JE, NI KAZI YA UBUNI?
Uwezo wa Homoni wa Kudhibiti Jinsi Mwili Unavyofanya Kazi
Ili mwili wetu ufanye kazi vizuri, damu yetu inahitaji kiwango hususa cha madini kama vile kalisiamu. Hata hivyo, kiwango cha madini kwenye damu hubadilika kila siku ikitegemea vyakula unavyokula. Mwili wako unahakikishaje kuna kiwango kinachofaa cha madini kwenye damu?
Mwili wenye afya husawazisha kiwango cha madini kwa kutengeneza, kuhifadhi, na kupeleka homoni kwenye damu. Homoni ni kemikali ambazo husaidia kudhibiti kazi mbalimbali mwilini. Hata badiliko dogo tu la kiwango cha homoni linaweza kutokeza mabadiliko makubwa katika mwili. Encyclopedia Britannica inasema kwamba “homoni hazitokezwi tu bila mpangilio maalum, bali zinatokezwa kwa njia tata iliyodhibitiwa.”
Kwa mfano, tezi za parathiroidi (parathyroid glands) zilizo kwenye shingo, hutambua mabadiliko madogo sana ya kiwango cha kalisiamu kwenye damu. Kwa kawaida tezi hizo zinakuwa nne na zina ukubwa wa punje ya mchele.
Tezi hizi zinapotambua kwamba kiwango cha kalisiamu kwenye damu kimepungua, zinatokeza homoni ambayo huelekeza mifupa iachilie kalisiamu iliyohifadhiwa iingie kwenye damu. Nyakati nyingine hilo hufanyika ndani ya sekunde chache tu. Homoni hiyo pia huelekeza figo ziache kuchuja kalisiamu kutoka kwenye damu na pia inaelekeza utumbo mdogo uongeze kiasi cha kalisiamu unaofyonza kutoka kwenye chakula.
Hata hivyo, kiwango cha kalisiamu kikizidi katika damu, tezi dundumio (thyroid glands) hutokeza homoni tofauti. Homoni hii huelekeza mifupa ifyonze na kuhifadhi kalisiamu nyingi zaidi na pia inaelekeza figo zichuje na kuondoa kalisiamu iliyozidi kutoka kwenye damu.
Homoni hizi mbili ni kati ya mamia ya homoni ambazo mwili wa mwanadamu hutumia kusawazisha na kudhibiti jinsi mwili unavyofanya kazi.
Una maoni gani? Je, uwezo wa homoni wa kudhibiti jinsi mwili wako unavyofanya kazi ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?