Lile Baraza la Kuhukumu Wazushi Mexico— Lilitendekaje?
WAZIA kwamba uko mbele ya mahakama ya kidini itakayo kukulazimisha uamini yafundishwayo na dini hiyo. Hujui anayekushtaki wala unaloshtakiwa. Badala ya kuambiwa, unalazimishwa kuandaa sababu ya wewe kukamatwa, ili ueleze waamini shtaka lako ni nini, na ili useme mshtaki ni nani.
Jiangalie utajibuje—ungeweza kuungama jambo ambalo hujashtakiwa na kujiharibia mambo zaidi! Ungeweza pia kuhusisha watu wasiokuwa wamehusika na shtaka liletwalo dhidi yako.
Usipoungama, huenda ukateswa-teswa kwa kumezeshwa kinguvu maji mengi. Au huenda mikono na miguu yako ikakazwa-kazwa zaidi na zaidi juu ya meza ya mateso mpaka maumivu yakupindukie. Tayari umekwisha kupokonywa mali yako na mahakama, na yaelekea sana hutaipata tena. Kila jambo lafanywa kwa siri. Ukipatikana na hatia, huenda ukahamishwa nchi yako au hata kuteketezwa ukiwa hai.
Katika karne hii ya 20, huenda ukaona ni vigumu kuelewa jinsi kungekuwa na kitendo kibaya hivyo cha kidini. Lakini karne kadhaa zilizopita, vitendo vya uhabithi huo vilitukia Mexico.
“Kuongoa” Wenyeji
Wakati ile ambayo sasa ni Mexico iliposhindwa ikatwaliwa na Wahispania karne ya 16, ushinde wa kidini ulitukia pia. Uongofu wa kidini uliofanywa kwa makabila ya wenyeji haukutimiza mengi sana isipokuwa kubadili tu mapokeo na desturi zao, kwa kuwa ni mapadri wachache Wakatoliki waliojihangaisha na kufundisha Biblia. Wao hawakujishughulisha kujifunza lugha ya wenyeji wala kuwafundisha Kilatini, ambacho fundisho la kidini lilipatikana kwacho.
Wengine walifikiri kwamba Mhindi apaswa kupokea mafundisho kamili ya kidini. Lakini wengine walikuwa na maoni yaleyale ya Ndugu-Mtawa Domingo de Betanzos, ambaye, kulingana na Richard E. Greenleaf katika kitabu chake Zumárraga and the Mexican Inquisition, “aliamini kwamba Mhindi apaswa kunyimwa mafundisho ya Kilatini kwa sababu hiyo ingemwongoza kung’amua jinsi makasisi wasivyo na ujuzi.”
Baraza la Kuhukumu Dhidi ya Wazushi Wenyeji
Ikiwa wenyeji waliozaliwa Mexico hawakupokea ile dini mpya kwa shauku, walichukuliwa kuwa waabudu-sanamu na kuteswa vibaya sana. Kwa kielelezo, mmoja wao alicharazwa mijeledi mia moja kwa kuabudu sanamu zake za kipagani, alizokuwa amefukia chini ya sanamu moja ya Jumuiya ya Wakristo kwa kusingizia eti anafanya ibada “ya Kikristo.”
Kwa upande mwingine, Don Carlos Ometochtzin, chifu wa kikabila wa Texcoco na mjukuu wa mfalme wa Waazteki, Netzahualcóyotl, alilishambulia kanisa kwa maneno. Greenleaf ataarifu kwamba “Don Carlos hasa alikuwa ameliudhi Kanisa kwa sababu ya kuwa amewahubiria wenyeji juu ya ufasiki wa mandugu-watawa.”
Wakati Ndugu-Mtawa Juan de Zumárraga, aliyekuwa mwanabaraza wa kuhukumu wazushi wakati huo, alipopata habari hizo, aliagiza kukamatwa kwa Don Carlos. Kwa kushtakiwa kuwa “mzushi mwenye kung’ang’ania kufundisha kauli yake,” Don Carlos aliteketezwa mtini Novemba 30, 1539. Wenyeji wengine wengi waliadhibiwa kwa mashtaka ya uaguzi.
Kuhukumu Wazushi Wageni
Wageni waliokuwa wakiishi Mexico wakakataa kuikubali dini ya Katoliki walishtakiwa kuwa wazushi, Walutheri, au watetezi wa Dini ya Kiyahudi. Familia ya Kireno ya Carvajal ilikuwa kielelezo kimoja cha jambo hili. Kwa kushtakiwa kuifuata dini ya Kiyahudi, karibu wote waliteswa-teswa na lile Baraza la Kuhukumu Wazushi. Hukumu inayofuata iliyotamkwa dhidi ya mshiriki mmoja wa familia hii yaonyesha mateso hayo ya kuogofya: “Huyo asemwaye kuwa Doña Mariana de Carvajal [mimi nam]hukumu . . . apewe garoti [chombo cha kukaba mtu shingo] mpaka afe kiasili, kisha ateketezwe katika moto unaowaka vikali mpaka ageuke majivu na hata kusibaki kumbukumbu lolote juu yake.” Ilitendeka hivyo hasa.
Wakati wowote mgeni alipoingilia mamlaka ya makasisi, aliletwa kufanyiwa kesi. Mwanamume mmoja jina lake Don Guillén Lombardo de Guzman alishtakiwa kutaka kuiweka Mexico huru. Hata hivyo, shtaka lililoletwa na ile Ofisi Takatifu (baraza la kuitetea imani) ili akamatwe na kufanyiwa kesi kwa kuwa mnajimu na mzushi aliye mfuasi wa Calvin mwenye kusababisha migawanyiko ya kidhehebu. Alipokuwa amefungwa gerezani alirukwa na akili. Hatimaye aliteketezwa mtini akiwa hai Novemba 6, 1659.
Kitabu Inquisition and Crimes, kilichotungwa na Don Artemio de Valle-Arizpe, chaeleza pindi hiyo: “Walienda wakifunga-funga wakosaji, wakiwafungilia mtini kwa kuwazungushia kola ya chuma kooni. . . . Ile mioto mitakatifu ya imani ilianza kuwaka kwa fujo kama kimbunga cha rangi nyekundu na nyeusi. Don Guillén . . . alijiachilia akaanguka ghafula kisha ile kola iliyokuwa ikimshikilia shingoni ikamkaba koo, na mwili wake ukatoweka baadaye katika ule mng’ao wa kuogofya wa moto mkali sana. Yeye aliyaacha maisha haya baada ya miaka kumi na saba ya kuteseka polepole na kwa uendelevu katika zile jela zenye majonzi za Ofisi Takatifu. Mioto hiyo iliendelea kupoa kidogo kidogo, huku miali yayo myekundu-samawati ikififia, na ilipozimika, ni rundo jangavu la kuni tu lililobaki likitoa nuru hafifu usiku.”
“Ofisi Takatifu” Yaanzishwa
Kama ilivyoonwa tayari, watu wengi wenyeji na wageni-wazaliwa wa Mexico waliadhibiwa, na wengine waliuawa kwa kuchambua au kwa kutokubali ile dini mpya. Jambo hili lilitokeza baraza la kuhukumu wazushi lililofanyizwa na mandugu-watawa na baadaye na maaskofu. Hata hivyo, aliyekuwa wa kwanza kuwa Mkuu wa Baraza la Kuhukumu Wazushi katika Mexico, Don Pedro Moya de Contreras, alitoka Hispania katika 1571 kuja kuanzisha rasmi huko Mahakama ya Ofisi Takatifu ya Baraza la Kuhukumu Wazushi. Mahakama hii iliacha kutenda kazi katika 1820. Hivyo, kuanzia 1539, kulikuwako miaka kama mia tatu ya kunyanyasa, kutesa-tesa, na kuua wale wasioshiriki imani za Kikatoliki.
Mtu fulani aliposhtakiwa, aliteswa-teswa mpaka akaungama. Mahakama ilimtarajia akane mazoea yake ya kupinga Ukatoliki na azikubali imani za kanisa. Mshtakiwa aliachwa huru ikiwa tu alithibitisha hana hatia, ikiwa hatia yake haingeweza kuthibitishwa, au, mwisho, ikiwa aliungama na kutubu. Katika kisa hiki cha mwisho, taarifa yake ya kwamba alichukizwa sana na kosa lake na kuahidi kufanya marekebisho ya alilokuwa amefanya ilisomwa hadharani. Vyovyote vile, alipoteza mali yake na ilikuwa lazima alipe faini kubwa. Alipopatikana mwenye hatia, alipelekwa kwa wenye mamlaka ya kiserikali kuadhibiwa. Kwa jumla jambo hili lilifikia mwisho kwa kumteketeza mtini, ama akiwa bado hai ama baada ya kuuawa muda mchache kabla ya hapo.
Kwa hukumu za kuuawa hadharani, sherehe kubwa sana ya kujulisha umma juu ya mteketezo ilifanywa. Mbiu ya kutangazia umma ingefanywa sehemu zote za jiji kujulisha kila mtu siku na mahali pa kukutania. Siku hiyo wahukumiwa wangetoka kwenye jela za ile Mahakama ya Ofisi Takatifu wakiwa wamevalia sambenito (joho la aina fulani lisilo na mikono), wakichukua mshumaa katikati ya mikono yao, wakiwa wamezungushiwa kamba shingoni, na coroza (kofia yenye muundo wa pia) ikiwa juu ya kichwa chao. Baada ya matendo ya uhalifu dhidi ya imani ya Kikatoliki kusomwa, adhabu iliyoamuliwa kwa kila mhukumiwa ingetekelezwa.
Kwa njia hii wengi walihukumiwa na kuadhibiwa kwa jina la dini. Ukatili na ukosefu wa kuvumilia watu kwa upande wa makasisi ulionekana wazi kwa umati uliowaona wahukumiwa wakifa mtini.
Upinzani wa Moja kwa Moja kwa Ukristo
Kristo Yesu aliwapa wanafunzi wake agizo la kuongoa watu kwenye Ukristo wa kweli. Aliamuru hivi: “Kwa hiyo nendeni mkafanye wanafunzi kutoka kwa watu wa mataifa yote, kuwabatiza katika jina la Baba na la Mwana na la roho takatifu, kuwafundisha kushika mambo yote ambayo mimi nimewaamuru nyinyi.”—Mathayo 28:19, 20, NW.
Hata hivyo, Yesu hakuonyesha kamwe kwamba watu wapaswa kuongolewa kinguvu. Bali, Yesu alisema: “Mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu.” (Mathayo 10:14) Hukumu ya mwisho ya watu hawa huachiwa Mungu Mweza Yote, Yehova, bila Wakristo kufanya mwingilio wa kimwili.
Basi, ni wazi kwamba wakati wowote Baraza la Kuhukumu Wazushi lilipotekelezwa ulimwenguni, hilo lilifanywa kwa kupinga kabisa kanuni za Kikristo.
Ile hali ya dini kuvumilia maoni ya wengine iliyopo kwa wingi sasa katika Mexico yaruhusu watu kutumia uhuru juu ya njia watakayo kumwabudu Mungu. Lakini karne nyingi za lile lililoitwa Baraza Takatifu la Kuhukumu Wazushi zabaki zikiwa ukurasa mwovu katika historia wa kumbukumbu juu ya lile Kanisa Katoliki la Mexico.