Mlima Athos—Je, Ni “Mlima Mtakatifu”?
KWA zaidi ya waumini 220 wa Kanisa Othodoksi, Mlima Athos, ambao ni rasi yenye mawemawe iliyo kaskazini mwa Ugiriki, ndio “mlima mtakatifu zaidi kwa jamii ya Wakristo wa Othodoksi.” Wengi wao hutamani sana kwenda kuuzuru “mlima mtakatifu” wa Athos. “Mlima [huo] mtakatifu” ni nini? Kwa nini ukawa muhimu sana? Na je, huo ni “mlima” ambao watu wenye kumhofu Mungu wapaswa kuuendea ili kupata mwongozo wa kiroho na ibada ya kweli?
Usemi “mlima mtakatifu” umo katika Biblia. Nao unahusishwa na ibada takatifu, safi, na iliyokwezwa ya Mungu wa kweli Yehova. Mlima Zayoni katika Yerusalemu la kale ulipata kuwa ‘mlima mtakatifu’ wakati Mfalme Daudi alipopeleka sanduku la agano huko. (Zaburi 15:1; 43:3; 2 Samweli 6:12, 17) Baada ya hekalu la Solomoni kujengwa kwenye Mlima Moria, mahali palipojengwa hekalu hilo pakawa sehemu ya “Zayoni”; hivyo, Zayoni ikaendelea kuwa ‘mlima mtakatifu’ wa Mungu. (Zaburi 2:6; Yoeli 3:17) Kwa kuwa hekalu la Mungu lilikuwa Yerusalemu, nyakati nyingine jiji hilo liliitwa ‘mlima mtakatifu’ wa Mungu.—Isaya 66:20; Danieli 9:16, 20.
Namna gani leo? Je, Mlima Athos—au mlima mwingineo wowote—ndio “mlima mtakatifu” ambapo watu wapaswa kumiminika ili kumwabudu Mungu kwa njia yenye kukubalika?
“Mlima Mtakatifu” wa Watawa
Mlima Athos uko katika ukingo wa mashariki mwa Peninsula ya Chalcidice, kwenye ncha ya ukanda wa ardhi unaotokeza na kuingia katika Bahari ya Aegea karibu na upande wa mashariki wa Thessaloníki ya siku hizi. Kilele chake chenye rangi ya marumaru kina mwinuko mkali wa meta 2,032 kutoka baharini.
Athos umeonwa kwa muda mrefu kuwa mahali patakatifu. Kulingana na ngano za Wagiriki miungu walikaa kwenye mlima huo kabla ya kufanya Mlima Olympus kuwa makao yao. Wakati fulani baada ya Konstantino Mkuu (karne ya nne W.K.), Athos ukawa mahali patakatifu pa makanisa ya Kikristo. Kwa mujibu wa hekaya moja, “bikira” Maria, pamoja na Mweneza-Evanjeli Yohana, alitua Athos baada ya kubebwa na dhoruba kali ya ghafula wakiwa njiani kwenda Saiprasi kumtembelea Lazaro. Alivutiwa sana na mlima huo na kumwomba Yesu ampe uwe wake. Hivyo, Athos ukaanza kuitwa “Bustani ya Bikira Mtakatifu.” Kufikia katikati ya enzi ya Byzantium, sehemu yote hiyo yenye mawemawe ikaanza kuitwa Mlima Mtakatifu. Jina hilo lilikubaliwa rasmi na kuidhinishwa katikati ya karne ya 11 kwa agizo la Maliki Konstantino Monomachus wa Tisa.
Athos ni mlima ufaao kwa wale wanaoishi maisha ya kujinyima kwa sababu una mawemawe na umejitenga. Kwa karne nyingi, mlima huo umevutia wanadini wengi kotekote katika jamii ya Waothodoksi—Wagiriki, Waserbia, Warumania, Wabulgaria, Warusi, na wengineo—ambao walijenga makao mengi ya watawa, pamoja na makanisa yao na jumuiya zao. Majengo 20 hivi kati ya hayo yamesalia.
Mlima Athos Leo
Leo, Athos ni eneo linalojitawala, kwa mkataba ulioidhinishwa mwaka wa 1926. Idadi ya watawa wa kiume wanaokaa huko imeongezeka kufikia watu zaidi ya 2,000 baada ya kuendelea kupungua kwa miaka mingi.
Kila mojawapo ya makao hayo yana mashamba yake, makanisa, na makazi. Penye kijiji cha Karoúlia, kilichojengwa kwenye kilele cha Mlima Athos, ndipo mahali patakatifu zaidi pa watu hao wenye kujitenga. Hapa kikundi cha nyumba zilizojengwa moja-moja chaweza kufikiwa kwa kutumia vijia vya miguu vyenye kupinda-pinda, ngazi za mawe, na minyororo. Huko Athos watawa hao hufuata kawaida yao ya kale ya kila siku, wakitumia saa zilizotumiwa katika enzi ya Byzantium (siku ikianza jua linaposhuka) na kalenda ya Julian (ambayo iko nyuma ya kalenda ya Gregorian kwa siku 13).
Ingawa yasemekana “utakatifu” wa mahali hapa pa kidini ulitokana na mwanamke, kwa miaka zaidi ya 1,000 watawa na watu wenye kujitenga wanaoishi huko wametangaza peninsula yote kuwa marufuku kwa viumbe wote wa kike—wanadamu na wanyama—pamoja na matowashi au mwanamume yeyote asiye na ndevu. Hivi karibuni, sheria ya kuwazuia watu wasio na ndevu na wanyama wa kike wasiingie humo imelegezwa, lakini wanawake bado hawaruhusiwi kabisa kupita eneo la meta 500 kutoka ukingo wa bahari.
“Mlima Mtakatifu” kwa Wote
Je, Athos ndio “mlima mtakatifu” ambapo Wakristo wenye kumhofu Mungu wapaswa kwenda kuabudia? Akizungumza na mwanamke Msamaria aliyeamini kwamba Mungu apaswa kuabudiwa kwenye Mlima Gerizimu, Yesu alieleza wazi kwamba hakuna mlima halisi ambao ungetengwa tena kuwa mahali patakatifu pa kuabudia Mungu. “Saa inakuja wakati ambapo wala si katika mlima huu wala katika Yerusalemu nyinyi watu mtamwabudu Baba,” Yesu akasema. Kwa nini? “Mungu ni Roho, na wale wanaomwabudu yeye lazima waabudu kwa roho na kweli.”—Yohana 4:21, 24.
Akizungumzia wakati wetu, nabii Isaya alitabiri kwamba “mlima [wa mfano] wa nyumba ya BWANA” “[unge]wekwa imara juu ya milima” na “[ku]inuliwa juu ya vilima,” na watu wa mataifa yote wangemiminika huko, kusema kitamathali.—Isaya 2:2, 3.
Wanaume kwa wanawake wanaotaka kuwa na uhusiano wenye kukubaliwa na Mungu wanatakiwa wamwabudu Yehova kwa “roho na kweli.” Mamilioni ya watu ulimwenguni kote wamepata njia iongozayo kwenye ‘mlima wa Yehova.’ Wao ni miongoni mwa wale wenye hisia zinazofanana na za mwanasheria Mgiriki aliyesema hivi kuhusu Athos: “Siamini kama hali ya kiroho hupatikana tu katika maeneo fulani yaliyozingirwa kwa kuta au katika nyumba za watawa.”—Linganisha Matendo 17:24.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Hazina Iliyofichwa kwa Muda Mrefu
Kwa karne nyingi, watawa wa Athos wamekusanya hazina ambayo yatia ndani hati zikadiriwazo kuwa 15,000, na inasemekana kwamba nyingine ni za tangu karne ya nne, jambo ambalo lafanya hazina hiyo iwe mkusanyo wenye thamani zaidi ulimwenguni. Kuna hati-kunjo, mabuku mazima na ukurasa mmoja-mmoja wa Gospeli, zaburi na nyimbo, mbali na michoro ya kale, sanamu, na vitu vilivyotengenezwa kwa chuma. Inakadiriwa kwamba robo ya hati zote za Kigiriki ulimwenguni zinapatikana kwenye Mlima Athos, ingawa nyingi za hati hizo bado zahitaji kuingizwa katika orodha ya majina ya vitabu. Katika mwaka wa 1997, watawa hao walikubali baadhi ya hazina zao zionyeshwe kwa mara ya kwanza huko Thessaloníki.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Telis/Greek National Tourist Organization