Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w89 3/1 kur. 30-31
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Habari Zinazolingana
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Maswali Kutoka Kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu
    Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu
  • Kuokoa Uhai kwa Damu—Jinsi Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
w89 3/1 kur. 30-31

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

◼ Je! Mashahidi wa Yehova huruhusu utumizi wa kuondoa damu yao wenyewe na kuiweka akibani na baadaye irudishwe ndani yao?

Mara nyingi wafanya kazi wa tiba hutofautisha kati ya damu homologasi (inayotoka kwa mtu mwingine) na damu otologasi (ya mgonjwa mwenyewe). Inajulikana vizuri kwamba Mashahidi wa Yehova hawakubali damu kutoka kwa wanadamu wengine. Lakini namna gani kutumia damu otologasi, ambalo ni neno linalotumiwa kuhusu njia kadhaa za kuitia?

Baadhi ya njia hizo hazikubaliki kwa Wakristo kwa sababu zinapingana waziwazi na Biblia, lakini nyingine hutokeza mashaka. Bila shaka, wakati ambapo Biblia iliandikwa, kutiwa damu mishipani na kutumia damu kwa njia nyinginezo za kitiba hakukujulikana. Hata hivyo, Mungu aliandaa mielekezo inayowezesha watumishi wake waamue kama njia fulani za kitiba zinazohusisha damu zingeweza kumchukiza.

Mungu amekata shauri kwamba damu inawakilisha uhai na hivyo ni takatifu. Yeye aliamuru kwamba hakuna mwanadamu anayepaswa kuendeleza uhai wake kwa kutwaa ndani damu. Mathalani, Mungu alitaarifu hivi: “Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu . . . Bali nyama pamoja na uhai​—yaani damu​—yake, msile.” (Mwanzo 9:3, 4; Walawi 7:26, 27) Kulingana na Mpaji-Uhai, utumizi pekee wa damu uliokubalika ulikuwa katika dhabihu: “Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu.”​—Walawi 17:11, 12.

Ingawa Wakristo hawako chini ya Sheria ya Musa, Biblia inasema kwamba ni “lazima” sisi ‘tushike mwiko wa damu,’ tukiwa na rai ya kwamba ni takatifu. (Matendo 15:28, 29, NW) Hiyo inaeleweka, kwa maana dhabihu chini ya Sheria zilitangulia kuwa kivuli cha damu ya Kristo, ambayo ndiyo njia ya Mungu ya sisi kuweza kupata uhai wa milele.​—Waebrania 9:11-15, 22.

Damu ingeshughulikiwaje chini ya Sheria ikiwa haikutumiwa katika dhabihu? Tunasoma kwamba wakati mwindaji alipoua mnyama kwa chakula, “[lazima, NW] atamwaga damu yake, na kuifunika mchanga [mavumbi, NW].” (Walawi 17:13, 14; Kumbukumbu 12:22-24) Kwa hiyo damu haikupasa kutumiwa kwa ulishaji mwili wala vinginevyo. Ikiwa ilitolewa katika kiumbe na haikutumiwa katika dhabihu, ingeondolewa mbali iwe katika ardhi, kibago cha nyayo za Mungu.​—Isaya 66:1; linganisha Ezekieli 24:7, 8.

Hiyo inakataa katakata utumizi mmoja ulio wa kawaida sana wa damu otologasi​—kuikusanya damu kabla ya upasuaji, kuiweka akibani, na baadaye kuitia mishipani damu hiyo ya mgonjwa mwenyewe. Katika njia hiyo, mambo hufanywa namna hii: Kabla ya upasuaji wa hiari ya mtu, yuniti fulani za damu kamili-kamili ya mtu huwekwa benki au chembe nyekundu zinatenganishwa, zinagandishwa kwa barafu, na kuwekwa akibani. Halafu ikiwa inaonekana kwamba mgonjwa huyo anahitaji damu wakati au baada ya upasuaji, anaweza kurudishiwa damu yake mwenyewe iliyowekwa akibani. Wasiwasi wa hivi majuzi juu ya magonjwa ambayo huwa katika damu umefanya utumizi huo wa damu otologasi upendwe na watu wengi. Ingawa hivyo, Mashahidi wa Yehova HAWAKUBALI njia hiyo. Kwa muda mrefu sisi tumethamini kwamba kwa uhakika damu hiyo iliyowekwa akibani huwa si sehemu ya mtu yule tena. Imekwisha kuondolewa kabisa ndani yake, kwa hiyo inapasa kuondolewa mbali kupatana na Sheria ya Mungu: “Imwage juu ya nchi kama maji.”​—Kumbukumbu 12:24.

Katika njia iliyo tofauti kidogo ya kutia damu, damu otologasi (ya mgonjwa mwenyewe) inaweza kuelekezwa kando kutoka kwa mgonjwa iende kwenye chombo cha kusafisha damu (ambacho ni figo bandia) au kwenye bomba la kupiga-piga damu lililo mfano wa moyo-mapafu. Damu hiyo hutiririka nje kupita katika mrija na kwenda kwenye kile kiungo bandia kinachoipiga-piga na kuichunga vitakataka (au kuitia hewa safi ya oksijeni), halafu inarudi kwenye mfumo wa mzunguko wa damu ya mgonjwa. Wakristo fulani wameruhusu jambo hilo ikiwa vifaa vinavyotumiwa havikutangulia kutiwa damu iliyowekwa akibani. Wao wamekuwa na rai ya kwamba ule mrija wa kupeleka damu nje-nje unakuwa ni kurefusha mfumo wa mzunguko wa damu yao ili iweze kupita katika kiungo bandia. Wamehisi kwamba damu katika mzunguko huu unaofanya kazi ndani-ndani bila kutoka nje kabisa ingali ilikuwa ni sehemu yao na haikuhitaji ‘kumwagwa nchini.’a

Ingawa hivyo, namna gani ikiwa mtiririko wa damu hiyo otologasi (ya mgonjwa mwenyewe) ungesimama kwa muda mfupi, kama vile mashine ya moyo-mapafu ikifungwa iache kazi wakati daktari-mpasuaji anapochunguza ukamilifu wa mishipa koronari iliyopachikwa ili kupitisha damu kandokando?

Kwa kweli, kinachokaziwa na Biblia si suala la kuendelea kutiririka kwa damu. Hata bila upasuaji, moyo wa mtu ungeweza kusimama kwa muda mfupi kisha uanze tena kazi.b Haingekuwa lazima mfumo wake wa mzunguko wa damu uondolewe damu yote ile kisha damu yake iondolewe mbali kwa sababu tu mtiririko wa damu ulikuwa umesimama wakati moyo ulipokwama hivyo. Kwa sababu hiyo, Mkristo anayelazimika kuamua kama ataruhusu damu yake ielekezwe kando kupitia chombo fulani cha nje-nje ni sharti akaze fikira, si hasa juu ya kama mkatizo mfupi katika mtiririko ungeweza kutukia, bali juu ya kama yeye angeweza kuhisi akidhamiria kwamba damu ile iliyoelekezwa kando ingekuwa bado ni sehemu ya mfumo wake wa mzunguko wa damu.​—Wagalatia 6:5.

Namna gani kutohoa damu (kuifanya iwe nyepesi zaidi)? Wapasuaji fulani wanaitikadi kwamba kuna faida ya kutohoa damu ya mgonjwa wakati wa upasuaji. Hivyo, mwanzoni mwa upasuaji, wao wanaelekeza kiasi fulani cha damu kwenye mifuko ya akiba nje ya mwili wa mgonjwa na kujazia nafasi iliyobaki kwa majimaji ambayo si damu; baadaye, damu hiyo inaruhusiwa itiririke kutoka kwenye mifuko hiyo na kumrudia mgonjwa. Kwa kuwa Wakristo hawaruhusu damu yao iwekwe akibani, watabibu fulani wamerekebisha njia hiyo, wakipanga kuwe na kifaa katika mzunguko wa damu ambacho kinaunganishwa muda wote na mfumo wa mzunguko wa damu ya mgonjwa. Wakristo fulani wamekubalia jambo hilo, wengine wamekataa. Hapo tena, ni lazima kila mtu aamue kama angeona damu hiyo iliyoelekezwa kando katika mzunguko huo wa kutohoa damu kuwa ni kama tu ile inayotiririka ikipita katika mashine ya moyo-mapafu, au angeifikiria kuwa ni damu iliyotoka ndani yake na kwa hiyo inapasa kuondolewa mbali.

Kielelezo cha mwisho cha damu otologasi (ya mgonjwa mwenyewe) kinahusu kuokoa damu yenye kutoka na kuitumia upya wakati wa upasuaji. Vifaa vinatumiwa kuchochea damu iendelee kutoka katika jeraha, kuipiga bomba ipite katika kichungi (ili kuondoa migandamano au takataka) au kichujio kinachozunguka-zunguka mbio (kuondoa kabisa majimaji yaliyomo), halafu kuielekeza irudi ndani ya mgonjwa. Wakristo wengi wamehangaika sana juu ya kama kusafishwa damu kwa kutolewa nje na kurudishwa ndani jinsi hiyo kungeweza kuhusisha ndani mkatizo wa mtiririko wa damu kwa muda mfupi. Hata hivyo, kama ilivyotajwa, jambo la kuhangaikiwa zaidi Kibiblia ni kama damu inayotoka na kuingia ndani ya jeraha lililopasuliwa na daktari ingali ni sehemu ya mtu yule. Je! uhakika wa kwamba damu imetiririka kwa kutoka katika mfumo wa mzunguko wa damu yake na kuingia ndani ya jeraha hilo unamaanisha kwamba inapasa ‘kumwagwa nchini,’ kama damu ile inayotajwa kwenye Walawi 17:13? Ikiwa mtu anaitikadi hivyo, labda yeye hangeruhusu damu hiyo iliyotoka nje kusafishwa itumiwe katika mwili wake. Hata hivyo, Mkristo mwingine (ambaye pia hangeruhusu damu itiririke kwa kutoka ndani yake, iwekwe akibani kwa muda, na baadaye iingizwe tena ndani yake) angeweza kukata shauri kwamba kukubali kifaa kinachozungusha damu kwa kuitoa mahali palipopasuliwa na kuirudisha-rudisha tena mwilini hakungekuwa ni kuvunja dhamiri yake iliyozoezwa.

Kama tunavyoweza kuona, vifaa au mbinu za namna-namna zinaendelea kuongezeka kuhusiana na damu otologasi (ya mgonjwa mwenyewe). Sisi hatuwezi na hatupaswi kujaribu kutoa maelezo juu ya kila utofautiano wa hali. Wakati wa kukabiliwa na swali katika eneo hilo, kila Mkristo ana daraka la kujipatia maelezo marefu kutoka kwa wafanya kazi wa tiba halafu afanye uamuzi wa kibinafsi.

Ingawa mengi yamesemwa hapa juu ya mambo ya kitiba, masuala ya kidini ndiyo ya maana kubwa zaidi. Wakati Mkristo anapokuwa akitatua mashaka au maswali yoyote kuhusu njia za kitiba zinazohusisha damu, jambo la kwanza kabisa linapasa kuwa kwamba yeye anaonyesha imani, kwamba anastahi amri ya Mungu ‘kushika mwiko wa damu,’ na kwamba anadumisha dhamiri njema. Kwa nini? Kwa sababu njia ya msingi zaidi ambayo maisha zinaweza kuokolewa kwa damu si kupitia ufundi stadi wa kitiba bali ni kupitia nguvu ya uokozi ya damu ya Kristo. Mtume Paulo aliandika hivi: “Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu.” (Waefeso 1:7; Ufunuo 7:14,17) Ingawa huenda tiba ya ki-siku-hizi ikaweza kutusaidia kurefusha maisha zetu kwa muda, hakika hatungetaka kurefusha maisha yetu ya sasa kwa kufanya jambo lolote ambalo lingevunja dhamiri yetu ya Kikristo au kumchukiza Mpaji-Uhai wetu.​—Mathayo 16:25; 1 Timotheo 1:18, 19.

[Maelezo ya Chini]

a Ona Mnara wa Mlinzi, Novemba 15, 1978, kurasa 21, 22.

b Huenda jambo hilo likatokana na kupatwa ghafula na shambulio la ugonjwa wa moyo, kupata mshtuko kutokana na nguvu za umeme, au kushuka mno kwa joto la mwili, kama kwa kuzamishwa katika maji ya baridi-barafu.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Ukiwa pamoja na chombo cha moyo-mapafu, mzunguko huo ni kutia ndani: (1) mrija wa kutoa damu katika mfumo wa mishipa ya mgonjwa; (2) vibomba vya kufyonza damu hiyo ili irudi ndani; (3) kitia-oksijeni kinachoingiza ndani mapovu ya hewa; (4) kichungi cha kusafisha damu chenye utembo ulio na vishimo-shimo; (5) bomba kuu lenye kuzunguka; (6) ukanda wa kuirudisha damu katika mfumo wa mzunguko wa damu ya mgonjwa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki