Wanasarakasi wa Majabali ya Milima
JIJI la kale na la nyika iitwayo En-gedi iliyolizunguka yalikuwa kando ya ufuko wa magharibi wa Bahari Iliyokufa. Vijia vyenye miamba na maporomoko humwandalia makao bora mbuzi wa mwitu wa Bara lililoahidiwa, afananaye na waonekanao hapa.
Kiumbe huyo asiyeteleza yu miongoni mwa maajabu ya kuumbwa kwa wanyama. Acheni tufungue Biblia zetu na kumwangalia kwa ukaribu zaidi mnyama huyu mwenye kuvutia sana.
“Milima Mirefu Ndiko Waliko Mbuzi wa Mwitu”
Ndivyo alivyoimba mtunga-zaburi. (Zaburi 104:18) Mbuzi wa mwitu wameandaliwa vifaa vizuri vya kuishi katika mahali pa juu! Ni wepesi sana, wakijongea juu ya ardhi yenye mawemawe kwa uhakika mkubwa na kwa mwendo wa kasi. Kwa kiasi fulani hilo ni kwa sababu ya muundo wa kwato zao. Nafasi iliyo kati ya kwato yaweza kupanuka kulingana na uzito wa huyo mbuzi, ikimfanya huyo mnyama kuwa imara sana asimamapo au ajongeapo juu ya mitelemko yenye miamba myembamba.
Mbuzi wa mwitu pia wana usawaziko usio wa kawaida. Wanaweza kuruka umbali mkubwa na kutua juu ya mwamba mdogo sana uwezao tu kutoshea miguu yote minne. Wakati mmoja mwana-biolojia Douglas Chadwick alimchunguza kwa makini mbuzi wa mwitu wa aina nyingine akitumia usawaziko wake ili kuepuka kunaswa katika mwamba uliokuwa mdogo sana hivi kwamba hangeweza kugeuka. Yeye asema hivi: “Baada ya kuutupia jicho mwamba uliofuata ambao ulikuwa meta zipatazo 120 chini, huyo mbuzi aliweka imara miguu yake ya mbele na pole kwa pole akapitisha miguu yake ya nyuma juu ya kichwa chake kana kwamba alikuwa akitaka kuvingirika kisarakasi. Nilipokuwa nikizuia pumzi yangu, huyo mbuzi aliendelea kufanya hivyo hadi miguu yake ya nyuma ikatua hivi kwamba sasa alikuwa akikabili upande aliokuwa ametoka.” (National Geographic) Si ajabu kwamba mbuzi wa mwitu wameitwa “wanasarakasi wa majabali ya milima”!
“Je! Wajua Majira ya Kuzaa Kwao Mbuzi-Mwitu?”
Mbuzi wa mwitu ni viumbe waoga sana. Wanapendelea kukaa mbali na mwanadamu. Kwa kweli, ni vigumu kwa watu kuwakaribia na kuwachunguza kwa makini wakiwa katika hali yao ya asili. Hivyo, Mwenye “makundi juu ya milima elfu” kwa kufaa angeweza kumwuliza Ayubu hivi: “Je! wajua majira ya kuzaa kwao mbuzi-mwitu walio majabalini?”—Zaburi 50:10; Ayubu 39:1.
Silika aliyopewa na Mungu humjulisha mbuzi wa mwitu wa kike wakati wa kuzaa uwadiapo. Yeye hutafuta mahali salama na kuzaa mwana-mbuzi mmoja au wawili, kwa kawaida mwishoni mwa Mei au katika Juni. Wana-mbuzi waliotoka kuzaliwa hujipatia uthabiti wa kutoteleza baada ya siku chache tu.
“Ni Ayala Apendaye na Paa Apendezaye”
Mfalme Sulemani mwenye hekima aliwasihi sana waume hivi: “Umfurahie mke wa ujana wako. Ni ayala apendaye na paa apendezaye.” (Mithali 5:18, 19) Hilo halikukusudiwa kuwadunisha wanawake. Yaonekana, Sulemani alikuwa akirejezea kwa njia isiyo ya moja kwa moja urembo, madaha, na sifa nyingine zenye kutokeza za wanyama hao.
Mbuzi wa mwitu yu miongoni mwa ‘viumbe hai’ ambavyo ni ushahidi mwingi wa hekima ya Muumba. (Mwanzo 1:24, 25) Je, hatufurahi kwamba Mungu ametuzingira na viumbe vingi sana vyenye kuvutia sana?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Kwa hisani ya Chuo Kikuu cha Athens