuliko sehemu yoyote ya Ulaya. Jiji la Toulouse katika Languedoc lilikuwa la tatu kwa utajiri katika Ulaya. Ulikuwa ulimwengu ambamo watunga-mashairi walisitawi, ambao baadhi ya mashairi yao yaligusia mambo ya kisiasa na kidini.
Akifafanua hali ya kidini katika karne za 11 na 12, Revue d’histoire et de philosophie religieuses chasema hivi: “Katika karne ya 12, kama ilivyo katika karne iliyopita, maadili ya makasisi, utajiri wao, hali yao ya kuweza kuhongwa, na ukosefu wao wa maadili, ziliendelea kutiliwa shaka, lakini ni mali zao na mamlaka yao, ushirikiano wao wa kisiri na wenye mamlaka wa kilimwengu, na utii wao kwao ndio hasa uliochambuliwa.”
Wahubiri wa Kuhama-hama
Hata Papa Innocent 3 alitambua kwamba ufisadi mwingi sana katika kanisa ndio uliosababisha idadi yenye kuongezeka ya wahubiri wakaidi wenye kuhama-hama katika Ulaya, hasa katika kusini mwa Ufaransa na kaskazini mwa Italia. Wengi wao walikuwa ama Wakathari ama Wawaldo. Aliwashutumu makasisi kwa kutofundisha watu, akisema: “Watoto wanataka mkate ambao nyinyi hamjali kuwavunjia.” Lakini, badala ya kuendeleza kufundisha watu Biblia, Innocent alidai kwamba “Maandiko ya kimungu yana kina kirefu sana hivi kwamba si watu wa kawaida na wasio na elimu tu, bali pia hata watu wenye akili na waliosoma, hawawezi kujaribu kuyaelewa.” Watu wote walipigwa marufuku kusoma Biblia ila makasisi, nao waliruhusiwa kuisoma katika Kilatini pekee.
Ili kukinza mahubiri ya kuhama-hama ya wenye kukaidi, papa aliidhinisha kuanzishwa kwa Jamii ya Watawa Wahubiri, au Wadominika. Wakiwa tofauti na makasisi matajiri wa Katoliki, watawa hawa walikuwa wawe wahubiri wenye kusafiri waliopewa utume wa kutetea mafundisho ya kawaida ya Katoliki dhidi ya “wazushi” katika kusini mwa Ufaransa. Papa pia alituma wajumbe wake rasmi ili kusababu na Wakathari na kujaribu kuwarudisha katika Ukatoliki. Kwa kuwa jitihada hizo hazikufua dafu, na kwa kuuawa kwa mmoja wa wajumbe wake, yasemekana na mzushi mmoja, Innocent 3 aliamuru ile Krusedi ya Waalbi katika 1209. Albi ulikuwa mojawapo miji ambamo Wakathari walikuwa wamejaa hasa, kwa hiyo waandikaji wa matukio ya kanisa walirejezea Wakathari kuwa Waalbi (Kifaransa, Albigeois) na kutumia jina hilo kutaja “wazushi” wote katika eneo hilo, kutia ndani Wawaldo. (Ona sanduku iliyo chini.)
Wakathari Walikuwa Watu Gani?
Neno “kathari” latokana na neno la Kigiriki ka·tha·rosʹ, limaanishalo “takata.” Tangu karne ya 11 hadi 14, mafundisho ya Wakathari yalienea hasa katika Lombardy, kaskazini mwa Italia, na katika Languedoc. Itikadi za Wakathari zilikuwa mchanganyiko wa imani ya uwili ya sehemu za Mashariki na kwamba chochote kilichoumbwa ni kiovu, ambazo labda zililetwa na wafanyabiashara na wamishonari kutoka nchi za kigeni. The Encyclopedia of Religion chafafanua imani ya uwili ya Wakathari kuwa itikadi ya “kanuni mbili: moja nzuri, ikiongoza mambo yote ya kiroho, na ile nyingine ovu, ikitokeza ulimwengu halisi, kutia ndani mwili wa binadamu.” Wakathari waliamini kwamba Shetani aliumba ulimwengu halisi, ambao ulipewa hukumu ya uangamizo isiyoweza kubadilishwa. Tumaini lao lilikuwa kuepuka ulimwengu halisi wenye uovu.
Wakathari walijigawanya katika jamii mbili, wakamilifu na waamini. Wale wakamilifu walifanywa kuwa wakamilifu kwa sherehe fulani ya ubatizo wa kiroho, ulioitwa consolamentum. Hiyo ilifanywa kwa kuwekewa mikono, baada ya kuchunguzwa kwa mwaka mmoja. Sherehe hiyo ilifikiriwa kuwa yamwondoa mtu huyo kutoka kwa utawala wa Shetani, yamtakasa kutoka kwa dhambi zote, na kumpa roho takatifu. Hiyo ilitokeza mtajo huo “wakamilifu,” uliotumiwa kurejezea idadi ndogo kwa kulinganisha ya walio bora waliotumikia wakiwa wahudumu kwa waamini. Wakamilifu waliweka nadhiri za maisha ya kujinyima, utakaso, na umaskini. Ikiwa walikuwa wameoa au kuolewa, ilikuwa lazima mkamilifu aache mke wake au mume wake, kwa kuwa Wakathari waliamini kwamba ngono ilikuwa ndiyo dhambi ya kwanza.
Waamini walikuwa watu ambao, ingawa hawakufuata mtindo-maisha wa kujinyima, bado walikubali mafundisho ya Wakathari. Kwa kupiga magoti kwa heshima ya yule mkamilifu katika sherehe iliyoitwa melioramentum, mwamini aliomba msamaha na baraka. Ili waweze kuishi maisha ya kawaida, waamini walifanya convenenza, au mapatano, pamoja na wakamilifu ya kupewa ubatizo wa kiroho au consolamentum, wanapoelekea kufa.
Mtazamo Kuelekea Biblia
Ingawa Wakathari walinukuu sana Biblia, waliiona hasa kuwa chanzo cha mafumbo na hekaya. Wao walifikiri kwamba sehemu kubwa ya Maandiko ya Kiebrania ilitokana na Ibilisi. Wao walitumia sehemu za Maandiko ya Kigiriki, kama vile maandiko yanayotofautisha mwili na roho, kuunga mkono falsafa yao ya uwili. Katika Sala ya Bwana, walisali kwa ajili ya “mkate wa kiroho” badala ya “mkate wetu wa kila siku,” kwa kuwa mkate halisi ulikuwa mwovu machoni pao.
Mafundisho mengi ya Wakathari yalipinga Biblia moja kwa moja. Mathalani, wao waliamini katika nafsi isiyoweza kufa na hali ya kuzaliwa upya katika umbo jingine. (Linganisha Mhubiri 9:5, 10; Ezekieli 18:4, 20.) Pia walitegemeza mafundisho yao katika maandiko ya kiapokrifa. Hata hivyo, maadamu Wakathari walitafsiri sehemu za Maandiko katika lugha yao, kwa kadiri fulani, walifanya Biblia iwe kitabu kilichojulikana zaidi katika Enzi za Kati.
Si Wakristo
Wale wakamilifu walijiona kuwa waandamizi halali wa mitume, wakajiita “Wakristo,” wakikazia jina hilo kwa kuongezea maneno “wa kweli” au “wazuri.” Hata hivyo, kwa kusema kweli, itikadi nyingi za Wakathari zilikuwa za kigeni kwa Ukristo. Ingawa Wakathari walimtambua Yesu kuwa Mwana wa Mungu, wao walikataa kule kuja kwake katika mwili na dhabihu yake ya kukomboa. Wakifasiri vibaya shutumu la Biblia juu ya mwili na ulimwengu, wao waliona vitu vyote vilivyoumbwa kuwa vyatokana na uovu. Basi, wao walisisitiza kwamba Yesu angeweza tu kuwa na mwili wa kiroho na kwamba alipokuwa duniani yeye alionekana tu kuwa na mwili halisi. Kama ilivyokuwa kwa wakana-imani wa karne ya kwanza, Wakathari walikuwa “hawaungami Yesu Kristo kuwa alikuja katika mwili.”—2 Yohana 7, NW.
Katika kitabu chake Medieval Heresy, M. D. Lambert aandika kwamba mafundisho ya Wakathari “yalibadili maadili ya Ukristo kuwa maisha ya kujinyima kwa lazima, . . . yakaondoa kabisa ukombozi kwa kukataa kukiri uwezo wa kuokoa wa [kifo cha Kristo].” Yeye aona kwamba “wakamilifu hao walivutiwa hasa na walimu wenye maisha ya kujinyima wa Mashariki, wale watawa wa kibuddha na wahindu wenye kuhama-hama wa China au India, wale wastadi wa mafumbo ya Kiofiri, au wafundishao kwamba kitu chochote kilicho halisi kilikuwa kiovu.” Katika itikadi ya Wakathari, wokovu haukutegemea dhabihu ya fidia ya Yesu Kristo, bali ulitegemea consolamentum, au ubatizo wa kuingia katika roho takatifu. Basi, kwa wale waliotakaswa, kifo kingeleta ondoleo la mwili.
Krusedi Isiyo Takatifu
Watu wa kawaida, wakichoshwa na matakwa yenye kupunja ya makasisi na upotovu wenye kuenea sana, walivutiwa na njia ya maisha ya Wakathari. Wakamilifu walilinganisha Kanisa Katoliki na viongozi walo na “sinagogi la Shetani” na “mama wa makahaba” wa Ufunuo 3:9 na 17:5. Mafundisho ya Wakathari yalikuwa yakisitawi sana na kuondoa kanisa kusini mwa Ufaransa. Itikio la Papa Innocent 3 lilikuwa ni kuanzisha na kutegemeza kifedha ile iliyoitwa Krusedi ya Waalbi, hiyo ikiwa krusedi ya kwanza iliyopangwa katika Jumuiya ya Wakristo dhidi ya watu waliodai kuwa Wakristo.
Kupitia barua na wajumbe rasmi, papa aliwanyanyasa wafalme, wafalme wadogo, na wakuu wa Ulaya waliokuwa Wakatoliki. Aliahidi kusamehewa dhambi na utajiri wa Languedoc kwa wale wote ambao wangepiga vita vya kuondosha kabisa ule uzushi “kwa njia yoyote ile.” Mwito wake haukupuuzwa. Wakiongozwa na viongozi wakuu na watawa wa Katoliki, jeshi lililochangamana la wakrusedi kutoka kaskazini mwa Ufaransa, Flanders, na Ujerumani lilielekea kusini kupitia Bonde la Rhône.
Uharibifu wa Béziers ulianzisha vita vya ushindi vilivyoteketeza kabisa Languedoc kwa moto na machinjo yasiyozuilika. Albi, Carcassonne, Castres, Foix, Narbonne, Termes, na Toulouse zote ziliangushwa na wakrusedi hao wenye tamaa ya kumwaga damu. Katika ngome za Wakathari kama vile Cassès, Minerve, na Lavaur, mamia ya wale wakamilifu walichomwa mtini. Kulingana na mtawa mmoja mwandika-matukio Pierre des Vaux-de-Cernay, wakrusedi ‘walichoma wale wakamilifu wakiwa hai, huku wakishangilia mioyoni mwao.’ Katika 1229, baada ya miaka 20 ya mapigano na uharibifu, Languedoc ilikuja kuwa chini ya Utawala wa Ufaransa. Lakini machinjo hayakuwa yameisha kamwe.
Baraza la Kuhukumu Wazushi Latoa Pigo la Mwisho
Katika 1231, Papa Gregory 9 alianzisha Baraza la Kuhukumu Wazushi ili kuunga mkono vile vita.a Njia iliyotumiwa na baraza hilo kwanza ilitegemea shutumu na vifungo na, baadaye, mateso makali. Kusudi lalo kuu lilikuwa kuondosha kabisa yale ambayo upanga ulishindwa kuangamiza. Mahakimu wa Baraza la Kuhukumu Wazushi—wengi wao wakiwa watawa wa Kidominika na wa Kifransiska—waliwajibika kwa papa peke yake. Kifo kwa kuchomwa kilikuwa adhabu rasmi ya uzushi. Ushupavu na ukatili wa wahukumu wa baraza hilo ulikuwa mbaya kiasi cha kwamba maasi yalizuka Albi na Toulouse, miongoni mwa sehemu nyinginezo. Katika Avignonet, washiriki wote wa Baraza la Kuhukumu Wazushi walichinjwa.
Katika 1244 kusalimu amri kwa ngome iliyokuwa mlimani ya Montségur, iliyokuwa kimbilio la mwisho la wakamilifu wengi, kulikuwa pigo la mwisho kwa mafundisho ya Wakathari. Wanaume kwa wanawake wapatao 200 walikufa kwa kuchomwa kwa wingi kwenye mti. Katika miaka iliyofuata, Baraza la Kuhukumu Wazushi liliwasaka Wakathari waliosalia. Inaripotiwa kwamba Mkathari wa mwisho alichomwa kwenye mti katika Languedoc katika 1330. Kitabu Medieval Heresy chasema hivi: “Kuanguka kwa mafundisho ya Wakathari kulikuwa utimizo mkubwa zaidi wa Baraza la Kuhukumu Wazushi.”
Kwa hakika Wakathari hawakuwa Wakristo wa kweli. Lakini je, uchambuzi wao wa Kanisa Katoliki ulistahili kule kuangamizwa kwao kwa njia ya ukatili na wale waitwao eti Wakristo? Wanyanyasi wao na wauaji wao kimakusudi waliokuwa Wakatoliki hawakuheshimu Mungu na Kristo nao waliwakilisha vibaya Ukristo wa kweli walipotesa na kuchinja yale makumi ya maelfu ya wakaidi.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari zaidi juu ya Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi katika enzi za kati, ona “Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi Yenye Kuogofya” katika Amkeni! la Aprili 22, 1986, Kiingereza, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., kurasa 20-23.
[Sanduku katika ukurasa wa 28]
WAWALDO
Kuelekea mwisho wa karne ya 12 W.K., Pierre Valdès, au Peter Waldo, mfanya biashara tajiri wa Lyons, alidhamini kifedha tafsiri za kwanza za sehemu za Biblia katika lahaja kadhaa za Kiprovençal, lugha ya wenyeji iliyosemwa katika kusini na kusini-mashariki mwa Ufaransa. Akiwa Mkatoliki mnyoofu, aliacha biashara yake na kujitoa kuhubiri Gospeli. Wakiudhiwa na makasisi wenye ufisadi, Wakatoliki wengine wengi walimfuata na kuwa wahubiri wa kuhama-hama.
Upesi Waldo alikabili uhasama kutoka kwa makasisi wa kwao, waliomwomba papa ampige marufuku asitoe ushahidi peupe. Inaripotiwa kwamba jibu lake lilikuwa: “Tunapaswa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” (Linganisha Matendo 5:29.) Kwa sababu ya udumifu wake, Waldo aliondolewa kanisani. Wafuasi wake, walioitwa Wawaldo, au Watu Maskini wa Lyons, walijaribu kwa bidii kufuata kielelezo chake, wakihubiri wawili-wawili katika nyumba za watu. Kufanya hivyo kulitokeza mwenezo wa haraka wa mafundisho yao kotekote kusini, mashariki, na sehemu za kaskazini mwa Ufaransa, na vilevile kaskazini mwa Italia.
Wao hasa walihubiri kurudia itikadi na matendo ya Ukristo wa mapema. Waliteta dhidi ya purgatori, sala kwa wafu, ibada ya Mariamu, sala kwa “watakatifu,” ibada ya kisalaba, kusamehewa dhambi na makasisi, Ukaristo, na ubatizo wa vitoto, miongoni mwa mafundisho mengine.b
Mafundisho ya Wawaldo yalitofautiana kabisa na mafundisho yasiyo ya Kikristo ya uwili ya Wakathari, ambao mara nyingi watu waliwachanganya nao kimakosa. Hali hiyo ya kuchanganyikiwa hasa ilitokezwa na wapinzani wakali Wakatoliki waliojaribu kuchanganya kimakusudi mahubiri ya Wawaldo na mafundisho ya Waalbi, au Wakathari.
[Maelezo ya Chini]
b Kwa habari zaidi juu ya Wawaldo, ona makala “Wawaldo—Wazushi au Watafuta-Kweli?” katika Mnara wa Mlinzi la Agosti 1, 1981, kurasa 12-15, Kiingereza.
[Picha katika ukurasa wa29]
Watu elfu saba walikufa katika Kanisa la St. Mary Magdalene katika Béziers, ambako wakrusedi waliwachinja wanaume, wanawake, na watoto 20,000