Tertio—Mwandishi Mwaminifu wa Paulo
TERTIO alikabili kazi ngumu. Mtume Paulo alitaka kumtumia akiwa mwandishi wake alipokuwa akiandika barua ndefu kwa Wakristo wenzi katika Roma. Hii ingekuwa kazi ngumu.
Kwa nini lilikuwa jambo gumu kuwa mwandishi katika karne ya kwanza W.K.? Kazi kama hiyo ilifanywa namna gani? Ni vifaa gani vya kuandikia vilivyotumiwa wakati huo?
Waandishi Katika Nyakati za Kale
Katika jamii ya kale ya Kigiriki na Kiroma, kulikuwa na waandishi wa aina tofauti-tofauti. Baadhi ya watu walitumikia wakiwa waandishi wa serikali—waandishi wa umma ambao walifanya kazi katika ofisi za serikali. Pia kulikuwa na waandishi wa umma wakitoa huduma zao kwa wananchi katika masoko. Waandishi wa watu binafsi (kwa kawaida watumwa) waliwekwa na matajiri. Kisha, pia, kulikuwa na marafiki ambao walifurahia kuandika barua kwa niaba ya wengine. Kulingana na msomi E. Randolph Richards, stadi za hawa waandishi wasio rasmi “zingeweza kutofautiana kati ya uwezo wa chini kabisa wa lugha na/au utaratibu wa uandishi bora hadi utokezaji wa haraka wa barua sahihi, wa kufaa, na wa kufurahisha.”
Nani angeweza kuwatumia waandishi? Kwanza, wale ambao hawakujua kusoma wala kuandika. Mikataba mingi ya kale na barua za kibiashara zilimalizwa kwa kuandikwa maelezo ambayo mwandishi alithibitisha kwamba alikuwa ameandika hiyo hati kwa sababu mtu aliyemkabidhi hiyo kazi hakuwa na uwezo. Sababu ya pili ya kuajiri mwandishi inaelezwa na barua ya kale kutoka Thebes, Misri. Iliandikwa kwa Asklepiades fulani, ilisema mwishoni: “Eumelus, mwana wa Herma, aliandika kwa niaba yake . . . kwani, kwa kiasi fulani yeye huandika polepole.”
Na bado, kujua jinsi ya kuandika na kusoma haionekani kuwa sababu ya msingi katika kutumia mwandishi. Kulingana na mfafanuzi wa Biblia, John L. McKenzie, “pengine hata jambo la kuhangaisha halikuwa usomekaji, bali lilikuwa uzuri katika uandishi, au angalau kwa ajili ya unadhifu” ambao uliwachochea watu kuchagua huduma za mwandishi. Hata kwa wasomi, uandishi ulikuwa wenye kuchosha, hasa kama maandishi marefu na yaliyonakshiwa sana yalihusika. Msomi J. A. Eschlimann asema kwamba yeyote ambaye angeweza kufanya hivyo “aliepuka kwa furaha kazi hii ya uandishi, akiikabidhi chini ya uangalizi wa watumwa, waandishi wa kitaaluma.” Isitoshe, ni rahisi kueleweka kwa nini watu hawakupenda kuandika barua zao kwa kufikiria vifaa vilivyotumiwa na hali ya kazi.
Kwa kawaida kifaa kilichotumiwa kuandikia katika karne ya kwanza W.K. kilikuwa mafunjo. Chane nyembamba zilipatikana kutoka mmea huu kwa kukata sehemu za katikati zilizo nyororo za mashina yake kwa marefu. Safu ya chane ilitandazwa. Safu nyingine iliwekwa kwa pembe mraba juu ya safu ya kwanza. Hizi mbili zilishikanishwa kwa msongo, ikitokeza “karatasi.”
Haikuwa rahisi kuandika juu yake. Ilikuwa yenye kukwaruza na yenye nyuzinyuzi. Kulingana na msomi Angelo Penna, “nyuzinyuzi zilizo kama sifongo za mafunjo zilichangia katika usambaaji wa wino, hasa katika mifereji midogo sana ambayo ilibaki kati ya chane nyembamba.” Mwandishi angeweza kufanya kazi akiwa amekaa kimarufaa kwenye ardhi akishikilia karatasi juu ya ubao kwa mkono mmoja. Kama hakuwa mzoefu au kifaa hakikuwa bora, unyoya wa kuandikia, au tete-kalamu, ingeweza kukwama katika mafunjo, karatasi ingeweza kuchanika, au maandishi kutosomeka.
Wino ulitengenezwa kutokana na mchanganyiko wa masizi na gundi. Ukiuzwa ukiwa mgumu, ulipasa uchanganywe na maji katika kidau kabla haujatumiwa kuandika. Kati ya zana ambazo mwandishi kama vile Tertio bila shaka angekuwa nazo ni kisu kwa ajili ya kunoa tete-kalamu na sifongo iliyo chepechepe ili kufuta makosa yake. Kila herufi ilipasa kuandikwa kwa uangalifu. Hivyo basi, uandishi uliendelea kwa taratibu sana na kwa ugumu fulani.
‘Mimi, Tertio, Nawasalimu’
Kati ya salamu zilizotiwa ndani mwishoni mwa barua kwa Waroma ni za mwandishi wa Paulo, ambaye aliandika: “Mimi, Tertio, ambaye nimeufanya uandikaji wa barua hii, nawasalimu nyinyi katika Bwana.” (Waroma 16:22) Hii ni pindi pekee katika maandishi ya Paulo ambapo rejezo la wazi linafanywa kwa mmoja wa waandishi wake.
Twajua kidogo kuhusu Tertio. Kutokana na salamu zake “katika Bwana,” twaweza kufikia mkataa kwamba alikuwa Mkristo mwaminifu. Labda alikuwa mshiriki wa kutaniko la Korintho na huenda ikawa aliwajua Wakristo wengi katika Roma. Msomi wa Biblia Giuseppe Barbaglio adokeza kwamba Tertio alikuwa mtumwa au aliyewekwa-huru. Kwa nini? Kwanza, kwa sababu, “kwa ujumla waandishi walikuwa wa tabaka hili; kisha, kwa sababu jina lake la Kilatini . . . lilikuwa la kawaida sana miongoni mwa watumwa au waliowekwa-huru.” “Kwa hiyo,” asema Barbaglio, “hakuwa mwandishi mtaaluma, alikuwa mfanyakazi mwenzi ambaye kwa njia hii alimsaidia Paulo kuandika maandishi yake marefu zaidi na yenye kuelezwa kwa ufasaha zaidi: utumishi wa thamani sana, uliomsaidia Paulo kuokoa wakati na asiwe mchovu.”
Kwa hakika kazi hii ya Tertio ni ya thamani sana. Baruku alimfanyia Yeremia kazi kama hiyo, kama vile Silvano alivyomfanyia Petro. (Yeremia 36:4; 1 Petro 5:12) Ni pendeleo kama nini wafanyakazi-wenzi hao walikuwa nalo!
Kuwaandikia Waroma
Barua kwa Waroma iliandikwa Paulo alipokuwa mgeni wa Gayo, labda katika Korintho. Hiyo ilikuwa karibu 56 W.K., wakati wa safari ya tatu ya umishonari ya mtume huyo. (Waroma 16:23) Ingawa tunajua kwa hakika kwamba Paulo alimtumia Tertio akiwa mwandishi wake kuandika barua hii, hatujui jinsi gani hasa alivyomtumia. Njia yoyote aliyotumia, kazi hiyo haiwezi kuwa ilifanywa kwa urahisi. Lakini tunaweza kuwa na hakika juu ya jambo hili: Kama sehemu nyingine ya Biblia, barua ya Paulo kwa Waroma ‘ilipuliziwa na Mungu.’—2 Timotheo 3:16, 17.
Barua hii ilipomalizwa, Tertio na Paulo walikuwa wameandika maelfu ya maneno, wakitumia karatasi kadhaa za mafunjo. Baada ya kushikanishwa pamoja kwa gundi pambizoni, karatasi hizi zilifanyiza hatikunjo, labda zikiwa na urefu wa meta tatu hadi nne. Barua hiyo ilikunjwa kwa uangalifu na kufungwa kabisa. Kisha inaonekana Paulo aliikabidhi kwa Fibi, dada kutoka kutaniko la Kenkrea, ambaye alikuwa karibu kuanza safari ya kwenda Roma.—Waroma 16:1, 2.
Tangu karne ya kwanza, njia zilizotumiwa kutokeza vifaa vya kuandikia zimebadilika sana. Lakini katika karne zote, barua kwa Wakristo Waroma imehifadhiwa na Mungu. Twaweza kuwa wenye shukrani kama nini kwa sehemu hii ya Neno la Yehova, iliyoandikwa kwa msaada wa mwandishi wa Paulo aliye mwaminifu na mwenye bidii Tertio!