Marko
2 Hata hivyo, baada ya siku kadhaa akaingia tena Kapernaumu naye akaripotiwa kuwa nyumbani. 2 Kwa sababu hiyo wengi wakakusanyika, kadiri ya kwamba hakukuwa na nafasi tena, wala hata karibu na mlango, naye akaanza kuwaambia lile neno. 3 Na watu wakaja wakimletea mwenye kupooza akichukuliwa na watu wanne. 4 Lakini kwa kutoweza kumleta moja kwa moja hadi alipo Yesu kwa sababu ya umati, wakaiondoa paa juu ya mahali alipokuwa, na wakiisha kuchimba kipenyo wakateremsha kitanda ambacho juu yacho yule mwenye kupooza alikuwa akilala. 5 Na Yesu alipoona imani yao akamwambia yule mwenye kupooza: “Mtoto, dhambi zako zimesamehewa.” 6 Basi hapo palikuwa na baadhi ya waandishi, wakiwa wameketi na wakiwazawaza mioyoni mwao: 7 “Kwa nini mtu huyu anaongea namna hii? Anakufuru. Nani awezaye kusamehe dhambi ila mmoja, Mungu?” 8 Lakini Yesu, akiisha kufahamu mara hiyo kwa roho yake kwamba walikuwa wakiwazawaza kwa njia hiyo ndani yao wenyewe, akawaambia: “Kwa nini mnawazawaza mambo haya mioyoni mwenu? 9 Ni jipi lililo rahisi zaidi, kuambia mwenye kupooza, ‘Dhambi zako zimesamehewa,’ au kusema, ‘Inuka uchukue kitanda chako utembee’? 10 Lakini kusudi nyinyi watu mjue kwamba Mwana wa binadamu ana mamlaka kusamehe dhambi juu ya dunia,”—akamwambia yule mwenye kupooza: 11 “Mimi nakuambia, Inuka, chukua kitanda chako, uende nyumbani kwako.” 12 Ndipo akaondoka, na mara akachukua kitanda chake akatembea mbele yao wote kwenda nje, hivi kwamba wote walivutwa na hisia, nao wakamtukuza Mungu, wakisema: “Hatujaona kamwe lenye kufanana na hilo.”
13 Tena akatoka kwenda kando ya bahari; na umati wote ukafuliza kumjia, naye akaanza kuufundisha. 14 Lakini alipokuwa akipita kandokando, akaona mara hiyo Lawi mwana wa Alfayo akiwa ameketi kwenye ofisi ya kodi, naye akamwambia: “Uwe mfuasi wangu.” Na akiondoka akamfuata. 15 Baadaye ilitukia kuwa ameegama kwenye meza katika nyumba yake, na wakusanya-kodi wengi na watenda-dhambi walikuwa wakiegama na Yesu na wanafunzi wake, kwa maana walikuwa wengi nao wakaanza kumfuata. 16 Lakini waandishi wa Mafarisayo, walipoona alikuwa akila pamoja na watenda-dhambi na wakusanya-kodi, wakaanza kuwaambia wanafunzi wake: “Je, yeye hula pamoja na wakusanya-kodi na watenda-dhambi?” 17 Aliposikia hilo Yesu akawaambia: “Wale walio na nguvu hawahitaji tabibu, bali wale walio wagonjwa wahitaji. Nilikuja kuita, si watu waadilifu, bali watenda-dhambi.”
18 Basi wanafunzi wa Yohana na Mafarisayo walizoea kufunga. Kwa hiyo wakaja wakamwambia: “Ni kwa nini wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo huzoea kufunga, lakini wanafunzi wako hawazoei kufunga?” 19 Na Yesu akawaambia: “Wakati bwana-arusi yupo pamoja nao marafiki wa bwana-arusi hawawezi kufunga, je, waweza? Maadamu wana bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga. 20 Lakini siku zitakuja wakati bwana-arusi atakapoondolewa mbali kutoka kwao, na ndipo watakapofunga siku hiyo. 21 Hakuna mtu ashonaye juu ya vazi la nje kuukuu kiraka cha nguo ambayo haijaruka; akifanya hivyo, nguvu yacho kamili huvuta kutoka kwenye hilo, lile jipya kutoka kwenye lile kuukuu, na mraruko huwa mbaya zaidi. 22 Pia, hakuna mtu awekaye divai mpya ndani ya viriba vikuukuu vya divai; akifanya hivyo, divai hupasua ngozi, na divai hupotezwa na vilevile ngozi. Bali watu huweka divai mpya ndani ya viriba vipya vya divai.”
23 Basi ikatukia kwamba alikuwa akiendelea kwa kupita katikati ya mashamba ya nafaka siku ya sabato, na wanafunzi wake wakaanza kushika njia yao wakikwanyua masuke ya nafaka. 24 Kwa hiyo Mafarisayo wakaanza kumwambia: “Tazama sasa! Kwa nini wanafanya lisiloruhusiwa kisheria siku ya sabato?” 25 Lakini yeye akawaambia: “Je, hamjasoma kamwe hata mara moja alilofanya Daudi alipokuwa na uhitaji akaona njaa, yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye? 26 Jinsi alivyoingia ndani ya nyumba ya Mungu, katika lile simulizi juu ya Abiathari kuhani mkuu, akala mikate ya toleo, ambayo hairuhusiki kisheria mtu yeyote kula ila makuhani, naye akawapa wale watu waliokuwa pamoja naye baadhi yayo pia?” 27 Kwa hiyo akaendelea kuwaambia: “Sabato ilikuja kuwako kwa ajili ya binadamu, na si binadamu kwa ajili ya sabato; 28 kwa sababu hiyo Mwana wa binadamu ni Bwana hata wa sabato.”