Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w90 2/1 kur. 15-20
  • Hukumu ya Mungu Dhidi ya “Mtu wa Kuasi [Sheria]”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Hukumu ya Mungu Dhidi ya “Mtu wa Kuasi [Sheria]”
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uzaaji Mzuri wa Matunda ya Kikristo
  • Babuloni Mkubwa Mwenye Hatia ya Damu
  • Kumbukumbu la Kuvunjia Mungu Heshima
  • Hatia ya Damu Katika Karne ya 20
  • Kupasishwa Kutoa Hesabu
  • Kufichua “Mtu wa Kuasi [Sheria]”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Kutambulisha “Mtu wa Kuasi [Sheria]”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Kifo cha Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Je, Dini Zote Humpendeza Mungu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
w90 2/1 kur. 15-20

Hukumu ya Mungu Dhidi ya “Mtu wa Kuasi [Sheria]”

“Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.”​—MATHAYO 7:19, NW.

1, 2. Mtu wa kuasi sheria ni nini, na ilisitawi jinsi gani?

WAKATI mtume Paulo alipovuviwa na Mungu atabiri kuja kwa “mtu wa kuasi [sheria],” alisema kwamba jambo hilo lilikuwa likianza kutokea hata katika siku yake. Kama ilivyoeleza makala iliyotangulia, Paulo alikuwa akiongea kuhusu jamii ya watu mmoja mmoja ambao wangeongoza uasi-imani wa kutoka kwenye Ukristo wa kweli. Huko kugeuka mbali kutoka kwenye ukweli kulianza mwishoni mwa karne ya kwanza, hasa baada ya kifo cha mitume wale wa mwisho. Jamii ya mwasi sheria iliingiza mafundisho na mazoea yenye kupinga Neno la Mungu.​—2 Wathesalonike 2:3, 7; Matendo 20:29, 30; 2 Timotheo 3:16, 17; 4:3, 4.

2 Baada ya muda, jamii hii ya kuasi sheria ilisitawi ikawa makasisi wa Jumuiya ya Wakristo. Nguvu zayo ziliimarishwa na Konstantino mmaliki wa Roma katika karne ya nne wakati makanisa ya uasi-imani yalipooana na Serikali ya kipagani. Jumuiya ya Wakristo ilipoendelea kuvunjika-vunjika kuwa mafarakano mengi, makasisi waliendelea kujiinua juu ya watu wa kawaida na mara nyingi juu ya watawala wa kilimwengu pia.​—2 Wathesalonike 2:4.

3. Msiba wa mtu wa kuasi sheria utakuwa nini?

3 Yule mtu wa kuasi sheria angepatwa na msiba gani? Paulo alitabiri hivi: “Yule mwasi sheria atafunuliwa, ambaye Bwana Yesu atamwondolea mbali . . . na kumkomesha awe si kitu kwa udhihirisho wa kuwapo kwake.” (2 Wathesalonike 2:8, NW) Hii yamaanisha kwamba uharibifu wa makasisi utatukia Mungu aletapo mwisho wa mfumo mzima wa Shetani. Mungu atumia Mfalme wake wa kimbingu, Kristo Yesu, kuongoza majeshi ya malaika wafishaji. (2 Wathesalonike 1:6-9; Ufunuo 19:11-21) Msiba huu wawangoja makasisi kwa sababu wamewavunjia heshima Mungu na Kristo na wakaongoza mamilioni ya watu watoke kwenye ibada ya kweli.

4. Mtu wa kuasi sheria atahukumiwa kwa kanuni gani?

4 Yesu alitoa kanuni ambayo kwayo yule mtu wa kuasi sheria angehukumiwa, akisema: “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni... . Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”​—Mathayo 7:15-21; ona pia Tito 1:16; 1 Yohana 2:17.

Uzaaji Mzuri wa Matunda ya Kikristo

5. Ni nini msingi wa uzaaji mzuri wa matunda ya Kikristo, na ni nini amri moja ya msingi?

5 Msingi wa uzaaji mzuri wa matunda ya Kikristo waonwa kwenye 1 Yohana 5:3, ambayo yataarifu hivi: “Huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake.” Na takwa moja la msingi ni hili: “Ni lazima upende jirani yako kama wewe mwenyewe.” (Mathayo 22:39, NW) Hivyo, ni lazima watumishi wa kweli wa Mungu wawe na upendo kwa jirani zao hata kama hao ni wa rangi au utaifa gani.​—Mathayo 5:43-48; Warumi 12:17-21.

6. Upendo wa Kikristo ni lazima uonyeshwe kuelekea nani hasa?

6 Ni lazima hasa watumishi wa Mungu wawe na upendo kwa wale walio ndugu zao za kiroho. “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.” (1 Yohana 4:20, 21) Yesu alisema upendo huo ungekuwa alama yenye kutambulisha Wakristo wa kweli; “Mkipendana, watu wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu.”​—Yohana 13:35, HNWW; ona pia Warumi 14:19; Wagalatia 6:10; 1 Yohana 3:10-12.

7. Wakristo wa kweli hufunganishwaje pamoja ulimwenguni pote?

7 Upendo wa kidugu ndiyo “gundi” (guluu) ambayo hufunganisha watumishi wa Mungu katika muungamano: “Jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.” (Wakolosai 3:14) Na ni lazima Wakristo wa kweli wawe na muungamano pamoja na ndugu zao ulimwenguni pote, kwa maana Neno la Mungu laamuru hivi: “Nyote mnene mamoja . .. pasiwe kwenu faraka . . . mhitimu katika nia moja na shauri moja.” (1 Wakorintho 1:10) Ili kudumisha upendo na muungamano huu duniani pote, ni lazima watumishi wa Mungu wasiwemo katika mambo ya kisiasa ya ulimwengu huu. Yesu alisema: “Wao si sehemu ya ulimwengu, kama vile mimi si sehemu ya ulimwengu.”​—Yohana 17:16, NW.

8. Yesu alionyeshaje jambo ambalo ni lazima Wakristo wafanye?

8 Yesu alionyesha kadiri ya wazo alilokuwa akifikiria wakati Petro alipotumia upanga kuondosha sikio la mmoja wa wanaume waliokuwa wamekuja kukamata Yesu. Je! Yesu alitia moyo kutumia nguvu hata kulinda Mwana wa Mungu dhidi ya wapinzani? Sivyo, bali alimwambia Petro hivi: “Rudisha upanga wako mahali pake.” (Mathayo 26:52) Hivyo, Wakristo wa kweli hawajitii katika vita vya mataifa wala katika umwagaji wowote mwingine wa damu ya kibinadamu hata kama watafia imani kwa sababu ya msimamo wao wa kutokuwamo, kama vile imekuwa kwa wengi muda wa karne zilizopita na hata katika wakati wetu. Wao wajua kwamba ni Ufalme wa Mungu tu chini ya Kristo utakaokomesha vita na umwagaji damu milele.​—Zaburi 46:9; Mathayo 6:9, 10; 2 Petro 3:11-13.

9. (a) Historia yatuambia nini kuhusu Wakristo wa kwanza? (b) Hiyo yatofautianaje na dini za Jumuiya ya Wakristo?

9 Historia yahakikisha kwamba Wakristo wa karne ya kwanza walikataa kumwaga damu ya kibinadamu. Mtu mmoja aliyekuwa profesa wa theolojia kutoka Uingereza, Peter De Rosa, aandika hivi: “Kumwaga damu kulikuwa dhambi mbaya sana. Hii ndiyo sababu Wakristo walipinga pambano la kuuana katika nyanja za maonyesho. . . . Ingawa kufanya vita na kutumia nguvu kulihitajiwa kabisa ili kuhifadhi Roma, Wakristo walihisi hawawezi kujiunga humo. . . . Wakristo walijifikiria wenyewe, kama vile Yesu, kuwa wajumbe wa amani; wao hawangeweza kuwa mawakili wa kifo katika hali zozote.” Kwa upande ule mwingine, dini zisizo na muungamano za Jumuiya ya Wakristo zimeivunja amri ya upendo na kumwaga damu nyingi sana. Wao wamekuwa si wajumbe wa amani bali wamerudia-rudia kuwa mawakili wa kifo.

Babuloni Mkubwa Mwenye Hatia ya Damu

10. Babuloni Mkubwa ni nini, na kwa nini yaitwa hivyo?

10 Shetani ndiye “mtawala wa ulimwengu huu,” “mungu wa mfumo huu wa mambo.” (Yohana 12:31; 2 Wakorintho 4:4, NW) Sehemu ya ulimwengu wa Shetani ni mfumo wa duniani pote wa dini bandia ambao amejenga kwa karne kadhaa, kutia na Jumuiya ya Wakristo na makasisi wayo. Biblia yauita mfumo huu wa ulimwenguni pote wa dini bandia kuwa “Babuloni Mkubwa, mama ya makahaba [wa kiroho] na ya vitu vya kunyarafisha vya dunia.” (Ufunuo 17:5, NW) Mizizi ya dini bandia ya leo yarudi nyuma kwenye jiji la kale la Babuloni, ambalo lilikuwa limekolea katika dini bandia na katika mafundisho na mazoea yenye kuvunjia Mungu heshima. Ndiyo sababu kifanani cha Babuloni ya kale chaitwa Babuloni Mkubwa, milki ya ulimwengu ya dini bandia.

11. Biblia yasema nini kuhusu Babuloni Mkubwa, na kwa nini?

11 Kuhusu Babuloni wa kidini, Neno la Mungu lasema: “Katika yeye ilipatikana damu ya manabii na ya watakatifu na ya wale wote ambao wamechinjwa juu ya dunia.” (Ufunuo 18:24, NW) Ni jinsi gani dini za ulimwengu huu zilivyo na daraka kwa damu ya wote wale waliochinjwa? Katika jambo la kwamba dini zote hizi​—makanisa ya Jumuiya ya Wakristo na dini zisizo za Kikristo kadhalika​—zimeunga mkono, zikaachilia tu, au hata zikaongoza katika vita vya mataifa; pia zimenyanyasa na kuua watu wanaohofu Mungu ambao hawakukubaliana nao.

Kumbukumbu la Kuvunjia Mungu Heshima

12. Kwa nini makasisi wa Jumuiya ya Wakristo ndio wenye kulaumika zaidi ya viongozi wengine wa kidini?

12 Makasisi wa Jumuiya ya Wakristo ni wenye kulaumika zaidi katika kumwaga damu kuliko viongozi wengine wa kidini. Kwa nini? Kwa sababu zaidi ya kuchukua jina la Mungu liwe juu yao wenyewe, wamelichukua la Kristo pia. Kwa njia hiyo walijipatia wajibu wa kufuata mafundisho ya Yesu. (Yohana 15:10-14) Lakini hawakufuata mafundisho hayo, hivyo wakileta suto kubwa juu ya Mungu na Kristo pia. Daraka la damu yenye kumwagwa na makasisi limekuwa la moja kwa moja katika zile Krusedi (shughuli za kidini za kupambana na wazushi), katika vita vingine vya kidini, mabaraza ya kutesa wazushi, na minyanyaso. Na limekuwa lisilo la moja kwa moja katika kuachilia vita ambamo makanisa yameua wanadamu wenzao katika mabara mengine.

13. Makasisi walikuwa na daraka la nini kuanzia karne ya 11 hadi ya 13?

13 Kwa kielelezo, kuanzia karne ya 11 hadi ya 13, makasisi wa Jumuiya ya Wakristo walianzisha zile Krusedi. Zilitokeza umwagaji mbaya sana wa damu na utekaji nyara kwa jina la Mungu na la Kristo. Mamia kwa maelfu waliuawa. Krusedi hizo zilihusisha ndani kuchinja kijinga maelfu ya watoto walioshawishwa washiriki katika Krusedi ya Watoto ya mwaka 1212.

14, 15. Mtungaji mmoja Mkatoliki aelezaje juu ya kile ambacho Kanisa Katoliki lilianzisha katika karne ya 13?

14 Katika karne ya 13, Kanisa Katoliki la Kiroma liliidhinisha ogofyo jingine baya sana lenye kumvunjia Mungu heshima​—lile Baraza la Kutesa Wazushi. Lilianza katika Ulaya na kuenea likafikia zile Amerika, likiendelea kwa karne zaidi ya sita. Likiwa limeanzishwa na kutegemezwa na upapa, lilikuwa jaribio la kutesa-tesa na kufagilia mbali wote wasiokubaliana na kanisa. Ingawa hapo kwanza kanisa lilikuwa limenyanyasa watu wasio Wakatoliki, Baraza la Kutesa Wazushi lilikuwa na mweneo mkubwa zaidi.

15 Peter De Rosa, ambaye ataarifu kwamba yeye ni “Mkatoliki mzalendo,” asema hivi katika kitabu chake cha hivi majuzi Vicars of Christ​—The Dark Side of the Papacy: “Kanisa ndilo lilikuwa na daraka la kunyanyasa Wayahudi, daraka la lile Baraza la Kutesa Wazushi, daraka la kuchinja maelfu ya wazushi, daraka la kuanza tena utesi-tesi katika Ulaya ili uwe sehemu ya hatua za hukumu. .. . Mapapa waliwaweka rasmi na kufuta hata wamaliki, wakidai kwamba walazimishe raia zao kufuata Ukristo wakiwa chini ya tisho la kuteswa-teswa na kuuawa. . . . Hasara iliyotokana na ujumbe wa Gospeli ilikuwa ya kuogofya sana.” “Uhalifu” mmoja tu uliotendwa na baadhi ya waliouawa ni kwamba wao walikuwa na Biblia.

16, 17. Ni maelezo gani ambayo yatolewa kuhusu lile Baraza la Kutesa Wazushi?

16 Kuhusu Papa Innocent wa 3 wa mapema karne ya 13, De Rosa ataarifu hivi: “Imekadiriwa kwamba katika ule mnyanyaso wa mwisho uliokuwa ndio wa kinyama zaidi ya yote chini ya Mmaliki [Mroma] Diocletian [karne ya tatu] Wakristo wapatao elfu mbili waliangamia, ulimwenguni pote. Katika kituko cha kwanza cha ukatili wa Krusedi ya Papa Innocent [dhidi ya “wazushi” katika Ufaransa] mara kumi ya hesabu hiyo ya watu walichinjwa. . . . Yashtusha kugundua kwamba, kwa dharuba moja, papa mmoja aliua Wakristo wengi kuliko waliouawa na Diocletian. . . . [Innocent] hakuingiwa na mashaka ya dhamiri kuhusu kutumia jina la Kristo ili kufanya kila jambo ambalo Kristo alikataa.”

17 De Rosa ataarifu kwamba “kwa jina la papa, [washiriki wa baraza la kutesa wazushi] ndio waliokuwa na daraka la kushambulia ustahifu wa kibinadamu kwa njia iliyo ya kinyama zaidi na yenye kuchukua muda mwingi zaidi katika historia ya jamii ya watu.” Kuhusu Torquemada mshiriki wa baraza la kutesa wazushi katika Hispania, yeye asema hivi: “Alipowekwa rasmi katika 1483, yeye alitawala kimabavu kwa miaka kumi na mitano. Majeruhi wake walikuwa zaidi ya 114,000 na 10,220 kati yao walichomwa.”

18. Mwandikaji mmoja aelezaje hali ya lile Baraza la Kutesa Wazushi, naye atoa sababu gani ya kuendelea kwalo kwa karne zaidi ya sita?

18 Mwandikaji huyu amalizia hivi: “Kumbukumbu la mambo yaliyofanywa na Baraza la Kutesa Wazushi lingekuwa aibu kwa tengenezo lolote; kwa kanisa Katoliki, linawaharibia sifa kweli kweli. . . . Historia yaonyesha kwamba upapa uliapa kuwa adui mwenye kuchukia sana haki ya msingi, kwa zaidi ya karne sita mfululizo. Kati ya mapapa wanane mfululizo tangu karne ya kumi na tatu na kuendelea, hakuna hata mmoja wao aliyeonyesha kutokubaliana na theolojia na njia yenye kutumiwa na Baraza la Kutesa Wazushi. Bali, wao walifululiza mmoja baada ya mwingine kuongezea kuni za ukatili kwenye harakati hii yenye kuua. Fumbo ni hili: mapapa wangewezaje kuendelea katika uzushi huu usiofaa kizazi baada ya kizazi? Wangewezaje kukana Gospeli ya Yesu kwenye kila hatua?” Yeye ajibu hivi: “Mapontifu [mapapa] walipendelea kupinganisha Gospeli kuliko kumpinganisha mtangulizi ‘asiye na makosa,’ kwa maana kufanya hivyo kungeubomoa upapa wenyewe.”

19. Ni utendaji gani mwingine wa uasi sheria ulioachiliwa tu na makasisi walio wengi?

19 Pia ushiriki wa makasisi katika kuanzisha biashara ya utumwa kwa njia yenye jeuri iliasi sheria. Mataifa ya Jumuiya ya Wakristo yalitorosha maelfu mengi ya Waafrika, wakawapeleka mbali na mabara yao wenyewe, na kwa karne nyingi wakawatenda unyama kimwili na kiakili wakiwa watumwa. Ni wachache kati ya jamii ya makasisi waliopinga jambo hilo kwa bidii. Baadhi yao hata walidai yalikuwa mapenzi ya Mungu.​—Ona Mathayo 7:12.

Hatia ya Damu Katika Karne ya 20

20. Hatia ya damu ya yule mtu wa kuasi sheria imefikiaje kilele katika karne hii?

20 Hatia ya damu ya mtu wa kuasi sheria ilifikia kilele katika karne yetu. Makasisi wametegemeza vita ambavyo vimechukua uhai wa makumi ya mamilioni, vita vilivyo vibaya zaidi katika historia yote. Wao waliunga mkono pande zote mbili katika vita vile viwili vya ulimwengu, ambamo watu wa dini ile ile, “ndugu na ndugu,” waliuana. Mathalani, katika Vita ya Ulimwengu 2, Wakatoliki Wafaransa na Waamerika waliua Wakatoliki Wajeremani na Waitalia; Waprotestanti Waingereza na Waamerika waliua Waprotestanti Wajeremani. Nyakati fulani, waliua wengine wasiokuwa wa dini ile ile lakini wenye malezi ya taifa lile lile moja. Vita hivyo viwili vya ulimwengu vilifoka pale pale katikati ya Jumuiya ya Wakristo na visingaliwezekana kama makasisi wangalitii ile amri ya kupenda, na kufundisha wafuasi wao wafanye ivyo hivyo.

21. Vyanzo vya kilimwengu vyasema nini kuhusu mhusiko wa makasisi katika vita?

21 The New York Times ilijulisha hivi kwa uthabiti: “Mabaraza ya Kikatoliki ya utawala wa makasisi yaliunga mkono vita vya mataifa yao karibu sikuzote zilizopita, yakibariki vikosi na kutoa sala za ushindi, na kwa upande ule mwingine kikundi kingine cha maaskofu kikasali kwa ajili ya tokeo la kinyume. . . . Mpingano uliopo kati ya roho ya Kikristo na mwenendo wa vita . . . waelekea kuzidi kuonekana wazi kwa wengi, kwa kadiri ambavyo silaha zinakuwa za ukatili zaidi.” Na U.S.News & World Report ilisema hivi: “Heshima nyingi ya Ukristo katika ulimwengu imeharibiwa vibaya sana na wingi wa mara ambazo jeuri imetumiwa na yale yenye kuitwa mataifa ya Kikristo eti.”

22. Makasisi wana daraka la jambo gani jingine katika wakati wetu?

22 Pia, ingawa leo hakuna Baraza la Kutesa Wazushi, makasisi wametumia mkono wa Serikali kunyanyasa “manabii” na “watakatifu” ambao hutofautiana nao. Wamebana viongozi wa kisiasa ‘kutunga ukorofi kwa kusingizia kwamba sheria ndiyo yafuatwa.’ Kwa njia hii, wamesababisha au wakakubali watu wenye kuhofu Mungu katika karne yetu wapigwe marufuku, watiwe gerezani, wapigwe, wateswe-teswe, na hata wauawe.​—Ufunuo 17:6; Zaburi 94:20, The New English Bible.

Kupasishwa Kutoa Hesabu

23. Kwa nini Mungu atapasisha kutoa hesabu yule mtu wa kuasi sheria?

23 Kwa kweli, katika dini bandia imepatikana damu ya manabii, na ya watakatifu, na ya wote wale ambao wamechinjwa duniani. (Ufunuo 18:24) Kwa kuwa umwagaji damu ulio mbaya zaidi umetokea katika Jumuiya ya Wakristo, hatia ya makasisi ndiyo kubwa zaidi. Yafaa kama nini kwamba Biblia yawabandika jina la kuwa “mtu wa kuasi [sheria]”! Lakini Neno la Mungu lataarifu hivi pia: “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.” (Wagalatia 6:7) Kwa hiyo Mungu atawapasisha makasisi hao waasi sheria kutoa hesabu.

24. Ni matukio gani yenye kutikisa ulimwengu yatatokea karibuni?

24 Yesu alisema: “Ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.” (Mathayo 7:23) Na alijulisha wazi hivi: “Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.” (Mathayo 7:19) Wakati unakaribia kasi ambapo mwisho wenye moto utapata yule mtu wa kuasi sheria, pamoja na dini yote bandia, wakati ambapo viasili vya kisiasa ambavyo wamefanya ukahaba navyo vitageuka viwarukie: “Hao watamchukia yule kahaba, nao watamfanya kuwa mkiwa na uchi, watamla nyama yake, watamteketeza kabisa kwa moto.” (Ufunuo 17:16) Kwa kuwa matukio hayo yenye kutikisa ulimwengu yatatukia karibuni, ni lazima watumishi wa Mungu wayajulishe kwa wengine. Makala ifuatayo itachunguza jinsi wamekuwa wakifanya hivyo.

Maswali kwa Kupitia

◻ Mtu wa kuasi sheria ni nini, na ilisitawi jinsi gani?

◻ Ni lazima Wakristo wa kweli watokeze uzaaji gani wa matunda mazuri?

◻ Babuloni Mkubwa ni nani, na mwanamke huyo ana hatia ya damu kadiri gani?

◻ Yule mtu wa kuasi sheria amefanyiza kumbukumbu la matendo gani yenye kuvunjia Mungu heshima?

◻ Ni jinsi gani Mungu atapasisha kutoa hesabu yule mtu wa kuasi sheria?

[Picha katika ukurasa wa 18]

Zile Krusedi zilitokeza umwagaji damu ulio mbaya sana kwa jina la Mungu na la Kristo

[Hisani]

Kwa hisani ya Maktaba ya Uingereza

[Picha katika ukurasa wa 19]

“Mabaraza ya Kikatoliki ya utawala wa makasisi yaliunga mkono vita vya mataifa yao karibu sikuzote”

[Hisani]

U.S. Army

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki