Wale Watunga-Mashairi wa Zamani—Si Waimbaji Tu wa Nyimbo za Mapenzi
MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UFARANSA
WALE watunga-mashairi wa zamani walioitwa troubadour na wachezaji waliokuwa wahamaji—ni nini huja akilini mwako unaposikia maneno hayo? Labda nyimbo zinazohusu upendo mstahifu na za uungwana. Haujakosea, lakini kuna mengi zaidi yanayohusu watunga-mashairi kuliko hayo. Ingawa huenda walijulikana vizuri zaidi kwa ajili ya canso d’amor, au wimbo wa mapenzi—na hivyo mara nyingi huchorwa wakiwa na udi mkononi, wakiliwaza kwa wimbo mwanamke fulani—upendo haukuwa ndio hangaiko lao pekee. Hao watunga-mashairi walihusika katika masuala mengi ya kijamii, kisiasa, na ya kidini ya siku yao.
Hao watunga-mashairi walisitawi katika karne ya 12 na 13, kotekote katika eneo ambalo sasa ni kusini mwa Ufaransa. Walikuwa washairi-waimbaji ambao waliandika katika iliyokuwa lugha ya wenyeji sanifu zaidi kati ya lugha zote za Kiroma. Iliitwa langue d’oca—lugha ya kawaida iliyosemwa karibu Ufaransa kote kusini mwa Mto Loire na maeneo yanayopakana na Italia na Hispania.
Asili ya neno “troubadour” imejadiliwa sana, lakini linaonekana lilichimbuka kutokana na kitenzi cha Occitan trobar, kinachomaanisha “kutunga, buni, au pata.” Hivyo, troubadour wangeweza kupata neno lililo sahihi au lifanyalo kina ili kufaa shairi lao sanifu. Muziki uliandikwa ili kufaa ushairi wao, na kwa hiyo ungeweza kuimbwa. Wakisafiri kutoka mji hadi mji, mara nyingi wakiandamana na waimbaji stadi walioitwa jongleurs, hao watunga-mashairi waliimba nyimbo zao wakiwa na kinubi, fidla, filimbi, udi, au gitaa. Katika ukumbi wa matajiri na vilevile katika mahali pa soko au kwenye mashindano, maonyesho, misherehekeo, au karamu, mchezo wa uimbaji kwa kawaida ulikuwa sehemu ya vitumbuizo vyovyote rasmi.
Malezi Tofauti
Hao watunga-mashairi walitoka katika malezi ya namna mbalimbali. Wengine walizaliwa kutoka kwa familia mashuhuri; wachache walikuwa wafalme; na wengine walikuwa wa uzawa wa hali ya chini na kupanda kufikia daraja la kuwa watunga-mashairi. Baadhi yao walifikia hadhi kubwa. Wengi walikuwa wamesoma sana na kusafiri kwa mapana. Wote walipokea mazoezi ya hali ya juu katika kanuni za kuheshimu wanawake, adabu, ushairi, na muziki. Chanzo kimoja husema kwamba mtunga-mashairi mzuri alitarajiwa “ajue kikamilifu habari zote za wakati uliopo, arudie tasnifu zote zilizo mashuhuri za vyuo vikuu, afahamiane vizuri na kashfa za nyumba ya mfalme, . . . aweze kutunga mashairi kwa bwana au bibi kwa taarifa ya muda mfupi sana, na aweze kucheza angalau ala mbili zilizopendelewa katika nyumba ya mfalme wakati huo.”
Maendeleo ya biashara katika karne ya 12 yalileta mali nyingi kwa maeneo ya kusini mwa Ufaransa. Pamoja na ufanisi ulikuja wasaa wa mapumziko, elimu, na ukuzi wa mapendezi kwa ajili ya sanaa na maisha yenye kupendeza. Mabwana wakubwa na mabibi wa Languedoc na Provence walikuwa walezi wenye kujitoa zaidi wa hao watunga-mashairi. Washairi walistahiwa sana na wakaja kuwa na uvutano mkubwa juu ya mapendezi, mtindo, na adabu za makabaila. Wakawa waanzilishi wa bwalo la dansi ya Ulaya. Hata hivyo, The New Encyclopædia Britannica husema kwamba, “mafanikio yao makubwa yalikuwa kutokeza miongoni mwa mabibi wa nyumba ya mfalme hali inayoashiria mema yenye usalama wa kwamba hakuna kitu chochote kilichokuwa kinakaribia.”
Staha Mpya kwa Wanawake
Wakati mwanamume anapofungulia mwanamke mlango, anapomsaidia kuvaa koti lake, au kufanya hisani yoyote ya “kutanguliza wanawake” ambazo zimeshikiliwa kwa karne nyingi katika Ulaya Magharibi, huwa anaendeleza desturi inayoelekea kuwa ilianzishwa na hao watunga-mashairi.
Mitazamo ya enzi za kati kuelekea wanawake iliathiriwa sana na mafundisho ya kanisa, ambayo yaliwaona wanawake kuwa ndio waliosababisha mwanamume kutenda dhambi na kufukuzwa kutoka kwenye Paradiso. Alionwa kuwa mshawishi, chombo cha Ibilisi, uovu ambao mwanamume hangeweza kuishi bila huo. Mara nyingi ndoa ilifikiriwa kuwa hali iliyoshuka ya maisha. Sheria ya kanisa iliruhusu kupigwa kwa mke na kutengana, ikichangia kutwezwa kwa mwanamke na kutumikishwa. Karibu katika mambo yote, mwanamke alionwa kuwa hafifu alipolinganishwa na mwanamume. Lakini kuja kwa hao watunga-mashairi kulianza kubadili maoni ya wanaume.
Mtunga-mashairi wa kwanza aliyejulikana alikuwa William wa Tisa, Dyuki wa Aquitaine. Ushairi wake ulikuwa wa kwanza kuwa na sehemu muhimu ambazo zilijulisha wazo la kipekee la upendo wa hao watunga-mashairi, ambalo lilikuja kuitwa upendo mstahifu. Washairi wa Provençal waliuita verai’amors (upendo halisi) au fin’amors (upendo bora). Yalikuwa mapinduzi, kwa kuwa mwanamke sasa hakushikilia tena cheo hafifu na cha kudhalilishwa sana kwa mwanamume.
Ushairi wa hao watunga-mashairi ulimpa mwanamke adhama kubwa, heshima, na staha. Akawa mfano halisi wa tabia nzuri na sifa zenye wema adili. Nyimbo fulani ziliombolezea ubaridi wa mwanamke kuelekea kushangilia kwa mshairi. Angalau katika nadharia, upendo wa mtunga-mashairi ulipaswa kubaki ukiwa safi kiadili. Mradi wake wa msingi haukuwa kumpata mwanamke lakini, badala yake, ule utakaso wa kiadili ambao ungechochewa ndani yake na upendo kumwelekea. Ili kujifanya astahili, mshairi mwenye lengo la kumpata, alilazimika kusitawisha unyenyekevu, kujidhibiti, subira, uaminifu-mshikamanifu, na sifa zote njema ambazo mwanamke huyo alikuwa nazo. Hivyo, hata mwanamume aliye na utovu mkubwa sana wa adabu angebadilishwa na upendo.
Hao watunga-mashairi waliamini kwamba upendo mstahifu ulikuwa chanzo cha utakaso wa kijamii na kiadili, kwamba vitendo vya kiungwana na matendo mazuri asili yao ni upendo. Wazo hili liliposambazwa, likawa msingi wa aina ya mwenendo, ambao, baada ya muda, ulipenya ndani ya matabaka ya jamii ya kawaida. Tofauti na jamii ya kikabaila ambayo ilikuwa imekosa tabia na ya kinyama, njia mpya ya maisha ilikuwa imeanza. Wanawake sasa walitarajia wanaume wao wawe wenye kujidhabihu, wenye ufikirio, na wenye fadhili—wawe waungwana.
Upesi, sehemu nyingi za Ulaya zikaanza kufuatia sanaa ya hao watunga-mashairi. Hispania na Ureno zilikubali mawazo yao. Kaskazini mwa Ufaransa ikawa na shule zake za watunga-mashairi; Ujerumani ikawa na washairi wake; Italia, trovatori zake. Mawazo ya hao watunga-mashairi ya upendo mstahifu, yakiunganishwa na mawazo ya uungwana, yalitokeza mtindo wa fasihi unaojulikana kama mahaba.b Kwa kielelezo, kuchanganya ule upendo mstahifu ulio bora pamoja na hekaya za lugha ya Celtic ya Brittany, mtunga-mashairi Chrétien de Troyes alionyesha kwa muhtasari ubora wa ukarimu na kukingwa kwa walio dhaifu katika hadithi za Mfalme Arthur na Waheshimiwa walioketi kwenye meza moja na mfalme.
Athari Yake ya Kijamii
Ingawa nyimbo nyingi za hao watunga-mashairi zilisifu ubora wa upendo mstahifu, nyingine zilishughulika na masuala ya kijamii na ya kisiasa ya wakati huo. Mtungaji Mfaransa Martin Aurell, wa La vielle et l’épée (Fidla na Upanga), alieleza kwamba hao watunga-mashairi ‘walishiriki kikamili katika mapigano ambayo yalitenganisha wenzao na kwamba kupitia utungaji wao wa muziki, hao watunga-mashairi hata walichangia mafanikio ya kikundi hiki au kingine.’
Akieleza juu ya wadhifa wa kipekee wa hao watunga-mashairi katika jamii ya enzi ya kati, Robert Sabatier ataarifu: “Kabla ya hapo hakukuwa kamwe washairi waliopewa fahari kubwa namna hiyo; kabla ya hapo hakukuwa mtu yeyote kamwe aliyepewa uhuru wa kusema ulio mkubwa namna hiyo. Walisifu na kukemea, walieleza maoni ya watu, walikuwa na uvutano juu ya sera za kisiasa, na wakawa chombo cha kupitishia mawazo mapya.”—La Poésie du Moyen Age.
Vyombo vya Habari vya Siku Yao
Inaweza kusemwa vyema kwamba muda mrefu kabla matbaa haijabuniwa, hao watunga-mashairi na wachezaji-wahamaji wengine walitumika kama vyombo vya habari vya siku yao. Wachezaji wa enzi ya kati walikuwa wasafiri wa kimataifa. Kotekote katika nyumba za wafalme za Ulaya—kutoka Saiprasi mpaka Scotland na kutoka Ureno mpaka Ulaya Mashariki, popote walipoenda—walikusanya habari na kubadilishana hadithi, melodia, na nyimbo. Zikisambaa kwa haraka kwa njia ya maneno kutoka mwimbaji-mhamaji mmoja hadi mwingine, watu walijifunza tuni zenye kuvutia za nyimbo za hao watunga-mashairi, zikiathiri sana kauli ya umma na kuamsha nguvu mpya ya watu wa kawaida ya kufanya jambo moja au jingine.
Mojawapo ya miundo mingi ya kishairi iliyotumiwa na hao watunga-mashairi inaitwa sirvente, kihalisi ikimaanisha “wimbo wa mtumishi.” Baadhi yake zilifichua udhalimu wa watawala. Nyingine zilisherehekea vitendo vya ushujaa, kujidhabihu, ukarimu, na rehema, huku zikichambua ukatili wa kishenzi, woga, unafiki, na kujipenda. Nyimbo za watumishi za mapema mwa karne ya 13 huwapa wanahistoria kijia cha kupata habari za hali ya kisiasa na ya kidini ya Languedoc katika wakati wa mabadiliko makubwa.
Uchambuzi wa Kanisa
Krusedi zikiwa zimeshindwa, watu wengi walianza kutilia mashaka yale mamlaka ya kiroho na ya kimwili ya Kanisa Katoliki. Makasisi walidai kuwakilisha Kristo, lakini matendo yao kwa hakika hayakuwa kama ya Kristo. Unafiki wao, pupa, na ufisadi ukajulikana na watu wote. Sikuzote wakitafuta mali zaidi na mamlaka ya kisiasa, maaskofu wa kanisa na mapadri waliandalia matajiri. Kupuuza kwao mahitaji ya kiroho ya maskini na watu wa tabaka la kati kulichochea ukaidi usioepukika.
Katika Languedoc watu wengi wa matabaka ya kati na vilevile makabaila walikuwa wamesoma. Mwanahistoria H. R. Trevor-Roper alionelea kwamba watu wa kawaida zaidi waliokuwa wamesoma walikuwa wakivumbua kwamba kanisa la karne ya 12 “lilikuwa tofauti sana na kigezo cha kale ambacho lilidai kuiga.” Aongezea kwamba wanaume wengi walianza kufikiri: “Ni jinsi gani hata lilivyo tofauti . . . Kanisa lililokuwa bado kuanzishwa kabla ya Konstantino, lile Kanisa la Mitume, . . . la minyanyaso: lilikuwa kanisa bila papa au maaskofu wa kikabaila au mali zilizowekwa wakfu au mafundisho ya kipagani au vifungu vipya vilivyokusudiwa kuongeza mali na mamlaka yake!”
Languedoc lilikuwa bara la uvumilivu. Makabaila wa Toulouse na watawala wengine wa kusini walipatia watu uhuru wa kidini. Wawaldoc walikuwa wametafsiri Biblia katika langue d’oc na walikuwa na bidii ya kuhubiri juu yake, wawili-wawili, kotekote katika eneo hilo. Wakathari (pia wanaitwa Waelbi) pia walikuwa wakieneza mafundisho yao na kupata wafuasi wengi miongoni mwa makabaila.
Nyingi za nyimbo za watumishi za hao watunga-mashairi zilionyesha jinsi watu walivyokata tamaa na jinsi ambavyo hawakustahi, na vile walivyochukizwa sana na makasisi Wakatoliki. Wimbo mmoja wa watumishi wa Gui de Cavaillon ulilaumu makasisi kwa sababu ya “kuacha mwito wao wa msingi” ili wajishughulishe zaidi na masilahi ya ulimwengu. Maneno ya nyimbo za hao watunga-mashairi yalidhihaki moto wa helo, msalaba, ungamo, na “maji matakatifu.” Zilidhihaki kusamehewa dhambi na makasisi na vikumbushi na kushutumu makasisi wasio na adili na maaskofu wafisadi kuwa “wasaliti, waongo, na wanafiki.”
Pigano la Kanisa Dhidi ya Uhuru
Ingawa hivyo, Kanisa la Kiroma, lilijifikiria kuwa kuu kuliko milki na falme zote. Vita vikawa chombo chake cha mamlaka. Papa Innocent wa Tatu aliahidi kutoa mali yote ya Languedoc kwa jeshi lolote ambalo lingetiisha wakuu na kugandamiza ukaidi wote katika milki za kusini mwa Ufaransa. Kilichofuata kilikuwa mojawapo ya vipindi vyenye umwagikaji mkubwa sana wa damu na mateso na mauaji ya kukusudia katika historia ya Ufaransa. Kikaja kujulikana kuwa Krusedi ya Waelbi (1209-1229).d
Hao watunga-mashairi waliiita Krusedi Isiyo ya Kweli. Nyimbo zao zilionyesha ukatili wa jinsi kanisa lilivyowatendea kwa unyama wakaidi na namna papa alivyokubali kujitia mno katika mauaji ya wakaidi Wafaransa kama lilivyokubali kuua Waislamu, walioonekana kuwa makafiri. Kanisa lilijitajirisha sana wakati wa Krusedi ya Waelbi na lile Baraza la Kuhukumu Wazushi lililofuata. Familia zilinyang’anywa urithi wao, nyumba na mashamba yao zikatwaliwa.
Wakishtakiwa kuwa wazushi Wakathari, watunga-mashairi wengi walikimbilia kwenye mabara yaliyokuwa na uhasama kidogo. Krusedi hii ilitia alama mwisho wa ustaarabu wa Occitan, njia yake ya maisha, ushairi wake. Sheria ya Baraza la Kuhukumu Wazushi iliharamisha kuimba, au hata kuimba hali kinywa kimefumbwa, wimbo wa hao watunga-mashairi. Lakini urithi wao ulidumu. Kwa kweli, nyimbo zao dhidi ya makasisi zilitayarisha akili za watu kutenda kwa ajili ya yale ambayo yangekuja kuwa Marekebisho Makubwa ya Kidini. Kweli, hao watunga-mashairi waweza kukumbukwa kwa ajili ya mengi zaidi kuliko tu nyimbo zao za mapenzi.
[Maelezo ya chinis]
a Lugha ya Kilatini iliyorithiwa kutoka kwa lejioni za Waroma, iliyoitwa Kiroma, ilikuwa kufikia wakati huo imesitawi kuwa lugha mbili za kienyeji katika Ufaransa: Kusini mwa Ufaransa ilisema ile lugha langue d’oc (iliyojulikana pia kama Occitan, au Provençal), huku kaskazini mwa Ufaransa ikisema ile langue d’oïl, (namna ya awali ya Kifaransa ambayo nyakati nyingine huitwa Kifaransa cha Kale). Lugha hizi mbili zilitofautishwa, moja kutoka kwa nyingine, na neno walilotumia kusema ndiyo. Katika kusini lilikuwa oc (kutokana na Kilatini hoc); katika kaskazini, oïl (kutokana na Kilatini hoc ille), lililokuja kuwa oui katika Kifaransa cha kisasa.
b Vichapo vyovyote vilivyoandikwa ama kwa lugha ya wenyeji ya kaskazini au ya kusini ziliitwa kiroma. Kwa sababu nyingi za hadithi hizi za kiungwana zilishughulika na hisia za moyoni za upendo mstahifu, zikaja kuwa kiwango cha zote zinazofikiriwa kuwa za mahaba au za kimahaba.
c Ona Mnara wa Mlinzi, Agosti 1, 1981, ukurasa wa 12-15, la Kiingereza, lililochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]
Printer’s Ornaments/cha Carol Belanger Grafton/Dover Publications, Inc.
Bibliothèque Nationale, Paris
[Picha katika ukurasa wa 19]
Picha ndogo kutoka kwenye hati ya karne ya 12
[Hisani]
Bibliothèque Nationale, Paris