Krismasi—Sikukuu ya Kilimwengu Au Siku Takatifu ya Kidini?
HUKO China aitwa Mzee-Krismasi. Katika Uingereza, ajulikana kuwa Baba Krismasi. Urusi watu humwita Babu Jalidi, na huko Marekani, amepewa jina la utani Santa Klaus.
Watu wengi humwona mzee huyu mwenye furaha ambaye ana tumbo kubwa na ndevu nyeupe kama theluji kuwa ndiye wonyesho wenyewe wa Krismasi. Pia ni jambo lijulikanalo sana kwamba Santa Klaus ni ngano, hekaya itegemeayo mapokeo ambayo yashirikishwa na askofu wa Myra wa karne ya nne (katika Uturuki ya siku ya kisasa).
Sikuzote desturi na mapokeo yamekuwa na uvutano wenye nguvu juu ya sherehe mbalimbali, na ndivyo ilivyo Krismasi. Ngano ya Santa ni kimojawapo cha vielelezo vya sanaa-jadiiya yenye kuhusianishwa na sikukuu ipendwayo sana. Ingawa watu fulani hudai kwamba desturi za Krismasi zategemea matukio ambayo yamerekodiwa katika Biblia, kwa uhalisi nyingi za desturi hizi zina vyanzo vya kipagani.
Ule mti wa Krismasi ni kielelezo kingine. Kichapo The New Encyclopædia Britannica chasema hivi: “Baada ya kugeuzwa imani kwa Wazungu wapagani kuwa Wakristo, ibada ya mti, iliyo ya kawaida miongoni mwao, ilibaki katika desturi za Kiskandinavia za kurembesha nyumba na ghala kwa majani ya kijani kibichi katika Mwaka Mpya ili kufukuza ibilisi na katika desturi ya kusimamisha mti kwa ajili ya ndege wakati wa Krismasi, baada ya kugeuzwa imani kwao.
Kutengeneza shada za maua ya mholi au miti mingine isiyokauka ni pokeo jingine la Krismasi lipendwalo sana. Jambo hili pia, limetia mizizi kabisa katika ibada ya kipagani. Waroma wa kale walitumia matawi ya mholi kuremba mahekalu wakati wa Saratenalia, msherehekeo wa siku saba wa katikati ya majira ya baridi ambao ulikuwa umetolewa Sarateni, mungu wa kilimo. Msherehekeo huo wa kipagani ulijulikana hasa kwa sababu ya kelele za ulevi na ngono zisizozuiliwa.
Ile desturi ya Krismasi ya kubusu chini ya kitawi cha mlimbo (kionyeshwacho hapa) huenda ikaonekana kwa watu fulani kuwa ya kimahaba, lakini hiyo ni desturi iturejezayo kwenye Enzi za Kati. Makasisi wa Uingereza ya kale waliamini kwamba mlimbo ulikuwa na nguvu za mizungu; kwa sababu hiyo, ulitumiwa kuwa kinga dhidi ya roho waovu, mafumbo ya uchawi, na dhidi ya aina nyingine za uovu. Baada ya muda, ushirikina ulitokea kwamba kubusu chini ya mlimbo kungeongoza kwenye ndoa. Zoea hili bado ni lenye kupendwa sana miongoni mwa watu fulani karibu na wakati wa Krismasi.
Hizo ni chache kati ya desturi za Krismasi ya kisasa ambazo zimeathiriwa na mafundisho ya kipagani au ambazo zimetokana moja kwa moja nayo. Ingawa hivyo, huenda ukajiuliza jinsi mambo hayo yote yalivyotukia. Ni jinsi gani sikukuu ambayo yadai kuheshimu kuzaliwa kwa Kristo ilivyopata kutatanishwa hivyo na desturi zisizo za Kikristo? La maana hata zaidi, Mungu huonaje hilo jambo?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]
Ukurasa wa 3: Santa Klaus: Thomas Nast/Dover Publications, Inc., 1978; mlimbo kwenye ukurasa wa 3 na kielezi kwenye ukurasa wa 4: Kichapo Discovering Christmas Customs and Folklore cha Margaret Baker, kilichochapishwa na Shire Publications, 1994