Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 5/8 kur. 18-21
  • Kesi na Kufishwa kwa “Mzushi”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kesi na Kufishwa kwa “Mzushi”
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kesi na Auto-da-fé
  • Kesi ya Askofu
  • Kufishwa kwa Mwanafunzi Kijana
  • Sababu Nyingine ya Hatia Nzito
  • Lile Baraza la Kuhukumu Wazushi Mexico— Lilitendekaje?
    Amkeni!—1994
  • Hifadhi ya Nyaraka za Siri Yafunguliwa
    Amkeni!—1998
  • Vifaa vya Mnyanyaso Mkatili
    Amkeni!—1998
  • Hukumu ya Mungu Dhidi ya “Mtu wa Kuasi [Sheria]”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 5/8 kur. 18-21

Kesi na Kufishwa kwa “Mzushi”

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ITALIA

UPANDE mmoja wa mahakama yenye kufisha moyo pana kiti kikuu cha kifahari cha mahakimu. Kiti cha mwenyekiti kilichoko katikati kimefunikwa juu na kitambaa cheusi, ambacho juu yacho pamesimama msalaba mkubwa wa mbao ambao uko juu ya mahakama yote. Mbele ya kiti cha mwenyekiti, pana kizimba.

Hivi ndivyo mahakama zenye kuogofya za Baraza la Kuhukumu Wazushi la Katoliki zilivyofafanuliwa. Shtaka lenye kuogofya walilowekewa washtakiwa wa kuhurumiwa lilikuwa “uzushi,” neno ambalo huleta akilini picha za mateso na ufishaji kwa kuchomwa kwenye mti wa mateso. Baraza la Kuhukumu Wazushi lilikuwa mahakama ya kipekee ya kidini iliyoanzishwa ili kuondosha uzushi, yaani, maoni na mafundisho yasiyopatana na desturi za fundisho la Katoliki ya Kiroma.

Vitabu vya Kikatoliki vyasema kwamba hilo Baraza la Kuhukumu Wazushi lilianzishwa hatua kwa hatua. Papa Lucius wa Tatu alianzisha Baraza la Kuhukumu Wazushi kwenye Baraza la Verona katika 1184, na mpango na taratibu zalo zikakamilishwa—ikiwa neno hilo laweza kutumiwa kufafanua shirika hilo lenye kutia hofu—na mapapa wengine. Katika karne ya 13, Papa Gregory wa Tisa alianzisha mahakama za kuhukumu wazushi katika sehemu kadhaa za Ulaya.

Baraza la Kuhukumu Wazushi la Hispania lenye sifa mbaya lilianzishwa katika 1478 kwa amri ya Papa Sixtus wa Nne kwa kuombwa na watawala Ferdinand na Isabella. Lilianzishwa ili kupambana na Wamarano, Wayahudi ambao walijisingizia kugeuka kuwa Wakatoliki ili kuepuka kunyanyaswa; Wamorisko, wafuasi wa Uislamu waliogeuzwa imani kuwa Wakatoliki kwa sababu hiyohiyo; na wazushi Wahispania. Kwa sababu ya bidii yake ya kishupavu, mkuu wa kwanza wa kuhukumu wazushi katika Hispania, Tomás de Torquemada, ndugu-mtawa Mdominika, akaja kuwa ishara ya matendo mabaya sana ya Baraza la Kuhukumu Wazushi.

Katika 1542, Papa Paul wa Tatu alianzisha Baraza la Kiroma la Kuhukumu Wazushi, ambalo lilisimamia ulimwengu wote wa Katoliki. Yeye aliweka rasmi mahakama kuu ya makadinali sita, walioitwa Kutaniko la Roma Takatifu na Baraza la Kuhukumu Wazushi la Ulimwenguni Pote, kikundi cha kidini ambacho kilikuja kuwa “serikali ya ogofyo ambayo ilifanya Roma yote ijawe na hofu.” (Dizionario Enciclopedico Italiano) Kufishwa kwa wazushi kulitisha nchi ambazo mamlaka ya Kikatoliki ilimiliki kikamili.

Kesi na Auto-da-fé

Historia yathibitisha kwamba wenye kuhukumu wazushi walitesa walioshtakiwa uzushi ili wakiri kwamba wao ni wazushi. Katika jitihada ya kupunguza hatia ya Baraza la Kuhukumu Wazushi, waelezaji Wakatoliki wameandika kwamba kwa wakati huo, utesaji ulikuwa jambo la kawaida katika mahakama za kawaida pia. Lakini je, hilo lathibitisha kwamba kutesa kulikofanywa na wahudumu waliodai kuwa wawakilishi wa Kristo kulikuwa jambo la haki? Je, hawakupaswa kuonyesha huruma ambayo Kristo aliwaonyesha maadui wake? Ili kuona hili kwa maoni yafaayo, twaweza kufikiria swali moja sahili: Je, Kristo Yesu angetesa wale waliotofautiana naye katika mafundisho yake? Yesu alisema: “Endeleeni kupenda maadui wenu, kuwafanyia mema wale wanaowachukia.”—Luka 6:27.

Baraza la Kuhukumu Wazushi halikumhakikishia mshtakiwa haki yoyote. Katika utendaji wenyewe, mwenye kuhukumu wazushi alikuwa na uwezo usio na mipaka. “Kushuku, mashtaka, hata uvumi, vilitosha kumfanya mwenye kuhukumu wazushi kumwita mtu mbele yake.” (Enciclopedia Cattolica) Italo Mereu, mwanahistoria wa sheria, ahakikisha kwamba ni mamlaka ya Katoliki yenyewe iliyoanzisha na kukubali rasmi mfumo wa haki wa kuhukumu wazushi, wakiacha mfumo wa kale wa mashtaka ulioanzishwa na Waroma. Sheria ya Kiroma ilitaka mshtaki athibitishe madai yake. Ikiwa kulikuwa na shaka yoyote kuhusu hatia, ilikuwa afadhali kumwondolea hatia kuliko kujihatarisha kumhukumia adhabu mtu ambaye hakuwa na hatia. Mamlaka ya Katoliki ilibadili kanuni hii ya msingi na wazo kwamba kushuku kulifanya mtu awe na hatia, na ni mshtakiwa aliyepaswa kuthibitisha kwamba hana hatia. Majina ya mashahidi wa mashtaka (wenye kuleta habari dhidi ya wengine) yaliwekwa kuwa siri, na wakili wa utetezi, kulipokuwa na mmoja, alijihatarisha kupata sifa mbaya au kupoteza cheo chake ikiwa alimtetea mzushi kwa mafanikio. Likiwa tokeo, yakiri Enciclopedia Cattolica, “washtakiwa kwa hakika hawakuwa na kinga. Yote aliyoweza kufanya wakili ni kumshauri mwenye hatia aungame!”

Kesi ilimalizika kwa auto-da-fé, msemo wa Kireno unaomaanisha “kitendo cha imani.” Kilikuwa nini? Michoro ya kipindi fulani cha historia huonyesha kwamba watu walioshtakiwa uzushi na kuhukumiwa walikuja kuwa wahasiriwa wa tamasha zenye kuogofya. Dizionario Ecclesiastico hufafanua auto-da-fé kuwa “kitendo cha hadharani cha upatanishaji unaofanywa na wazushi waliohukumiwa adhabu na waliotubu” baada ya thibitisho la hatia kusomwa.

Kuthibitishwa kwa hatia na kufishwa kwa wazushi kuliahirishwa ili wazushi kadhaa waunganishwe katika tamasha moja yenye kuogofya sana mara mbili kwa mwaka au zaidi. Mwandamano mrefu wa wazushi ulipangwa mbele ya watazamaji, ambao walishiriki kwa mchanganyiko wa ogofyo na upendezi wa kufurahia ukatili. Waliohukumiwa hatia walilazimishwa kupanda kwenye jukwaa katikati ya mahali pakubwa palipo wazi, na hukumu zao zilisomwa kwa sauti kubwa. Wale waliokiri, yaani, kukana mafundisho ya kizushi, walisamehewa kutengwa na ushirika na walihukumiwa adhabu tofauti-tofauti kutia ndani kifungo cha maisha. Wale ambao hawakukiri makosa yao lakini kwenye dakika ya mwisho waliungama kwa kasisi walipelekwa kwenye mamlaka za serikali ili wasongolewe, wanyongwe, au wakatwe kichwa na hatimaye kuchomwa. Wale ambao hawakutubu walichomwa wakiwa hai. Ufishaji wenyewe ulitokea wakati fulani baadaye, kufuatia tamasha nyingine ya hadharani.

Utendaji wa Baraza la Kuhukumu Wazushi la Kiroma ulifunikwa kwa siri sana. Hata leo, wasomi hawaruhusiwi kutafuta habari katika makabathi ya baraza hilo. Hata hivyo, utafiti wenye subira umefunua idadi kadhaa ya hati za kesi ya mahakama ya Kiroma. Hizo hufunua nini?

Kesi ya Askofu

Pietro Carnesecchi, aliyezaliwa Florence mwanzoni mwa karne ya 16, alifanya maendeleo ya haraka katika kazi-maisha yake ya kidini kwenye makao ya Papa Clement wa Saba, ambaye alimweka rasmi kuwa karani wake wa kibinafsi. Hata hivyo, kazi-maisha ya Carnesecchi ikamalizika ghafula, wakati papa huyo alipokufa. Baadaye, akaja kufahamiana na makabaila na makasisi ambao, kama yeye, walikubali mafundisho kadhaa yaliyofundishwa na Marekebisho ya Waprotestanti. Tokeo ni kwamba alifanyiwa kesi mara tatu. Akiwa amehukumiwa kifo, alikatwa kichwa, na mwili wake ukachomwa.

Kifungo cha Carnesecchi kilifafanuliwa na waelezaji kuwa uhai usio na shangwe wala uradhi. Ili kumfanya akiri, aliteswa na kunyimwa chakula. Septemba 21, 1567, auto-da-fé yake ilifanywa mbele ya karibu makadinali wote katika Roma. Carnesecchi alisomewa hukumu yake jukwaani mbele ya umati huo. Ikamalizika kwa maneno ya kidesturi ya kawaida ya kidini na kwa sala kwa washiriki wa mahakama ya serikali, ambayo mzushi huyo alikuwa karibu kupelekwa, ili ‘wapunguze hukumu hiyo juu yake na kutomhukumia kifo au mateso mengi.’ Je, huu haukuwa unafiki wa kupita kiasi? Wenye kuhukumu wazushi walitaka kuwaondosha wazushi lakini, kwa wakati huohuo, walijifanya kuwa walikuwa wakiomba mamlaka za kilimwengu zidhihirishe rehema, hivyo wakizuia kuharibika kwa sifa yao na kujiondolea mzigo wa hatia ya damu. Baada ya hukumu ya Carnesecchi kusomwa, alifanywa avae sanbenito—vazi la gunia la rangi ya manjano lililopakwa rangi kwa misalaba myekundu kwa wenye kutubu au jeusi lenye cheche za moto na maibilisi kwa wasiotubu. Adhabu ilitekelezwa siku kumi baadaye.

Kwa nini huyu aliyekuwa hapo mbeleni karani wa papa alishtakiwa uzushi? Rekodi rasmi za kesi yake, ambazo ziligunduliwa mwishoni mwa karne iliyopita, hufunua kwamba alipatikana na hatia ya mashtaka 34 kulingana na mafundisho aliyopinga. Miongoni mwayo mlikuwa na mafundisho kuhusu purgatori, useja wa makasisi na watawa, kugeuka asili ya mwili, kipaimara, kuungama, kukatazwa vyakula fulani, kuondolewa adhabu ya purgatori, na sala kwa “watakatifu.” Shtaka la nane ndilo hasa lenye kuvuta fikira. (Ona sanduku, kwenye ukurasa 21.) Kwa kuwahukumia kifo wale waliokubali “neno la Mungu lililoelezwa katika Maandiko Matakatifu,” kuwa msingi pekee wa itikadi, hilo Baraza la Kuhukumu Wazushi kwa wazi lilionyesha kwamba Kanisa Katoliki halioni Biblia Takatifu kuwa ndicho kitabu pekee kilichopuliziwa. Kwa hiyo haishangazi kwamba mafundisho mengi ya kanisa hilo yanategemea, si Maandiko, bali mapokeo ya kanisa.

Kufishwa kwa Mwanafunzi Kijana

Simulizi fupi na lenye kugusa moyo la maisha ya Pomponio Algieri, aliyezaliwa karibu na Naples katika 1531, halijulikani sana, lakini limezuka kutoka kwa wakati uliopita usiojulikana, kwa sababu ya uchunguzi wenye bidii wa kihistoria wa wasomi kadhaa. Kwa kukutana kwake na walimu na wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za Ulaya alipokuwa akisoma kwenye Chuo Kikuu cha Padua, Algieri alijulishwa kwa walioitwa eti wazushi na kwa mafundisho ya Marekebisho ya Protestanti. Upendezi wake kwa Maandiko ukaongezeka.

Alianza kuamini kwamba Biblia pekee ndiyo imepuliziwa, na tokeo ni kwamba alikataa mafundisho kadhaa ya Katoliki, kama vile kuungama, kipaimara, purgatori, kugeuka asili ya mwili, na kwamba “watakatifu” ni waombezi na vilevile fundisho kwamba papa ni mwakilishi wa Kristo.

Algieri alikamatwa na kufanyiwa kesi na Baraza la Kuhukumu Wazushi katika Padua. Yeye aliwaambia wenye kumhukumu hivi: “Narudi gerezani kwa hiari, labda hata kwenye kifo changu ikiwa hayo ndiyo mapenzi ya Mungu. Kupitia utukufu wake, Mungu atahekimisha kiroho kila mmoja zaidi. Nitavumilia kila teso kwa furaha kwa sababu Kristo, Mfariji mkamilifu wa nafsi zinazotaabishwa, ambaye ndiye mmulikaji wangu na nuru ya kweli, aweza kuondoa giza lote la kiroho.” Baadaye, alipelekwa kwenye Baraza la Kuhukumu Wazushi la Kiroma na kuhukumiwa kifo.

Algieri alikuwa na umri wa miaka 25 alipokufa. Siku aliyouawa katika Roma, alikataa kuungama na kukubali Komunyo. Kifaa cha kumfishia kilikuwa chenye ukatili zaidi kuliko ilivyo kawaida. Hakuchomwa kwa tita la kuni. Badala ya hivyo, sufuria kubwa iliyojaa vitu viwezavyo kuwaka moto—oili, lami, na rezini—iliwekwa jukwaani ambapo umati ungeweza kuona vizuri. Akiwa amefungwa, mwanamume huyo kijana aliteremshwa ndani, na vitu hivyo kuwashwa moto. Alichomwa polepole akiwa hai.

Sababu Nyingine ya Hatia Nzito

Carnesecchi, Algieri, na wengineo ambao waliuawa na Baraza la Kuhukumu Wazushi hawakufahamu Maandiko kikamili. Bado ujuzi ulipaswa kuwa “mwingi” katika “wakati wa mwisho” wa mfumo huu wa mambo. Hata hivyo, walikuwa tayari kufa kwa sababu ya kiwango kidogo cha “ujuzi wa kweli” ambao walikuwa wameweza kupata kutoka kwa Neno la Mungu.—Danieli 12:4, NW.

Hata Waprotestanti, kutia ndani baadhi ya Warekebishaji, waliondosha wasiokubaliana nao kwa kuwachoma kwenye mti wa mateso au kuhakikisha Wakatoliki wameuawa kwa msaada wa mamlaka za kilimwengu. Kwa kielelezo, ingawa Calvin alipendelea kukata vichwa vya wazushi, alifanya Michael Servetus achomwe angali hai kwa sababu alionwa kuwa mzushi mwenye kupinga Utatu.

Uhakika wa kwamba kunyanyaswa na kufishwa kwa wazushi kulikuwa kwa kawaida kwa Wakatoliki na vilevile Waprotestanti si udhuru wa kutetea matendo hayo. Lakini wenye mamlaka wa kidini wana lawama nzito zaidi—kwa kudai kwamba kuna sababu za kihalali za Kimaandiko kwa mauaji hayo na kisha kwa kutenda kana kwamba Mungu mwenyewe alikuwa ameamuru matendo hayo. Je, hilo halisuti jina la Mungu? Wasomi kadhaa wahakikisha kwamba Augustine, “Baba Kanisa” Mkatoliki ajulikanaye sana, alikuwa wa kwanza kuunga mkono kanuni ya uzuizi wa “kidini,” yaani, utumizi wa nguvu ili kupambana na uzushi. Katika jitihada za kutumia Biblia ili kutetea zoea hilo kuwa halali, yeye alinukuu maneno ya mfano wa Yesu upatikanao kwenye Luka 14:16-24: “Uwashurutishe waingie.” Kwa wazi, maneno haya, yaliyopotoshwa na Augustine, yalionyesha ukaribishaji wageni mkarimu, si ulazimishaji mkatili.

Yafaa kuonwa kwamba hata wakati Baraza la Kuhukumu Wazushi lilipokuwa tendaji, waungaji mkono wa ustahimilivu wa kidini walipinga kunyanyaswa kwa wazushi, wakinukuu mbazi ya ngano na magugu. (Mathayo 13:24-30, 36-43) Mmoja wao alikuwa Desiderius Erasmus, wa Rotterdam, ambaye alisema kwamba Mungu, Mwenye shamba, alitaka wazushi, magugu, wavumiliwe. Martin Luther, kwa upande ule mwingine, alichochea jeuri dhidi ya wakulima wasiokubaliana nao, na karibu 100,000 waliuawa.

Tukitambua lawama nzito ya dini za Jumuiya ya Wakristo kuendeleza mnyanyaso wa walioitwa eti wazushi, twapaswa kusukumwa kufanya nini? Kwa hakika twapaswa kutaka kutafuta ujuzi wa kweli wa Neno la Mungu. Yesu alisema kwamba ishara ya Wakristo wa kweli ni kumpenda Mungu na jirani—upendo ambao kwa wazi hauwezi kuruhusu jeuri.—Mathayo 22:37-40; Yohana 13:34, 35; 17:3.

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

Baadhi ya Mashtaka Ambayo Kwayo Carnesecchi Alipatikana na Hatia

8.“[Umesisitiza] kwamba hakuna chochote isipokuwa neno la Mungu lililoelezwa katika Maandiko Matakatifu lapaswa kuaminiwa.”

12.“[Umeamini] kwamba ungamo la kisakramenti si de jure Divino [halipatani na sheria ya kimungu], kwamba halikuanzishwa na Kristo wala kuthibitishwa na Maandiko, wala aina yoyote ile ya ungamo haifai isipokuwa ungamo kwa Mungu mwenyewe.”

15.“Umetilia shaka purgatori.”

16.“Umeona kitabu cha Makabayo, ambacho hushughulika na sala kwa wafu, kuwa cha kubuniwa tu.”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki