Mathayo
15 Ndipo Mafarisayo na waandishi kutoka Yerusalemu wakamjia Yesu, wakisema: 2 “Kwa nini wanafunzi wako hukiuka mapokeo ya watu wa nyakati za hapo zamani? Kwa kielelezo, hawaoshi mikono yao wakiwa karibu kula mlo.”
3 Kwa kujibu yeye akawaambia: “Ni kwa nini nyinyi pia hukiuka amri ya Mungu kwa sababu ya mapokeo yenu? 4 Kwa kielelezo, Mungu alisema, ‘Heshimu baba yako na mama yako’; na, ‘Acheni yeye ambaye hutukana baba au mama afikie mwisho katika kifo.’ 5 Lakini nyinyi husema, ‘Yeyote yule amwambiaye baba yake au mama: “Chochote kile nilicho nacho ambacho kwacho ungeweza kupata manufaa kutoka kwangu ni zawadi iliyowekwa wakfu kwa Mungu,” 6 lazima asimheshimu baba yake hata kidogo.’ Na kwa hiyo nyinyi mmelibatilisha neno la Mungu kwa sababu ya mapokeo yenu. 7 Nyinyi wanafiki, Isaya kwa kufaa alitoa unabii juu yenu, aliposema, 8 ‘Watu hawa huniheshimu mimi kwa midomo yao, bali moyo wao umeondolewa mbali nami. 9 Ni bure kwamba wao hufuliza kuniabudu, kwa sababu wao hufundisha amri za watu kuwa mafundisho.’” 10 Ndipo akauita umati karibu na kuwaambia: “Sikilizeni na mpate maana: 11 Si kile kiingiacho ndani ya kinywa chake hutia mtu unajisi; bali ni kile kitokacho katika kinywa chake ndicho hutia mtu unajisi.”
12 Ndipo wanafunzi wakaja na kumwambia: “Je, wajua kwamba Mafarisayo walikwazika waliposikia uliyosema?” 13 Kwa kujibu akasema: “Kila mmea ambao Baba yangu wa kimbingu hakuupanda utang’olewa. 14 Waacheni hivyo. Viongozi vipofu ndivyo walivyo. Basi, ikiwa kipofu aongoza kipofu, wote wawili wataanguka ndani ya shimo.” 15 Kwa kujibu Petro akamwambia: “Kifanye kielezi kiwe wazi kwetu.” 16 Ndipo yeye akasema: “Je, nyinyi pia mngali bila uelewevu? 17 Je, hamjui kwamba kila kitu kiingiacho katika kinywa hupita ndani ya matumbo na huondoshwa kuingia katika mtaro wa takataka? 18 Hata hivyo, mambo yanayotoka katika kinywa hutoka moyoni, na mambo hayo hutia mtu unajisi. 19 Kwa kielelezo, kutoka moyoni huja mawazowazo maovu, mauaji-kimakusudi, uzinzi, uasherati, wizi, shuhuda zisizo za kweli, makufuru. 20 Hayo ndiyo mambo yanayotia mtu unajisi; lakini kula mlo bila kuosha mikono hakutii mtu unajisi.”
21 Akiondoka hapo, Yesu sasa akatoka kuingia katika sehemu za Tiro na Sidoni, 22 Na, tazama! mwanamke Mfoinike kutoka katika mikoa hiyo akatoka na kulia kwa sauti kubwa, akisema: “Uwe na rehema juu yangu, Bwana, Mwana wa Daudi. Binti yangu ameshikwa vibaya na roho mwovu.” 23 Lakini yeye hakusema neno kwa kujibu huyo mwanamke. Kwa hiyo wanafunzi wake wakaja na kuanza kumwomba: “Mwache aende zake; kwa sababu yeye afuliza kupaaza kilio akitufuata nyuma.” 24 Kwa kujibu yeye akasema: “Sikutumwa kwa wowote ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” 25 Mwanamke huyo alipokuja akaanza kumsujudia, akisema: “Bwana, nisaidie!” 26 Kwa kujibu akasema: “Si sawa kuuchukua mkate wa watoto na kuutupa kwa mbwa wadogo.” 27 Yeye akasema: “Ndiyo, Bwana; lakini kwa kweli hao mbwa wadogo hula baadhi ya makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza ya mabwana-wakubwa wao.” 28 Ndipo Yesu akasema kwa kumjibu: “Ewe mwanamke, ni kubwa imani yako; acha itukie kwako kama utakavyo.” Na binti yake akaponywa tangu saa hiyo na kuendelea.
29 Akivuka nchi kutoka hapo, Yesu akaja karibu na bahari ya Galilaya, na, baada ya kupanda kwenda kuingia katika mlima, alikuwa ameketi huko. 30 Ndipo umati mkubwa ukamkaribia yeye, ukiwa pamoja na watu waliokuwa vilema, walioharibika viungo, walio vipofu, mabubu, na wengi wa hali tofauti, nao wakawatupa kabisa miguuni pake, naye akawaponya; 31 hivi kwamba umati ukahisi mshangao ulipoona mabubu wakisema na vilema wakitembea na vipofu wakiona, nao ukatukuza Mungu wa Israeli.
32 Lakini Yesu akawaita wanafunzi wake kwake na kusema: “Nahisi sikitiko kwa ajili ya umati, kwa sababu tayari ni siku tatu ambazo umekaa pamoja nami nao hauna kitu cha kula; nami sitaki kuuacha uende zao ukifunga. Yawezekana ukazimia barabarani.” 33 Hata hivyo, wanafunzi wakamwambia: “Sisi tutapata wapi katika mahali hapa pa upweke mikate ya kutosha kushibisha umati wa ukubwa huu?” 34 Ndipo Yesu akawaambia: “Ni mikate mingapi mliyo nayo?” Wakasema: “Saba, na samaki wadogo wachache.” 35 Kwa hiyo, baada ya kuuagiza umati uegame juu ya ardhi, 36 akachukua ile mikate saba na wale samaki na, baada ya kushukuru, akavimega na kuanza kuvigawa kwa wanafunzi, nao wanafunzi wakavigawa kwa umati. 37 Na wote wakala na kushiba, na kama ziada ya vipande vidogo wakaokota makapu saba ya chakula yaliyojaa. 38 Na bado wale wenye kula walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto wachanga. 39 Mwishowe, baada ya kuuacha umati uende zao, akaingia katika mashua na kuja kuingia katika mikoa ya Magadani.