Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 4/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Fungu Jipya la Nikotini?
  • Jiji Linalozama
  • Watoto Wakaidi
  • Kimbunga Mitch Chenye Kufisha
  • Kukabiliana na Haya
  • Matokeo ya Kupunguza Kuzaa
  • Je, Mkanda wa Usalama Ni Dhidi ya Mapenzi ya Mungu?
  • Mlo wa Mafuta
  • Kujinyima Usingizi Kunaongezeka
  • Aksidenti—Si Ajali
  • Sababu ya Mwili Wako Kuhitaji Usingizi
    Amkeni!—1995
  • Je, Watu Wengi Wana Deni la Usingizi?
    Amkeni!—2004
  • Kuokolewa Kutoka Kwenye Dhoruba Yenye Kufisha!
    Amkeni!—1999
  • Watetea Tumbaku Waanzisha Puto la Hewa-Joto
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 4/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Fungu Jipya la Nikotini?

Makampuni ya madawa huuza chingamu iliyotiwa nikotini na vibandiko vinavyotia nikotini mwilini kupitia ngozi ikiwa misaada ya muda mfupi ya kuacha uvutaji wa sigareti. Ijapokuwa bidhaa hizi hazipasi kutumiwa kwa zaidi ya majuma 6 hadi 12, wavutaji wengi wa sigareti huendelea kuzitumia kwa miaka mingi, laripoti The Wall Street Journal. Sasa makampuni ya madawa yanataka kanuni za serikali zibadilishwe ili kuwe na ruhusa ya kuuza vitu vinavyotia nikotini vinavyotumiwa kwa muda mrefu. Makampuni fulani hayajali kwamba watumiaji wengi wataendelea kuwa waraibu wa nikotini ingawa makampuni ya madawa hayataki kujulikana kuwa yenye kujipatia faida kutokana na uraibu kama vile makampuni ya tumbaku. Hata hivyo, David Sachs, mkurugenzi wa Kituo cha Kinga ya Maradhi ya Mapafu cha Palo Alto, California, alisema hivi: “Karibu kila kampuni ya madawa huona sehemu hii kuwa yenye faida kubwa.”

Jiji Linalozama

“Mexico City linazama,” lataarifu The New York Times. “Maji mengi sana yamevutwa kutoka kwenye mwamba wenye maji ulio chini yake ili kuwatosheleza wakazi milioni 18 wa eneo la jiji kuu hivi kwamba ardhi iliyo chini yake inazama kwa kiwango cha kufadhaisha.” Na jambo linalozidisha tatizo hilo ni uhakika wa kwamba “mfumo wa kugawanya maji wa Mexico City ni mojawapo ya mifumo inayovuja sana ulimwenguni pote. Karibu thuluthi moja ya kila galoni moja ya maji safi yanayopitishwa kwa mfumo huo huvuja.” Hili lamaanisha kwamba lazima maji mengi zaidi yavutwe kutoka chini na kwa hiyo jiji huzama zaidi. Kila mwaka vikundi vya warekebishaji hurekebisha sehemu zaidi ya 40,000 zilizotoboka, na bado sehemu nyingi zilizotoboka haziripotiwi. Bila shaka, si Mexico City peke yake linalozama. Kwa mfano, katika karne ya 20, jiji la Venice, Italia, limezama kwa sentimeta 23. Lakini Mexico City limezama kwa meta tisa!

Watoto Wakaidi

Uchunguzi mmoja wa vijana Wamarekani 16,262 umeonyesha kwamba takriban kijana 1 kati ya 5 hubeba silaha na 1 kati ya 10 amejaribu kujiua, laripoti The New York Times. Wanafunzi kutoka shule 151 nchini kote walihusika katika uchunguzi huo. Maswali ya siri yalitumiwa ili kupata habari kuhusu utendaji wa kimwili na kingono wa wanafunzi hao na pia kuhusu utumiaji wao wa dawa za kulevya, vileo, na tumbaku. Laura Kann, wa Kituo cha Kuzuia Maradhi Sugu na cha Kuendeleza Afya, asema hivi: “Somo lililopo ni kwamba vijana wengi sana wanaendelea kuzoea tabia ambazo zinawahatarisha—ya kujeruhiwa au kufa sasa au hata kupata maradhi ya kudumu baadaye.”

Kimbunga Mitch Chenye Kufisha

Mnamo Oktoba 27, 1998, Kimbunga Mitch kilikumba Amerika ya Kati, kikasababisha vifo vya watu zaidi ya 11,000. Maelfu wengine hawakujulikana waliko nao walidhaniwa kuwa wamekufa, na yaripotiwa kwamba watu wapatao milioni 2.3 waliachwa bila makao. Nchi zilizopata pigo kubwa zilikuwa Honduras na Nikaragua. Mvua iliyoleta mafuriko yaliyozidi meta moja ilinyesha kwenye sehemu za mashambani, ikitokeza kile ambacho kimetajwa kuwa msiba wa asili ulio mbaya zaidi kuwahi kutukia katika eneo hili kwa muda wa karne mbili zilizopita. Vijiji vingi vilifunikwa kwa maporomoko ya matope au vikafagiliwa mbali na maji ya mafuriko yenye kuongezeka. Rais wa Honduras, Carlos Flores Facusse, alisema: “Katika muda wa saa 72, tumepoteza vitu tulivyojenga, pole kwa pole, kwa miaka 50.” Upweke uliongeza idadi ya vifo na uharibifu. Nyaya za umeme na simu zilizounganisha miji mingi midogo iliyokuwa katika njia ya kimbunga hicho zilikatwa. Mamia ya barabara na madaraja yalibomolewa kabisa, huku waokokaji wakiachwa bila chakula, maji safi, au dawa kwa siku nyingi. Mashirika ya kutoa msaada yalikuwa na chakula cha kutosha lakini hayakuwa na njia za kukigawa. Kwa kuongezea hasara ya vitu vya kimwili, watu wengi walipoteza kazi zao. Kadiri ya asilimia 70 ya mazao muhimu kama vile ndizi, matikiti-maji, buni, na mchele yalifagiliwa mbali. “Kimbunga Fifi cha mwaka wa 1974 si kitu kikilinganishwa na Mitch,” akasema makamu wa rais wa Honduras, William Handal. “Ilichukua muda wa miaka 12 hadi 14 ya jitihada ili kurekebisha uharibifu wa Fifi. Urekebishaji wa sasa utachukua miaka 30 au 40.”

Kukabiliana na Haya

Kulingana na gazeti Toronto Star la Kanada, “karibu asilimia 13 ya watu wazima huona haya sana.” Gazeti hilo laripoti kwamba haya “huwazuia kuishi maisha kamili.” Wataalamu walitoa madokezo ya kukabiliana na haya: “Fikiria mambo ya kuanzishia mazungumzo kutoka kwa habari za matukio, makala za magazeti, vitabu, shughuli za kujifurahisha au sinema.” “Jizoeze stadi za mawasiliano ya mazungumzo na yasiyo ya mazungumzo, kutia ndani kumtazama mtu kwa macho [na] kusikiliza kwa makini sana.” “Jilazimishe kufanya mambo unayohofu.” “Ikiwa wewe ni mzazi wa mtoto mwenye haya, ni muhimu kwako kutokeza fursa nyingi ili mtoto wako ashirikiane na wengine.” Kitia-moyo kilikuwa kwamba usikate tamaa, kwa sababu mambo yaliyoonwa yanaonyesha kwamba kadiri mtu ajitahidivyo kukabiliana na haya, ndivyo inavyokuwa rahisi zaidi.

Matokeo ya Kupunguza Kuzaa

“Kupunguza kuzaa sasa kumetokeza hangaiko katika nchi zilizoendelea kiviwanda,” laripoti International Herald Tribune la Paris. Kwa nini? Kwa sababu yamaanisha kwamba hatimaye hakutakuwa na vijana wa kutosha wa kuwatunza watu wanaozeeka. Kwa kielelezo, nchi kadhaa za Ulaya zina hali inayokaribia hatua ya kuwa na watu wengi zaidi wenye umri wa miaka 60 kuliko wale wenye umri wa chini ya miaka 20. Miongoni mwa sababu zilizotolewa kwa ajili ya idadi hiyo ya watu wanaozeeka ni mwelekeo wa wenzi kuahirisha kupata watoto ili wasafiri, wafuatie kazi-maisha fulani, au waboreshe elimu yao. Sababu nyingine zilizotolewa ni mikazo ya kiuchumi, inayofanya kuwa na watoto kuwe “mzigo wenye kulemea” au “jambo lenye kusumbua,” na uhakika wa kwamba sasa watu wanaishi muda mrefu kuliko walivyoishi zamani.

Je, Mkanda wa Usalama Ni Dhidi ya Mapenzi ya Mungu?

Mwanamume mmoja Mholanzi mwenye umri wa miaka 65 ameomba ruhusa ya kutofuata sheria ya Uholanzi ya kutumia mkanda wa usalama kwa sababu ya imani yake ya kidini. Kulingana na gazeti la habari la Frankfurter Allgemeine Zeitung, mtu huyo ni mfuasi wa kanisa la Reformed Church. Mafundisho ya kanisa lake hudai kwamba mtu hapaswi kujikinga kutokana na aksidenti bali anapaswa kuziona kuwa zinasababishwa na Mungu. Washiriki wengine wa kanisa hilo hawakati bima ya gari nao hukataa chanjo kwa msingi wa kwamba hizo huhitilafiana na “mpango wa Mungu.” Baada ya kuchunguza kisa hicho, mahakama kuu ya Uholanzi iliamua dhidi ya mkata-rufani huyo, ikitaarifu kwamba kujifunga mkanda wa usalama hakuzuii uhuru wa mtu wa kidini.

Mlo wa Mafuta

Mnamo Machi 1978, meli kubwa ya mafuta Amoco Cadiz ilikwama kwenye pwani ya Brit­ta­ny, Ufaransa, ikamwaga tani 230,000 za mafuta-ghafi na kuchafua eneo la kilometa 350 za pwani. Ni madhara gani yaliyoachwa? Tangu mwaka wa 1992, athari za uchafuzi huo zimekwisha kabisa, hata chini kabisa kwenye mchanga wa fuo, asema Profesa Gilbert Mille wa kitivo cha sayansi katika Marseilles. Sifa kwa ajili ya usafishaji huu wa kustaajabisha inaenda kwa bakteria za kiasili zinazomeng’enya misombo ya kikaboni. Moluska na minyoo hushirikiana na bakteria hizi kwa kupindua mchanga daima, zikileta mafuta yoyote juu, ambapo humeng’enywa na bakteria hizo zenye njaa.

Kujinyima Usingizi Kunaongezeka

Wamarekani “wamepunguza usingizi wao kwa muda wa saa moja na nusu usiku kuliko [walivyokuwa] wakilala mwanzoni mwa karne,” lasema Newsweek, “na yaelekea kwamba tatizo hilo litazidi kuwa baya zaidi.” Kwa nini? “Watu wameuona usingizi kuwa kitu kinachoweza kupunguzwa,” asema Terry Young, profesa wa utafiti wa dawa za kinga katika Chuo Kikuu cha Wisconsin. “Mtu huonwa kuwa mfanya-kazi mzuri anapoweza kufanya kazi kwa bidii bila kupata usingizi wa kutosha.” Lakini kujinyima usingizi kwaweza kutokeza madhara mengi, kutia ndani mshuko-moyo na magonjwa ya moyo. Panya walionyimwa usingizi walikufa baada ya majuma mawili na nusu. “Huenda usife ghafula kama panya hao,” lataarifu Newsweek, “lakini huenda kujinyima usingizi kukasababisha kifo chako kwa njia isiyo ya moja kwa moja, wakati daktari mwenye uchovu anapokuagiza utumie dawa zisizofaa au dereva mwenye usingizi anapoyumbayumba na kuingia katika sehemu ya barabara unayoitumia.” Mtafiti wa usingizi James Walsh asema: “Watu wanahitaji kuelimishwa kwamba kulala vya kutosha na kupata pumziko la muda linalofaa ndizo njia zenye kutegemeka zaidi za kukusaidia ubaki ukiwa macho unapoendesha gari au unapofanya kazi.”

Aksidenti—Si Ajali

Wizara ya Afya ya Brazili yaripoti kwamba angalau watoto na wabalehe wapatao 22,000 hufa kila mwaka huko Brazili kwa sababu ya aksidenti. Vifo vingi husababishwa na aksidenti za magari. Hata hivyo, msimamizi wa shirika la Matibabu ya Watoto la Brazili, Lincoln Freire, alitangaza hivi: “Aksidenti zaweza kuepukwa na hivyo haziwezi tena kuonwa kuwa ajali.” Isitoshe, Tereza Costa, mratibu wa kampeni ya kitaifa ya kuzuia aksidenti, alitoa hoja ya kwamba kwa kuwa ‘hatua za serikali katika miaka 15 iliyopita zimepunguza idadi ya vifo vinavyosababishwa na kuhara, maambukizo yanayohusiana na upumuaji, na maradhi ya kuambukizwa,’ kuzuia aksidenti kwaweza pia kuokoa uhai.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki