Kuutazama Ulimwengu
Kutafuta Kuelimishwa Kiroho
“Mwisho wa karne unapokaribia, Waingereza wanatafuta jambo fulani la kiroho maishani mwao, jambo linaloonyeshwa na tamaa yao kubwa ya vitabu vinavyohusu imani, mambo ya kimafumbo na nguvu zinazozidi zile za kibinadamu,” lasema gazeti la habari The Times. Kulingana na uchunguzi katika Cultural Trends, idadi ya vitabu vyenye vichwa vya kidini imeongezeka kwa kiwango cha asilimia 83 katika miaka mitano iliyopita na vile vinavyohusu Muhula Mpya na mambo ya kimafumbo kwa kiwango cha asilimia 75. Kwa kutofautisha, idadi ya vitabu vya sayansi vinavyochapishwa imepungua, huku vya kemia na fizikia vikipungua kwa asilimia 27. Akitafakari juu ya takwimu hizi, Sara Selwood, mhariri wa ripoti hiyo, alidokeza kwamba, “kuelekea mwisho wa karne, watu hujichunguza zaidi na kushangazwa na kusudi halisi la maisha.” Basi kwa nini atlasi na vitabu vya jiografia vimeongezeka kwa kiwango cha asilimia 185? Huenda ikadokeza “uhitaji wa kukwepa matatizo,” akasema.
Uhuru wa Kidini Wakiukwa Ulaya
Shirika la International Helsinki Federation “limeshtaki nchi 19 za Ulaya kwa kukiuka uhuru wa kidini,” laripoti gazeti Catholic International. Shirika hilo lilisema kwamba kumekuwa na mkazo mkubwa dhidi ya dini ndogondogo hasa katika nchi za Othodoksi. Kwa kuongezea, nchi kadhaa za Muungano wa Ulaya “zinatunga sheria ili kuimarisha hadhi ya itikadi za kidesturi huku wakizuia vikundi vidogo zaidi kama vile [Mashahidi wa Yehova],” likasema gazeti hilo. Mkurugenzi wa shirika hilo, Aaron Rhodes, aliongezea hivi: “Jamii za Magharibi zinaonyesha kwamba hofu yao ya ‘kuvamiwa na mafarakano’ inawafanya wakandamize dini ndogondogo. Hali hiyo itazidi kuwa mbaya mpaka watu waje kutambua uhuru wa itikadi kuwa sehemu ya maadili na sheria zilizowekwa ambazo lazima zitegemezwe kwa njia sawa kwa kila mtu.”
“Theolojia ya Ufanisi”
“Makanisa ya Kiprotestanti ya jadi katika Amerika ya Latini ‘yanashindwa kwa idadi ya washiriki’ na makanisa mapya yanayokua haraka ambayo yanahubiri ‘theolojia ya ufanisi,’” lasema ENI Bulletin, likinukuu mwanatheolojia Mlutheri Wanda Deifelt. Kulingana na Deifelt, makanisa ya Brazili ya Kipentekoste na ya karama sasa yana “washiriki mara mbili au tatu zaidi ya makanisa makubwa-makubwa ya jadi.” “Theolojia ya ufanisi” huahidi waumini “thawabu za papo hapo kwa kutoa michango ya kifedha kwa kanisa,” akasema. “Kusali kwa Mungu ni kama mapatano ya kibiashara . . . Nikimpa Mungu kitu fulani, Mungu anapaswa kunipa kitu fulani.” Makanisa hayo huandikisha washiriki kutoka watu walio maskini wa Brazili. Kwa nini washiriki hubaki hata wanapokosa kupata ufanisi ulioahidiwa na huku viongozi wa kanisa ndio wanaofaidika zaidi? Asema Deifelt: “Mtazamo ulio wa kawaida zaidi ni kuwa na [dini] mbili ili kuhakikisha kwamba ikiwa moja haitaleta ufanisi, ile nyingine italeta.” Mbali na hilo, “wao huzungumza juu ya mambo ambayo watu wanahangaikia, na kusema mambo ambayo watu wanataka kusikia.”
Kagueni Michezo ya Vidio
“Wazazi wanaonwa kuwa wajinga,” lasema gazeti la habari la Ufaransa Le Figaro. Kwa nini? Kwa sababu yaelekea wengi wao hawajui mambo yaliyo katika michezo ya vidio ya vijana. Kwa mfano, kusudi la mchezo mmoja ni kumtesa adui, kusudi la mwingine ni kuwakanyaga watu wanaotembea kwa miguu. Mojawapo ya michezo ambayo imependwa sana hivi karibuni huonyesha njia kumi za hila za kutesa mwanamke. Gazeti Le Figaro linawatia moyo wazazi “wachunguze kwa makini kabisa” michezo ya watoto wao ili kufahamu “unyama uliojificha,” unaokuwapo mara nyingi. Kukubali “kununua kile ambacho vijana wanaomba bila kukikagua ni jambo linalozidi kuwa hatari,” lasema gazeti hilo la habari. Pia lilizusha swali hili, “Je si ufidhuli kuendelea kuzungumza juu ya haki za kibinadamu huku tukiacha rafu zikiwa zimejaa vitu ambavyo hukiuka waziwazi haki hizo?”
“Msaidiaji Aliyepuuzwa”
Jambo la maana katika kupona kwa wagonjwa walio hospitalini limepuuzwa kwa muda mrefu, lasema jarida la Ujerumani Psychologie Heute. Ni mgonjwa aliye katika kitanda kilicho karibu. Uchunguzi ulionyesha kwamba kuwa na mgonjwa mwenzi karibu husaidia kuponya mgonjwa na kwamba kinyume na itikadi inayopendwa, ni wagonjwa wachache sana kati ya wote, karibu asilimia 7, wanaotaka kuwa peke yao. Wengi wao hutaka kushiriki chumba cha hospitali na mgonjwa mmoja au wawili. Hata hivyo, ikitegemea wao ni watu wa aina gani wanaweza kuathiri kupona kwa mgonjwa. Mshiriki wa chumba aliye bora “kwanza kabisa apaswa kuwa mwenye urafiki na mvumilivu,” ikasema makala hiyo. Sifa zifuatazo zenye kutamanika ziliorodheshwa kwa kufuatana na umuhimu wazo: “uelewevu, ucheshi, usafi, utayari wa kupokea mawazo, utayari wa kusaidia, ufikirio, utaratibu, urafiki, ufuatiaji haki, unadhifu, usawaziko, saburi, busara, fadhili, utulivu, kuwa na akili, kubadilikana, na kuwa chonjo.”
Hatari za Kufanya Mazoezi Kupita Kiasi
Ingawa mazoezi hunufaisha moyo na mapafu, mazoezi yanayopita kiasi yanaweza kudhoofisha mifupa, na kusababisha matatizo baadaye maishani. Ndivyo ilivyoripotiwa kwenye mkutano unaoshughulika na athari za mazoezi kwa kiunzi cha binadamu, kulingana na The Guardian la London. Wakimbiaji na wale “wanaofuatia afya bora kabisa” ndio wanaokabili hatari kubwa zaidi. Wanawake wachanga wanaofanya mazoezi ya viungo au kucheza dansi mara nyingi, hupatwa na msuguano zaidi na wanasemekana kuwa wanaelekeana na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa mifupa wanapokuwa na umri mkubwa zaidi. “Wanariadha walionywa kwamba wanapaswa kuimarisha mifupa yao wanapofikia umri wa miaka 18 au 19 kabla haijaanza kudhoofika zaidi baada ya muda,” ikasema makala hiyo. “Skwoshi na tenisi ilitajwa kuwa michezo bora ya kuongeza nguvu za mifupa.” Michael Horton, mkuu wa kituo cha mifupa cha University College ya London, alishauri kudumisha usawaziko unaofaa kati ya mazoezi na afya. Alionya: “Serikali inazidi kusema kwamba vijana wanapaswa kufanya mazoezi mengi. Huenda yakawa na manufaa kwa muda fulani, lakini hakuna mtu ajuaye matokeo yatakuwa nini vijana hawa watakapofikisha umri wa miaka 50.”
Tatizo la Uzito
Tangu mwisho-mwisho wa miaka ya 1880, Le Grand K, mcheduara wa platinamu-iridiamu wenye ukubwa wa kopo la kuwekea filamu, umekuwa kiwango cha ulimwenguni pote cha kupima kilogramu moja. Hata pauni ya Marekani inautegemea. Hata hivyo, wanasayansi wana wasiwasi kwamba uzito wa mcheduara huu unabadilika. Ukiwa umefungiwa ndani ya mitungi mitatu yenye umbo la kengele na kufungiwa ndani ya sefu katika kitongoji kimoja cha Paris, Ufaransa, mcheduara huo umetolewa mara tatu tu kwa karne moja. Gazeti Science laripoti kwamba baada ya vipindi vya karibuni zaidi, wanasayansi “walifikia mkataa kwamba uzito wake ulikuwa ukibadilika kwa sehemu bilioni 5 za gramu kwa mwaka mmoja.” Tofauti hii ndogo—labda punje moja—yaweza kuwa inachangiwa na uchafu ambao hurundamana kwenye sehemu ya juu ya kitu hiki licha ya jitihada ya kukisafisha. Tekinolojia ya leo hutaka vipimo vilivyo sahihi hata zaidi. Kwa kielelezo, safari za kwenda angani hutegemea saa za atomi ambazo hupoteza sekunde moja tu katika kipindi cha miaka milioni 1.4. Hivyo wanasayansi wangali wanajadiliana jinsi ya kuanzisha kiwango kisichobadilika cha kupima kilogramu. Hata hivyo, lasema gazeti la Science, huenda hili likataka “kiwango kilicho sahihi kitakachowafanya wanasayansi wawe na wasiwasi kuhusu athari ndogo kama vile kupotea kwa atomu.”
Je, Hakuna Ponyo la Mafua?
Baada ya miaka kumi ya utafiti uliogharimu dola milioni nane, Kituo cha Mafua cha Uingereza hatimaye kimekubali kushindwa. Kukiwa na zaidi ya virusi tofauti-tofauti 200 vinavyosababisha mafua, kujaribu kupata ponyo moja la mafua ni “sawa na kujaribu kutibu surua, tetekuwanga, matumbwitumbwi na surua ya Ujerumani mara moja,” asema Profesa Ronald Eccles, mkurugenzi wa kituo hicho kwenye Chuo Kikuu cha Wales, Cardiff. “Sioni kimbele ponyo litakalotusaidia kumaliza kabisa virusi vyote. Nafikiri itakuwa bora kutoifikiria kupita kiasi.”
Mambo Yaliyotimizwa na Kimbunga Mitch
Ijapokuwa kimbunga Mitch kilicholeta uharibifu mwaka jana, kiliua maelfu kama tokeo na kuathiri takriban watu milioni moja, kilikuwa na manufaa moja ya matokeo ya baadaye. Kilisaidia waakiolojia waliokuwa wakichimbua magofu ya León Viejo, Nikaragua—yaliyo kilometa zipatazo 90 kusini-mashariki ya jiji kuu—kwa “kufunua kuta mpya, mifupa, na vitu kadhaa vya kiakiolojia,” laripoti gazeti la habari Excelsior, la Mexico City. Rigoberto Navarro, mkurugenzi wa León Viejo Ruins Historical Site, alifafanua kwamba kimbunga Mitch kiliosha ardhi na kufunua mahali ambapo waakiolojia walikuwa wakipatafuta kwa muda mrefu bila kufanikiwa. Ukuta wenye kimo cha meta 2.5, upana wa sentimeta 70 na urefu wa meta 100 ulifukuliwa. Kulingana na Navarro, “kwa siku tatu kimbunga hicho kilifanya kazi ambayo ingewachukua waakiolojia muda wa miaka kumi,” likasema gazeti hilo la habari.