Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w01 6/1 kur. 3-4
  • Viwango Vyabadilika na Matumaini Yavunjwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Viwango Vyabadilika na Matumaini Yavunjwa
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Familia na Viwango vya Maadili
  • Viwango vya Yehova Vinatusaidia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1983
  • Mtumikie Yehova Kulingana na Viwango Vyake vya Juu
    Izingatie Siku ya Yehova Maishani
  • Unaweza Kutumaini Viwango vya Nani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Dumisha Viwango vya Yehova vya Maadili
    Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha Yetu ya Kikristo—2017
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
w01 6/1 kur. 3-4

Viwango Vyabadilika na Matumaini Yavunjwa

Katika siku za Mfalme Henry wa Kwanza wa Uingereza (1100-1135), yadi moja (kipimo fulani cha urefu) ilidhaniwa kuwa “urefu kati ya pua ya Mfalme na ncha ya kidole-gumba cha mkono wake ulionyooshwa mbele yake.” Vipimo vya yadi vya raia wa Mfalme Henry vilikuwa sahihi kadiri gani? Njia ya pekee ya kujua urefu huo ilikuwa kumtembelea mfalme huyo.

LEO vipimo vinaweza kubainishwa kwa usahihi zaidi kwa kutumia viwango fulani. Hivyo, meta hubainishwa kuwa umbali ambao mwanga husafiri kupitia mahali pasipo na kitu kwa muda wa sekunde moja iliyogawanywa kwa 299,792,458. Watu popote pale wanaweza kuhakikisha kwamba urefu wa vipimo vyao ni sawa na wa watu wengine iwapo wana vifaa vinavyoonyesha viwango vya kupimia.

Mabadiliko katika viwango vya kupimia, hata yawe madogo kadiri gani, yanaweza kuleta wasiwasi, hivyo jitihada kubwa hufanywa ili kuhifadhi viwango hivyo. Kwa mfano, huko Uingereza kiwango cha kupimia uzito ni kipande cha platinamu ambacho kina uzito wakilogramu moja. Kipande hicho kimewekwa katika maabara iitwayo National Physical Laboratory. Hewa iliyochafuka inayotokana na magari na ndege zinazopita juu ya maabara hiyo huzidisha uzito wa kipande hicho kila siku. Hata hivyo, kipande hicho cha chuma, au mcheduara, kimetengenezwa kikiwa na uzito ulio sawa kabisa na chuma kinachotumiwa kama kiwango cha kupimia cha ulimwengu. Kipande hicho kimewekwa chini ya chupa tatu zinazofanana na kengele kwenye chumba cha chini ya ardhi cha Shirika la Kimataifa la Uzito na Vipimo (International Bureau of Weights and Measures) huko Sèvres, Ufaransa. Hata hivyo, uzito wa kipande hicho hubadilika-badilika kutokana na uchafuzi ambao hauwezi kuonekana bila hadubini. Kufikia sasa, wataalamu wa vipimo hawajatokeza kiwango cha kupimia ambacho hakibadiliki-badiliki.

Mabadiliko madogomadogo si muhimu sana kwa mtu wa kawaida. Lakini kubadilika kabisa kwa kiwango cha kupimia kwaweza kuleta mvurugo. Huko Uingereza, vipimo rasmi vya uzito, (ambavyo ni ratili na aunsi), vilipobadilishwa kufuata mfumo wa meta (ambavyo ni kilogramu na gramu), watu walikuwa na wasiwasi mkubwa—na kwa sababu nzuri. Baadhi ya wenye duka wasio wanyofu walifaulu kuwadanganya wateja wao kwa sababu wengi hawakuelewa kipimo hicho kipya.

Familia na Viwango vya Maadili

Namna gani mabadiliko katika viwango vya familia na maadili? Matokeo ya mabadiliko hayo yanaweza kuwa yenye madhara makubwa sana. Ripoti za hivi karibuni kuhusu kuvunjika kwa familia, kufanya ngono ovyoovyo, na kudhulumiwa kwa watoto, ambako kumeenea sana, huchukiza wengi na huthibitisha kwamba tunaishi wakati ambapo viwango vinazidi kushuka. Familia za mzazi mmoja, watoto wanaolelewa na “wazazi” wa jinsia moja, na hali ya kuogofya ya kunajisiwa kwa watoto wanaotunzwa na halmashauri za mitaa, ni mambo yanayofanywa na watu wanaokataa viwango vinavyokubalika. Watu wengi wanakuwa “wenye kujipenda wenyewe, . . . wasio na shauku ya kiasili, . . . wasio na upendo wa wema, . . . wenye kuzipenda raha badala ya kuwa wapenda Mungu,” kama vile Biblia ilivyotabiri miaka elfu mbili hivi iliyopita.—2 Timotheo 3:1-4.

Kushuka kwa viwango vya maadili huenda sambamba na kuvunja matumaini ya wengine bila kujali. Hivi majuzi, ukiukaji ulio wazi wa viwango vya juu vya kazi ya udaktari ulifunuliwa huko Hyde, mji ulio kaskazini mwa Uingereza, ambako wakazi waliwatumaini madaktari “walioheshimika na kutumainika.” Lakini inasikitisha kwamba alivunja matumaini yao. Jinsi gani? Ripoti za uchunguzi wa mahakama zilionyesha kwamba daktari mmoja alisababisha vifo vya angalau wanawake 15 aliokuwa anawatibu. Ilibidi polisi wachunguze upya vifo vya watu wengine 130 ambavyo vilisababishwa na daktari huyo. Daktari huyo alipatikana na hatia na kufungwa gerezani, jambo lililodhihirisha kadiri alivyokuwa amevunja matumaini ya wengine. Maofisa wawili wa gereza ambao huenda mama yao aliuawa na daktari huyo walipewa kazi nyingine ili wasilazimike kumtunza mfungwa huyo mwenye sifa mbaya. Si ajabu kwamba ripoti ya kesi hiyo kwenye gazeti la The Daily Telegraph ilimwita “Daktari ‘Ibilisi.’”

Ni nani ambaye kwa hakika unaweza kumtumaini unapozingatia viwango vyenye kubadilika-badilika na vyenye kushuka katika sehemu nyingi sana za maisha? Unaweza kupata wapi viwango visivyobadilika-badilika, vinavyoungwa mkono na mamlaka ambayo ina uwezo wa kuvidumisha? Makala ifuatayo itajibu maswali hayo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki