Wafa kwa Kupiga Makasia
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Ufaransa
TWAWEZA kuwazia tu kilichotukia. Umati wa watu watazama meli mpya aina ya manchani ya mfalme wa Ufaransa inapoanza safari yake kutoka kwenye bandari ya Marseilles katika Mediterania. Ni mojawapo ya manchani maridadi zaidi zilizowahi kuabiri baharini. Tezi yake imerembwa kwa nakshi tata hali kadhalika madoido yenye dhahabu na lulu kemkemu. Fahari ya kifalme ya sitaha yazidishwa na vitambaa bora sana vilivyopambwa kwa tarizi. Nuru ya asubuhi inapometameta katika umaridadi huo usio na kifani, baadhi ya watu wafikiria kwa fahari sifa ya Mfalme Louis wa 14 ya kuwa “Mfalme wa Jua.”
Kufikia karne ya 17, manchani zilitumiwa tu katika harakati chache za kijeshi, lakini Mfalme Louis wa 14 aliamua kuongeza idadi ya manchani zake hadi 40—kundi kubwa zaidi la manchani katika Mediterania. Wataalamu wanakadiria kwamba manchani 20 zingemudu mahitaji yake kabisa. Alikusudia kutumiaje kundi hilo kubwa la manchani?
Mshauri wa mfalme Jean-Baptiste Colbert alieleza: “Hakuna uwezo unaothibitisha ukuu wa mfalme na kumpa umashuhuri zaidi miongoni mwa wageni kuliko uwezo wa manchani.” Kwa kweli, sababu kuu ya Louis kuzidisha manchani zake ilikuwa fahari. Lakini, fahari hiyo ingepatikana kwa thamani gani?
Fikiria wanadamu walivyoteseka. Wapiga-makasia 450 walijazwa kwenye sitaha yenye urefu usiozidi meta 45 na upana usiozidi meta 9. Waliishi na kufanya kazi kwenye mazingira hayo yaliyosongamana kwa miezi mingi mfululizo. Ngozi ya mwili wao ilichubuliwa na hewa ya baharini yenye chumvi, na miili yao ilikuwa na makovu yaliyotokana na kupigwa mijeledi mara nyingi. Nusu kati yao wangefia katika ile inayoitwa na wanahistoria Wafaransa “mharabu mkuu wa wanaume” katika Ufaransa.
Kwa kweli, jambo lililowaletea watu wachache fahari na utukufu lilisababisha mateso na kifo kwa wengine wengi. Lakini mfalme alipata wapi maelfu mengi ya wapiga-makasia waliohitajiwa kuendesha manchani zake 40?
Kupata Wapiga-Makasia
Katika Enzi za Kati, wapiga-makasia wa manchani—au galeotti, kama walivyoitwa—walikuwa watu huru, na kupiga-makasia kulionwa kuwa kazi yenye kuheshimiwa. Hata hivyo, kufikia karne ya 17 mambo yalikuwa yamebadilika. Wapiga-makasia fulani, walioitwa Waturuki, walinunuliwa kutoka Milki ya Uturuki. Wengi wao walikuwa Waislamu, ingawa baadhi yao walikuwa waumini wa Kanisa Othodoksi. Wafungwa wa vita walitumiwa pia.
Wanahistoria Wafaransa wasema kwamba “miongoni mwa hatua zenye kuchukiza na za kipumbavu zaidi kuchukuliwa ili ‘kuimarisha’ wafanyakazi hao, pasina shaka ilikuwa kutumia wapiganaji wa jamii ya Wahindi Wamarekani kwenye manchani za Mfalme wa Jua.” Kuwashika Wahindi Wamarekani kulikuwa kosa. Mnamo mwaka wa 1689 walirejeshwa nyumbani baada ya mataifa ya jamii ya Wahindi Wamarekani kuwatisha wakoloni Wafaransa wa mapema.
Lakini miradi ya Louis ya kujitafutia umashuhuri, ilihitaji wapiga-makasia zaidi. Colbert alipata suluhisho. Aliwaeleza mahakimu mapenzi ya mfalme kwamba “wawahukumu wahalifu wengi zaidi iwezekanavyo na kwamba hata hukumu ya kifo ibadilishwe na kuwa hukumu ya kupiga-makasia kwenye manchani.” Kuwatumia wahalifu kwa njia hiyo halikuwa jambo jipya. Wafungwa walikuwa wametumiwa kuwa watumwa wa kuendesha manchani wakati wa vita na Italia karne mbili mapema. Hata hivyo, idadi ya wafungwa waliotumiwa kwenye manchani wakati wa utawala wa Louis wa 14 na kilembwe wake Louis wa 15 ilipita ya wakati mwingine wowote. Baina ya mwaka wa 1680 na 1748, takriban wanaume 60,000 walihukumiwa kupiga-makasia. Watumwa hao wa kupiga makasia kwenye manchani walikuwa nani?
Ni Nani Walioandikishwa?
Karibu nusu ya wale waliohukumiwa kupiga-makasia kwenye manchani walikuwa wahalifu wa kawaida. Kuanzia kwa wauaji hadi kwa wezi wa kawaida. Wafanya-magendo waliadhibiwa pia vivyo hivyo, nyakati nyingine walifanyiza idadi kubwa ya wapiga-makasia.
Kwa kuongezea, watu waliodunishwa na jamii walitumikishwa kwenye manchani. Mnamo mwaka wa 1666 ofisa aliyesimamia manchani hizo huko Marseilles aliandika hivi: “Ningependa uamuzi ufanywe wa kusomba watu wazembe, mahujaji, . . . Wahindi-wahamaji, na wazururaji wengine na kuwajaza kabisa kwenye manchani. . . . Kufanya hivyo kungeondoa watu wasiofaa wenye kulemea ulimwenguni.” Hivyo basi, kwa udhuru wa kudumisha utaratibu wa kijamii, Wahindi-wahamaji na omba-omba waliandikishwa. Na katika mwaka wa 1660, hata mahujaji wa Poland waliokuwa wakizuru madhabahu moja Ufaransa waliandikishwa kwa lazima!
Wengine waliotumiwa kufanya kazi hiyo ni watoro wa jeshi ambao, baada ya kukamatwa, walihukumiwa maisha kwenye manchani hizo. Watoro walikatwa pua na masikio yao, mashavu yao yalitiwa alama kwa kifaa maalum chenye maumbo ya maua, na vichwa vyao vilinyolewa. Wakati wa vita vingi vya Louis wa 14 toka mwaka wa 1685 hadi 1715, takriban watoro 17,000 walihukumiwa kupiga-makasia kwenye manchani. Wangetazamia nini?
Mateso Yao
Mateso ya wapiga-makasia wa manchani hizo yalianza hata kabla ya safari ya baharini kuanza. Mwanzoni, walifungiwa kwenye magereza ya muda kwa muda wa miezi sita hivi kabla ya kufungwa minyororo pamoja na mamia ya wafungwa wengine na kupelekwa kwa lazima huko Marseilles. Baadhi yao, kama wale waliotoka Brittany au Paris, waliona cha mtema kuni kwani walilazimishwa kusafiri kwa miguu umbali wa kilometa 800 kwa zaidi ya mwezi mmoja. Mhusika mmoja aliita safari hiyo “adhabu mbaya kupita zote kwa wafungwa.” Wengi walifia njiani.
Lakini, hawakufa tu kutokana na urefu wa safari au chakula kidogo walichopewa. Walinzi waliwatesa vibaya sana wafungwa hao. Wengi walikufa kutokana na mapigo na kunyimwa chakula na usingizi wa kutosha. Isitoshe, watu waliokutana nao njiani hawakuwahurumia wanaume hao waliopita kwa ukawaida katika maeneo ya Ufaransa. Yasemekana kwamba mfungwa mmoja alipowasihi sana wampe maji, wanawake wenyeji walimjibu hivi: “Tembea, tembea! Utapata maji tele huko uendako!”
Nusu Yao Walikufa
Wafungwa wengi hawakuwa wamewahi kuona bahari, sembuse manchani. Mara tu walipowasili kwenye bandari ya Marseilles, waliona kifo kikiwakodolea macho. Wafungwa hao walikusanywa kwenye manchani iliyo tupu na kuchunguzwa, mmoja wao aliandika kwamba, walikuwa kama “ng’ombe walionunuliwa sokoni.” Mambo binafsi ya kila mmoja yaliandikwa, nao wafungwa waliitwa kwa nambari badala ya majina yao kwenye manchani. “Bila shaka kuwa mmoja wa wapiga-makasia kwenye manchani lilikuwa jambo lenye kutatanisha sana, nalo lilivuruga sana kisaikolojia na kimwili,” asema mwanahistoria mmoja. Hata hivyo, mateso mabaya hata zaidi yangewakumba.
Katika chumba chenye urefu wa meta 2.3 na upana wa meta 1.25 tu, wanaume watano waliishi na kupiga makasia kwa miezi mingi mfululizo huku wakiwa wamefungwa minyororo kwenye benchi walizokalia. Kila mpiga-makasia aliketi kwenye kisehemu chenye ukubwa wa sentimeta 45 tu. Chumba kilisongamana sana hivi kwamba wanaume hao hawangeweza hata kukunja mikono yao walipovuta makasia, kila kasia lilikuwa na urefu wa angalau meta 12 na uzito wa zaidi ya kilogramu 130. Kupiga makasia kwa saa nyingi sana ilikuwa kazi ya sulubu ambayo ilitanua misuli ya wapiga-makasia hao, iliwachosha sana na kushinda ustahimilivu wao. “Ililingana na kufanya kazi ya sulubu katika eneo la kitropiki,” aeleza mwanahistoria mmoja.
Manchani hizo zilikuwa chini sana, na wapiga-makasia walikuwa takriban meta moja tu kutoka uso wa maji. Walilowa maji wakati wote, kwa kuwa kwa kawaida walipiga makasia huku miguu yao ikiwa majini, na ngozi ya mwili wao ilimong’onyolewa na hewa yenye chumvi. Walipewa kiasi kidogo mno cha chakula. “Wafungwa walifanya juu chini ili kuokoka,” asema mwanahistoria mmoja. Halikuwa jambo rahisi hata kidogo kutoroka. Zawadi za kuwapata watoro ziliwachochea wakulima wenyeji kujiunga na harakati za kumtafuta yeyote aliyejaribu kutoroka. Ni mfungwa 1 tu kati ya 100 aliyefaulu.
Ilikuwa nadra sana kufuata hukumu zilizotolewa. Hivyo basi, mpiga-makasia aliyehukumiwa adhabu ya miaka michache angeendelea kupiga makasia kwenye manchani miaka 25 baada ya hukumu kwisha. Karibu thuluthi ya wanaume walikufa kabla ya miaka mitatu kutimia. Kwa ujumla, nusu ya wapiga-makasia walikufa. Hata wapiga-makasia walioacha kazi hiyo walikufa sawa na wale waliokuwa wakiendelea baharini. Katika majira ya baridi kali ya mwaka wa 1709/1710, thuluthi kati yao walikufa kutokana na njaa kali na hali mbaya ya hewa. Kwa kusikitisha, baadhi yao walihukumiwa kupiga-makasia kwa sababu ya dini yao.
Wahukumiwa kwa Sababu ya Itikadi Yao
Mwaka wa 1685, Mfalme Louis wa 14 alifutilia mbali Amri ya Nantes, na Uprotestanti ukapigwa marufuku nchini Ufaransa.a Waprotestanti wapatao 1,500 walihukumiwa kupiga-makasia kwenye manchani kwa sababu walikataa kuwa Wakatoliki au walijaribu kutoroka nchini. Kuwaadhibu “waasi wa kidini” kwa njia hiyo kulikuwa kumejaribiwa mwaka wa 1545, wakati ambapo wafuasi 600 wa Waldensesb walipelekwa kwenye manchani kwa amri ya Mfalme Francis wa Kwanza. Wakati wa Louis wa 14, yule aliyeitwa eti mfalme Mkristo, mnyanyaso ulipamba moto.
Kwa nini Waprotestanti wakapelekwa kwenye manchani? Ofisa mmoja wa mfalme alitaja sababu: “Waasi wa kidini hawawezi kurejeshwa [kwenye Ukatoliki] kwa njia iwayo yote ila kwa lazima.” Mwanahistoria mmoja aongezea hivi: “Mfalme alitumaini kwamba mara baada ya kuonja ‘maisha ya manchani,’ Waprotestanti wengi waliohukumiwa wangeacha dini ambayo walikuwa wamejidhabihu kwelikweli kwa ajili yake.” Hata hivyo, wengi wao walikataa kukana imani yao ili kuwekwa huru. Kama tokeo, kwa kawaida walipigwa kinyama hadharani kwa sababu ya uchochezi wa makasisi wa jeshi Wakatoliki wa manchani hizo. Baadhi yao walikufa; wengine walibaki na makovu ya mapigo kwa maisha yao yote.
Licha ya jeuri hiyo ya kikatili, Waprotestanti walishiriki kwa bidii imani yao na wengine. Kama tokeo, watu fulani, kutia ndani angalau kasisi mmoja Mkatoliki, wakawa Waprotestanti. Wale walioonwa kuwa hatari sana, Waprotestanti walioelimika, waliondolewa kutoka kwenye manchani na kutupwa katika magereza yaliyo ardhini ili wafie humo. Lakini hilo halikuwazuia wapiga-makasia Waprotestanti kusaidiana, hata walipanga madarasa ya kuwafunza wenzao kujua kusoma na kuandika.
Wafungwa walitilia maanani kilichowafanya wanyanyaswe. “Kadiri ninavyoteseka, ndivyo ninavyozidi kupenda kweli inayonifanya niteseke,” akaandika Mprotestanti Pierre Serres. Nchi nyingi zilishtuka kusikia kuhusu mnyanyaso wa kidini nchini Ufaransa. Mwaka wa 1713, Malkia Anne wa Uingereza alifaulu kuomba kuachiliwa huru kwa wafungwa wengi. Jambo la kustaajabisha ni kwamba, Waprotestanti waliokuwa wamepigwa marufuku kuondoka Ufaransa sasa walifukuzwa.
Kutokomea kwa Manchani
Hatimaye, manchani hizo zilitokomea kabisa, kwa sababu ya uvumbuzi mpya wa vyombo vya baharini na uhaba wa fedha. Matatizo ya kifedha ya Mfalme Louis wa 14 yalimlazimu kupunguza manchani zake. Kufikia mwaka wa 1720, ni manchani 15 tu zilizosalia, na matumizi yake yalipungua sana. Kwa muda mwingi, wapiga-makasia walibaki Marseilles, ambako walikuwa wafanyakazi wa kawaida jijini, walifanya kazi katika viwanda vya sabuni vilivyokuwa karibu au waliuza mavazi waliyoshona. Hatimaye, sheria iliyoashiria kutokomea kabisa kwa manchani hizo ilipitishwa mwaka wa 1748.
Wafaransa bado hukumbuka kwa majuto manchani hizo. Wanapokabili tatizo, kwa kawaida Wafaransa husema hivi kwa mshangao: “Quelle galère!” au tafsiri sisisi ya Kiswahili ni, “Ni manchani iliyoje!” Mengi tunayojua kuhusu maisha kwenye manchani hizo yanatokana na masimulizi ya kibinafsi yaliyoandikwa na wapiga-makasia Waprotestanti. Licha ya ubaguzi mbaya sana wa kidini, walifanyiza shirika la pamoja la kutoa msaada na utegemezo. Walihitaji kuwa na uvumilivu na tumaini ili waweze kunusurika, nao hawakuwa tayari kuridhiana.
Inashangaza, hata ufikiripo kutovumiliana kidini kulikoenea pindi hiyo, kwani wanahistoria wameeleza walivyostaajabu kuona mahakimu wakiwa tayari “kutekeleza mara moja sheria ambayo iliwaona raia wanyoofu na waaminifu kuwa sawa na wahalifu sugu.”
Kwa kweli, kumbukumbu la watumwa wa manchani labaki ushuhuda thabiti wa ukosefu mbaya wa haki wa wanadamu kuwaelekea wenzao. Naam, ‘mtu huwa na uwezo juu ya mwenzake kwa kumwumiza.’ (Mhubiri 8:9, Zaire Swahili Bible) Jambo la kufurahisha ni kwamba wakati umekaribia ambapo Mtawala aliyewekwa rasmi na Mungu, Yesu Kristo, “atamkomboa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.”—Zaburi 72:12-14.
[Maelezo ya Chini]
b Ona Mnara wa Mlinzi, Agosti 1, 1981, ukurasa wa 12-15, Kiingereza.
[Picha katika ukurasa wa 13]
Walipiga makasia chini ya hali za kusikitisha
[Hisani]
© Musée de la Marine, Paris
[Picha katika ukurasa wa 15]
Maelezo ya Kifaransa yaliyo juu ya picha yasema hivi: “Njia hakika na za unyofu za kuwarejesha waasi wa kidini kwa imani ya Katoliki.” Picha hiyo ni ya mwaka wa 1686
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]
Ukurasa wa 2, 12, na 15: © Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris