-
Ugonjwa wa Kisukari “Huua Kimyakimya”Amkeni!—2003 | Mei 8
-
-
Ugonjwa wa Kisukari “Huua Kimyakimya”
ALIPOKUWA mwenye umri wa miaka 21, Ken alianza kuhisi kiu kisichoisha na ambacho hakikuwa cha kawaida. Pia alihitaji kwenda haja ndogo mara nyingi, na baadaye akahitaji kufanya hivyo kila baada ya dakika 20. Punde si punde, Ken alianza kuhisi uzito miguuni. Alikuwa mchovu kila wakati, na macho yake hayakuweza kuona vizuri.
Mambo yalibadilika wakati Ken alipopata mafua. Daktari alimwambia kwamba hakuwa na mafua tu, bali pia ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 1 (Type 1 diabetes mellitus). Ugonjwa huo huathiri uwezo wa mwili wa kutumia virutubisho fulani, hasa aina ya sukari inayoitwa glukosi inayopatikana kwenye damu. Ken alikaa hospitalini kwa majuma sita kabla ya kiwango cha sukari mwilini mwake kurudia hali ya kawaida.
Hilo lilitukia zaidi ya miaka 50 iliyopita, na njia za matibabu zimeboreshwa sana tangu wakati huo. Hata hivyo, Ken bado anaugua ugonjwa wa kisukari, na si yeye tu. Inakisiwa kuwa watu milioni 140 wana ugonjwa wa kisukari ulimwenguni pote, na kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, idadi hiyo huenda ikaongezeka mara mbili kufikia mwaka wa 2025. Kwa hiyo, wataalamu wana sababu ya kuhangaika. Mkurugenzi mmoja wa kituo kimoja cha tiba nchini Marekani anayeitwa Dakt. Robin S. Goland, anasema: “Kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaougua ugonjwa wa kisukari, huenda tumeanza kukabili janga kubwa.”
Hebu fikiria takwimu zifuatazo kutoka sehemu mbalimbali duniani.
AUSTRALIA: Kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Ugonjwa wa Kisukari ya Australia, “ugonjwa wa kisukari ni mojawapo ya magonjwa magumu sana kutibu katika karne ya 21.”
INDIA: Angalau watu milioni 30 wanaugua ugonjwa wa kisukari. Daktari mmoja anasema: “Miaka 15 hivi iliyopita, watu wenye umri wa chini ya miaka 40 hawakuwa wakiugua ugonjwa wa kisukari. Hata hivyo, nusu ya watu wanaougua kisukari siku hizi wana umri wa chini ya miaka 40.”
SINGAPORE: Karibu thuluthi moja ya watu walio na umri wa kati ya miaka 30 na 69 wanaugua ugonjwa wa kisukari. Watoto wengi, hata wale walio na umri wa chini ya miaka kumi, wamepimwa na kupatikana na ugonjwa huo.
MAREKANI: Inakadiriwa kuwa watu milioni 16 wana ugonjwa wa kisukari, na kwamba wengine 800,000 wanapatwa na ugonjwa huo kila mwaka. Mamilioni ya watu wana ugonjwa huo lakini hawana habari.
Ni vigumu zaidi kutibu ugonjwa wa kisukari kwa kuwa mtu anaweza kuishi nao kwa muda mrefu kabla haujagunduliwa. Gazeti la Asiaweek linasema: “Kwa kuwa dalili za mapema za ugonjwa wa kisukari hazionekani waziwazi, mara nyingi ugonjwa huo haugunduliwi.” Hiyo ndiyo sababu watu husema kwamba ugonjwa huo huua kimyakimya.
Kwa vile ugonjwa huo umeenea sana, makala zifuatazo zitazungumzia maswali haya:
● Ugonjwa wa kisukari husababishwa na nini?
● Watu wanaougua ugonjwa huo wanawezaje kukabiliana nao?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]
Maana ya Jina Hilo
Jina “diabetes mellitus” linatokana na neno la Kigiriki linalomaanisha “kunyonya” na neno la Kilatini linalomaanisha “tamu kama asali.” Maneno hayo yanafafanua vizuri sana ugonjwa huo, kwani maji hupita mwilini mwa mtu aliye na ugonjwa wa kisukari kana kwamba yananyonywa na mdomo na kupitia kwenye njia ya mkojo kisha kutoka nje ya mwili. Isitoshe, mkojo huwa na ladha tamu kwa kuwa una sukari. Ndiyo sababu kabla ya kuvumbua njia bora za kupima ugonjwa huo, mbinu moja ya kutambua kama mtu ana ugonjwa wa kisukari ilikuwa kumwaga mkojo wa mgonjwa karibu na kichuguu cha sisimizi. Ikiwa sisimizi wangevutiwa na mkojo huo, basi hilo lilimaanisha kwamba mkojo una sukari.
-
-
Ugumu wa MatibabuAmkeni!—2003 | Mei 8
-
-
Ugumu wa Matibabu
“Hakuna ugonjwa wa kisukari ulio mzuri. Aina zote za kisukari ni hatari.”—Anne Daly, Shirika la Ugonjwa wa Kisukari la Marekani.
“MATOKEO ya uchunguzi wa damu yako yanaonyesha kasoro nyingi. Unahitaji kupata matibabu haraka.” Maneno hayo ya daktari yalimshtua sana Deborah. “Usiku huo, nilifikiri matokeo hayo ndiyo yaliyokuwa na kasoro,” anasema. “Sikuamini kamwe kwamba nilikuwa mgonjwa.”
Kama wafanyavyo watu wengi, Deborah alipuuza dalili za ugonjwa huo kwa sababu alidhani kwamba afya yake ni nzuri kiasi. Alidhani kwamba alikuwa na kiu kwa sababu ya dawa fulani alizokuwa akitumia. Alifikiri kwamba alienda haja ndogo mara nyingi kwa sababu ya kunywa maji mengi, na kwamba uchovu wake ulitokana na majukumu yake mengi kazini na nyumbani akiwa mama.
Hata hivyo, uchunguzi wa kitiba ulionyesha kwamba Deborah alikuwa na ugonjwa wa kisukari. Haikuwa rahisi kwake kukubali matokeo hayo. Deborah asema: “Sikumweleza yeyote kwamba nilikuwa mgonjwa.” Kisha aongeza: “Usiku, wakati familia yangu ilipokuwa imelala, nilikuwa nikitazama nje dirishani huku nikilia.” Watu wengine wanapogundua kwamba wana ugonjwa wa kisukari, wao hushuka moyo kama Deborah na hata kukasirika. Karen anasema: “Nilikataa katakata kuamini kwamba nina ugonjwa wa kisukari huku nikilia.”
Hivyo ndivyo watu hutenda kwa kawaida wanapopatwa na jambo lenye kuhuzunisha. Hata hivyo, watu wanaougua kisukari wakitegemezwa wanaweza kuzoeleana na hali yao. “Mwuguzi aliyekuwa akinihudumia alinisaidia nikubali hali hiyo,” asema Karen. “Alinihakikishia kwamba si vibaya kulia. Kulia kulinisaidia kukabiliana na hali hiyo.”
Kwa Nini Ugonjwa Huo Ni Hatari?
Ugonjwa wa kisukari umeitwa kwa kufaa “ugonjwa unaoathiri kiini cha nishati ya mwili.” Mwili unaposhindwa kutumia glukosi, mifumo mbalimbali ya mwili inaweza kuacha kufanya kazi au hata kusababisha kifo. Kulingana na Dakt. Harvey Katzeff, “watu wanaougua kisukari hawafi moja kwa moja kutokana na ugonjwa huo, bali hufa kutokana na magonjwa mengine. Sisi hufaulu kuzuia magonjwa hayo, lakini hushindwa kuyatibu yanapotokea.”a
Je, watu wanaougua kisukari wana matumaini yoyote? Naam, wanayo, ikiwa tu watatambua kwamba ugonjwa huo ni hatari na kuanza kupata matibabu.b
Kula na Kufanya Mazoezi
Ijapokuwa ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 1 hauwezi kuzuiwa, wanasayansi wanachunguza mambo fulani katika chembe za urithi ambayo huenda husababisha ugonjwa huo, na wanajaribu kutafuta njia za kuzuia mfumo wa kinga mwilini usishambulie chembe za kongosho ambazo hutokeza insulini. (Ona sanduku “Kazi ya Glukosi,” katika ukurasa wa 8.) “Ugonjwa wa kisukari wa aina ya 2 ni afadhali zaidi,” chasema kitabu Diabetes—Caring for Your Emotions as Well as Your Health. “Watu wengi ambao wanaweza kurithi ugonjwa huo huenda wasionyeshe dalili zozote za ugonjwa huo kwa sababu ya kupata lishe bora na kufanya mazoezi kwa ukawaida. Hivyo wanakuwa na afya bora na wanadhibiti uzito wao.”c
Likielezea umuhimu wa kufanya mazoezi, jarida la Journal of the American Medical Association liliripoti kuhusu uchunguzi mkubwa uliofanywa kuhusu wanawake. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba “kufanya mazoezi kidogo tu huongeza uwezo [wa chembe za mwili] wa kufyonza glukosi kwa msaada wa insulini kwa zaidi ya saa 24.” Hivyo, ripoti hiyo inakata kauli hii: “Kutembea na kufanya mazoezi mengi hupunguza uwezekano wa wanawake kupata ugonjwa wa kisukari wa aina ya 2.” Wachunguzi hao wanapendekeza watu wafanye mazoezi ya kiasi kwa angalau dakika 30, na ikiwezekana, kila siku. Mazoezi hayo yanaweza kutia ndani jambo rahisi kama vile kutembea. Kitabu American Diabetes Association Complete Guide to Diabetes kinasema kwamba “huenda kutembea ndio mazoezi bora, yaliyo salama zaidi, na yasiyo na gharama kubwa.”
Hata hivyo, watu wanaougua kisukari wanapaswa kufanya mazoezi kupatana na mashauri ya wataalamu wa tiba. Sababu moja ni kwamba ugonjwa wa kisukari unaweza kuharibu mfumo wa mishipa na neva, na hivyo kuathiri mzunguko wa damu na hisi. Kwa hiyo, mtu anayeugua kisukari anaweza kukwaruzwa kidogo tu mguuni bila kujua na kupata ambukizo ambalo huenda likasababisha kidonda. Hali hiyo ni hatari sana na inaweza kufanya kiungo kilichoathiriwa kikatwe ikiwa hakitatibiwa mara moja.d
Hata hivyo, kuwa na programu ya kufanya mazoezi kwaweza kusaidia kudhibiti ugonjwa huo. Kitabu ADA Complete Guide, kinasema “watafiti wanagundua faida nyingi zaidi za kufanya mazoezi kadiri wanavyoendelea kufanya uchunguzi.”
Kutumia Insulini
Zaidi ya kufanya mazoezi na kupata lishe bora, watu wengi walio na ugonjwa wa kisukari huhitaji kupima viwango vya glukosi katika damu yao na kujidunga sindano za insulini. Kwa kupata lishe bora na kufanya mazoezi ya kutosha, watu wengine wanaougua ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 2 wameacha kutumia insulini angalau kwa muda fulani.e Karen, ambaye anaugua ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 1, aligundua kwamba kufanya mazoezi kunaiwezesha insulini ifanye kazi vizuri zaidi. Hivyo, amefaulu kupunguza kiwango cha insulini ambacho anahitaji kila siku kwa asilimia 20.
Mgonjwa hapaswi kuvunjika moyo ikiwa analazimika kutumia insulini. Mary Ann, ambaye ni muuguzi anayewatunza watu kadhaa wanaougua kisukari, anasema hivi: “Kutumia insulini hakumaanishi kwamba wewe ndiwe umejisababishia tatizo hilo.” Kisha anaongeza: “Hata uwe unaugua aina gani ya kisukari, ukidhibiti kiwango cha sukari katika damu yako, utazuia matatizo mengine ya afya yanayoweza kuzuka baadaye.” Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi ulionyesha kwamba watu wanaougua ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 1 ambao walidhibiti kabisa viwango vya sukari vilivyo katika damu yao “hawakupata sana magonjwa ya macho, ya figo, na ya neva ambayo husababishwa na kisukari.” Kwa mfano, uwezekano wa kupata ugonjwa wa macho ulipungua kwa asilimia 76! Watu wanaougua ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 2 ambao hudhibiti viwango vya sukari katika damu hupata matokeo hayo mazuri pia.
Ili kufanya matibabu ya kutumia insulini yawe rahisi na yasisababishe maumivu mengi, mara nyingi sindano mbalimbali hutumiwa. Sindano nyingine hufanana na kalamu. Sindano hizo za insulini huwa ndogo sana, hivyo hazisababishi maumivu mengi. Mary Ann anasema hivi: “Sindano ya kwanza ndiyo yenye maumivu makali.” Halafu anaongeza hivi: “Baada ya hapo, wagonjwa wengi husema kwamba hawahisi maumivu yoyote.” Sindano nyingine hupenya ngozini bila kusababisha maumivu yoyote, nyingine hupenyeza insulini ngozini kwa nguvu, na nyingine zenye mirija huwekwa kwenye ngozi na kubaki hapo kwa muda wa siku mbili au tatu. Kifaa fulani cha insulini chenye ukubwa wa simu ndogo ya mkononi kimeanza kutumiwa sana katika miaka ya majuzi. Kifaa hicho kimetengenezwa ili kiingize insulini mwilini kupitia kwa mrija kulingana na mahitaji ya mwili. Kwa njia hiyo mgonjwa anaweza kupata kiwango kamili cha insulini kwa wakati unaofaa.
Endelea Kuongeza Maarifa
Ugonjwa wa kisukari hauna tiba. Mtu anapochagua matibabu, anapaswa kuzingatia mambo kadhaa ili afanye uamuzi wake. Mary Ann anasema hivi: “Hata kama unatunzwa na madaktari, wewe ndiwe mwenye daraka kubwa.” Jarida Diabetes Care linasema hivi: “Haitoshi tu kupata matibabu ya kisukari, kwani mtu anahitaji kuongeza maarifa yake ili ajitunze kikamili.”
Wale wanaougua kisukari wakiendelea kuongeza maarifa yao kuhusu ugonjwa huo, wataweza kujitunza vizuri zaidi na kuongeza matumaini yao ya kuishi kwa muda mrefu. Hata hivyo, mgonjwa anahitaji subira ili ajifunze mengi. Kitabu Diabetes—Caring for Your Emotions as Well as Your Health kinaeleza hivi: “Ukijaribu kujifunza mambo yote mara moja, unaweza kuchanganyikiwa na kukosa kutumia habari hiyo kwa njia inayofaa. Isitoshe, habari nyingi unazohitaji kujifunza hazimo katika vitabu au magazeti. Mengi yanategemea . . . jinsi kiwango cha sukari katika damu yako kinavyobadilika unapofanya shughuli mbalimbali. Maarifa yako yataongezeka baada ya muda, kadiri unavyozoeleana na hali yako.”
Kwa mfano, ukijichunguza kwa makini utajua jinsi mwili wako unavyofanya kazi unapopatwa na mfadhaiko, kwani mfadhaiko unaweza kuongeza sana kiwango cha sukari katika damu. Ken anasema hivi: “Nimeugua ugonjwa wa kisukari kwa miaka 50 nami ninajua ishara ambazo mwili wangu hutoa.” Kuelewa ishara ambazo mwili wake hutoa kumemsaidia sana, kwani bado Ken anaweza kufanya kazi ya wakati wote hata ingawa ana umri wa zaidi ya miaka 70!
Utegemezo wa Familia Ni Muhimu
Jambo moja muhimu linaloweza kufanikisha matibabu ya ugonjwa wa kisukari ni utegemezo wa familia. Kitabu kimoja kinasema kwamba “maisha bora ya familia ni muhimu zaidi” katika kupambana na ugonjwa wa kisukari kwa watoto na vijana.
Ni muhimu washiriki wa familia wajifunze kuhusu ugonjwa wa kisukari. Wanaweza hata kuwa na zamu za kumpeleka mgonjwa kwa daktari. Wakijifunza juu ya ugonjwa huo wataweza kumsaidia mgonjwa, watatambua dalili mbalimbali za ugonjwa huo, na watajua mambo wanayopaswa kufanya wanapoziona. Mke wa Ted ameugua ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 1 tangu alipokuwa na umri wa miaka minne. Ted anasema hivi: “Ninaweza kutambua wakati ambapo kiwango cha sukari cha Barbara kimepungua sana. Ikiwa mlikuwa mnaongea, atanyamaza. Yeye hutokwa na jasho jingi, hukasirika bila sababu, naye hafanyi mambo chapuchapu.”
Vivyo hivyo, Catherine anapoona kwamba mwili wa mume wake, Ken, umekuwa baridi, uso wake umebadilika na kwamba hana furaha, yeye humuuliza swali rahisi la hesabu. Ken akichanganyikiwa, basi Catherine anatambua kwamba anapaswa kufanya maamuzi yote na kuchukua hatua mara moja kurekebisha hali hiyo. Ken na Barbara wanathamini sana kuwa na wenzi wa ndoa ambao wanawapenda na kuwatumaini kabisa.f
Washiriki wa familia wenye upendo wanapaswa kujitahidi kusaidia, kuwa wenye fadhili na wenye subira kwani mambo hayo yanaweza kumsaidia mgonjwa kukabiliana vyema na matatizo yake na hata kuboresha hali yake. Mume wa Karen alimhakikishia Karen kwamba anampenda na jambo hilo lilimsaidia sana. Karen anasema hivi: “Nigel aliniambia, ‘Watu wanahitaji chakula na maji ili waishi, nawe unahitaji chakula na maji na insulini kidogo tu.’ Maneno hayo yenye kutia moyo na ya kweli kabisa yalinisaidia sana.”
Washiriki wa familia na marafiki wanahitaji pia kuelewa kwamba mtazamo wa mtu anayeugua kisukari unaweza kubadilika kadiri viwango vya sukari katika damu vinavyobadilika-badilika. Mwanamke mmoja asema hivi: “Kiwango cha sukari kinapobadilika mimi hunyamaza sana, mtazamo wangu hubadilika, nami hukasirika haraka, na kufadhaika. Halafu mimi hujihisi vibaya kwa sababu ya kufanya mambo hayo ya kitoto. Lakini mimi hufarijika ninapotambua kwamba wengine wanaelewa hisia zangu, nami hujaribu kuzidhibiti.”
Mtu anayeugua kisukari na hasa yule mwenye marafiki na familia yenye ushirikiano aweza kukabiliana vyema na ugonjwa huo. Kanuni za Biblia zinaweza pia kusaidia. Jinsi gani?
[Maelezo ya Chini]
a Magonjwa hayo hutia ndani ugonjwa wa moyo, kiharusi, ugonjwa wa figo, ugonjwa wa mishipa ya damu, na kuharibika kwa neva. Mtu asipopata damu ya kutosha miguuni anaweza kupata vidonda, na nyakati nyingine inabidi mguu ulioathiriwa ukatwe. Mara nyingi, ugonjwa wa kisukari ndio husababisha watu wazima kuwa vipofu.
b Gazeti la Amkeni! halipendekezi aina fulani hususa ya tiba. Wale wanaodhani kwamba wana ugonjwa huo wanapaswa kumwona daktari aliye na ujuzi wa kuzuia na kudhibiti ugonjwa huo.
c Kuna hatari kubwa ya kuugua ugonjwa huo ikiwa mtu ana mafuta mengi katika tumbo lake kuliko katika mapaja yake.
d Wavutaji wa sigara wanakabili hatari kubwa zaidi kwani zoea hilo hudhuru moyo na mfumo wa mzunguko wa damu na kubana mishipa ya damu. Kitabu kimoja kinasema kwamba asilimia 95 ya watu wanaougua kisukari ambao hulazimika kukatwa viungo ni wavutaji wa sigara.
e Baadhi ya wagonjwa hao walisaidiwa na dawa za kumeza. Dawa hizo zatia ndani zile ambazo huchochea kongosho kutokeza insulini zaidi, nyingine hudhibiti ongezeko la sukari katika damu, na nyingine huwezesha chembe za mwili kupokea insulini. (Kwa kawaida, watu wanaougua ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 1 hawapewi dawa za kumeza.) Kwa sasa, insulini haiwezi kumezwa kama dawa za kawaida, kwani protini hiyo humeng’enywa kabla haijafika kwenye damu. Hata ikiwa mgonjwa anatumia insulini na dawa za kumeza, bado anahitaji kufanya mazoezi na kupata lishe bora.
f Wataalamu wa tiba hupendekeza kwamba watu wanaougua kisukari wabebe kitambulisho na kuvaa mkufu unaoweza kuwatambulisha. Kitambulisho hicho kinaweza kuokoa uhai hali ya dharura ikitokea. Kwa mfano, mtu aliyepungukiwa sukari mwilini anaweza kueleweka kimakosa kuwa ana ugonjwa mwingine au kwamba yeye ni mlevi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Je, Ugonjwa Huo Unawapata Vijana?
Ugonjwa wa kisukari “umeanza kuwapata vijana,” asema Dakt. Arthur Rubenstein, mtaalamu wa tezi zinazozalisha homoni wa Taasisi ya Kitiba ya Mount Sinai huko New York. Ugonjwa wa kisukari unazidi kuwapata vijana wengi zaidi. Dakt. Robin S. Goland, mtaalamu wa ugonjwa wa kisukari, alisema hivi akizungumzia ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 2: “Miaka kumi iliyopita, tuliwafundisha wanafunzi wa kitiba kwamba watu walio chini ya umri wa miaka 40 hawapati ugonjwa huo. Lakini siku hizi hata watoto walio chini ya umri wa miaka 10 wanaugua ugonjwa huo.”
Kwa nini vijana wengi zaidi wanaugua kisukari? Wengine wao wamerithi ugonjwa huo. Lakini unene na mazingira ni mambo mengine yanayoweza pia kusababisha ugonjwa huo. Idadi ya watoto wanene kupita kiasi imeongezeka mara mbili katika miaka 20 iliyopita. Ni nini kimesababisha hali hiyo? Dakt. William Dietz wa Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa anasema hivi: “Mazoea ya kula na ya kucheza yamebadilika katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Mabadiliko hayo yanatia ndani kula vyakula mikahawani; kutopata kifungua-kinywa wakati mwingine; kunywa soda na vitafuno vingi visivyo na lishe; kupunguzwa kwa wakati wa kucheza na kutopata wakati wa kupumzika shuleni.”
Ugonjwa wa kisukari hauna tiba. Basi, ni jambo la busara kufuata shauri hili la kijana mmoja anayeugua ugonjwa huo: “Dumisha afya bora kwa kuepuka vyakula visivyo na lishe.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Kazi ya Glukosi
Glukosi ni aina ya sukari ambayo huzipa chembe za mwili nishati. Hata hivyo, ili glukosi iingie ndani ya chembe hizo inahitaji insulini. Insulini ni kemikali ambayo hutokezwa na kongosho. Mtu anayeugua Aina ya 1 ya kisukari hana insulini yoyote mwilini. Mara nyingi, mtu anayeugua Aina ya 2 ya kisukari huwa na insulini lakini haitoshi.g Zaidi ya hayo, chembe haziruhusu insulini iingie kwa urahisi. Athari za magonjwa hayo mawili zinafanana, yaani, chembe za mtu anayeugua hukosa nishati na damu yake huwa na viwango hatari vya sukari.
Katika ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 1, mfumo wa kinga mwilini hushambulia chembe aina ya beta zilizo kwenye kongosho. Chembe hizo ndizo hutokeza insulini. Baadhi ya vitu vinavyoweza kusababisha mfumo wa kinga kushambulia chembe za beta vinatia ndani virusi, kemikali zenye sumu, na dawa fulani. Pia, huenda chembe za urithi zikachangia ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 1. Wahindi-Wazungu ndio wenye tatizo hilo hasa.
Ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 2 ndio hurithiwa hata zaidi, lakini Wahindi-Wazungu hawarithi ugonjwa huo sana. Waaustralia wa asili na Wahindi-Wamarekani ndio wanaougua ugonjwa huo zaidi. Wahindi-Wamarekani ndio wanaofanyiza idadi ya juu zaidi ya watu wanaougua ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 2 ulimwenguni pote. Watafiti wanachunguza uhusiano uliopo kati ya chembe za urithi na unene wa kupita kiasi na vilevile jinsi ambavyo mafuta mengi katika miili ya watu wanaorithi ugonjwa huo yanavyofanya insulini isiingie ndani ya chembe.h Tofauti na ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 1, Aina ya 2 huwapata hasa watu ambao wamepita umri wa miaka 40.
[Maelezo ya Chini]
g Asilimia 90 ya watu wanaougua kisukari huugua Aina ya 2. Hapo zamani aina hiyo ya kisukari ilijulikana kama kisukari “kisichotegemea insulini” au kisukari “kinachowapata watu wazima.” Lakini semi hizo hazielezei waziwazi ugonjwa huo, kwani asilimia 40 ya watu wanaougua ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 2 wanahitaji insulini. Isitoshe, vijana wengi zaidi—hata wale walio chini ya umri wa miaka 13—wanaugua ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 2.
h Kwa kawaida mtu aliyenenepa kupita kiasi huwa amezidi uzito wa kawaida kwa asilimia 20 au zaidi.
[Picha]
Molekuli ya glukosi
[Hisani]
Courtesy: Pacific Northwest National Laboratory
[Sanduku katika ukurasa wa 9]
Kazi ya Kongosho
Kongosho ina ukubwa wa ndizi na inapatikana nyuma ya tumbo. Kulingana na kitabu The Unofficial Guide to Living With Diabetes, “kongosho isiyo na kasoro yoyote hufanya kazi ya kusawazisha na kudumisha utaratibu mzuri wa viwango vya sukari katika damu kwa kutokeza kiwango kinachofaa cha insulini kadiri viwango vya glukosi vinavyobadilika-badilika.” Chembe za beta zilizo katika kongosho ndizo hutokeza homoni ya insulini.
Wakati ambapo chembe za beta hazitokezi insulini ya kutosha, glukosi huongezeka katika damu. Kwa upande mwingine, kiwango cha sukari kinaweza kupungua katika damu. Ini hufanya kazi pamoja na kongosho ili kudhibiti viwango vya sukari katika damu kwa kuhifadhi glukosi ya ziada. Glukosi hiyo huhifadhiwa ikiwa glikojeni. Kongosho hutuma ishara kwenye ini, kisha ini hubadilisha glikojeni kuwa glukosi ili itumiwe mwilini.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Kazi ya Sukari
Watu hudhani kimakosa kwamba ukila sukari nyingi utapatwa na ugonjwa wa kisukari. Uthibitisho wa kitiba unaonyesha kwamba mtu mwenye chembe za urithi za kisukari anaponenepa, anakabili hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa huo hata iwe anakula sukari au la. Hata hivyo, kula sukari nyingi ni hatari kwani sukari haina virutubisho vingi na huchangia kunenepa kupita kiasi.
Pia, inaeleweka kimakosa kwamba watu wanaougua kisukari hutamani sukari kupita kiasi. Lakini ukweli ni kwamba watu wanaougua kisukari wanapenda vitu vitamu kama watu wengine. Ugonjwa wa kisukari usipodhibitiwa, unaweza kumfanya mtu ahisi njaa—lakini si lazima njaa hiyo iwe imesababishwa na kutamani sukari. Watu wenye kisukari wanaweza kula peremende, lakini wanapaswa kudhibiti kiasi cha sukari wanachokula.
Uchunguzi mbalimbali uliofanywa hivi majuzi umeonyesha kwamba wanyama wenye uzito wowote ule wanapokula matunda na mboga nyingi zenye sukari, wanaweza kufanya insulini isiingie ndani ya chembe na hata kuwafanya wapate kisukari.
[Michoro/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Kueleza Kisukari kwa Njia Rahisi
KONGOSHO
Mtu Ambaye Hana Kisukari
Baada ya mlo, glukosi huongezeka kwenye damu, hivyo kongosho hutokeza kiwango kinachofaa cha insulini
Molekuli za insulini hushikamana na vipokezi vilivyo kwenye chembe za misuli na chembe nyinginezo. Jambo hilo hufanya milango ya chembe za misuli iruhusu molekuli za glukosi kuingia ndani ya chembe
Ugonjwa wa Kisukari wa Aina ya 1
Chembe za beta zinazotokeza insulini zilizo kwenye kongosho hushambuliwa na mfumo wa kinga. Hivyo, insulini haitokezwi
Molekuli za glukosi haziwezi kuingia ndani ya chembe za misuli bila insulini
Ugonjwa wa Kisukari wa Aina ya 2
Kwa kawaida kongosho haitoi insulini ya kutosha
Ikiwa vipokezi havifanyi kazi vizuri, basi milango ya chembe ambayo hufyonza glukosi kutoka kwenye damu haitafanya kazi
Chembe za misuli hufyonza glukosi na kuitumia. Kwa hiyo kiwango cha glukosi katika damu hurudia hali yake ya kawaida
▲ Glukosi huongezeka kwenye damu, na hivyo kuzuia utendaji muhimu mwilini na kuharibu kuta za mishipa ▼
[Mchoro]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
CHEMBE
Kipokezi
Mlango wa chembe
Insulini
Kiini
Glukosi
[Mchoro]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MSHIPA
Chembe nyekundu za damu
Glukosi
[Hisani]
Man: The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck
[Picha katika ukurasa wa 7]
Chakula chenye lishe ni muhimu sana kwa watu wanaougua kisukari
[Picha katika ukurasa wa 10]
Watu wanaougua kisukari wanaweza kufanya shughuli za kawaida
-
-
Jinsi Biblia Inavyoweza Kuwasaidia Wanaougua KisukariAmkeni!—2003 | Mei 8
-
-
Jinsi Biblia Inavyoweza Kuwasaidia Wanaougua Kisukari
NI MUHIMU sana watu wanaougua ugonjwa wa kisukari wajidhibiti na kuwa na mtazamo unaofaa ili wadumishe afya bora. Lakini ili wasitawishe sifa hizo, wanahitaji kutegemezwa daima. Kwa hiyo haifai washiriki wa familia na marafiki kuwashawishi wale vyakula vinavyoweza kuwadhuru, labda wakisema, ‘Kula kidogo tu, hakitakudhuru.’ “Mke wangu hunitegemeza sana,” asema Harry, anayeugua ugonjwa wa moyo na ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 2. “Hawezi kununua vyakula vinavyoweza kunidhuru. Lakini watu wengine hawaelewi, wala hawajui jinsi ilivyo vigumu kujizuia kula vyakula ambavyo vinatamanisha.”
Ikiwa wewe hushirikiana kwa ukawaida na mtu anayeugua ugonjwa wa kisukari, zingatia kanuni hizi mbili zinazopatikana katika Biblia: “Acheni kila mmoja afulize kutafuta sana, si faida yake mwenyewe, bali ya mtu yule mwingine,” na “Upendo . . . hautafuti masilahi yao wenyewe.”—1 Wakorintho 10:24; 13:4, 5.
Watu wote wanaojali afya yao wanapaswa kudhibiti ulaji wao, iwe wanaugua kisukari au la. Biblia inatoa msaada kuhusiana na hilo, kwani inaonyesha kwamba tunahitaji kusitawisha sifa ya kujidhibiti. Je, umeazimia kusitawisha sifa hiyo maishani mwako? (Wagalatia 5:22, 23) Pia, mifano ya watu wanaotajwa katika Biblia inaweza kukusaidia, kama vile mfano wa mtume Paulo. Mtu mmoja anayeugua ugonjwa wa kisukari anasema hivi: “Paulo alikuwa na mwiba wa kudumu katika mwili wake, lakini alimtumikia Mungu kwa uaminifu na kwa ukamili. Basi, mimi pia ninaweza!”
Naam, Paulo alizoea hali hiyo ambayo hangeweza kuibadili na akapata mafanikio mengi akiwa mishonari. (2 Wakorintho 12:7-9) Dustin, ambaye ana umri wa miaka 18, alizaliwa akiwa kipofu, naye amekuwa akiugua ugonjwa wa kisukari tangu alipokuwa na umri wa miaka 12. Anaandika hivi: “Ninajua kwamba hakuna mtu duniani aliye na maisha makamilifu. Ninatarajia wakati ambapo nitapona katika ulimwengu mpya wa Mungu. Ninaona ugonjwa huu kuwa wa muda tu. Huenda ugonjwa huu ukadumu kwa muda mrefu kuliko mafua au homa, lakini hatimaye utakwisha.”
Dustin alikuwa akizungumzia tumaini linaloonyeshwa katika Biblia la kuishi maisha makamilifu katika dunia paradiso kupitia Ufalme wa Mungu. (Ufunuo 21:3, 4) Neno la Mungu linaahidi kwamba chini ya utawala wa Mungu, “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24; Mathayo 6:9, 10) Je, ungependa kujua mengi zaidi kuhusu ahadi hiyo inayoelezwa katika Biblia? Wasiliana na Mashahidi wa Yehova wa eneo lako, au uwaandikie wachapishaji wa gazeti hili ukitumia anwani ifaayo iliyoorodheshwa kwenye ukurasa wa 5.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Ni muhimu kujidhibiti na kuwa na mtazamo unaofaa
-