Soko Lililokuwa Kitovu cha Athene la Kale
JUMUIYA ya watu wenye akili wa Athene ilikuwa katika hali ya ghasia! Sikuzote mawazo mapya yalikuwa yakitangazwa hadharani katika soko kuu la jiji hilo la Ugiriki. Hata hivyo, wakati huu mambo yalikuwa tofauti. Myahudi fulani aliyekuwa amewasili tu katika jiji hilo, alionekana kuwa “mtangazaji wa miungu migeni.” Alikuwa akitoa taarifa zenye kutokeza kwa “wale waliotukia kuwa hapo.” “Ni nini ambalo mpiga-domo huyu angependa kusimulia?” wakauliza Waepikurea wenye kiburi na Wastoa wenye nyuso ngumu. Naam, mahali pa soko la Athene ndipo palipofanyiwa mijadala ya hadharani juu ya habari yoyote ile. Lakini lingekuwa jambo lisilo la kawaida kabisa kuleta habari ya miungu migeni!—Matendo 17:17, 18.
Hilo ndilo itikio lenye shaka la Waathene wakati ambapo mtume Paulo alianza kuhubiri kwa mara ya kwanza katika soko la Athene. Alikuwa akizungumza juu ya Yesu Kristo na ufufuo. Kwa nini lilikuwa jambo lisilo la kawaida kabisa kuleta dhana hizo mpya katika soko hilo, ingawa utamaduni wa Waathene ulionekana kuwa tayari kupokea dhana mpya?
Athene Lapata Uwanja Wake wa Umma
Soko lenyewe na fungu muhimu lililotimiza katika maisha ya kidini na ya umma wa Athene, ndiyo kwa kweli mambo ambayo hayakuwa ya kawaida kabisa. Soko la Athene ni eneo la ekari zipatazo 25 la mteremko usio mkali, ambalo liko kaskazini-magharibi mwa Acropolis. Yaonekana kwamba mapema katika karne ya sita K.W.K., wakati ambapo mwanasiasa wa Athene na mtunga-sheria Solon alikuwa hai, kipande hicho cha ardhi kilichaguliwa kuwa uwanja wa umma wa hilo jiji. Kuanzishwa kwa demokrasi katika Athene, iliyokazia zaidi maisha ya kiraia, kulitokeza shughuli nyingi za ujenzi katika miaka ya mapema ya karne iliyofuata. Mambo hayo yalitokeza shughuli nyingi zaidi katika hilo soko na kulipa fungu muhimu zaidi la kutimiza.
Neno la Kigiriki, a·go·raʹ, linalomaanisha soko, latokana na kitenzi kinachomaanisha “kusanya, leta pamoja.” Neno hilo lafaa matumizi ya soko hilo likiwa mahali pa jiji pa kukutania. Hilo soko lilikuja kuwa kitovu cha maisha ya kijamii na umma. Lilikuwa kitovu cha utawala wa kiraia na shughuli za kihukumu, soko kuu la biashara, mahali pa maonyesho ya michezo iliyokazia drama ya Kigiriki, mahali pa maonyesho ya riadha, na mahali ambapo wenye akili walipenda kukutana kwa ajili ya mazungumzo.
Je, ungependa kutalii mabaki ya hekalu, safu za nguzo, sanamu, nguzo za ukumbusho, na majengo ya umma ya soko la Athene? Katika jitihada za kuchunguza wakati uliopita wa hilo soko, acheni tusahau kelele na pilikapilika za jiji la kisasa na tusafiri kupitia vijia vya changarawe, miongoni mwa magofu matulivu ya marumaru, mawe yaliyochongwa, malango yanayoporomoka ambayo yamefunikwa kwa magugu na mimea ya mwituni.
Mahekalu, Vihekalu, na Miungu-Wafadhili
Wageni huvutiwa na kuwapo kwa mahekalu mengi, vihekalu, na sehemu takatifu zilizotengewa miungu mbalimbali. Vitu hivyo vyote vilisaidia kufanya hilo soko kuwa kitovu kikuu cha ibada, cha pili tu kwa Acropolis. Wakati wa Kipindi cha Upeo wa ustawi wa fasihi na sanaa za Athene, dini ilikuwa imepenya kila sehemu ya maisha ya umma. Jambo hilo ni lazima liwe lilimaanisha kwamba, miungu tofauti-tofauti iliyochaguliwa kuwa “miungu-wafadhili” wa idara za serikali na utumishi wa utawala, walipewa sehemu takatifu za hekalu katika hilo soko.
Hekalu la mungu Hephaestus ndilo lililokuwa mashuhuri miongoni mwa majengo hayo. Mungu-mke Athena alihusianishwa na Hephaestus. Miungu hiyo miwili iliabudiwa hapa ikiwa miungu-wafadhili wa sanaa na kazi za mkono. Uvumbuzi mbalimbali wa akiolojia wa ufuaji chuma na ufinyanzi karibu na hekalu hilo umelitambulisha kuwa hekalu la Hephaestus, mungu wa Wagiriki wa sanaa, jambo linalomaanisha kwamba moto ulitumiwa. Labda katika karne ya saba W.K., hekalu hilo lililotunzwa vizuri liligeuzwa kuwa Kanisa Othodoksi la Kigiriki la St. George, ijapokuwa leo halitumiki hivyo.
Bila shaka, hilo soko lilihitaji mungu-mfadhili wake lenyewe. Mungu huyo alikuwa Zeus Agoraios, aliyedhaniwa kutokeza ufasaha wa kusema. Madhabahu iliyopambwa ambayo ilichongwa kutoka kwa marumaru yenye thamani, ilikuwa imewekwa wakfu kwake. (Linganisha Matendo 14:11, 12.) Kando ya madhabahu ya Mama wa Miungu iliyokuwa karibu, palikuwa pamepangwa nguzo za ukumbusho zenye kutokeza za watu mashujaa.
Tukienda mbele kidogo, twapata hekalu dogo la Waioni. Mtaalamu wa jiografia, Pausanias, alilitambulisha kuwa Hekalu la Apollo aliye Baba. Kwa sababu gani? Kwa sababu kulingana na hekaya fulani ya kale ya Wagiriki, Apollo alikuwa baba wa Ioni, mwanzilishi wa jamii ya Waioni ambayo Waathene walikuwa sehemu yake.a Akiwa katika cheo hicho, Apollo alikuwa mmojawapo wa miungu-wafadhili wa mpango wa utawala, hasa kuhusiana na mashirika mbalimbali yaliyokuwa jijini humo.
Karibu sana na upande wa kaskazini, twaona magofu ya mawe ya chokaa ya hekalu ndogo zaidi, lililojengwa katikati mwa karne ya nne K.W.K. Zeus na Athena Phatrios waliabudiwa hapa, hiyo ilikuwa miungu mikuu ya mashirika mbalimbali ya kidini ya mababa wa kale. Kuwa mshiriki wa mashirika hayo lilikuwa jambo la lazima ili kupewa uraia wa Athene. Ng’ambo ile nyingine tu ya barabara, twaona magofu ya madhabahu ya ile iitwayo Miungu Kumi na Miwili.
Katika Safu ya Nguzo ya Zeus Eleutherios iliyoko karibu, huyo mungu mkuu wa Ugiriki alipewa adhama tena, wakati huu akiwa mungu wa uhuru na ukombozi. Safu hiyo ya nguzo, ilikuwa mahali pa matembezi na pa kukutania. Yasemekana kwamba Socrates, yule mwanafalsafa mwenye kujulikana sana alikuwa akikutana na marafiki wake kwenye safu hiyo ya nguzo, ambapo wangeweza kuketi na kupiga gumzo au kutembea polepole. Uwekaji wakfu mbalimbali na matoleo yaliyofanywa ili kupamba safu hiyo ya nguzo, kama yale ya ngao za wapiganaji waliokuwa wamekufa wakipigana kulinda Athene, yalihusiana na ukombozi wa hilo jiji kutoka kwa adui zake au uhifadhi wa uhuru wake.
Ile Barabara Iitwayo Panathenaean Way
Barabara ya changarawe iitwayo Panathenaean Way, hupita katika hilo soko, kutoka upande wa juu kulia hadi upande wa chini kushoto. Jina la barabara hiyo na pia sifa yake ya pekee ilitokana na msherehekeo wa kitaifa wa Athene, uitwao Panathenaea. Wakati wa msheherekeo huo shela ya mungu-mke Athena ilibebwa kupitia barabara hiyo, kutoka Nyumba ya Mwandamano (iliyokuwa karibu na lango la jiji) hadi Acropolis. Mapambo ya picha ya hekalu la Athena hutusaidia tuwazie fahari na utukufu mwingi wa mwandamano huo wa msherehekeo—askari wapanda farasi, magari ya mashindano ya mbio, ng’ombe na kondoo wa kutolewa dhabihu, wanaume wachanga na wasichana wakibeba vifaa vya kutumiwa katika kutoa dhabihu. Mwandamano huo uliadhimishwa na raia wa Athene na wageni wao, ambao kwa manufaa yao, wasanifuujenzi walikuwa wamefanya maandalizi ya kutosha walipobuni hilo soko. Kwa mfano, safu za nguzo zilizokuwa na ngazi-pana upande wa mbele na vipandio, zilikuwa zimepangwa kwa ustadi kuelekeana na njia ya mwandamano. Vipandio vingi vilivyochongwa upande wa mbele wa safu hizo za nguzo vingeweza kukaliwa na watazamaji wengi.
“Lilijaa Sanamu”
Kukiwa na mahekalu mengi hivyo, sanamu, na nguzo za ukumbusho zilizorundikana mahali pamoja, si ajabu kwamba ‘roho ya mtume Paulo ilikuwa yenye kuudhika ndani yake kwa kuona kwamba hilo jiji lilijaa sanamu.’ (Matendo 17:16) Paulo lazima alishtushwa na mambo aliyoona alipoingia katika soko hilo. Sanamu za mungu Hermesi zilizoonyesha uume zilikuwa nyingi sana hivi kwamba varanda nzima, iitwayo Safu ya Nguzo ya Hermesi, ilihitajika ili kuziweka. Mavazi yaliyo kwenye sanamu za kuchorwa za Hermesi yaonyesha alama za swastika—ishara ya uwezo wa kuzaa na uhai. Kulikuwa na sanamu ya Venus Genetrix, mungu wa upendo wa kingono, na vilevile sanamu ya Dionysus ambayo ina misalaba yenye muundo wa uume. “Utakatifu” wa hilo soko ulitambulishwa na jiwe la mpakani lenye beseni iliyojaa maji “matakatifu” ya kuwatakasa kisherehe wote walioingia humo.
Kwa kufikiria hali hiyo yenye mambo mengi sana ya kidini, twaweza kuelewa kwa urahisi ni kwa nini Paulo alikuwa katika hali ya hatari sana. Alishukiwa kuwa “mtangazaji wa miungu migeni,” na sheria ya wakati huo iliweka masharti kwamba ‘hakuna mtu atakayekuwa na miungu tofauti, au mipya; wala kuabudu faraghani miungu migeni yoyote isipokuwa iwe imeruhusiwa hadharani.’ Basi si ajabu kwamba, mtume alipelekwa kwenye Areopago ili akahojiwe.—Matendo 17: 18, 19.
Kitovu cha Usimamizi
Jengo la mviringo liitwalo Tholos ndilo lililokuwa makao makuu ya serikali ya Athene. Ili maofisa wenye daraka waweze kupatikana sikuzote, wenyekiti wengi wa hilo jiji walikuwa wakilala ndani ya jengo hilo usiku. Mawe kadhaa ya mizani zilizokubaliwa yaliwekwa humo Tholos. Majengo ya idara mbalimbali za usimamizi yalikuwa karibu. Nyumba ya Baraza ilikuwa kwenye ngazi-pana iliyochimbwa kwenye upande wa kilima kaskazini-magharibi mwa Tholos. Humo, washiriki 500 wa hilo Baraza walifanya mikutano ambamo walifanya kazi ya halmashauri na kutayarisha sheria kwa ajili ya Bunge.
Jengo jingine la kiraia lenye maana lilikuwa Safu ya Nguzo ya Kifalme. Humo, ndimo Hakimu mkuu wa Kifalme wa Athene—mmojawapo wa mahakimu wakuu watatu wa jiji—alimofanyia kazi yake. Akiwa humo, alishughulikia madaraka mengi ya usimamizi yaliyohusiana na mambo ya kidini na ya kisheria. Yaelekea sana kwamba, humo ndimo Socrates alimohitajika kujitokeza wakati aliposhtakiwa kwa kosa la kutostahi miungu. Sheria za mababa wa kale wa Athene zilikuwa zimechongwa juu ya kuta za jengo lililoelekeana na hiyo Safu ya Nguzo ya Kifalme. Kila mwaka, hao mahakimu wakuu walisimama kwenye jiwe lililowekwa mbele ya jengo hilo kubwa ili kula kiapo cha kazi.
Safu ya Nguzo ya Attalus
Safu ya Nguzo ya Attalus ndilo jengo la hilo soko ambalo limehifadhiwa vizuri zaidi. Akiwa kijana, Attalus, Mfalme wa Pergamum (wa karne ya pili K.W.K.), alikuwa amesomea shule za Athene, sawa na watoto wengine kadhaa wa familia za kifalme katika ulimwengu wa Mediterania. Alipoanza kutawala, alitoa zawadi hiyo yenye fahari—Safu ya Nguzo ya Attalus—kwa jiji alilosomea.
Kazi kuu ya hiyo Safu ya Nguzo ya Attalus ilikuwa kuandaa mahali palipositirika na maridadi kwa ajili ya ushirika na mazungumzo yasiyo rasmi. Sakafu zake na ngazi-pana zilifanyiza mahali bora kabisa pa kutazama maandamano. Ni lazima pia kupendwa kwa Nguzo hiyo ya Attalus pakiwa mahali pa matembezi kuwe kulihakikisha ufanisi wake pakiwa mahali pa maduka. Yaelekea maduka hayo yalipangishwa na Serikali ili hilo jengo liweze kutokeza mapato.
Likiwa limerudishwa katika hali yake ya hapo awali, safu ya Nguzo ya Attalus hutoa mfano bora kabisa wa ubuni wa kijiometri. Vipimo vyake vya ujumla, tofauti zenye kupendeza za vipimo kati ya taratibu za safu za upande wa chini na wa juu, mchanganyiko wa nuru na kivuli wenye kupendeza, na wingi na uzuri wa vifaa vya ujenzi, vyote huifanya Safu ya Nguzo ya Attalus kuwa ya pekee. Ukinaifu wa kuona vitu vilevile umepunguzwa kwa njia mbalimbali, hasa kwa kutumia aina tatu za nguzo za juu, kama vile miundo ya nguzo iliyotoka kwa Wagiriki, Waioni, na Wamisri.
Mahali pa Shughuli za Kitamaduni
Jumba la Maonyesho, lilitumika likiwa jukwaa la matukio mengi ya kitamaduni katika Athene. Jengo hilo lilikuwa zawadi kutoka kwa Vipsanius Agrippa, mkwe wa Augusto, Maliki wa Roma. Sehemu yake ya mbele ilipambwa kwa marumaru yenye rangi nyingi. Ukumbi uliokuwa na upana wa meta 25, ambao ungetoshea watu wapatao 1,000, ulikuwa umefunikwa kwa paa bila nguzo za kuitegemeza upande wa ndani. Hayo yalikuwa majaribio ya utiaji paa yenye ujasiri zaidi kuwahi kufanywa katika ulimwengu wa kale! Hata hivyo, yaelekea kwamba vitumbuizo vingi vilivyoonyeshwa humo vingekuwa vyenye kutilika shaka kwa Wakristo wa kweli, ambao walikuwa na viwango vya juu vya adili.—Waefeso 5:3-5.
Yaelekea kwamba, wadadisi wa nyakati za kale walizuru Maktaba ya Pantainos. Kuta zake zilijaa kabati ambamo hatikunjo za mafunjo na za ngozi ziliwekwa. Chumba kikuu cha hiyo maktaba kilielekea upande wa magharibi, na kupitia katikati ya ua, mtu aweza kuona safu za nguzo—mahali palipopendeza pa kutembea polepole, kusoma, au kutafakari. Mwandiko wenye sheria mbili umepatikana humo. Hizo sheria zilikuwa: “Hakuna kitabu chochote kipaswacho kuondolewa,” na “[Maktaba hufunguliwa] kuanzia saa moja hadi saa sita.”
Hilo Soko Leo
Katika miaka ya majuzi, Shule ya Marekani ya Utafiti wa Fasihi na Sanaa imefukua karibu soko lote. Likiwa chini ya kivuli cha lile jengo refu la Acropolis, soko hilo limekuwa mahali papendwapo sana na mtalii atakaye kuchunguza kifupi historia ya Athene la kale.
Soko la Mitumba, Monastiraki, lililoko karibu—hatua chache kutoka soko hilo na jengo la Acropolis—ni mahali pengine penye kuvutia sana. Mwenye kuzuru soko hilo aweza kuona sanaa za kale za Wagiriki zenye kushangaza na zenye kupendeza pia, na vilevile shughuli za biashara na za kujadiliana bei zifananazo na za Mashariki ya Kati. Bila shaka mwenye kuzuru pia atawaona Mashahidi wa Yehova huko wakifanya kwa shangwe kazi ileile mtume Paulo aliyofanya zaidi ya miaka 1,900 iliyopita—ya kuhubiri hadharani habari njema ya Ufalme ‘kwa wale watukiao kuwa hapo.’
[Maelezo ya Chini]
a Jina Waioni latokana na lile la Yavani, mwana wa Yafethi na mjukuu wa Noa.—Mwanzo 10:1, 2, 4, 5.
[Sanduku katika ukurasa wa 28]
Shughuli za Biashara Katika Athene
Hilo soko halikuwa kitovu cha kielimu na mambo ya sheria ya Athene tu bali pia soko kuu la shughuli za biashara. Athene lilikuja kuwa kitovu cha biashara, lilojulikana sana kwa sababu ya thamani ya fedha zake taslimu, na unyofu wa mahakimu wake, waliokuwa na mamlaka ya kuhakikisha kwamba shughuli za kibiashara zilikuwa zenye uaminifu na za haki.
Athene liliuza nje divai, mafuta ya zeituni, asali, marumaru, na bidhaa za viwandani kama vile vyombo vya kufinyangwa na vyuma vilivyosafishwa. Ngano ndiyo hasa iliyoingizwa kutoka nje ili kubadilishana na bidhaa hizo. Kwa kuwa eneo la Attica lililokuwa karibu na Athene halikuzalisha bidhaa za kutosha kulisha wakazi wake, viwango vya biashara vilikuwa vikali. Soko la Piraeus lililokuwa kwenye bandari ya Athene sikuzote lililazimika kuwa na chakula cha kutosha cha karibuni ili kugawia wakazi wa jiji na jeshi. Nao wafanya-biashara hawakuruhusiwa kuweka akiba bidhaa za chakula ili kuziuza kwa bei za juu zaidi nyakati za uhitaji.