Marko
3 Mara nyingine tena akaingia katika sinagogi, na mtu mmoja mwenye mkono uliokauka kabisa alikuwa humo. 2 Kwa hiyo walikuwa wakimchunguza sana kuona kama angeponya huyo mtu siku ya sabato, ili wapate kumshtaki. 3 Naye akamwambia huyo mtu mwenye mkono ulionyauka: “Inuka uje katikati.” 4 Halafu akawaambia: “Je, yaruhusika kisheria siku ya sabato kutenda kitendo chema au kutenda kitendo kibaya, kuokoa au kuua nafsi?” Lakini wao wakafuliza kukaa kimya. 5 Na baada ya kuwatazama huku na huku kwa ghadhabu, akiwa ametiwa kihoro kabisa kwa ukosefu-hisia wa mioyo yao, akamwambia huyo mtu: “Nyoosha mkono wako.” Naye akaunyoosha, na mkono wake ukaponywa. 6 Ndipo Mafarisayo wakatoka na mara wakaanza kufanya baraza pamoja na wafuasi wa chama cha Herode dhidi yake, kusudi wamwangamize.
7 Lakini Yesu pamoja na wanafunzi wake wakaondoka kwenda baharini; na umati mkubwa kutoka Galilaya na kutoka Yudea ukamfuata. 8 Hata kutoka Yerusalemu na kutoka Idumea na kutoka ng’ambo ya Yordani na kuzunguka Tiro na Sidoni, umati mkubwa, uliposikia ni mambo mengi kadiri gani aliyokuwa akifanya, ukamjia. 9 Naye akawaambia wanafunzi wake waendelee kuwa na mashua ndogo ya kumtumikia ili umati usiweze kumsonga. 10 Kwa maana aliponya wengi, tokeo likiwa kwamba wote wale waliokuwa na maradhi yenye kutia kihoro walikuwa wakimwangukia ili wamguse. 11 Hata roho wasio safi, wakati wowote ule walipokuwa wakimwona, walikuwa wakijiangusha wenyewe chini mbele yake na kupaaza kilio, wakisema: “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.” 12 Lakini mara nyingi aliwaagiza kwa kusisitiza wasimfanye ajulikane.
13 Naye akapanda mlima na kuwaita wale aliotaka, nao wakamwendea. 14 Naye akafanyiza kikundi cha kumi na wawili, ambao pia aliwaita jina “mitume,” ili wapate kuendelea kuwa pamoja naye na kwamba apate kuwatuma wahubiri 15 na kuwa na mamlaka ya kuwafukuza roho waovu.
16 Na kikundi cha wale kumi na wawili aliofanyiza walikuwa Simoni, ambaye pia alimpa jina la ziada Petro, 17 na Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana ndugu ya Yakobo (hawa pia aliwapa jina la ziada Boanerge, ambalo lamaanisha Wana wa Ngurumo), 18 na Andrea na Filipo na Bartholomayo na Mathayo na Tomasi na Yakobo mwana wa Alfayo na Thadayo na Simoni Mkananayo 19 na Yuda Iskariote, ambaye baadaye alimsaliti.
Naye akaenda ndani ya nyumba. 20 Mara nyingine tena umati ukakusanyika, hivi kwamba hawakuweza hata kula mlo. 21 Lakini jamaa zake waliposikia juu ya hilo, wakatoka kwenda kumshika, kwa maana walikuwa wakisema: “Amerukwa na akili.” 22 Pia, waandishi walioteremka kutoka Yerusalemu walikuwa wakisema: “Ana Beelzebubi, naye huwafukuza roho waovu kwa njia ya mtawala wa roho waovu.” 23 Kwa hiyo, baada ya kuwaita waje kwake, akaanza kuwaambia kwa vielezi: “Shetani awezaje kufukuza Shetani? 24 Kwani, ufalme ukipata kuwa wenye kugawanyika dhidi yao wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama; 25 na nyumba ikipata kuwa yenye kugawanyika dhidi yayo yenyewe, nyumba hiyo haitaweza kusimama. 26 Pia, ikiwa Shetani ameinuka dhidi yake mwenyewe na kuwa mwenye kugawanyika, hawezi kusimama, bali anakuja kwenye mwisho. 27 Kwa kweli, hakuna yeyote ambaye ameingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu awezaye kupora bidhaa zake zenye kuchukulika isipokuwa kwanza amfunge huyo mtu mwenye nguvu, na ndipo atakapoipora nyumba yake. 28 Kwa kweli nawaambia nyinyi kwamba mambo yote watasamehewa wana wa wanadamu, hata ziwe ni dhambi gani na makufuru wafanyayo kwa kukufuru. 29 Hata hivyo, yeyote yule akufuruye dhidi ya roho takatifu hana msamaha milele, bali ni mwenye hatia ya dhambi idumuyo milele.” 30 Hii ni kwa sababu walikuwa wakisema: “Ana roho asiye safi.”
31 Sasa mama yake na ndugu zake wakaja, na, walipokuwa wamesimama nje, wakapeleka ujumbe ndani kwake ili aitwe. 32 Ikawa kwamba, umati ulikuwa umeketi kumzunguka, kwa hiyo wakamwambia: “Tazama! Mama yako na ndugu zako nje wanakutafuta sana.” 33 Lakini kwa kujibu akawaambia: “Ni nani mama yangu na ndugu zangu?” 34 Na akiisha kuwatazama huku na huku wale walioketi kumzunguka katika duara, akasema: “Ona, mama yangu na ndugu zangu! 35 Yeyote yule afanyaye mapenzi ya Mungu, huyo ni ndugu yangu na dada na mama.”