Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 12/8 kur. 12-13
  • Hifadhi ya Nyaraka za Siri Yafunguliwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Hifadhi ya Nyaraka za Siri Yafunguliwa
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Je, Zina Nini?
  • Uchambuzi
  • ‘Hakuna Chochote Kilichofunikwa Ambacho Hakitajulikana’
  • Kesi na Kufishwa kwa “Mzushi”
    Amkeni!—1997
  • Vifaa vya Mnyanyaso Mkatili
    Amkeni!—1998
  • Lile Baraza la Kuhukumu Wazushi Mexico— Lilitendekaje?
    Amkeni!—1994
  • Je! Kweli Biblia Ni Zawadi Kutoka kwa Mungu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 12/8 kur. 12-13

Hifadhi ya Nyaraka za Siri Yafunguliwa

NA MLETA-HABARI WA Amkeni! KATIKA ITALIA

“Hifadhi ya nyaraka za Baraza la Kuhukumu Wazushi yafunguliwa.” Hivi ndivyo vyombo vya habari vilivyoripoti kwamba Vatikani imeruhusu wasomi kuingia katika hifadhi ya nyaraka za Kundi la Fundisho la Imani, ambalo liliitwa Ofisi Takatifu kufikia mwaka 1965.

ILITAARIFIWA kwamba hatua hiyo yapaswa kueleweka “katika muktadha wa utaratibu mzuri na mrefu wa pitio la historia ambao John Paul wa Pili anataka kumaliza kabla ya mwaka 2000.”a Kwa nini kuna upendezi mwingi sana katika nyaraka hizi? Zinadhaniwa kuwa na siri zipi?

Ofisi Takatifu ilianzishwa na Papa Paul wa Tatu mwaka wa 1542. Chombo hiki cha papa cha kukomesha “uzushi” kiliitwa pia Baraza la Roma la Kuhukumu Wazushi, ili kulitofautisha na lile Baraza la Hispania la Kuhukumu Wazushi lililoanzishwa mwaka wa 1478.b Kundi la makadinali lililoanzishwa mwaka wa 1542 lilipaswa “lijishughulishe na suala la uzushi katika Jumuiya ya Wakristo yote,” aeleza Adriano Prosperi, ambaye ni mtaalamu wa mambo hayo. Kati ya Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi yaliyokuwa yakitenda kazi katika karne ya 16, ni Baraza la Roma la Kuhukumu Wazushi pekee ambalo lingali linatenda kazi, ingawa lina jina tofauti na wajibu tofauti.

Rekodi za Baraza la Kuhukumu Wazushi zilikusanywa. Baada ya muda, zilifanyiza hifadhi ya nyaraka za siri ya Ofisi Takatifu. Mwaka wa 1559 nyaraka hizo ziliporwa na baadhi ya watu wa Roma, ambao waliasi ili “kusherehekea” kifo cha Papa Paul wa Nne, aliyeonwa kuwa mtetezi mkuu wa Baraza la Roma la Kuhukumu Wazushi. Katika mwaka wa 1810, baada ya kushinda Roma, Napoléon wa Kwanza alihamisha nyaraka hizo hadi Paris. Wakati huo na baadaye wakati wa kuzirudisha kwa papa, nyaraka nyingi zilipotea au kuharibiwa.

Je, Zina Nini?

Hati hizo zinazozidi 4,300 ambazo hufanyiza hifadhi hiyo ya nyaraka zimo katika vyumba viwili karibu na St. Peter’s Basilica. Kulingana na kadinali Joseph Ratzinger—mkuu wa hifadhi hiyo ya Vatikani—mambo yaliyo katika nyaraka hizi yanahusu kwa njia isiyo ya moja kwa moja masuala ya kihistoria ingawa “hasa yanahusu elimu ya kidini.”

Wanahistoria wanakubaliana kwamba nyaraka hizo haziwezi kutazamiwa kufunua mengi. Profesa Prosperi aeleza kwamba mijadala ya mikutano ya Baraza la Roma la Kuhukumu Wazushi imo lakini “hati, rekodi, na karibu hati za kesi zote za mashtaka zinakosekana. Nyingi ziliharibiwa kati ya mwaka wa 1815 na 1817 katika Paris kwa amri ya Monsignor Marino Marini, aliyetumwa kutoka Roma kuzitwaa hati zilizochukuliwa na Napoléon.”

Vatikani imewaruhusu wasomi wazione hati zilizokusanywa kabla ya kifo cha Leo wa 13, Julai 1903. Ili kuruhusiwa kuziona, lazima watafiti watoe barua za kuwajulisha kutoka kwa mamlaka za kidini au za kielimu.

Uchambuzi

Ingawa wengi walifurahia habari za kufunguliwa kwa hifadhi hiyo ya nyaraka, wachambuzi walisikika. Akifikiri kwa uzito ni kwa nini hati za kabla ya 1903 pekee ndizo zilizotolewa, mwanatheolojia Mkatoliki Hans Küng auliza: “Je, huenda ni kwa sababu mwaka wa 1903 ndio hasa rekodi hiyo inaanza kupendeza, kwa vile ni katika mwaka huo ndipo Papa Pius wa Kumi, aliyetoka tu kuchukua cheo cha papa, alipoanza kampeni ya kupinga Umamboleo, ambayo iliathiri idadi kubwa ya wanatheolojia na kutokeza magumu kwa maaskofu wa Italia, Ufaransa, na Ujerumani, na kuwatenga watu wengi sana kutoka kwa kanisa?”

Kulingana na mwanahistoria wa sheria Italo Mereu, ijapokuwa walibadilisha jina na kufungua hifadhi hiyo ya nyaraka, “[Kundi la Fundisho la Imani] hufanya kazi inayofanana na ile ya Baraza la Kuhukumu Wazushi la zamani, na mbinu zake za zamani,” kama vile kuwakataza wale wanaochunguzwa kuona zile hati zinazowarejezea.

‘Hakuna Chochote Kilichofunikwa Ambacho Hakitajulikana’

Kwa ujumla, wanahistoria hawana tumaini la kugundua mambo yoyote yenye kutokeza katika “hifadhi ya nyaraka za Baraza la Kuhukumu Wazushi.” Hata hivyo, ni jambo lenye kutokeza kwamba Kanisa Katoliki linahisi limelazimika kukubali kutii maoni ya watu wengi.

Ingawa hivyo, maoni yaliyo na uzito zaidi ni ya Mungu. Kwa wakati unaostahili yeye atahukumu dini ambayo ilidai kuwa ya Kikristo lakini kwa karne nyingi ikavunja amri za Mungu na kukiuka mafundisho ya Yesu kwa kufanyiza Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi yenye ukatili. Katika Mabaraza haya, idadi kubwa ya watu wasio na hatia waliteswa vibaya sana na kuuawa, eti kwa sababu tu walikataa mafundisho na mazoea ya kanisa hilo.—Mathayo 26:52; Yohana 14:15; Waroma 14:12.

Hata wasomi wachanganue kindani nyaraka hizo kwa kadiri gani, bado uchanganuzi huo hautakamilika kamwe. Kwa upande mwingine, “hakuna kiumbe kisichokuwa dhahiri machoni [pa Mungu], bali vitu vyote viko uchi na vikiwa vimefunuliwa wazi machoni pake ambaye kwake sisi tuna kutoa hesabu.” (Waebrania 4:13) Hiyo ndiyo sababu Yesu, akiwarejezea viongozi wa kidini waliompinga, aliwaambia wanafunzi wake: “Msiwahofu; kwa maana hakuna kitu chochote kilichofunikwa kabisa ambacho hakitakuwa chenye kufunuliwa, na cha siri ambacho hakitakuwa chenye kujulikana.”—Mathayo 10:26.

[Maelezo ya Chini]

a Ona Mnara wa Mlinzi, Machi 1, 1998, ukurasa wa 3-7.

b Ijapokuwa njia yao na matokeo yao yalitofautiana kidogo, mabaraza mawili haya yalikuwa mapya yakilinganishwa na lile Baraza la Kuhukumu Wazushi la enzi ya kati lililokuwa limeanza mwaka wa 1231 katika Italia na Ufaransa.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

Palace of the Holy Office, Rome, Italy

Michoro: From the book Bildersaal deutscher Geschichte

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki