Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w97 5/1 kur. 30-31
  • Imani ya Wazazi Yathawabishwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Imani ya Wazazi Yathawabishwa
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kutenda kwa Imani
  • Yule Mtoto Mchanga Agunduliwa
  • Somo Kwetu Sisi
  • Musa Aliamua Kumwabudu Yehova
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Kitu Chenye Thamani Zaidi Kuliko Hazina za Misri
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2002
  • Musa—Mtu Halisi au wa Hadithi?
    Amkeni!—2004
  • “Mwimbieni Yehova”!
    Igeni Imani Yao
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
w97 5/1 kur. 30-31

Walifanya Mapenzi ya Yehova

Imani ya Wazazi Yathawabishwa

KWA Waisraeli, kuzaliwa kwa mtoto wa kiume kulikuwa sababu ya kushangilia sana. Kulimaanisha kwamba nasaba ingeendelea na kwamba urithi wa shamba ungebaki katika hiyo familia. Lakini wapata mwaka wa 1593 K.W.K., kwa Waebrania, huenda ikawa kuzaa mwana kulionekana kuwa laana zaidi kuliko kuwa baraka. Kwa nini? Kwa sababu Farao wa Misri, akiwa na wasiwasi juu ya kuongezeka haraka kwa idadi ya Wayahudi katika eneo lililokuwa chini ya uongozi wake, alikuwa ameamuru kwamba watoto wa kiume wao wote waliozaliwa karibuni walipaswa kuuawa.—Kutoka 1:12, 15-22.

Ilikuwa ni wakati huo wa jaribio hilo ovu sana la kuangamiza jamii nzima-nzima kwamba Amramu na Yokebedi, wenzi waliooana Waebrania, walipozaa mtoto mchanga, mzuri mvulana. Ni rahisi kuwazia jinsi shangwe yao ilivyofunikwa na woga walipokumbuka agizo la Farao. Hata hivyo, Amramu na Yokebedi walipomwangalia mtoto wao mchanga mvulana, waliazimia kwa uthabiti kutomwacha, hata matokeo yaweje.—Kutoka 2:1, 2; 6:20.

Kutenda kwa Imani

Kwa miezi mitatu Amramu na Yokebedi walimficha mtoto wao mchanga. (Kutoka 2:2) Hata hivyo, hilo lilikuwa hatari, kwa kuwa Waebrania na Wamisri waliishi karibu-karibu. Yamkini yeyote aliyepatikana akijaribu kuhepa agizo la Farao angeadhibiwa kwa kuuawa—na huyo mtoto mchanga angeuawa pia. Hivyo basi, wazazi hao wenye kujitoa wangeweza kufanya nini ili mwanao na wao wenyewe waendelee kuwa hai?

Yokebedi alikusanya machipukizi ya mafunjo. Mafunjo ni tete ngumu, sawa na mianzi, na yana mabua yenye pande tatu zenye unene upatao wa kidole. Yaweza kufika kimo cha meta sita. Wamisri walitumia mmea huo kutengeneza karatasi, mikeka, tanga, makubazi, na mashua nyepesi.

Yokebedi alitengeneza kwa mafunjo kisanduku chenye kutoshea mtoto wake mchanga. Kisha akakipaka lami na bereu kukiunganisha na kukifanya kisivuje maji. Ndipo Yokebedi akamweka mtoto wake mchanga ndani ya hicho chombo na kukiweka katikati ya tete ukingoni mwa Mto Naili.—Kutoka 2:3.

Yule Mtoto Mchanga Agunduliwa

Binti ya Yokebedi, Miriamu, alisimama karibu ili kuona kile ambacho kingetukia baadaye. Kisha binti ya Farao akaja kwenye Mto Naili kuoga.a Labda Yokebedi alijua kwamba binti-mfalme alizuru sehemu hiyo ya Mto Naili mara nyingi, akaacha kimakusudi hicho kisanduku mahali kingegunduliwa kwa urahisi. Kwa vyovyote, binti ya Farao alikiona upesi hicho kisanduku kilichofichwa katika tete, na alimwita mmojawapo wa vijakazi wake kukileta. Alipoona mtoto anayetoa machozi ndani yacho, huruma yake iliamshwa. Alitambua kwamba huyo alikuwa mtoto mchanga Mwebrania. Hata hivyo, angewezaje kufanya mtoto mzuri hivyo auawe kimakusudi? Mbali na huruma za kibinadamu, huenda ikawa binti ya Farao alikuwa amevutiwa na itikadi ya Kimisri yenye kupendwa kwamba kuingia mbinguni kulitegemea rekodi ya matendo yenye fadhili maishani mwa mtu.b—Kutoka 2:5, 6.

Miriamu, aliyekuwa akiangalia kutoka mbali, alimfikia binti ya Farao. “Je, niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu?” akauliza. Binti-mfalme akajibu: “Haya! enenda.” Miriamu akakimbia hadi kwa mama yake. Punde si punde, Yokebedi alikuwa akisimama mbele ya binti ya Farao. “Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee,” binti-mfalme akamwambia, “nami nitakupa mshahara wako.” Huenda ikawa kwamba kufikia wakati huu binti Farao aling’amua kwamba Yokebedi alikuwa mama ya huyo mtoto mchanga.—Kutoka 2:7-9.

Yokebedi alimlea mtoto wake hadi alipoachishwa kunyonya.c Hilo lilimpa fursa nyingi zenye thamani za kumfundisha juu ya Mungu wa kweli, Yehova. Kisha Yokebedi akamrudisha mtoto kwa binti Farao, aliyemwita huyo mvulana Musa, jina linalomaanisha ‘alitolewa majini.’—Kutoka 2:10.

Somo Kwetu Sisi

Amramu na Yokebedi walitumia kikamili fursa fupi waliyopata kumfundisha mwana wao kanuni za ibada safi. Wazazi leo wapaswa kufanya hivyohivyo. Kwa kweli, ni muhimu wafanye hivyo. Shetani Ibilisi “hutembea huku na huku kama simba anayenguruma, akitafuta sana kunyafua mtu fulani.” (1 Petro 5:8) Angependa vijana wenye thamani wawe wahasiriwa wake—wavulana na wasichana—walio na tazamio la kuwa watumishi wazuri wa Yehova. Umri wao mchanga haumfanyi Shetani awaonee huruma vijana! Kwa sababu hiyo, wazazi wenye hekima huzoeza watoto wao wachanga kumhofu Mungu wa kweli, Yehova.—Mithali 22:6; 2 Timotheo 3:14, 15.

Kwenye Waebrania 11:23, ile jitihada ya Amramu na Yokebedi kumficha mtoto wao mchanga katika miezi mitatu ya kwanza ya maisha yake imerekodiwa kuwa tendo la imani. Wazazi hao wawili wenye kuhofu Mungu walionyesha itibari katika uwezo wa Yehova wa kuokoa kwa kukataa kumwacha pekee mtoto wao, na kwa ajili ya hilo walibarikiwa. Sisi pia twapaswa kuonyesha ushikamano kabisa kwa sheria na kanuni za Yehova, tukiwa na uhakika kwamba chochote ambacho Yehova huruhusu kitupate hatimaye kitatokeza hali-njema na furaha ya milele.—Waroma 8:28.

[Maelezo ya Chini]

a Wamisri waliabudu Mto Naili ukiwa mungu wa uzazi. Waliamini kwamba maji yao yalikuwa na nguvu za kutokeza uwezo wa kuzaa sana na hata kurefusha maisha.

b Wamisri waliamini kwamba wakati wa kufa roho ya mtu ingekariri mbele ya Osiris maneno thabiti kama “Sikutaabisha mtu yeyote,” “Sikuvinyima maziwa vinywa vya watoto wanyonyao,” na “Nilimpa mkate mwenye njaa na kinywaji yule mwenye kiu.”

c Nyakati za kale, watoto wengi walinyonyeshwa kwa kipindi kirefu zaidi kuliko ilivyo leo. Yamkini Samweli alikuwa angalau na umri wa miaka mitatu alipoachishwa kunyonya, na Isaka alikuwa na umri wa miaka mitano hivi.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki