Marko
Kulingana na Marko
1 Mwanzo wa habari njema juu ya Yesu Kristo: 2 Kama vile imeandikwa katika Isaya nabii: “(Tazama! Ninatuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, ambaye atatayarisha njia yako;) 3 sikilizeni! mtu fulani anapaaza kilio nyikani, ‘Tayarisheni njia ya Yehova, nyinyi watu, fanyeni barabara zake ziwe nyoofu,’” 4 Yohana mbatizaji alitokea nyikani, akihubiri ubatizo katika ufananisho wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 5 Kwa sababu hiyo eneo lote la Yudea na wakaaji wote wa Yerusalemu walishika njia yao kumwendea, nao walibatizwa naye katika Mto Yordani, wakiungama waziwazi dhambi zao. 6 Basi Yohana alikuwa amevaa nywele za ngamia na mshipi wa ngozi kuzunguka viuno vyake, na alikuwa akiwala nzige na asali-mwitu. 7 Naye alikuwa akihubiri, akisema: “Baada yangu mtu fulani mwenye nguvu zaidi kuliko mimi anakuja; mimi sistahili kuinama nizifungue gidamu za makubazi yake. 8 Mimi niliwabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa roho takatifu.”
9 Baada ya siku hizo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya akabatizwa na Yohana katika Yordani. 10 Na mara hiyo alipopanda kutoka majini akaona mbingu zikiachanishwa, na, kama njiwa, roho ikiteremka juu yake; 11 na sauti ikaja kutoka katika mbingu: “Wewe ni Mwana wangu, mpendwa; nimekukubali wewe.”
12 Na mara hiyo ile roho ikamshurutisha kwenda nyikani. 13 Kwa hiyo akaendelea nyikani siku arobaini, akishawishwa na Shetani, naye alikuwa pamoja na mahayawani-mwitu, lakini malaika walikuwa wakimhudumia.
14 Basi baada ya Yohana kukamatwa Yesu akaenda katika Galilaya, akihubiri habari njema ya Mungu 15 na kusema: “Wakati uliowekwa rasmi umetimizwa, na ufalme wa Mungu umekaribia. Iweni wenye kutubu, nyinyi watu, na iweni na imani katika habari njema.”
16 Alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya aliona Simoni na Andrea ndugu ya Simoni wakitupa nyavu zao huku na huku katika bahari, kwa maana walikuwa wavuvi. 17 Kwa hiyo Yesu akawaambia: “Nifuateni, nami nitawafanya nyinyi kuwa wavuvi wa watu.” 18 Na mara moja wakaacha nyavu zao na kumfuata. 19 Na baada ya kwenda mbele kidogo akaona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana ndugu yake, kwa kweli, walipokuwa katika mashua yao wakitengeneza nyavu zao; 20 na bila kukawia akawaita. Nao wakaacha baba yao Zebedayo katika hiyo mashua pamoja na watu walioajiriwa wakaenda zao wakimfuata. 21 Nao wakashika njia yao kwenda Kapernaumu.
Mara baada ya hapo ilipokuwa siku ya sabato akaingia katika sinagogi akaanza kufundisha. 22 Nao wakawa wenye kustaajabishwa na njia yake ya kufundisha, kwa maana huko alikuwa akiwafundisha kama mwenye mamlaka, na si kama waandishi. 23 Pia, wakati huohuo kulikuwako katika sinagogi lao mtu aliyekuwa chini ya nguvu ya roho asiye safi, naye akapaaza sauti, 24 akisema: “Tuna jambo gani nawe, Yesu wewe Mnazareti? Je, ulikuja kutuangamiza sisi? Najua sawasawa wewe ni nani, Mtakatifu wa Mungu.” 25 Lakini Yesu akamkemea, akisema: “Kimya, na umtoke!” 26 Na yule roho asiye safi, baada ya kumtupa kuingia katika mfurukuto na kupiga kelele kwa sauti ya juu, akamtoka. 27 Basi, watu wote wakashangaa sana hivi kwamba wakaanza mazungumzo miongoni mwao wenyewe, wakisema: “Ni nini hili? Ni fundisho jipya! Yeye aagiza kwa nguvu yenye mamlaka hata roho wasio safi, nao humtii.” 28 Kwa hiyo ripoti juu yake ikasambaa mara hiyo katika pande zote katika nchi yote yenye kuzunguka katika Galilaya.
29 Na mara hiyo wakatoka katika sinagogi wakaingia katika nyumba ya Simoni na Andrea pamoja na Yakobo na Yohana. 30 Basi mama-mkwe wa Simoni alikuwa amelala chini akiwa mgonjwa wa homa, nao mara moja wakamwambia Yesu juu yake. 31 Naye akimwendea akamwinua, akimshika mkono; na homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.
32 Baada ya kuwa jioni, wakati jua lilipokuwa limetua, watu wakaanza kumletea wote wale waliokuwa wagonjwa na wale waliopagawa na roho waovu; 33 na jiji lote lilikuwa limekusanyika palepale penye mlango. 34 Kwa hiyo akaponya wengi waliokuwa na magonjwa ya namna mbalimbali, naye akafukuza roho waovu wengi, lakini alikuwa hawaachi roho waovu waseme, kwa sababu walimjua yeye kuwa Kristo.
35 Na mapema asubuhi, kulipokuwa bado kuna giza, akaondoka akatoka nje akaenda mahali pa upweke, na huko akaanza kusali. 36 Hata hivyo, Simoni na wale walio pamoja naye wakamtafuta kwa bidii 37 na kumpata, nao wakamwambia: “Wote wanakutafuta wewe.” 38 Lakini yeye akawaambia: “Acheni twende mahali pengine, katika miji ya vijiji iliyo karibu, ili nipate kuhubiri huko pia, kwa maana ni kwa kusudi hilo nimetokea.” 39 Naye akaenda, akihubiri katika masinagogi yao kotekote katika Galilaya yote na kufukuza roho waovu.
40 Huko pia mwenye ukoma akaja kwake, akimsihi sana hata kwa kukunja magoti, akimwambia: “Ikiwa tu wewe wataka, waweza kunifanya safi.” 41 Ndipo akasukumwa na sikitiko, naye akanyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia: “Mimi nataka. Fanywa safi.” 42 Na mara hiyo ule ukoma ukamtoka, naye akawa safi. 43 Zaidi ya hilo, akampa maagizo ya nguvu na mara moja akamwacha aende, 44 na kumwambia: “Angalia kwamba huambii mtu yeyote hata jambo moja, bali nenda ujionyeshe mwenyewe kwa kuhani na kutoa kwa ajili ya kutakaswa kwako vile vitu alivyoamuru Musa, kuwa ushahidi kwao.” 45 Lakini baada ya kwenda zake mtu huyo akaanza kupiga mbiu sana juu ya hilo na kusambaza hayo masimulizi kotekote, hivi kwamba Yesu hakuweza tena kuingia waziwazi katika jiji, lakini akakaa nje katika mahali pa upweke. Na bado wakafuliza kumjia kutoka pande zote.