Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w90 2/1 kur. 10-14
  • Kutambulisha “Mtu wa Kuasi [Sheria]”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutambulisha “Mtu wa Kuasi [Sheria]”
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mwanzo wa Mtu wa Kuasi Sheria
  • Kutambulisha Mwasi Sheria Huyo
  • Kujikweza Wenyewe
  • Uasi Dhidi ya Ibada ya Kweli
  • Jamii ya Makasisi Wasiofuata Maandiko Yasitawi
  • Mafundisho ya Kipagani
  • Upapa
  • Kifo cha Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Uasi Juu ya Mungu Unafunuka
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Hukumu ya Mungu Dhidi ya “Mtu wa Kuasi [Sheria]”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Kufunuliwa kwa Yule Mwasi Sheria
    Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha Yetu ya Kikristo—2019
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
w90 2/1 kur. 10-14

Kutambulisha “Mtu wa Kuasi [Sheria]”

“Yule mwasi sheria atafunuliwa, ambaye Bwana Yesu atamwondolea mbali.”​—2 WATHESALONIKE 2:8, NW.

1, 2. Kwa nini ni muhimu tutambulishe mtu wa kuasi sheria?

TWAISHI katika muda wa kuasi sheria. Ni tukio lenye kustaajabisha ulimwenguni pote. Kila mahali kuna hofu ya wahalifu wenye kuasi sheria na tisho lao kwa mwili na mali zetu. Hata hivyo, kuna kiasili fulani chenye kudhuru zaidi kisiri ambacho kimekuwa kikifanya kazi kwa karne nyingi. Katika Biblia chaitwa “mtu wa kuasi [sheria].”

2 Ni muhimu tutambulishe mtu huyu wa kuasi sheria. Kwa nini? Kwa sababu ameazimia kubomoa msimamo wetu mwema pamoja na Mungu na tumaini letu la uhai wa milele. Jinsi gani? Kwa kutufanya tuuache ukweli na mahali pao tuamini mambo bandia, hivyo akitupotosha tuache kuabudu Mungu “katika roho na kweli.” (Yohana 4:23) Ni wazi kutokana na vitendo vyake kwamba kiasili hiki hususa chenye kuasi sheria hupinga Mungu na makusudi yake, na pia watu wake waliojiweka wakfu.

3. Biblia yaelekezaje uangalifu wetu kwenye mwasi sheria?

3 Biblia yaeleza juu ya mtu huyu wa kuasi sheria kwenye 2 Wathesalonike 2:3. Kwa kuvuviwa na roho ya Mungu, mtume Paulo aliandika hivi: “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana [siku ya Yehova ya kuharibu mfumo huu mwovu] haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu [uasi-imani, NW]; akafunuliwa yule mtu wa kuasi [sheria].” Hapa Paulo alitoa unabii kwamba uasi-imani ungesitawi, na mtu wa kuasi sheria angetokea kabla ya mwisho wa mfumo huu. Kwa uhakika, Paulo alitaarifu hivi katika 2Th 2 mstari wa 7: “Ile siri [fumbo, NW] ya kuasi hivi sasa inatenda kazi.” Kwa hiyo katika karne ya kwanza, mwasi sheria huyu alikuwa ameanza kujidhihirisha.

Mwanzo wa Mtu wa Kuasi Sheria

4. Ni nani mwanzishi na mtegemezaji wa yule mtu wa kuasi sheria?

4 Ni nani aliyeanzisha na kuunga mkono mtu huyu wa kuasi sheria? Paulo ajibu hivi: “Kuwapo kwa huyo mwenye kuasi sheria ni kulingana na uendeshaji shughuli wa Shetani pamoja na kila kazi yenye nguvu nyingi na ishara na vionyeshi vyenye kusema uwongo na pamoja na kila udanganyifu usio mwadilifu kwa ajili ya wale wanaoangamia, liwe kama lipizo kwa sababu wao hawakuukubali upendo wa ule ukweli ili wapate kuokolewa.” (2 Wathesalonike 2:9, 10, NW) Kwa hiyo Shetani ndiye baba na mtegemezaji wa mtu wa kuasi sheria. Na sawa na vile Shetani apinga Yehova, makusudi Yake, na watu Wake, ndivyo pia afanyavyo mtu wa kuasi sheria, awe atambua au hatambui hivyo.

5. Ni msiba gani wamngoja mwasi sheria huyo na wale wenye kumfuata?

5 Wale ambao waambatana na mtu huyu wa kuasi sheria watapata msiba ule ule utakaompata yeye​—uharibifu: “Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake.” (2 Wathesalonike 2:8) Wakati huo wa kuharibiwa kwa mtu wa kuasi sheria na kwa wenye kumuunga mkono (“hao wanaopotea”) utakuja karibuni “wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake; katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele.”​—2 Wathesalonike 1:6-9.

6. Ni habari gani zaidi ambazo Paulo atoa kuhusu mwasi sheria huyo?

6 Paulo aeleza zaidi juu ya mtu huyu mwenye kuasi sheria, akisema: “Yeye amejiweka katika hali ya kupinga na hujiinua mwenyewe juu ya kila mmoja aitwaye ‘mungu’ au kitu cha uchaji, hivi kwamba yeye huketi katika hekalu la Yule Mungu, akijionyesha peupe kuwa ni mungu.” (2 Wathesalonike 2:4, NW) Kwa hiyo Paulo aonya kwamba Shetani angeinua mwasi sheria, kitu bandia cha uchaji, ambaye hata angejiweka mwenyewe juu ya sheria ya Mungu.

Kutambulisha Mwasi Sheria Huyo

7. Kwa nini twakata shauri kwamba Paulo hakuwa akiongea kuhusu mtu mmoja, na mtu wa kuasi sheria asimamia nini?

7 Je! Paulo alikuwa akinena juu ya mtu mmoja? Hapana, kwa maana yeye ataarifu kwamba “mtu” huyu alikuwa akionekana wazi katika siku ya Paulo na angeendelea kuwako mpaka Yehova amharibu kwenye mwisho wa mfumo huu. Hivyo, yeye amekuwako kwa karne nyingi. Kwa uwazi, hakuna mtu halisi ambaye ameishi muda mrefu jinsi hiyo. Kwa hiyo ni lazima usemi “mtu wa kuasi [sheria]” uwe wasimamia baraza la watu, au jamii.

8. Mtu wa kuasi sheria ni nani, na ni nini baadhi ya mambo yenye kumtambulisha?

8 Wao ni akina nani? Ushuhuda waonyesha kwamba wao ni lile baraza la makasisi wenye kiburi, wenye kujitakia makuu wa Jumuiya ya Wakristo, ambao kwa muda wa karne zilizopita wamejipandisha juu katika mamlaka ya kuwa wakijiamulia mambo kama watakavyo. Hilo laweza kuonwa kwa uhakika wa kwamba kuna maelfu ya dini tofauti-tofauti na mafarakano ya ibada katika Jumuiya ya Wakristo, kila moja ikiwa na makasisi wayo yenyewe, na bado kila moja ikihitilafiana na nyinginezo katika jambo fulani la fundisho au zoea. Hali hii ya kugawanyika ni ushuhuda wa wazi kwamba hazifuati sheria ya Mungu. Haziwezi kuwa zatoka kwa Mungu. (Linganisha Mika 2:12; Marko 3:24; Warumi 16:17; 1 Wakorintho 1:10.) Jambo la ujumla lililo katika dini zote hizi ni kwamba haziyashiki imara mafundisho ya Biblia, kwa kuwa zimekwisha kuvunja ile kanuni ya kwamba: ‘Msiyapite yale yaliyoandikwa.’​—1 Wakorintho 4:6; ona pia Mathayo 15:3, 9, 14.

9. Ni imani gani zisizo za Kimaandiko ambazo yule mwasi sheria ameweka mahali pa kweli za Biblia?

9 Hivyo, mwasi sheria huyu ni jumla ya watu wengi: makasisi wa Jumuiya ya Wakristo. Wote pamoja, wawe ni mapapa, mapadri, mapatriaki, au wahubiri wa Kiprotestanti, hushiriki daraka kwa dhambi za kidini za Jumuiya ya Wakristo. Wamebadili kweli za Mungu kwa uwongo wa kipagani, wakifundisha mafundisho yasiyo ya Kimaandiko kama vile kutokufa kwa nafsi ya kibinadamu, moto wa helo, pargatori, na Utatu. Wao ni kama viongozi wa kidini ambao Yesu aliambia hivi: “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. . . . Yeye ni mwongo, na baba wa huo [uwongo].” (Yohana 8:44) Mazoea yao yawafichua pia kuwa waasi sheria, kwa maana wao hushiriki katika utendaji mbalimbali wenye kuvunja sheria za Mungu. Kwa watu hao Yesu asema hivi: “Ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”​—Mathayo 7:21-23.

Kujikweza Wenyewe

10. Yule mwasi sheria amekuwa na uhusiano gani pamoja na watawala wa kisiasa?

10 Historia yaonyesha kwamba wale walio katika jamii hii ya mtu wa kuasi wameonyesha kiburi na majivuno mengi sana hivi kwamba kwa kweli wameamrisha watawala wa ulimwengu. Kwa kusingizia kufuata fundisho la ‘haki ya kimungu ya wafalme,’ makasisi wamedai kwamba wao ndio wapatanishi muhimu kati ya watawala na Mungu. Wamewavika taji wafalme na wamaliki na kuwaondoa katika kiti cha kifalme na wakaweza kugeuza matungamo ya watu yaunge mkono au yawe dhidi ya watawala. Kwa kweli, wao wamesema, kama walivyosema wakuu wa makuhani Wayahudi ambao walimkataa Yesu: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.” (Yohana 19:15) Hata hivyo, Yesu alifundisha wazi hivi: “Ufalme wangu si sehemu ya ulimwengu huu.”​—Yohana 18:36, NW.

11. Makasisi wamejikwezaje?

11 Ili ijikweze hata zaidi juu ya watu wa kawaida, jamii hii yenye kuasi sheria imejichagulia mavazi tofauti, kwa kawaida yakiwa meusi. Zaidi ya hilo, wamejivika aina zote za mapambo yenye uvutio wa kifalme, pamoja na mataji, misalaba, na kofia za kiaskofu. (Linganisha Mathayo 23:5, 6.) Lakini Yesu na wafuasi wake hawakuwa na nguo za jinsi hiyo; walivalia kama watu wa kawaida. Pia makasisi wamejitwalia vyeo kama “Baba,” “Baba Mtakatifu,” “Reverendi,” “Reverendi Mkubwa Zaidi,” “Mtukufu,” na “Mwadhamu,” ambavyo vyaongezea ‘kujiinua wenyewe juu ya kila mtu.’ Hata hivyo, Yesu alifundisha hivi kuhusu vyeo vya kidini: “Msimwite mtu baba duniani.” (Mathayo 23:9) Vivyo hivyo, Elihu, katika kuwakanusha wafariji wanafiki wa Ayubu, alisema: “Tafadhali, nisiupendelee uso wa mtu; wala sitajipendekeza kwa mtu ye yote.”​—Ayubu 32:21.

12. Paulo alisema makasisi walikuwa wakitumikia nani kwa kweli?

12 Wakati Paulo alipotaarifu kule nyuma kwamba mtu wa kuasi sheria alikuwa tayari ameanza utendaji wake, pia alisema hivi kuhusu wale ambao huonyesha mtazamo wa kuasi sheria wa mtu huyo: “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.”​—2 Wakorintho 11:13-15.

Uasi Dhidi ya Ibada ya Kweli

13. Ni nini uasi-imani ambao Paulo alitabiri?

13 Paulo alisema kwamba mtu huyu wa kuasi sheria angesitawi pamoja na uasi-imani. Kwa uhakika, kidokezo cha kwanza ambacho Paulo alitoa kuhusu kutambulishwa kwa jamii hii ya kuasi sheria ni kwamba “siku ya Yehova [wakati ambapo Yehova ataharibu mfumo huu mwovu wa mambo] . . . haitakuja isipokuwa uasi-imani uje kwanza.” (2 Wathesalonike 2:2, 3, NW) Lakini “uasi-imani” wamaanisha nini? Katika maana yenye kuhusika hapa, haumaanishi kurudi nyuma au kuangukia mbali tu kwa sababu ya udhaifu wa kiroho. Neno la Kigiriki lililotumiwa hapa kwa “uasi-imani” lilimaanisha, miongoni mwa mambo mengine, “mpotoko wa kuacha uaminifu-mshikamanifu” au “ukaidi.” Tafsiri kadhaa hulifasiri kuwa “uasi.” Tafsiri ya William Barclay yataarifu hivi: “Siku hiyo haiwezi kuja mpaka ule Uasi Mkubwa uwe umetukia.” The Jerusalem Bible yauita “ule Ukaidi Mkubwa.” Kwa hiyo, kuhusiana na habari ambayo Paulo anazungumza, “uasi-imani” wamaanisha ukaidi dhidi ya ibada ya kweli.

14. Ni wakati gani uasi-imani ulipoanza kusitawi kwa bidii?

14 Huku kuasi imani kulisitawi jinsi gani? Kwenye 2 Wathesalonike 2:6, NW, Paulo aliandika, kuhusu siku yake, juu ya “kitu ambacho hutenda kama kizuizi” juu ya yule mwasi sheria. Hicho kilikuwa nini? Ilikuwa ile kani ya uzuizi wa mitume. Kuwapo kwao, wakiwa na zawadi zao zenye nguvu nyingi walizopewa na roho takatifu, kulizuia uasi-imani usienee kwa kipuku. (Matendo 2:1-4; 1 Wakorintho 12:28) Lakini mitume walipokufa, kufikia karibu mwisho wa karne ya kwanza, zile breki za uzuizi ziliondolewa.

Jamii ya Makasisi Wasiofuata Maandiko Yasitawi

15. Ni mpango gani ulioanzishwa imara na Yesu kwa ajili ya kundi la Kikristo?

15 Kundi ambalo Yesu alianzisha lilisitawi katika karne ya kwanza chini ya mwongozo wa wazee (waangalizi) na watumishi wa huduma. (Mathayo 20:25-27; 1 Timotheo 3:1-13; Tito 1:5-9) Watu hawa walichukuliwa kutokana na kundi. Walikuwa wanaume wa kiroho wenye kuweza mambo wasio na mazoezi maalumu ya kitheolojia, sawa na vile Yesu asivyokuwa na mazoezi hayo. Kwa kweli, wapinzani wake walijiuliza hivi kwa mshangao: “Imekuwaje mtu huyu ana maarifa ya herufi, hali yeye hajajifunza kwenye zile shule?” (Yohana 7:15, NW) Na kwa habari ya mitume, viongozi wa kidini walionelea ivyo hivyo: “Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.”​—Matendo 4:13.

16. Uasi-imani huo ulisababishaje mgeuko wa kuacha kile kigezo cha Ukristo wa karne ya kwanza kwa tengenezo la kundi?

16 Hata hivyo, uasi-imani huo uliingiza mawazo yaliyotolewa kwa makasisi wa Kiyahudi na hatimaye kwa muundo wa kidini wa Roma. Wakati ulipokuwa ukipita na kukatukia mgeuko wa kuacha imani ya kweli, jamii ya makasisi isiyo ya Kimaandiko ilisitawi. Papa mwenye kuvikwa taji akaanza kutawala juu ya jamii ya makardinali, nao wakachukuliwa kutoka kati ya mamia ya maaskofu na maaskofu wakuu, nao wakapandishwa cheo kutoka kuwa mapadri wenye kuzoezwa katika seminari. Hivyo, si muda mrefu baada ya karne ya kwanza, jamii ya kifumbo ya makasisi ilichukua uongozi katika Jumuiya ya Wakristo. Jamii hii haikufuata kigezo cha wazee Wakristo na watumishi wa huduma wa karne ya kwanza bali ilifuata kigezo cha mifumo ya dini ya kipagani.

17. Ni lini, hasa, nguvu za yule mwasi sheria zilipoimarika?

17 Mapema hata kwenye karne ya tatu W.K., waamini wa kawaida walikuwa wameshushwa wakawa na cheo cha daraja la pili la watu wa kawaida tu. Pole kwa pole yule mtu wa kuasi sheria akajitwalia hatamu za mamlaka. Mamlaka hii ilitiliwa nguvu wakati wa utawala wa mmaliki Mroma Konstantino, hasa baada ya Baraza la Nikaya katika 325 W.K. Ndipo Kanisa na Serikali zikaungamanishwa pamoja. Hivyo, mtu wa kuasi sheria​—makasisi wa Jumuiya ya Wakristo​—kwa karne nyingi wakawa mlolongo wa waasi-imani kwa kufanya ukaidi dhidi ya Mungu wa kweli, Yehova. Sheria na mipango ambayo wamefuata ni yao wenyewe wala si ya Mungu.

Mafundisho ya Kipagani

18. Yule mwasi sheria alichagua kufuata mafundisho gani ya kipagani yenye kukufuru?

18 Pia mtu huyo wa kuasi sheria mwenye kusitawi aliazima mafundisho ya kipagani. Kwa kielelezo, mungu wa fumbo la Utatu usioeleweka aliwekwa badala ya yule Mmoja ambaye husema: “Mimi ni Bwana [Yehova, AW]; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine.” “Mimi ni Bwana [Yehova, NW], wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu.” (Isaya 42:8; 45:5) Huku kubadilisha kweli za Mungu kwa kuweka mahali pazo mawazo ya kibinadamu, hata ya kipagani, kulipanuliwa kukahusisha kufuru moja zaidi: kumstahi mno Mariamu mnyenyekevu wa Biblia kuwa “Mama ya Mungu” wa Jumuiya ya Wakristo. Hivyo, wenye kuendeleza mafundisho hayo bandia, jamii ya makasisi, wakaja kuwa ndio “magugu” mabaya zaidi yaliyopandwa na Shetani ili kujaribu kusonga ile mbegu nzuri iliyopandwa na Kristo.​—Mathayo 13:36-39.

19. Jumuiya ya Wakristo imevunjika-vunjika jinsi gani muda wa karne zilizopita, lakini ni nini kilichoendelezwa?

19 Mitengano na migawanyiko mikubwa ilipotokea, Jumuiya ya Wakristo ilivunjika-vunjika ikawa mamia ya dini na mafarakano. Lakini kila dini au farakano jipya, isipokuwa katika visa vichache, ilidumisha mgawanyiko wayo kati ya makasisi na watu wa kawaida. Hivyo, jamii ya yule mtu wa kuasi sheria imeendelezwa kufikia leo hii. Na ingali yaendelea kujiweka juu ya watu wa kawaida ikiwa na mavazi na vyeo vyenye majina makubwa-makubwa. Kwa uwazi, Paulo hakutia chumvi aliposema kwamba jamii ya yule mtu wa kuasi sheria ingejitukuza na kujikweza kwenye cheo kama cha mungu.

Upapa

20. Chanzo kimoja cha Kikatoliki chaelezaje juu ya papa?

20 Kielelezo kimoja cha utukuzaji huo ni kile cha upapa wa Roma. Kamusi ya kidini iliyotungwa na Lucio Ferraris, ikatangazwa kwa chapa katika Italia, yaeleza papa kuwa “wa adhama na ukuu mwingi sana hivi kwamba yeye si mtu tu bali, ni kama Mungu, na Vikari wa Mungu.” Taji lake ni taji mara tatu “akiwa mfalme wa mbingu, wa dunia na wa helo.” Kamusi iyo hiyo yaendelea kusema: “Papa ni kama Mungu duniani, mwana-mfalme pekee wa waaminifu wa Kristo, mfalme mkuu zaidi ya wafalme wote.” Yaongezea hivi: “Nyakati fulani papa aweza kuitangua sheria ya kimungu.” Pia, The New Catholic Dictionary yataarifu hivi juu ya papa: “Mabalozi wake hutangulizwa mbele ya washiriki wengine wa baraza la mabalozi.”

21. Tofautisha vitendo vya papa na vile vya Petro na malaika mmoja.

21 Tofauti na wanafunzi wa Yesu, mara nyingi papa huvaa mavazi yenye madoido sana na hukubali kupokea sifa nyingi mno za wanadamu. Papa huruhusu watu wamwinamie, waipige busu pete yake, na kumbeba juu ya mabega yao akiwa katika kiti maalumu. Lo, ni ubatili ulioje ambao mapapa wameonyesha muda wa karne zilizopita! Ni tofauti sana na usahili wa kujinyenyekeza kwa Petro, ambaye alimwambia hivi Kornelio, ofisa Mroma wa jeshi aliyepiga magoti ili ampe ushikamoo: “Simama, . . . kwa vyovyote mimi ni binadamu tu”! (Matendo 10:25, 26, Jerusalem Bible ya Kikatoliki) Tena ni tofauti kama nini na yule malaika aliyempa mtume Yohana Ufunuo! Yohana alijaribu kumwinamia malaika huyo kwa kumwabudu, lakini malaika akajulisha wazi hivi: “Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako, na wa ndugu zako manabii, na wa wale wayashikao maneno ya kitabu hiki. Msujudie [Mwabudu, NW] Mungu.”​—Ufunuo 22:8, 9.

22. Yule mwasi sheria aweza kutambulishwa kwa kanuni gani ya Kimaandiko?

22 Je! huu ni mkadirio mkali mno kuhusu jamii ya makasisi? Twaweza kuamua jambo hili kwa kutumia kanuni ambayo Yesu alitoa kutambulisha manabii bandia: “Mtawatambua kwa matunda yao.” (Mathayo 7:15, 16) Basi, tunda la makasisi limekuwa nini muda wa karne zilizopita na katika karne yetu wenyewe ya 20? Ni msiba gani utapata mtu huyu wa kuasi sheria, na ni nani atashiriki msiba huo? Wale wenye kuhofu Mungu kikweli wana daraka gani kuhusiana na mwasi sheria huyu? Makala zinazofuata zitazungumza mambo haya.

Maswali ya Kupitia:

◻ Mtu wa kuasi sheria ni nini, nayo ilidhihirika lini?

◻ Biblia yatambulishaje mtungaji wa jamii hii ya kuasi sheria?

◻ Makasisi wamejikwezaje juu ya watu?

◻ Ni mafundisho na mazoea gani ya uasi-imani yalisitawishwa na makasisi?

◻ Mtazamo wa mapapa watofautianaje na ule wa Petro na malaika mmoja?

[Picha katika ukurasa wa 14]

Mtume Petro, tofauti na mapapa, hakuruhusu mwanadamu amsujudie

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki