Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g04 9/8 kur. 18-19
  • Natto—Soya za Pekee za Japani

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Natto—Soya za Pekee za Japani
  • Amkeni!—2004
  • Habari Zinazolingana
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2004
  • Wali au Mchele—Wapenda Upi Zaidi?
    Amkeni!—1995
  • Chakula Chako ni Chenye Lishe Kadiri Gani?
    Amkeni!—1995
  • Vitu Ambavyo “Ufalme wa Mbinguni” Unafanana Navyo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2004
g04 9/8 kur. 18-19

Natto—Soya za Pekee za Japani

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Japani

Je, ungependa kula maharagwe ya soya yaliyochacha na yenye nyuzi zenye kunata? Labda hungependa! Lakini natto—maharagwe yanayopikwa kwa mvuke na kuchachushwa—ni chakula kinachopendwa sana nchini Japani. Hata inakadiriwa kwamba kila mwaka zaidi ya tani 110,000 za maharagwe ya soya hutumiwa kutayarisha tani 220,000 za natto.

KULINGANA na hekaya, yapata miaka elfu moja iliyopita, shujaa aliyeitwa Minamoto Yoshiie alipata na kuonja soya zilizokuwa zimechemshwa na kuachwa kwenye mabua, kisha zikachachuka. Hivyo ndivyo chakula cha natto kilivyotokea. Inaaminika kwamba kufikia mwisho wa enzi ya Edo (1603-1867), natto kilikuwa chakula cha pekee katika sehemu fulani za Japani.

Natto hutayarishwaje? Zamani, matita ya mpunga yalijazwa maharagwe yaliyopikwa kwa mvuke kisha yakawekwa mahali penye joto na unyevu. Hivyo, yalichachushwa na bakteria inayoitwa Bacillus natto inayopatikana katika mabua ya mpunga. Wakati wa uchachishaji, protini na glucide zilizo katika soya huoza na kutokeza nyuzi za natto zinazoweza kufikia meta sita!

Siku hizi, natto hutokezwa kwa wingi viwandani. Katika viwanda hivyo, kiasi kinachofaa cha bakteria ya Bacillus natto hunyunyizwa kwenye soya zilizopikwa kwa mvuke. Kisha, kwa kutumia mashine maharagwe hayo huhamishiwa kwenye vyombo vidogo. Mashine nyingine huzipeleka kwenye hifadhi, ambapo halijoto na unyevunyevu huziwezesha kuchacha na kukomaa. Baada ya kupakiwa, natto huwa tayari kuuzwa.

Natto ina harufu fulani ambayo huwachukiza watu wengine. Lakini maharagwe hayo yenye nyuzinyuzi yana lishe bora. Wakati wa uchachishaji, vitamini B2 na K na madini kama vile chuma, kalisi, na potasiamu hufanyizwa. Isitoshe, natto ina vimeng’enya vinavyosaidia kusaga chakula. Kimeng’enya kinachoitwa nattokinase ambacho huyeyusha damu iliyoganda, hupatikana pia katika natto.

Zaidi ya kuliwa, nyuzi za natto zina matumizi mengine. Kwa mfano, natto hutumiwa kutengeneza nyuzi fulani, plastiki inayoweza kuoza, na utomvu. Utomvu wa natto huhifadhi maji.

Uchachishaji hutokeza joto na vitu vingine ambavyo huzuia bakteria nyingine. Hivyo, natto ikitayarishwa vizuri, inaweza kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika. Katika jaribio fulani, bakteria za natto zilitayarishwa kwa kutumia bakteria ya E. coli O157 inayoweza kusababisha ugonjwa wa tumbo unaoweza kuua. Bakteria hiyo ikafa. Hata hivyo, inapendekezwa natto ihifadhiwe katika friji na kuliwa kabla ya juma moja kwisha kwa sababu ladha yake hubadilika pole kwa pole. Uchachishaji ukiendelea kwa muda mrefu, maharagwe hayo huyeyuka kabisa na kutokeza harufu kali kama ya amonia.

Watu wengi hula natto kwa njia ya kienyeji kwa kuikoleza na mchuzi wa soya. Wengine hupenda kuongeza haradali au vitunguu vya majani vilivyosagwa, hali wengine huongeza gugu-maji au yai. Natto huwa tamu inapoliwa pamoja na wali mweupe ulio moto. Pia inaweza kuliwa na spageti, tambi za Japani, na hata supu. Wengine hufurahia kuila kwa mkate uliopakwa siagi. Unapoila kwa wali, unahitaji kukoroga maharagwe kabisa. Kadiri unavyoyakoroga, ndivyo nyuzi zaidi zinavyojitokeza.

Natto inazidi kupendwa kadiri watu wanavyojua umuhimu wake kwa afya. Kwa hakika, natto isiyo na harufu huuzwa, nayo imependwa sana na wale walioiepuka kwa sababu ya harufu yake. Vyovyote vile, jaribu kula natto.a Huenda wewe pia ukapenda ladha ya soya za Japani zenye nyuzinyuzi zilizochachushwa!

[Maelezo ya Chini]

a Wale wanaotumia dawa ya warfarin kwa sababu ya magonjwa ya moyo wanapaswa kujihadhari kwani vitamini K iliyo kwenye natto inaweza kuhitilafiana na utendaji wa dawa hiyo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki