Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w95 11/15 kur. 26-30
  • William Tyndale—Mwanamume Mwenye Busara

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • William Tyndale—Mwanamume Mwenye Busara
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Hatua ya Imani
  • Katazo—Kwa Sababu Gani?
  • Kwenda Ulaya na Matatizo Zaidi
  • Ushindi—Ujapokuwa Upinzani
  • Antwerp, Kusalitiwa, na Kifo
  • Biblia ya William Tyndale Kwa Ajili ya Watu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
  • Jinsi Biblia Ilivyotufikia—Sehemu ya Pili
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Kimbilio la Wachapaji wa Biblia
    Amkeni!—2002
  • Kutafsiri Biblia Kulikuwa Hatari
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
w95 11/15 kur. 26-30

William Tyndale—Mwanamume Mwenye Busara

William Tyndale alizaliwa katika Uingereza “kwenye mipaka ya Wales,” yaelekea katika Gloucestershire, ingawa mahali penyewe na tarehe kamili hazijulikani. Katika Oktoba 1994, Uingereza ilisherehekea mwaka wa 500 wa kuzaliwa kwa mwanamume “aliyetupatia Biblia yetu ya Kiingereza.” Kwa ajili ya kazi hiyo Tyndale aliuawa. Kwa sababu gani?

WILLIAM TYNDALE alihitimu katika somo la Kigiriki na Kilatini. Katika Julai 1515, akiwa na umri wa miaka 21 tu, alipokea digrii katika elimu kwenye Chuo Kikuu cha Oxford. Kufikia 1521 alitawazwa kuwa kasisi wa Katoliki ya Kiroma. Wakati huo dini ya Kikatoliki katika Ujerumani ilikuwa katika msukosuko kwa sababu ya utendaji wa Martin Luther. Lakini Uingereza ilibaki kuwa nchi ya Kikatoliki hadi King Henry 8 alipojitenga hatimaye na Roma katika 1534.

Ingawa Kiingereza kilikuwa lugha ya kawaida katika siku ya Tyndale, elimu yote ilikuwa katika Kilatini. Pia Kilatini kilikuwa lugha ya kanisa na ya Biblia. Katika 1546 Baraza la Trent lilisisitiza kwamba Vulgate ya Kilatini ya Jerome ya karne ya tano ilikuwa itumiwe kipekee. Hata hivyo, ni wenye elimu tu wangeweza kuisoma. Kwa nini watu wa Uingereza wanyimwe Biblia kwa Kiingereza na uhuru wa kuisoma? “Jerom[e] pia alitafsiri biblia kwa lugha yake: kwa nini tusiitafsiri pia?” ndio uliokuwa utetezi wa Tyndale.

Hatua ya Imani

Kufuatia wakati alipokuwa Oxford na labda masomo ya ziada kwenye Cambridge, Tyndale aliwafunza wana wachanga wa John Walsh kwa muda wa miaka miwili katika Gloucestershire. Katika kipindi hicho alisitawisha tamaa yake ya kutafsiri Biblia katika Kiingereza, na bila shaka alikuwa na fursa ya kusitawisha ustadi wake wa kutafsiri kwa msaada wa maandishi ya Biblia mpya ya Erasmus iliyokuwa na maneno ya Kigiriki na ya Kilatini katika safu zilizo sambamba. Katika 1523, Tyndale aliiacha familia ya Walsh akasafiri kwenda London. Kusudi lake lilikuwa aombe ruhusa ya kutafsiri kutoka kwa Cuthbert Tunstall, askofu wa London.

Ruhusa kutoka kwa Tunstall ilikuwa ya lazima kwa sababu ya maafikiano ya 1408 ya katiba ya kidini ya Oxford, yajulikanayo kuwa Mabaraza ya Sheria ya Oxford, yalitia ndani marufuku ya kutafsiri au kusoma Biblia katika lugha ya kijamii, ila kwa ruhusa ya askofu. Kwa kuthubutu kukaidi katazo hilo, wahubiri wengi wa kusafiri-safiri waliojulikana kuwa Lollards walichomwa kama wazushi. Lollards hao waliisoma na kugawanya Biblia ya John Wycliffe, tafsiri ya Kiingereza kutoka kwa Vulgate. Tyndale alihisi kwamba wakati ulikuwa umefika wa kutafsiri maandishi ya Kikristo kutoka Kigiriki hadi tafsiri mpya ya asilia kwa ajili ya kanisa lake na kwa ajili ya watu wa Uingereza.

Askofu Tunstall alikuwa mtu mwenye elimu aliyekuwa amefanya mengi kumtia moyo Erasmus. Ukiwa uthibitisho wa ustadi wake, Tyndale alikuwa ametafsiri moja ya hotuba za Isocrates, maandishi magumu sana ya Kigiriki, ili kupata kibali cha Tunstall. Tyndale alikuwa amepata matumaini kwamba Tunstall angeendeleza urafiki na udhamini na kukubali dokezo lake la kutafsiri Maandiko. Askofu huyo angefanya nini?

Katazo—Kwa Sababu Gani?

Ingawa Tyndale alikuwa na barua rasmi ya kujijulisha Tunstall hakukubali amtembelee. Hivyo ilimbidi Tyndale aandike akiomba wakutane. Kwamba hatimaye Tunstall alijishusha akutane na Tyndale haijulikani, lakini jibu lake lilikuwa, ‘Sina nafasi katika nyumba yangu ya mtu kufanya kazi ya utafsiri.’ Kwa nini Tunstall alimpuuza Tyndale kimakusudi hivyo?

Kazi ya marekebisho ya Luther katika kontinenti ya Ulaya ilikuwa ikisababishia Kanisa Katoliki hangaiko kubwa, kukiwa na matokeo mabaya katika Uingereza. Katika 1521, King Henry 8 alichapisha makala yenye nguvu akimtetea papa dhidi ya Luther. Kwa shukrani papa akampa Henry cheo cha “Mtetea-Imani.”a Kadinali Wolsey wa Henry pia alikuwa na shughuli nyingi, akiharibu vitabu vya Luther vilivyoingizwa nchini isivyo halali. Akiwa askofu Mkatoliki mwaminifu-mshikamanifu kwa papa, kwa mfalme, na kadinali wake, Tunstall alihisi kuwa na wajibu wa kukomesha kufikiri kokote ambako huenda kukaunga mkono mwasi Luther. Tyndale alikuwa mshukiwa wa kwanza. Kwa sababu gani?

Alipokuwa akikaa na familia ya Walsh, Tyndale alikuwa amesema kwa ujasiri dhidi ya kutokuwa na ujuzi na ushupavu wa makasisi wa mahali hapo. Miongoni mwao alikuwa John Stokesley aliyekuwa amemjua Tyndale katika Oxford. Mwishowe alichukua mahali pa Cuthbert Tunstall akiwa askofu wa London.

Upinzani kwa Tyndale ni dhahiri pia katika bishano pamoja na kasisi mwenye cheo kikubwa aliyesema: “Afadhali tukose sheria ya Mungu kuliko kukosa ya papa.” Kwa maneno yenye kukumbukwa, jibu la Tyndale lilikuwa: ‘Namkaidi Papa na sheria zake zote. Ikiwa Mungu ataniruhusu niishi, kwa muda mfupi, nitamfanya kijana mkulima ajue Maandiko zaidi kuliko ujuavyo.’

Ilimbidi Tyndale kusimama mbele ya msimamizi wa diosisi ya Worcester kwa mashtaka ya uwongo ya uzushi. “Alinitisha vibaya sana, na kunitusi,” Tyndale akakumbuka baadaye, akiongezea kwamba alikuwa ametendwa kama “mbwa.” Lakini hakukuwa na ushahidi wa kumthibitisha Tyndale kuwa mzushi. Wanahistoria huamini kwamba mambo hayo yote yalielezwa Tunstall kwa siri ili kuchochea uamuzi wake.

Baada ya kukaa London mwaka mmoja, Tyndale akafikia mkataa huu: “Hakuna nafasi katika jumba la kifalme la bwana wangu la London la kutafsiri Testamenti mpya, lakini pia . . . hakuna yeyote angeruhusu kutafsiriwa kwa Biblia katika Uingereza yote.” Hakukosea. Chini ya hali yenye kizuizi iliyosababishwa na utendaji wa Luther, ni mchapishaji yupi katika Uingereza angethubutu kutokeza Biblia katika Kiingereza? Hivyo katika 1524, Tyndale alivuka Mlango-Bahari wa Uingereza, pasipo kurudi kamwe.

Kwenda Ulaya na Matatizo Zaidi

Pamoja na vitabu vyake vya thamani, William Tyndale alipata kimbilio Ujerumani. Alienda na Pauni 10 ambazo rafiki yake Humphrey Monmouth, mfanya-biashara mashuhuri wa London alizokuwa amempa kwa fadhili. Zawadi hiyo katika nyakati zile ilikuwa karibu itoshe kumwezesha Tyndale achapishe Maandiko ya Kigiriki aliyokusudia kutafsiri. Baadaye Monmouth akafungwa kwa kumsaidia Tyndale na eti kwa kumuunga mkono Luther. Akiwa amehojiwa na kutupwa katika gereza la Tower la London, Monmouth aliachiliwa baada tu ya kumsihi Kadinali Wolsey amsamehe.

Mahali penyewe ambapo Tyndale alienda katika Ujerumani hapajulikani. Ushahidi fulani hulenga Hamburg, ambapo huenda alikaa mwaka mmoja. Je, alikutana na Luther? Jambo hilo halijulikani, hata ingawa shtaka dhidi ya Monmouth lasema kwamba alikutana naye. Jambo moja ni hakika: Tyndale alikuwa na shughuli nyingi akitafsiri Maandiko ya Kigiriki. Angechapishia hati zake wapi? Alimkabidhi Peter Quentell katika Cologne kazi hiyo.

Mambo yote yalikuwa yakiendelea vizuri hadi mpinzani John Dobneck, aliyejulikana kwa jina jingine kuwa Cochlaeus, alipojua kilichokuwa kikitendeka. Bila kukawia Cochlaeus akaripoti aliyopata kujua kwa rafiki wa karibu wa Henry 8 ambaye upesi akatafuta katazo dhidi ya kuchapishwa kwa tafsiri ya Tyndale na Quentell.

Tyndale na msaidizi wake, William Roye, wakakimbia wasiuawe, wakibeba kurasa za Gospeli ya Mathayo zilizokuwa zimechapishwa. Walisafiri kwa meli kwenye mto Rhine hadi Worms, ambako walimaliza kazi yao. Muda si muda nakala 6,000 za chapa ya kwanza ya New Testament ya Tyndale zikafanyizwa.b

Ushindi—Ujapokuwa Upinzani

Kutafsiri na kuchapisha lilikuwa tatizo moja. Kupeleka Biblia Uingereza lilikuwa tatizo jingine. Wapelelezi wa kanisa na mamlaka za kiserikali walikuwa wameazimia kuzuia usafirishaji hadi ng’ambo ya Mlango-Bahari wa Uingereza, lakini wanabiashara wenye urafiki walikuwa na jawabu. Yakiwa yamefichwa kwenye mabunda ya nguo na bidhaa nyingine za biashara, mabuku hayo yaliingizwa kwa siri hadi fuo za Uingereza na hadi Scotland. Tyndale alitiwa moyo, lakini pigano lake lilikuwa tu ndio limeanza.

Katika Februari 11, 1526, Kardinali Wolsey, akiandamana na maaskofu 36 na waheshimiwa wengine wa kanisa, walikusanyika karibu na Kathedro ya St. Paul katika London ili “kuona vikapu vilivyojaa vitabu vikitupwa motoni.” Miongoni mwavyo mlikuwa nakala fulani za tafsiri yenye thamani ya Tyndale. Katika chapa hiyo ya kwanza, sasa kuna nakala mbili tu zilizoko. Iliyo kamili pekee (ikikosa tu ukurasa wenye kichwa) imo katika Maktaba ya Uingereza. Kiajabu, nyingine isiyo na kurasa 71, ilipatikana katika Maktaba ya Kathedro ya St. Paul. Namna ilivyofika humo hakuna ajuaye.

Akiwa na ujasiri, Tyndale aliendelea kutokeza chapa mpya za tafsiri yake, zilizotwaliwa moja kwa moja na kuchomwa na makasisi Waingereza. Kisha Tunstall akabadili hila zake. Alifanya mapatano na mfanya-biashara aliyeitwa Augustine Packington anunue vitabu vyovyote vilivyoandikwa na Tyndale, kutia ndani New Testament, ili avichome. Packington akafanya mpango na Tyndale, wakakubaliana. Chronicle ya Halle husema: “Askofu huyo alipata vitabu, Packington akapata shukrani, naye Tyndale akapata pesa. Baadaye wakati Testamenti Mpya zaidi zilipochapishwa, hizo ziliingia Uingereza kwa wingi sana.”

Kwa nini makasisi walikuwa wenye upinzani mwingi kuelekea tafsiri ya Tyndale? Ilhali Vulgate ya Kilatini ilijaribu kufunika andiko takatifu, tafsiri ya Tyndale kutoka Kigiriki cha awali ilitoa kwa mara ya kwanza ujumbe wa Biblia kwa lugha yenye kueleweka kwa Waingereza. Kwa kielelezo, katika 1 Wakorintho sura ya 13, Tyndale alichagua kutafsiri neno la Kigiriki a·gaʹpe kuwa “upendo” badala ya “hisani.” Alisisitiza juu ya “kutaniko” badala ya “kanisa” ili kukazia waabudu, si majengo ya kanisa. Hata hivyo, jambo la mwisho lisilovumilika kwa makasisi lilitokea wakati Tyndale alipoweka neno “mzee” mahali pa neno “kuhani” na kutumia “toba” badala ya “fanya utubio,” kwa njia hiyo akiwavua makasisi uwezo wa kikuhani waliodhani kuwa nao. Kuhusu jambo hilo David Daniell asema: “Hakuna Purgatori; hakuna ungamo na utubio. Yale mafundisho mawili yaliyolipatia Kanisa utajiri na nguvu yaliporomoka.” (William Tyndale—A Biography) Hiyo ndiyo sai ambayo tafsiri ya Tyndale ilitokeza, na usomi wa kisasa hukubali kabisa usahihi wa uteuzi wake wa maneno.

Antwerp, Kusalitiwa, na Kifo

Katikati ya 1526 na 1528, Tyndale alihamia Antwerp, ambapo angeweza kuhisi salama miongoni mwa wafanya-biashara Waingereza. Huko aliandika The Parable of the Wicked Mammon, The Obedience of a Christian Man, na The Practice of Prelates. Tyndale akaendeleza kazi yake ya kutafsiri naye alikuwa wa kwanza kutumia jina la Mungu, Yehova, katika tafsiri ya Kiingereza ya Maandiko ya Kiebrania. Jina hilo hupatikana mara 20.

Maadamu Tyndale alikaa na rafikiye na mfadhili wake Thomas Poyntz katika Antwerp, alikuwa salama kutokana na hila za Wolsey na wapelelezi wake. Alijulikana sana kwa utunzaji wake wa wagonjwa na maskini. Hatimaye, Mwingereza Henry Phillips akajiingiza kwa ujanja kwenye mambo ya siri ya Tyndale. Tokeo likawa kwamba katika 1535, Tyndale alisalitiwa na kupelekwa hadi Ngome ya Vilvorde kilometa kumi kaskazini mwa Brussels. Huko akatiwa gerezani kwa miezi 16.

Haijulikani vizuri ni nani aliyemhonga Phillips, lakini aliyeshukiwa ni Askofu Stokesley, aliyekuwa na shughuli nyingi wakati huo za kuwachoma “wazushi” katika London. Kwenye kitanda chake cha kifo katika 1539, Stokesley “alifurahia kwamba katika muda wa maisha yake alikuwa amechoma wazushi hamsini,” asema W. J. Heaton katika The Bible of the Reformation. Aliyetiwa katika idadi hiyo alikuwa William Tyndale, aliyenyongwa kabla ya mwili wake kuchomwa hadharani katika Oktoba 1536.

Wanatheolojia mashuhuri watatu kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Louvain, ambapo Phillips alikuwa, walikuwa katika baraza lililomhukumu Tyndale. Makasisi watatu kutoka Louvain na maaskofu watatu pamoja na waheshimiwa wengine walikuwepo pia kuona Tyndale akihukumiwa uzushi na kuondolewa mamlaka yake ya ukasisi. Wote walifurahia kifo chake akiwa na umri upatao miaka 42.

“Tyndale,” akasema Robert Demaus aliyekuwa mwandikaji wa habari za maisha ya watu zaidi ya miaka mia moja iliyopita, “alikuwa mwenye kutokeza sikuzote kwa unyofu wake wenye uhodari.” Kwa John Frith, msaidizi wake aliyechomwa na Stokesley katika London, Tyndale aliandika hivi: “Sikubadili silabi moja ya neno la Mungu dhidi ya dhamiri yangu, wala sitafanya hivyo leo, hata ikiwa huenda nikapewa vyote vilivyoko duniani, viwe ni anasa, heshima, au utajiri.”

Hivyo ndivyo William Tyndale alivyotoa uhai wake kwa ajili ya pendeleo la kuwapa watu wa Uingereza Biblia ambayo wangeweza kuelewa kwa urahisi. Alilipa gharama kubwa kadiri gani—lakini alitoa zawadi yenye thamani kubwa kama nini!

[Maelezo ya chinis]

a Fidei Defensor [Mtetea-Imani] baadaye lilipigwa chapa kwenye sarafu za nchi hiyo, na Henry akaomba jina hilo la cheo lipewe watakaotawala baada yake. Leo linaonekana kwenye sarafu za Uingereza likizingira kichwa cha mtawala likiwa Fid. Def., au likiwa tu F.D. Kwa kupendeza, “Mtetea-Imani” baadaye lilichapishwa kwa ukumbusho wa King James katika King James Version ya 1611.

b Hesabu hii haijulikani vizuri; vyanzo vingine husema 3,000.

[Sanduku katika ukurasa wa 29]

TAFSIRI ZA MAPEMA

OMBI la Tyndale la kutafsiri Biblia kwa lugha ya watu wa kawaida halikuwa lisilo la akili au la kwanza. Tafsiri katika lugha ya Anglo-Saxon ilifanywa katika karne ya kumi. Biblia zilizochapishwa kutoka Kilatini zilikuwa zimegawanywa bila kizuizi katika Ulaya mwishoni mwa karne ya 15: Kijerumani (1466), Kiitaliano (1471), Kifaransa (1474), Kicheki (1475), Kiholanzi (1477), na Kikatalani (1478). Katika 1522, Martin Luther alichapisha New Testament katika Kijerumani. Swali pekee ambalo Tyndale aliuliza lilikuwa ni kwa nini Uingereza isiruhusiwe kufanya vivyo hivyo.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

Biblia katika Mandhari ya nyuma: © The British Library Board; William Tyndale: Kwa ruhusa ya fadhili ya Principal, Fellows and Scholars of Hertford College, Oxford

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki