Je, Una Malaika Mlinzi?
JE, WEWE waamini una malaika mlinzi? Watu wengi hudhani kwamba wanao. Kwa sababu hiyo, mwanamke fulani katika Kanada magharibi asemekana kuwa mwenye kipawa cha kipekee kinachohusu malaika. Ukimwambia jina lako kamili pamoja na $200 [za Kanada], yeye adai kwamba atakuwezesha kuwasiliana na malaika wako mlinzi. Kwanza yeye hutafakari akikazia fikira mwali wa mshumaa. Kisha, yeye hupata ono ambalo malaika wako humpa ujumbe wako. Ikiwa bakshishi, mwanamke huyo hukupa mchoro wa jinsi malaika wako anavyofanana.
Kwa wengine, huenda hilo likaonekana kupatana na ile hadithi juu ya Mfalme Mfaransa Louis wa Tisa. Yadhaniwa kwamba alinunua manyoya yenye bei ghali yaliyosemekana kuwa yalianguka kutoka kwenye mabawa ya Malaika Mkuu Mikaeli. Wajapoitilia shaka hadithi hiyo, watu wengi hawangesita kamwe kuyakubali madai ya mwanamke huyo Mkanada.
Kuvutiwa na Malaika
Katika miaka ya karibuni kumekuwa na kupendezwa kwingi juu ya malaika. Kwenye televisheni na katika sinema, vitabu, magazeti, na majarida, twaambiwa juu ya malaika ambao huwafariji wagonjwa mahututi, huwaliwaza waliofiwa, hupa hekima, na kuwaponya watu kutokana na mauti. Katika Marekani, watazamaji wapatao milioni 20 hutazama mfululizo wa vipindi vya televisheni ambavyo huonyesha malaika wakiingilia maisha ya watu. Duka moja la vitabu lina zaidi ya vitabu 400 juu ya malaika.
Kitabu cha hivi majuzi husimulia mambo yaliyoonwa juu ya malaika walinzi ambao waliokoa maisha ya askari katika pigano. Vibandiko kwenye magari hutaarifu kuwa madereva wanalindwa na malaika walinzi. Mashirika, mikutano, na semina huendeleza uchunguzi wa malaika, na husemekana kwamba huwasaidia watu kuwasiliana na malaika.
Eileen Freeman ndiye mwandishi wa vitabu vitatu juu ya malaika, na mchapishaji wa jarida juu ya malaika pekee. Yeye asisitiza hivi: “Naamini kwamba kila malaika mbinguni anawakilishwa na malaika mlinzi Duniani, kiumbe ambaye wajibu wake si kumsifu Mungu katika mazingira ya kimbingu tu, bali kulinda hasa wanadamu na namna nyingine za uhai duniani. Malaika mlinzi amegawiwa kila mmoja wetu tunapochukuliwa mimba, na huangalia ukuzi wetu katika tumbo la uzazi, kuzaliwa kwetu, maisha yetu katika ulimwengu huu, hadi malaika huyo anapotuongoza kutoka kwenye mipaka ya ulimwengu huu hadi kwenye utukufu wa mbingu.” Hili husimulia vizuri maoni yenye kupendwa na wengi juu ya malaika walinzi.
Katika nyakati hizi zenye kuleta mkazo, ni jambo lenye kufariji kuamini kwamba tuna malaika mlinzi wetu binafsi, ambaye wajibu wake ni kutulinda sisi. Neno la Mungu, Biblia, husema nini kuhusu jambo hili? Je, twapaswa kujaribu kuwasiliana na malaika? Je, wao hujali viwango vyetu vya kiadili na imani za kidini? Ni msaada gani tuwezao kutarajia kutoka kwao? Maswali haya yatajibiwa katika makala inayofuata.